Tuesday, August 30, 2016

Video: Ziara ya Waziri Mkuu Mh. Kasim Majaliwa Wilayani Kalambo - Rukwa


Mkuu wa Mkoa adhamiria kumaliza malalamiko ya ardhi Rukwa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amedhamiria kumaliza kabisa malalamiko yanayotolewa na wananchi wa mkoa wa Rukwa katika migogoro ya ardhi iliyopo katika Mkoa wake.

Alionesha dhamira hiyo pale alipotembelea ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kuangalia zoezi linaloendelea la kusikiliza walalmikaji wamiliki wa ardhi kutoka katika maeneo mbalimbali ya Mkoa.

Zoezi hili lilianza baada ya maafisa wa Ardhi wa Mkoa na wa Manispaa ya Sumbawanga kupewa agizo na Waziri Mkuu Mh. Kasim Majaliwa alipofanya ziara tarehe 24, August, 2016 katika mji wa Sumbawanga na kubaini ukubwa wa tatizo la migogoro ya ardhi katika mkoa wa Rukwa.

Wakati anatoa maagizo hayo Waziri Mkuu, aliwapa maafisa ardhi hao siku mbili kuanza kusikiliza malalamiko hayo.

Mwenyekiti wa kamati ya kusikiliza malalamiko ambae pia ni mkuu wa idara ya Miundombinu kutoka katika ofisi ya Mkuu wa  Mkoa wa Rukwa Seti George Mwakyembe amesema kuwa zoezi hilo lilianza tarehe 26, August na linatazamiwa kuisha tarehe 2, Septemba, 2016 kwa Wakazi 300 wa Manispaa ya Sumbawanga.

Ndugu Mwakyembe alieleza kuwa kutokana na maagizo ya Mkuu wa Mkoa, watatangaza ratiba ya kuweza kuzungukia wilaya na Halmashauri zilizobaki ili kuweza kumfikia kila mlalamikaji wa migogoro ya Ardhi katika Mkoa wa Rukwa.


“Tunataka ifikie hatua tuseme migogoro ya ardhi kwa Mkoa wa Rukwa sasa basi, Maana majibu ya maswali yote ya wananchi yapo” Mkuu wa Mkoa alisema.

Thursday, August 25, 2016

Waziri Mkuu: Tatizo La Maji Sumbawanga Kuwa Historia.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa inatarajiwa kupata huduma ya maji safi na salama kuanzia mwezi ujao baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji uliokuwa unajengwa.

Mradi huo unajengwa kwa usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, Manispaa ya Sumbawanga (SUWASA), kwa ufadhili wa nchi za Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Ujerumani kupitia benki yake ya Maendeleo (KfW), sh. bilioni 31 utakapokamilika.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo Jumatano, Agosti 24, 2016, wakati na akiweka jiwe la msingi la mradi wa maji safi na usafi wa mazingira katika Manispaa ya Sumbawanga na kuitaka kampuni ya kampuni ya Techno Fab Gammon Joint Venture ya India kumaliza ujenzi wa mradi huo haraka iwezekanavyo.

Amesema mradi huo ambao tayari umekamilika kwa asilimia 85 unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu, hivyo aliwataka wananchi kuhakikisha wanashirikiana na Manispaa katika kulinda miundombinu ya mradi huo mara utakapokamilika pamoja na kutunza vyanzo vya maji.

“Pamoja na Serikali kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kugharamia miradi ya maji inayojengwa katika maeneo mbalimbali nchini,changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo imekuwa kubwa kutokana na baadhi ya visima vimeanza kukauka hali inayosababishwa na uharibifu wa mazingira,” amesema.

Amesema kumekuwa na uvamizi mkubwa katika maeneo ya vyanzo vya maji ambapo wananchi wanajishughulisha na shughuli za ulimaji, uchungaji wa mifugo, ujenzi wa nyumba za makazi na uchomaji misitu hivyo kusababisha uchafuzi wa mazingira na hatimaye vyanzo hivyo hukauka.

Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu amewaagiza wakuu wote wa wilaya na wenyeviti wa vijiji nchini kuyasimamia maeneo yenye vyanzo vya maji na kuwaondoa watu wotewalioyavamia kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria pamoja na kuwafikisha mahakamani.

Naye Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe ambaye alimuwakilisha Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge katika hafla hiyo alisema aliishukuru Serikali ya Ujerumani na Umoja wa nchi za Ulaya kwa kufadhili mradi huo.

Hata hivyo Mhandisi Kamwelwe alisema suala la kuhifadhi mazingira ni msingi endelevu wa upatikanaji wa maji safi na salama, hivyo aliwaomba wananchi kujiepusha na uchafuzi wa vyanzo vya maji na uharibifu wa mazingira ili kuepuka athari ya Taifa kukubwa na janga la ukame.


“Wananchi wanatakiwa kuacha kufanya shughuli za maendeleo ikiwemo kulima, kufuga ndani ya mita 60 kutoka katika mito, maziwa na vyanzo vingine vya maji ili kuepusha uharibifu wa mazingira ambao madhara yake ni makubwa kwa viumbe wote,” alisema.

JKT yatoa siku 7 wabunge wachukue madawati yao, wamo wa Nkasi Kusini na Kaskazini.

JESHI la Kujenga Taifa (JKT), limetoa siku saba kwa wabunge wa majimbo 18 yaliyopo ndani ya mikoa saba nchini kuhakikisha wanachukua madawati yao yaliyotengenezwa na jeshi hilo kabla ya Agosti 30, mwaka huu.

Madawati hayo 9,666 ni kati ya 30,000 ya awamu ya kwanza yaliyotengenezwa na jeshi hilo baada ya Ofisi ya Bunge kulipa zabuni ya kutengeneza madawati 60,000 kwa Sh bilioni tatu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JWTZ), Dk Hussein Mwinyi, alisema jeshi hilo limelikabidhi Bunge madawati 30,000, lakini madawati 9,666 kati ya hayo hayajachuliwa.

Hata hivyo, alisema kulingana na mgawo ambao jeshi hilo lilikabidhiwa na Kamati ya Bunge, madawati hayo yaligawanywa katika majimbo ya mikoa tisa, lakini hadi sasa majimbo 18 katika mikoa saba hayajachukua madawati hayo.

Aliitaja mikoa iliyopo kwenye mgawo huo na idadi ya madawati kwenye mabano kuwa ni Tanga ( 6,444), Njombe (3,222), Iringa (3,790), Mbeya (3,759), Mbeya Songwe (3,222), Rukwa (1,611), Ruvuma (4,833), Unguja (3,200) na Pemba (1,800).

“Mpaka sasa madawati yaliyokwishachukuliwa ni 22,721, madawati 9,666 kati ya 30,000 yaliyokwishakamilika sawa na asilimia 30 hayajachukuliwa na majimbo husika. Tunawaomba wabunge husika waje kuyachukua kabla ya Agosti 30, vinginevyo tutaziomba mamlaka husika ziyagawe kwenye maeneo yenye mahitaji,” alisema.

Dk Mwinyi aliyataja majimbo na mikoa ambayo hadi sasa hayajachukua madawati hayo kuwa ni Tanga katika majimbo ya Kilindi na Pangani (1,611) na Njombe majimbo ya Makambako, Ludewa, Wanging’ombe na Makete (2,148).

Maeneo mengine ni Iringa katika majimbo ya Iringa Mjini, Mbeya Mjini na Mbeya Vijijini (91,611), Ruvuma Jimbo la Tunduru Kaskazini ( 537) na Mbeya katika majimbo ya Ileje, Kyela, Rungwe na Busokelo ( 2,148).

Mengine ni Songwe ( 537) na Kwela, Nkasi Kaskazini na Nkasi Kusini (Rukwa) (1,611). Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, kutochukuliwa kwa madawati hayo kunasababisha kukosekana kwa nafasi ya kuweka madawati mengine yanayotengenezwa kwenye vituo mbalimbali vya JKT.

