Friday, October 21, 2016

Mkuu wa Mkoa atoa siku 30 kwa walio kwenye vyanzo vya maji Kuondolewa.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Steven amewapa siku 30 mamlaka ya maji ya mji wa Sumbawanga (SUWASA), idara ya maji ya Manispaa pamoja na ofisi ya Mkoa kuungana pamoja ili kuwaondoa wananchi wanaofanya shughuli za kibinaadamu karibu na vyanzo vya maji.

Aliagiza hayo baada ya kutembelea chanzo kikubwa cha maji ya mto Ndua kilichopo katika kijiji cha Ulinji kinachotegemewa na wakazi wa mji wa Sumbawanga na kuona shughuli za kibinaadamu zikiendelea ndani ya mita 60 kutoka katika chanzo hicho cha maji.

Mkuu wa Mkoa alisisitiza utekelezwaji wa sheria zilizopo ili kulinda vyanzo hivyo na kuongeza kuwa yeyote atakayekamatwa akifanya shughuli za kibinaadamu katika maeneo ya vyanzo vya maji wakamatwe.

"Maana wanachi hao hao ambao wanaharibu vyanzo vya maji ndio wa kwanza kulalamika kuwa hakuna maji, sasa serikali ipo kusimamia vyanzo hivi viendelee kudumu kwa kuboreshewa ulinzi na hakuna kinacholinda vyanzo hivi zaidi ya kutumia sheria zilizopo," Mkuu wa Mkoa alisisitiza.

                                       

Friday, October 14, 2016

Mkuu wa Mkoa aahidi Milioni Moja kwa Shule ya Kwanza Kimkoa mtihani wa Darasa la Saba.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameahidi kutoa Shilingi Milioni Moja kwa Shule itakayokuwa ya Kwanza Kimkoa katika Mitihani ya darasa la saba iliyokuwa imeshafanyika.
Aliyasema hayo alipokuwa akitoa hotuba mbele ya
waalimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika maadhimisho ya siku ya Mwalimu Duniani (tarehe 5.10.2016) yaliyofanyika katika Viwanja va Nelson Mandela ambapo Mkuu wa Mkoa aliuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.
Mkuu wa Mkoa aliwakumbusha waalimu wao kuacha uvivu na kuona aibu kwa kuwa mkoa wa 22 kati ya 26 katika mitihani ya darasa la saba, wakati Mkoa wa Katavi ambao ni mtoto wa Mkoa wa Rukwa ni wa Kwanza kitaifa.
"Kama mimi ndio ningekuwa mwalimu na nasikia matokeo kama hayo, ningekuwa najificha kwa aibu...aaaahhhhaaaa... hivi ninyi hamuoni aibu?," Mkuu wa Mkoa alieleza kwa masikitiko.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Kamisna Mstaafu Zelote Stephen
Lakini pia Kamisna Mstaafu Zelote Stephen aliwashukuru walimu kwa kuona juhudi za serikali kushughulikia uozo uliokuwepo serikalini kwani bila kuchukua hatua ya kuondoa uovu serikalini watumishi hawawezi kupata maslahi hayawezi kuwa mazuri kwani mapato yataendelea kupita katika mikono isiyo salama na kufujwa.

Aliwataka walimu kujichunguza kama hawamo katika makundi waliyoyataja ya ufisadi, utumishi hewa na uzembe kazini na kama wakibaini kuwa wako safi wachape kazi serikali inawaandalia mambo mazuri sana.
Kama hamko katika makundi ya mafisadi, wazembe, watumishi hewa na yanayofanana na hayo, basi nawaomba mchape kazi kwa nguvu zenu zote bila hofu serikali inayafanyia kazi mnayoyahitaji”. Alisema Zelote
Mkuu wa mkoa aliwaomba walimu kuiunga mkono serikali ya awamu ya tano katika juhudi zake za kuleta maendeleo hasa kwa wananchi wa kipato cha chini na kuwahakikishia kuwa kero za watumishi wote zitatatuliwa mapema iwezekanavyo kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu zilizopo.


