Tuesday, September 27, 2016

Mkuu wa Mkoa kukomesha mauaji kwa kisingizio cha ushirikina.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameahidi kukomesha mauaji yaliyofanyika kwa kisngizio cha ushirikina katika kijiji cha Kazila, kata ya Mwazye wilaya ya kalambo.

Mkuu wa Mkoa akiwa na serikali ya kijiji pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wakipita kuangalia nyumba zilizounguzwa.

Aliyasema hayo wakati alipohudhuria katika mazishi ya mzee Atanas Teremka aliyeuwawa na vijana waliyokuwa wakichoma moto nyumba tano za wanaodhaniwa kuwa ni washirikina na hatimae kuanza kuchoma moto nyumba zenye hifadhi ya mazao na kuiba.

Katika tukio hilo magunia 60 ya mahindi yaliibiwa, pamoja na magunia mawili ya alizeti na kuku na vijana hao kutokomea kusikojulikana ambapo kwa siku hiyo vijana tisa walikamatwa akiwemo mwenyekiti wa kitongoji cha Kazila.

 “Serikali ya Mkoa wa Rukwa, hii ambayo mimi ndio kiongozi hapa, wa tukio hili, itabaki ni histori, kwasababu cha kwanza mimi ni mzoefu, sitakubali kitendo cha namna hii kwa mtu yeyote, serilkali ya Tanzania inasisitiza maendeleo, maisha bora na wala haisisitizi, kuua, kuchoma moto mali za watu, haisisitizi kuharibu Amani ya nchi,” Mkuu wa Mkoa alifafanua.
Moja ya nyumba iliyounguzwa na vijana hao wasiojulikana
Katika kuwahakikishia wananchi hao kuwa Mkono wa Serikali ni mrefu na haki ya mtu haipotei Mkuu wa Mkoa alisema “Damu ya huu mzee haitakwenda bure, na imeanza kuchemka kwasababu wengine hata ile kuonekana hawaonekani, kukimbia na kujificha haisaiidii mkono wa serikali ni mrefu, utafanya kazi na utakuja na suluhu.”

Mkuu wa Mkoa aliyaongea maneno hayo akiwa na Mkuu wa wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura pamoja na Kamanda wa polisi Mkoa wa Rukwa George Kyando, na wakati huo huo alimuamuru Mkuu wa Wilaya ya kalambo atoe namba yake ya simu na Mkuu wa Mkoa nae pia aliwapa wananchi hao namba yake ya simu na kuwaasa watoe ushirikiano katika kuitokomeza tabia hiyo.

“Wote waliohusika kwa njia moja ama nyingine watakamatwa, ndipo watakapokuja kujua kuna kitu kinaitwa serikali na serikali ni nyie wananchi, hii itakuwa fundisho kwa watu wengine katika mkoa huu na ndani ya nchi,” Mkuu wa Mkoa aliwahakikishia.

Msemaji wa familia ya mzee Teremka Conrad Nyambe alisema kuwa maneno ya mkuu wa mkoa yanampa matumaini na faraja kubwa na kuona kuwa haki itapatikana na serikali inawajali wananchi wa hali zote.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen akitoa Mkono wa pole kwa msemaji wa familia Conrad Mwambi. alimkabidhi kiasi cha pesa Tsh. 121,500 zilizochangwa kutoka katika kanisa la Anglican alipokwenda kuswali Mkuu wa Mkoa siku ya Jumapili.

“Kweli nimefarijika sana na maneno ya Mkuu wa Mkoa, maana toka jana hawa watu hawapo na kwakuwa ametupa mawasiliano basi hii namba tutaitumia kumjulisha, hii inatuonesha kweli serikali inajali sauti ya kila mwananchi,” Conrad alisema.


Tuesday, September 20, 2016

Mkuu wa Mkoa ajiunga kwenye foleni ya wanafunzi kupata chakula cha “boarding”.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen alijiunga kwenye foleni ya wananfunzi wa Shule ya Sekondari ya Miangalua iliyopo katika kijiji cha Miangalua kata ya Miangalua, wilaya ya Sumbawanga ili kula pamoja nao chakula cha “boarding”.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen akipatiwa ugali na maharage.

Mkuu wa Mkoa alifanya kitendo hicho baada ya kufika katika shule hiyo bila ya taarifa ili kufahamu mazingira halisi ya maisha ya wananfunzi hao wanaoishi katika shule ya bweni yenye mchanganyiko wa wasichana na wavulana kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.