Pia, alisema yanapoendelea kubaki mahali hapo yanapigwa jua, kunyeshwa na kupungua ubora. Pamoja na hayo, alisema kuwa awamu ya pili ya madawati 30,000 inaendelea vyema kwa kuwa tayari madawati 20,000 yamekamilika na yanaweza kuchukuliwa na kugawanywa panapohusika.

Alisema, “madawati 10,000 yaliyobaki yatakamilika kabla ya Oktoba 30,000 kama ilivyopangwa na yatagawanywa katika majimbo 51”.


Aprili 11, mwaka huu, Bunge lilimkabidhi Dk Magufuli Sh bilioni sita ilizoziokoa kwa kubana matumizi katika maeneo mbalimbali kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, ikiwemo posho, safari za nje na viburudisho, ambazo Rais aliagiza zitumike kununua madawati kwa kila jimbo.

Waziri Mkuu: Hakuna Mwanasiasa Atakayeruhusiwa Kuvuruga Amani


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha inalinda amani ya nchi kwa gharama zozote na kamwe haitoruhusu mwanasiasa yeyote kusababisha vurugu zitakazochochea uvunjifu wa amani.

“Hatuzuii kuwa na vyama vya siasa ila haturuhusu vurugu kupitia vyama vya siasa na hakuna jambo lisilokuwa na mipaka. Mambo ya kuhamasishana kufanya vurugu hatutayaruhusu, tunataka watu wafanye kazi,” alisisitiza.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jumanne, Agosti 23, 2016, wakati akizungumza na viongozi wa dini pamoja na wazee wa mkoa wa Rukwa mara baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

Alisema Serikali inataka Watanzania wawe na uhakika wa kuendelea kufanya kazi zao za kuwaingizia kipato na kuwaletea tija, hivyo suala la kudumisha amani ni muhimu kwani vurugu zikitokea hawatakuwa na mahali pa kukimbilia na hakuna shughuli ya maendeleo itakayofanyika.

“Suala la uhamasishaji wananchi juu ya utunzaji wa amani ni la lazima hivyo viongozi wa dini na wazee kwa pamoja tushirikiane katika kukemea vitendo vya uchochezi kwasababu vurugu zikitokea Watanzania hatuna mahali pa kukimbilia,” alisema.

Aidha, Waziri Mkuu aliwaomba viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa pamoja na viongozi wake kwa sababu kazi ya uongozi ni ngumu na inachangamoto nyingi.Pia aliwaagiza viongozi wa dini wa mkoa wa Rukwa kuharakisha uundwaji wa Kamati ya Amani ya mkoa huo.

Awali, Sheikh wa mkoa wa Rukwa, Sheikh Rashid Akilimali amesema madhehebu ya dini hayawezi kuvuruga amani ya nchi ila anahofu na viongozi wa vyama vya siasa kutokana na vitendo vyao vya kuhamasisha vurugu.
 
Kufuatia hali hiyo Sheikh Akilimali aliwaomba wanasiasa nchini kutovuruga amani kwani machafuko yakitokea watashindwa kufanya ibada mbalimbali ikiwemo kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Sheikh Akilimali alisema kwa sasa wananchi wako huru kwenda kufanya ibada misikiti na makanisani kutokana na uwepo wa amani, hivyo aliwasisitiza wanasiasa kutothubutu kuichezea amani.

“Tafadhalini wanasiasa msituharibie amani ya nchi yetu. Amani haichezewi tunaona kwa wenzetu wanavyohangaika, wanaishi kwa tabu sisi hatujazoea  kukimbia. Sisi Watanzania ni moja na tunaishi kwenye nyumba moja hivyo hatuna budi kushirikiana kuilinda amani yetu,” alisema.

Kwa upande Katibu wa Wazee mkoani Rukwa, Kanali Mstaafu, John Mzurikwao alimuomba kiongozi huyo kuwasaidia  kutatua kero mbalimbali zinazoukabili mkoa huo zikiwemo za malipo ya pembejeo kwa mawakala wa kilimo pamoja na mgogoro wa ardhi katika shamba ya Efatha.