Katika kupiga vita vya ukatili dhidi ya walimu vinavyofanyika katika baadhi ya maeneo hasa ya vijijini, mkuu wa mkoa alimuagiza kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa kushughulikia ipasavyo malalamiko ya walimu kufanyiwa ukatili popote ndani ya mkoa wa Rukwa.
Akisoma risala ya walimu mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Kamishna Mstaafu Zelote Stephen  Katibu wa chama cha walimu Manispaa ya Sumbawanga, Polycarp Mwanahanja alisema hatua zinazochukuliwa na serikali zinaungwa mkono na walimu mkoani hapa na kuwa wanaamini zoezi hilo linalenga kujenga uwezo kwa serikali kuboresha maslahi ya watumishi.
Aidha walimu hao wameipongeza serikali kwa kuanzisha tume ya utumishi wa walimu (TSC) ambayo wameomba iwe na majukumu yote ya mwajiri kwa lengo la kupunguza idadi ya waajiri wanaomuhudumia mwalimu na hivyo wameomba tume ipewe meno zaidi kuliko ilivyo hivi sasa kwa tume ya utumishi wa walimu nchini (TSD).
Kwa kutumia fursa hiyo waliwasilisha baadhi ya changamoto kwa mkuu wa mkoa wa Rukwa wanazokabiliana nazo walimu katika halmashauri, mkoa na taifa zima ambazo walidai ni kuwa na kipato duni kisichoendana na mfumuko wa bei nchini hali ambayo imepelekea baadhi ya walimu kuingia katika mikopo yenye riba kubwa inayoishia kuwadhalilisha walimu hao.
Wameleza suala la kuchelewa kuwapandisha madaraja walimu kuwa ni kikwazo kwa serikali kufikia malengo ya kulipa madeni ya walimu kwani mrundikano unakuwa mkubwa wakati wa kuwapandisha madaraja unapofanywa kwa kundi kubwa lililolimbikizwa mfano katika Manispaa ya Sumbawanga zaidi ya walimu 745 wanadai kupandishwa madaraja kwakuwa hawakupandisha madaraja mwaka 2015/16, 2016/17 hivyo wote wanalazimika kuingizwa katika bajeti ya 2016/17.
Walimu hao walimuomba mkuu wa mkoa kuwafikishia maombi yao serikali ya posho za mazingira magumu na usafiri kurejeshwa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma pamoja na kuanza mikakati ya kuondoa uhaba wa vyumba vya madarasa na nyumba za walimu ili mazingira ya uwajibikaji kwa mwalimu yawe rafiki.

Thursday, October 13, 2016

Mkoa wa Rukwa waishukuru Tigo kwa madawati.

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Halfan Haule aishukuru kampuni ya simu ya Tigo baada ya kupokea madawati 50 yenye thamani ya Shilingi Milioni 8.2/= katika hafla fupi iliyofanyika nje ya jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.


(Kutoka Kulia) Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Halfan Haule (shati la Kitenge), Jackson Kiswaga Mkurugenzi mtendaji wa Kanda - Tigo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Nixon Nzunda (Mwenye Miwani)
Alitoa shukrani hizo akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa pamoja na wananchi wa Mkoa wa Rukwa Dk. Haule alisema “Kwa msaada huu wa madawati 50 ambayo kampuni ya Tigo imetuletea itakuwa imepunguza kile kiwango cha upungufu, kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Rukwa tunaomba kutoa shurani kwa Kampuni ya Tigo.”

Picha ya pamoja Mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Halfan Haule na wafanyakazi wa Tigo. 

Dk. Haule aliongeza kuwa madawati hayo yamewasogeza mbele katika kumaliza tatizo la upungufu wa madawati katika Mkoa wa Rukwa.

“Mkoa wa Rukwa ambao ulikuwa na upungufu wa madawati 84,000 kwa shule za msingi na 26,000 kwa shule za sekondari ambapo mpaka sasa madawati 75,000 ya shule za msingi yameshatengenezwa na madawati karibu 25,000 yameshatengenezwa na kusababisha upungufu wa madawati 9,000 kwa shule za msingi na upungufu wa madawati 800 kwa shule za sekondari,” Dk. Haule alifafanua.
Picha ya pamoja, Mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Halfan Haule pamoja na wafanyakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga na Watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa. 

Nae Mkurugenzi mtendaji wa Tigo nyanda za juu Kusini Jackson Kiswaga alisema kuwa kwa kutoa madawati hayo wanaunga mkono moja kwa moja juhudi za serikali ya Tanzania na agizo la Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.