Kabla ya kujiunga kwenye foleni ya Chakula Mkuu wa Mkoa aliweza kuingia kwenye madarasa amatatu ambayo yanaandaliwa kuwa maabara ya shule hiyo na kisha kuangalia upatikanaji wa maji katika shule hiyo ndipo Makamu Mkuu wa Shule wa Shule hiyo Josephat Mwakasitu alipomwambia kuwa maji hutoka kwa masaa maalum.

Wakati Mkuu wa Mkoa akiendelea kula Ugali na maharage, wanafunzi wengi waliweza kumshangaa nae aliweza kuwauliza maswali mbalimbali yaliyohusiana na lishe inayopatikana katika shule hiyo.

“Wanafunzi huwa mnakula mboga za majani? Nyama? Wali?” Mkuu wa Mkoa aliuliza, na maswali yote hayo majibu yake yalikuwa, “Hapana”.

Baada ya kumaliza kula Mkuu wa Mkoa aliyatembelea mabweni ya wasichana na wavulana na kisha kuona ubora wa vyoo vinavyotumika na wananfunzi hao kisha alihitaji kuonana na wanafunzi pamoja na waalimu na kuweza kuwapa nasaha juu ya namna ya kuboresha chakula pamoja na mazingira ya hapo shuleni.

Pamoja na hayo Mkuu wa Mkoa hakusita kusisitiza juu ya ulinzi wa mabweni kutokana na matukio ya moto yaliyokithiri na kuwasihi wanafunzi na waalimu kuwa waangalifu na matumizi ya mishumaa, taa za chemli, vibatari, viberiti pamoja na wanafunzi wa kiume wenye tabia za kuvuta sigara.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen akikagua mabweni 
“Katika Shule ya Nkomolo huko Nkasi kulitokea moto katika mabweni na baada ya kufika pale usiku niliwauliza wale wanafunzi kama walikuiwa wanatumia vibatari au mishumaa wakanikatalia katakata, lakini baada ya polisi kufanya msako katika yale mabweni walikuja kugundua taa nne za Chemli ndipo walipotajana.” Mkuu wa Mkoa alielezea tukio hilo.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen akimpa zawadi mwanafunzi wa kidato cha tatu Happy Joseph

Katika kuwachangamsha wanafunzi Mkuu wa Mkoa aliuliza maswali kwa wanafunzi na kuweza kutoa zawadi kwa kila aliyejibu Saali vizuri kitendo ambacho kiliwaacha wanafunzi wakiwa na furaha.


Thursday, September 15, 2016

Mkuu wa Mkoa asaidia ulinzi na Usalama kwa watendaji wa mtaa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewataka watendaji wa mtaa wampe kesi moja ambayo ilionekana kutopata suluhisho la kuondoa kero ya wizi katika baadhi ya mitaa, Kata ya Majengo Sumbawanga mjini.

akiongelea kuhusu Kesi hiyo Mtendaji wa mtaa Celina Moyo alisema kuwa kuna kijana waliwahi kumkamata na Ushahidi wa gunia la ngani akiwa ameiba na kumpeleka polisi lakini hatimae kijana huyo ameachiwa na kurudi mtaani.

"Mimi nilishawahi kuiba gunia nane za ngano, na nikaachiwa nyie mmenikamata na kigunia kimoja tu mnadhani ntafungwa?" Bi. Celina akimuigiza kijana huyo aliyeonekana kujitapa mbele ya wanachi na Viongozi wa mtaa.

Mkuu wa Mkoa alichukua namba ya kesi na kuahidi kufuatilia, Na kuwaasa watendaji hao kutokuwa waoga katika kufuata sheria kwa yeyote anaepindisha sheria hizo.

"Sheria zikifuatwa wala hakuna shida zinatokea," Mkuu wa Mkoa alisisitiza. 


Mkuu wa Mkoa afuatilia wananfunzi hewa na kukuta kufuli ofisi ya Mwalimu Mkuu

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amekuta kufuli katia ofisi ya mwalimu mkuu wa shule ya msingi Majengo, wilayani sumbawanga baada ya kuamua kufuatilia suala la wananfunzi hewa.

Mkuu wa Mkoa alifia shuleni hapo muda wa Saa 5:50 asubuhi akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Hamid Njovu, Mtendaji wa Kata ya majengo, Lucy Mwakyusa pamoja na Mratibu elimu kata ya Majengo Patricia Maembe.

Baaa ya kukuta kufuli Mkuu wa Mkoa alimuagiza Mkurugenzi kumpigia simu afisa elimu wa manispaa ya Sumbawanga na kuweka "loud speaker" ili kujua utaratibu upoje wakati wa likizo ya waalimu.