Waziri Mkuu alisema suala la malipo kwa mawakala wa pembejeo za kilimo linafanyiwa kazi na watalipwa baada ya Serikali kukamisha zoezi la uhakiki wa madeni hayo ili kujiridhisha kama kweli wakulima wapatiwa pembejeo na kwa kiwango gani.Waziri Mkuu: Watumishi Watakaokula Fedha Za CHF Wafukuzwe Kazi Na Wafikishwe Mahakamani

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakifurahia ngoma ya asili ya kabila la Wafipa wakati walipowasili kwenye kijiji cha Mtowisa mkoani Rukwa kuzungumza na wanachi Agosti 24, 2016. 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kufukuzwa kazi na kufikishwa mahakamani kwa watumishi wote wa sekta ya afya watakaobainika kula fedha zinazochangwa na wananchi kwa ajili ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Pia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Kamishna Mstaafu Zelote Stephen pamoja na Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk. John Gurisha kusimamia na kulinda fedha  za CHF zinazochangwa na wananchi  na kuhakikisha zinatumika kama zilivyokusudiwa.

Waziri Mkuu ametoa agizo Jumatano, Agosti 24, 2016, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye jimbo la Kwela, Tarafa ya Mtowisa wilayani Sumbawanga.

"Kitendo cha kula fedha zinazochangwa na wananchi kwa lengo la kupata huduma za afya kinawafanya wakatetamaa ya kuendelea kuchangia mfuko huo. Kama wako watumishi wenye tabia hizo waache mara moja," amesisitiza.

Mbali na kutoa agizo hilo kwa uongozi wa mkoa wa Rukwa, pia Waziri Mkuu amewataka wananchi kujiunga na CHF kwa sababu mfuko huo utawawezesha  kupata huduma za matibabu bure wao na familia zao katika kipindi cha mwaka mzima.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema barabara ya kutoka Ntendo hadi Muze yenye urefu wa kilometa 85  itajengwa kwa kiwango cha lami ili iweze kupitika kwa urahisi na kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa wakati.

“Mimi nilidhani mlima wa Kitonga ndio mkali kuliko yote na eneo la Sekenke ndio linatisha zaidi!. Kumbe barabara ya kuja huku Mtowisa ndiyo inatisha zaidi kuliko zote. Lazima tuweke lami ili iendelee kupitika kwa urahisi zaidi,” amesema.

Akizungumzia ombi lililotolewa na mbunge wa jimbo la Kwela, Ignas Malocha la kutaka tarafa hiyo ya Mtowisa kuwa wilaya au halmashauri, Waziri Mkuu amesema analichukua na kwenda kulifanyia tathmini na majibu atayapata kupitia uongozi wa mkoa.

Malocha alisema jimbo la Kwela linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya miundombinu ya barabara hali inayosababisha wananchi kushindwa kusafirisha mazao yao kwa urahisi.

Pia aliomba ukanda huo wa bonde la mto Rukwa upandishwe hadhi na kuwa wilaya au halmashauri ili kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Rukwa, Mhandisi Masuka Mkina ameelezea mkakati wa kuboresha miundombinu ya barabara mkoani hapa ikiwemo ya kutoka Ntendo hadi Muze wilayani iliyopo wilayani Sumbawanga.

Mhandisi Mkina amesema Serikali imetenga jumla ya sh. milioni 170 kwa ajili ya kuweka zege kwa ajili ya kurahisisha upandaji wa mlima hasa kwenye eneo la Kizungu katika barabara ya kutoka Ntendo hadi Muze.Atakayevamia Msitu Faini Mil. 70, Jela Miaka Saba - Waziri Mkuu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa akiwahutubia wananchi wa Nkasi, Mkoani Rukwa 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mtu yeyote atakayekutwa na hatia ya kuvunja sheria kwa kuvamia na kuharibu mazingira ya msitu wa Mfili ambao ndiyo chanzo pekee cha maji cha Wilayani Nkasi atatozwa faini ya sh. milioni 70 pamoja na kifungo miaka saba jela.