Mkurugenzi alimpigia simu afisa huyo na kupewa majibu kuwa katika wakati wa Likizo waalimu wanatakiwa kufika shule na kuondoka saa sita mchana.


Mkuu wa Mkoa aanza kushughulikia upatikanaji wa madawa katika zahanati za Mkoa

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kamishna Mstaafu Zelote Stephen amesikitishwa na hali mbaya ya ukosefu wa madawa katika vituo vya afya na zahanati nyingi zilizopo katika mkoa wake na kuahidi kulishughulikia suala hilo.

Aliyasema hayo baada ya kukutana na waganga wakuu wa Halmashauri ya Wilaya na Manispaa ya Sumbawanga pamoja na wakurugenzi wake, akiwemo mgamga mkuu wa mkoa katika kikao alichokifanya ofisini kwake.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na meneja wa MSD kanda ya nyanda za juu kusini Daudi Msasi ambae alipewa nafasi ya kuelezea namna upatikanaji na utoaji wa dawa kutoka bohari ya dawa hadi kufika katika vituo vya afya na Zahanati.

Ndugu Msasi alisema kuwa ucheleweshwaji wa pesa kutoka katika halmashauri umekuwa moja ya sababu ya wao kushindwa kufikisha dawa kwa wakati na kuongeza kuwa tangu kuagizwa kwa dawa hadi kupatikana kwake huchukua miezi sita, hivyo aliziomba halmashauri kupeleka pesa mapema ili dawa zipatikane mapema.

Mkuu wa mkoa pia alitaka kujua fedha za mfuko wa Basket Fund, CHF na NHIF zinapokwenda kama fehda hizo hazipo kwaajili ya kutatua matatizo ya wananchi pamoja na wanachama wa bima za afya.Tuesday, September 13, 2016

Mkuu wa Mkoa awafundisha wakurugenzi kuwajibika kupunguza shida za wananchi

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewaasa wagurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa katika mkoa wa Rukwa, kutokaa kwenye maofisi na kutegemea kila kitu kuwa vizuri. 

Wosia huo ameutoa katika kikao alichokifanya katika ofisi yake leo hii, baada ya kuzunguka katika zahanati kadhaa na kugundua uwozo uliopo katika zahanati hizo.

"Kwanini Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya ndio aende akaibue uwozo wakati zahanati ni ya Mkurugenzi," Mkuu wa Mkoa alisema

Mkuu wa Mkoa alisisitiza kuwa wakurugenzi wanansahili kwenda kwenye huduma ili kujua shida wanazopata wananchi wasiridhike kwenye maofisi na matokeo yake wale waliopo kwenye vituo kupata mwanya wa kuiibia serikali


Saturday, September 3, 2016

Mkuu wa Mkoa amuonya afisa elimu msingi Manispaa ya Sumbawanga.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amemuonya afisa elimu shule ya msingi wa Manispaa ya Sumbawanga kwa kutofuatilia mahudhurio ya ufundishaji wa waalimu katika shule za Msingi za Manispaa.

Alitoa onyo hilo wakati alipoitisha kikao cha dharura leo (jumamosi tarehe 3/09/2016) kwa maafisa wa elimu, Mkurugenzi wa Manispaa pamoja na watu wa idara ya afya katika ofisi yake ili kupata majibu ya matatizo aliyokumbana nayo alipofanya ziara ya kushtukiza katika shule ya Msingi malagano, iliyopo katika kata ya Pito, Wilaya ya Sumbawanga.

Katika ahadi zake za kuimarisha elimu katika mkoa wake,Siku ya Ijumaa (tarehe 2/09/2016), Mkuu wa Mkoa alitembelea shule ya Msingi malagano na kubaini mahudhurio hafifu ya walimu darasani na katika juhudi za kujiridhisha na fikra hiyo ndipo alipowahoji wanafunzi wa darasa la tano ambao walikiri kuwa baadhi ya masomo kama Tehama, Stadi za Kazi na Uraia hawafundishwi kabisa.

Pamoja na kufanya mahojiano na wanafunzi, Mkuu wa Mkoa alifanya mapitio ya Daftari la mahudhurio ya walimu darasani na kugundua kuwa idadi ya vipindi vilivyofundishwa kuanzia tarehe 4 Julai, 2016 hadi 2 September, 2016 ni 31 badala ya 248 kwa masomo 7 ambayo ni Hisabati, kiingereza, Kiswahili, Jiografia, Haiba na Michezo, Sayansi na Historia.

Kwa kuonesha ukubwa wa tatizo taasisi isiyo ya kiserikali ya Twaweza ilitangaza utafiti ilioufanya katika sekta ya elimu ambao matokeo yake yanaonyesha kuwa walimu watatu kati ya 10, sawa na asilimia 31 wa shule za msingi ni watoro kazini.


Vilevile, katika utafiti huo wa Sauti za Wananchi uliofanyika kati ya Aprili na Mei, 2014 ukihusisha shule za msingi za Serikali 1,309, kaya 16,013 na wanafunzi 32,694 katika mikoa yote nchini, uliitaja mikoa inayoongoza kwa utoro baada ya Singida na asilimia zake kwenye mabano kuwa ni Mbeya (53), Geita (44), Tanga (41), Simiyu (40), Iringa 39 na Rukwa (36). Mikoa mingine mbali ya Manyara na Ruvuma isiyo na idadi kubwa ya walimu watoro kwa mujibu wa utafiti huo ni Kilimanjaro (19), Arusha (20), Katavi (20), Tabora (22) na Mtwara (22).


 “Hii ni mfano wa shule moja tu, hii ni dalili kuwa shule nyingine za Manispaa na Mkoa mzima zina hali kama hii ama Zaidi” Mkuu wa Mkoa alisema.

Pamoja na hayo Mkuu wa Mkoa aliwasisitiza Maofisa wa elimu kuwakumbusha na kuwaelimisha wazazi wa watoto hao kuwapa walau uji watoto wao kabla ya kwenda shule.

“Wazazi wakumbushwe mtoto anapokwenda shule apate japo uji, katika Mkoa huu uji sio shida, mtoto hataelewa masomo kama tumbo liko tupu,ndio chanzo cha vidonda vya tumbo” Mkuu wa Mkoa alisisitiza.

Katika kuhakikisha kasoro hiyo ya mahudhurio inarekebishwa, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga D. Halfan Haule aliahidi kuwa kutaandliwa timu ya kuweza kuzunguka shule zote za msingi za Sumbawanga ili kuyabaini mapungufu na kuyatafutia dawa.

Pamoja na kupitia kwenye shule ya Msingi Malagano Mkuu wa Mkoa pia aliweza kupita katika Zahanati ya Kijiji cha malagano na kukumbana na hali isiyoridhisha kama vile Hospitali kutokuwa na “Gloves”, Kituo hakikuwa na dawa za kutosha, idadi ndogo ya wananchi waliojiunga CHF na watumishi wachache. Hivyo amewaagiza watu wa Afya kutafuta suluhisho haraka.

Friday, September 2, 2016

VIJIJI VYOTE NCHINI KUNUFAIKIA NA NISHATI YA UMEME IFIKAPO 2021

Na Georgina Misama
Mpaka kufikia 2021 serikali imeahidi kusambaza umeme wa kutosha na wa uhakika katika vijiji vyote nchini ili kuendana na dhamira ya kuelekea katika uchumi wa kati kupitia viwanda.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo wakati wa kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Televisheni ya Taifa ya TBC1 kwa ushirikiano na Idara ya Habari-MAELEZO.

Prof. Muhongo alisema kuwa kukamilika kwa miradi ya kuzalisha nishati ya umeme ikiwemo Mradi wa Kinyerezi 1 unaozalisha megawati 150 kwa siku umesaidia kuongeza upatikanaji wa huduma ya umeme wa kutosha mijini na baadhi ya vijiji.

“serikali sasa ipo katika kutekeleza miradi mikubwa ya nishati za umeme na gesi ikiwa ni jitihada za kuhakikisha mpaka kufikia 2021 vijiji vyote nchini viwe vimepata huduma ya nishati ya umeme”. Alisema Prof. Muhongo.

Aidha, Prof. Muhongo alisema kuwa utekelezaji wa Miradi hiyo unaenda sambamba na lengo la Serikali ya awamu ya Tano ya kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda ifikapo 2025.

Akizungumzia kuhusu mikakati ya kuthibiti utoroshaji wa madini nchini Prof. Muhongo alisema kuwa serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuwakamata  watoroshaji wa madini hasa katika maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege.

Prof. Muhungo alisema kuwa kuanzia mwaka 2012 wamekamata madini ya aina mbalimbali zaidi ya Tani 10 yaliyokuwa yanatoroshwa kutoka nchini kwenda nchi mbalimbali.


Prof. Muhongo amewataka watanzania kutumia fursa mbalimbali zitakazotokana na utekelezaji wa miradi katika sekta ya gesi na mafuta ili kujiongezea kipato na kuiwezesha nchi kutimiza malengo yake kuelekea kuwa nchi ya uchumi wa kati.