Katika kuhakikisha hatua zinachukuliwa Waziri Mkuu amemkabidhi mkuu wa wilaya ya Nkasi, Said Mtanda kitabu cha sheria kitachomuangoza katika kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kufanya uharibifu katika chanzo hicho cha maji.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jumanne, Agosti 23, 2016, wakati akizungumza na wananchi wa mji Mdogo wa Namanyere katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Sabasaba.

“Mkuu wa wilaya akishindwa kuwachukulia hatua za kuwaondoa wananchi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watu wote waliovamia maeneo ya hifadhi za misitu na kuanzisha makazi au kufanya shughuli za kijamii naye atakuwa jipu,” alisema.

Waziri Mkuu alisisitiza kuwa maeneo mengi nchini yanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji baada ya wananchi kuvamia katika vyanzo vya maji na kufanya shughuli za kibinadamu hivyo kusababisha vyanzo vingi kukakuka

“Serikali haitakubali kuona mtu anaharibu chanzo cha maji. Wananchi mnatakiwa kuwa walinzi wa maeneo hayo na atakayekutwa anachunga mifugo, analima, kukata nyasi au kufanya shughuli zozote za kijamii ndani ya maeneo hayo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Awali Waziri Mkuu alikagua mradi wa upanuzi wa bwawa la maji Mfili ambalo mwanzo lilikuwa na ujazo wa lita 1,500 ambapo litakapokamilika litakuwa na ujazo wa lija 248,067 hivyo kuwezesha wakazi 82,689 kunufaika.

Akizungumza kwenye eneo la mradi mara baada ya Waziri Mkuu kuwasili, Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya ya Nkasi, Julius Kaondo alisema hadi kukamilika mradi huo unatarajiwa kugharimu sh trilioni 1.011 ambapo Wizara ya Maji na Umwagiliaji imetoa sh. milioni 500 na OOfisi ya Rais TAMISEMI itatoa sh. milioni 500.

Mkurugenzi huyo alisema mradi unakabiliwa na changamoto ya ukosefu umeme ppamoja na mitambo ya kusukuma maji kwa kutumia nishati ya umeme, ambapo aliiomba Serikali kuipatia halmashauri hiyo sh. milioni 222.576 ikiwa ni gharama za kupeleka umeme kwenye eneo la mradi na kununua mitambo.

Mbali na kutembelea mradi wa upanuzi wa bwawa, pia Waziri Mkuu alitembelea hospitali teule ya wilaya ya Nkasi na kuzindua wodi mpya yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 72 kwa wakati mmoja


Waziri Mkuu Atoa Siku Mbili Kwa Maofisa Ardhi Kumaliza Kero Za Wananchi


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa akitoa maagizo kwa Mkuu wa Idara ya miundombinu ofisi ya Mkoa wa Rukwa Seti George Mwakyembe (wa kwaza kushoto) Pamoja na Mkuu wa Idara ya Ardhi Manispaa ya Sumbawanga Thadeo Maganga katika Viwanja vya Mandela.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku mbili kwa Mkuu wa Idara ya Ardhi na Miundombinu wa mkoa wa Rukwa pamoja na Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Sumbawanga kutatua matatizo ya ardhi yanayowakabili wakazi wa Manispaa hiyo.

“Ijumaa kuanzia saa 3.00 asubuhi wenye kero za ardhi wote waende kwenye ukumbi wa Manispaa mkuu wa idara atakuwa na watumishi wote na hapa mtasikilizwa kero zenu na kupatiwa ufumbuzi. Nasiku hiyo hakuna kazi nyingine ni kusikiliza wananchi tu,” alisema.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Agosti 24, 2016) wakati akizungumza na maelfu ya wakazi Mji wa Sumbawanga waliojitokeza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kiwanja cha Mandela katika jimbo la Sumbawanga mjini ambapo aliwasisitiza watendaji hao kuwasikiliza wananchi na kutatua kero zao.

Alisema tangu alivyoanza ziara yake katika mikoa ya Rukwa na Katavi kila eneo alilopita amekutana na wananchi wakiwa na mabango yanaeleza changamoto na hii inatokana na viongozi wa mikoa hiyo kushindwa kutenga siku maalumu kwa ajili ya kusikiliza kero hizo.

Waziri Mkuu alibainisha kwamba baadhi ya mikoa na halmashauri mbalimbali nchini zimeshaanza utaratibu huo wa kutenga siku maalumu katika wiki na kusikiliza matatizo yanayowakabili wananchi jambo ambalo limeanza kuonesha mafanikio ya utatuzi wa kero hizo.

Awali akizungumza katika mkutano huo mbunge wa jimbo la Sumbawanga Mjini Aeshi Hilaly alisema wakazi wa Manispaa ya Sumbawanga wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya migogoro mikubwa ya ardhi, hivyo alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidia katika kuipatia ufumbuzi.

Mbunge huyo alisema migogoro hiyo ambayo imedumu kwa muda mrefu imewasababishia usumbufu mkubwa wakazi wa jimbo hilo kukosa haki  zao na muda mwingi wamekuwa wakiutumia kufuatilia hatma ya ardhi yao bila ya mafanikio hivyo kurudi nyuma kimaendeleo.

Pia mbunge huyo alimuomba Waziri Mkuu kuwaondolea zuio la kuuza mazao yao nje ya nchi kwa sababu kitendo hicho kimesababisha kushuka bei ya mahindi na kusababisha hasara kubwa kwa wakulima ambao wametumia gharama kubwa katika kuandaa mashamba.

Akizungumzia zuio hilo Waziri Mkuu alisema lengo la Serikali kuzuia uuzwaji wa mazao nje ni kutaka kujiridhisha na uwepo wa chakula cha  kutosha nchini ili kuepuka kukumbwa na baa la njaa na kisha kwenda kuomba msaada kwenye nchi tuliowauzia.


 Kuhusu suala la soko la mahindi Waziri Mkuu alisema Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) watanunua kwa bei ya soko na kwamba wataruhusiwa kuuza nje ya nchi baada ya Serikali kujaza maghala yake huku wataalam wakimalizia kufanya tathmini ya hali ya chakula nchini


Waziri Mkuu Awataka Wakurugenzi Wasiowaondoe Walimu Wakuu Wasio na Shahada au Diploma badala yake wawahamasishe kwenda kusoma.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa akihutubia katika Viwanja vya Mandela Mjini Sumbawanga.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa halmashauri na Maofisa Elimu nchini kutowaondoa katika nyadhifa zao Waratibu wa Elimu Kata na Wakuu wa shule za sekondari wasiokuwa na shahada, walimu wakuu wa shule za msingi wasiokuwa na diploma badala yake wawahamasishe kwenda kusoma.

“Maofisa Elimu na Wakurugenzi msije mkawaondoa wale walimu wakuu kwa zile sifa nilizosema bado muda ukifika tutatangaza.Msije mkawakurupusha sasa hivi waacheni waendelee na kazi zao tutatoa muda ili wajipange viziri,” alisema.

 Agosti 20 mwaka huu Waziri Mkuu alisema Waratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata na Wakuu wa shule za sekondari wanatakiwa kuwa na shahada huku walimu wakuu kwenye shule wanatakiwa kuwa na diploma.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Jumatano, Agosti 24, 2016, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kiwanja cha Mandela katika jimbo la Sumbawanga mjini.

Alisema Mratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata ni lazima awe na shahada ili aweze kutekeleza majukumu yake ya kusimamia utolewaji wa elimu katika shule za sekondari na msingi.

“Wakuu wa shule za sekondari na waratibu wa elimu kata wasiokuwa na shahada wasiondolewe katika nafasi zao kabla ya kupewa nafasi ya kwenda kujiendeleza kwa masomo ili waweze kuwa na vigezo vya kuendelea kushika nyadhifa hizo,” alisema.

Alisema katika kuboresha maslahi ya walimu, Serikali imetenga zaidi ya sh. bilioni tano kwa mwezi ambazo ni posho ya madaraka. Waratibu Elimu Kata wanapewa sh 250,000 kwa mwezi huku Wakuu wa shule za sekondari na walimu wakuu katika shule za msingi wanapewa sh. 200,000.

Waziri Mkuu alisema badala ya kuwaondoa kwenye nyadhifa hizo ni vema Wakurugenzi wakawahamasisha walimu hao kwenda kusoma ili na wao wanufaike na posho ya madaraka iliyoanza kutolewa na Serikali hivi karibuni.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amewataka wazazi na walezi kwenda kuwaandisha watoto wenye umri wa miaka mitano katika shule za awali ambapo watapata fursa ya kujengewa msingi mzuri wa masomo kabla ya kuanza darasa la kwanza.

Pia aliagiza shule zote za msingi nchini zisizokuwa na madarasa ya awali kuhakikisha wanaanzisha madarasa hayo haraka na kuanza kutoa elimu hiyo.

Friday, August 19, 2016

"Rukwa kutajengwa Chuo cha VETA cha Kimkoa" Mh. Eng. Stella Manyanya

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Eng. Stella Manyanya akielezea Mipango ya Serikali juu ya maendeleo ya Elimu mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen.
"Katika Vyuo vinne vya VETA vitakavyojengwa nchini Kimojawapo kitajengwa katika Mkoa wa Rukwa"


Wednesday, August 17, 2016

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aahidi kuupandisha Mkoa Kielimu.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameonyesha kusikitishwa na hali ya Elimu ya Msingi katika Mkoa wake na kuahidi kuendelea kufuatilia na kuimarisha mikakati ya hali ya elimu katika mkoa.

Hayo aliyasema mbele ya  Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Eng. Stella Manyanya, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kujua maendeleo ya hali ya Elimu ya Mkoa wa Rukwa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen akitoa Ufafanuzi kwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Eng. Stella Manyanya.
Naibu Waziri Alisema kuwa serikali itaanza kuwashughulikia Walimu wakuu watakaoshindwa kutekeleza Wajibu wao.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Eng. Stella Manyanya akielezea Mipango ya Serikali juu ya maendeleo ya Elimu mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen.


                                       

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa awaasa wanarukwa kujitokeza kumpokea Waziri Mkuu 23/8/2016

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen Zelote awatangazia wananchi wa Mkoa wa Rukwa juu ya Ujio wa Waziri Mkuu Mh. Majaliwa Kasim Majaliwa mnamo tarehe 23/8/2016.
Aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza kupitia vyombo vya Habari mapema leo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen Zelote 
Thursday, August 4, 2016

Mkuu wa Mkoa aahidi kuumaliza Mgogoro wa Mbizi Forest na wachimba madini ya emerald

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameahidi kuwaita wahusika wote wa mgogoro kati ya watunza misitu pamoja na wachimba madini ya Emerald waliopo katika kijiji cha Mponda, Wilaya ya Sumbawanga.

Alitoa ahadi hiyo baada ya kutembelea hifadhi ya Msitu wa Mbizi baada ya kusikia kuna mgogoro na kutaka kujua chanzo chake na kusikiliza pande mbili ili kuweza kujua mahala pa kuanzia usuluhishi huo.

Katika ziara yake hiyo alionana na wachimba madini wa Emerald yanayosemekana kupatikana katika Mkoa wa Rukwa tu kwa Tanzania. lakini eneo la madini hilo limo ndani ya hifadhi ya Msitu wa Mbizi na kufanya eneo hilo kumilikiwa na watunza msitu wa Mbizi (Mbizi Forest).

Mkuu wa Mkoa alisema, "Hapa nimekuja kupata taarifa za mwanzo tu na hili jambo bado ni bichi, hivyo tutakaa pamoja na Mh. Mkuu wa Mkoa na wataalamu wote na wanasheria ili tujue nani ana haki ili tuepushe migongano, serikali ipo kuhudumia wananchi sio adui wa wananchi."