Ndugu Kiswaga alisema, “Katika kutekeleza sera ya elimu bure na kuhakikisha kuwa shule zinakuwa na madawati ya kutosha na kwamba tatizo la madawati linakwisha nchini kampuni ya Tigo imechangia madawati 5,745 kwa mikoa 18 na kufaidisha wanafunzi 17,100.”

Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Nixon Nzunda kwa niaba ya wafanyakazi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa aliweza kuishukuru Tigo kwa kuweza kuitikia wito wa Raisi Dk. John Pombe Magufuli kwa kusaidiana na serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunza kwa wanafunzi wa Mkoa wa Rukwa pamoja na nchi kwa jumla.
Picha ya pamoja Mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Halfan Haule na wafanyakazi wa kampuni ya simu ya Tigo  wanafunzi wa shule ya Msingi Chemchem.
“Kitendo ambacho kimefanywa na kampuni ya simu ya tigo leo hii ni kitendo ambacho kinafaa kuigwa na wadau wote wa maendeleo katika Mkoa wa Rukwa, na nitumie hadhara hii niwaobe wadau wote kuendelea kusaidia juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kuchangia madawati,” Ndugu, Nzunda alimalizia.

Kampuni ya Tigo ambayo ndio wadhamini waku wa tamasha la muziki la FIESTA kwa mwaka huu, wamekuwa wakitembelea mikoa mbalimbali kutoa madawati hayo.


Monday, October 10, 2016

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ahimiza ushirikiano kati ya Wajasiliamali, SIDO na Halmashauri

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa KAmishna Mstaafu Zelote Stephen aishauri SIDO kuboresha bidhaa za samaki na dagaa kutoka ziwa Tanganyika na ziwa Rukwa kwa lengo la kuzitangaza na kuvutia wawekezajikatika bidhaa hizo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aliyasema hayo alipohudhuria maonesho ya bidhaa za wajasiriamali wadogo na wa kati yaliyokuwa yameandaliwa na serikali ya Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na ofisi ya SIDO za mikoa ya Nyanda za Juu kusini.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen Alipotembelea banda la wahunzi
Na kwa kusaidia katika kutangaza soko la bidhaa hizo Kamishna Mstaafu Zelote Stephen aliwataka wajasiriamali hao kumpatia “sample” za bidhaa hizo ili aweze kuwaonesha wageni mbalimbali wanaotembelea ofisini kwake.

Mh. Zeloyte Stephen alizitaka halmashauri zishirikiane na SIDO na kuhakikisha wajasiriamali wanawezeshwa katika yanja zote ili kuzalisha ajira kwa vijana na kukuza viwanda vidogovidogo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen Alipotembelea banda la mtengeneza asali kwa kufuga nyuki wasiouma, dumu akiuza kwa shilingi 30,000/=.
“Viwanda vinaanza hatua kwa hatua na hatua ndo hii ambayo wajasiriamali wameionesha katika maonesho haya. Hivyo, juhudi za Wajasiriamali hawa ziungwe Mkono kwa kutumia bidhaa wanazozizalisha” Mh. Zelote alisema.

Katika maonesho hayo wajasiriamali kutoka katika mikoa ya nyanda za juu kusini pamoja na nchi za jirani za Kenya, Zambia na Malawi walishiriki kuonesha bidhaa zao mbali mbali ili kuweza kujitangaza na kufahamika na wananchi pamoja na serikali. Mbali na wajasiriamali hao mabanda mbalimbali ya Taasisi za Kiserikali na mabenki pia walishiriki.
Miongoni mwa washiriki kutoka Wilaya ya Kalambo.
Kwa niaba ya mgeni rasmi wa maonesho hayo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Amos Makala aliwasisitiza wajasiriamali nchini kuboresha bidhaa zao kwa lengo la kuendana na ushindani wa soko la kitaifa na kimataifa.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Songwe Kapteni Mstaafu Chiku Galawa alizitaka Halamshauri kushirikiana na wajasiriamali wadogo kwa kuwapa elimu ya kibiashara pamoja na kuwawezesha kimtaji, pia aliwasisitiza wanachi kutumia bidhaa za nyumbani, kuzithamini nakuzipenda na kuwa zina ubora Zaidi za zile za nje.

Nao wamiliki wa viwanda vidogo hawakusita utoa kilio chao kwa viongozi hao wakuu wa mikoa katika kuhakikisha wanasaidiwa kuepukana na changamoto mbalimbali zinazowakwamisha katika ndoto zao.

Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja kusikitishwa na upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kuwa midogo nakuongeza kuwa mikopo mingi inayopatikana ni ya masharti magumu, pampja na hayo malipo ya vibali kufanyika kwa Dola za kimarekani jambo ambalo linaongeza ghara za bidhaa zao kutokana na kuimarika kwa dola kila kukicha.

Kwa Niaba ya Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Amos Makalla nae alizitaka Halmashauri kuhakikisha zinasimamia na kuwa bidii katika kuzalisha  bidhaa kwa wingi na zenye ubora wa hali ya juu inaongezeka katika maeneo yao ili kujenga imani kuwa “Tanzania ya Viwanda inawezekana”"Njooni Kalambo Falls Kuwekeza" Kamishna Mstaafu Zelote Stephen.

Maporomoko   ya kalambo yapo katika Wilaya ya Kalambo Mkoa wa Rukwa, Ni maporomoko ya pili kwa urefu Africa baada ya Victoria Falls. Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen Zelote. anawaasa wawekezaji wote kuweza kupeleka nguvu zao katika Maporomoko hayo ili kuvutia wawekezaji.Tuesday, October 4, 2016

Katibu Tawala wa Mkoa atoa siku saba idara ya kilimo kuwa na mpango wa kuwawezesha wakulima.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa ametoa siku saba kwa idara ya kilimo kuandaa mpango unaotekelezeka wa kuwawezesha wakulima kulima chakula chenye tija na chenye kuwaondoa kwenye umasikini.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Nixon Nzunda.
Katibu Tawala aliyasema hayo walipofanya kikao maalum kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen cha kujua maendeleo na mipango ya kilimo kabla ya kuanza kwa mvua mwezi wa 11 mwaka huu.

Kabla ya Katibu tawala kuweza kuongea lolote Mkuu wa Idara ya Kilimo Hamza aliweza kutoa taarifa fupi iliyoelezea changamoto wanazopambana nazo pamoja na namna ya kuweza kukabilina nazo ili kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Katibu Tawala alisisitiza kuwa kwa muda mrefu kumekuwa na mipango ambayo ni mizuri lakini haitekelezwi inavyostahili kwa lengo la kuwafaidisha wananchi wanaotegemea kilimo ili kujiendesha maisha yao.

“Mipango ni mizuri sana lakini kama ingetekelezwa walau kwa asilimia 10 basi mkoa wetu ungekuwa mbali” Katibu Tawala alifafanua.

Katibu Tawala aliongeza kuwa maafisa ugani wengi wamekuwa hawafanyi kazi zao kwa ufanisi, hivyo aliagiza kila afisa ugani kuwa na mpango kazi utakaomwongoza kufanya kazi zake za kila siku ikiwa ni pamoja na kuwajua wazalishaji wakubwa na wadogo wa mazao mbalimbali na kuweza kuwa na ratiba ya kuwafuatilia.

“Tunafahamu kwamba serikali imepoteza pesa nyingi sana kuwawezesha mafia ugani lakini hawafanyi kazi zao walizopangiwa kwa usahihi, hivyo kila afisa ugani lazima awe na idadi maalum ya kuwafikia na kuwahudumia tena kwa muda maalum na ofisi ya Mkoa ifanye kazi ya kuthibitisha kwamba afisa ugani huyu anafanya hayo aliyopangiwa” Katibu tawala alisisitiza.

Mbali na kusisitiza hayo Katibu tawala pia aliwataka waweze kubainisha mazao ya kipaumbele ili mkulima ajue mazao yenye tija na yenye kumpa kipato kitakachomtoa kwenye umasikini, na kuwakumbusha kitengo cha ushirika kuweza kutafuta masoo kwa mazao hayo, ili wakulime wasipate tabu ya kuuza mazao yao.

“Ukifanya biashara bila ya kujua soko la bidhaa unayoiuza linapatikana wapi ni sawa na hakuna, maana yake kama mkulima hajui soko kilimo haiwezi kumfaidisha na kumtoa kwenye umasikini, Hivyo bwana ushirika una wajibu wa kuyatambua masoko na kuweza kuwaunganisha wakulima na masoko hayo.” Katibu tawala alimalizia.

Katika kulikazia suala hilo na kuliunga mkono Mkuu wa Mkoa aliongeza, “katika awamu hii ya tano wananchi wanamatumaini makubwa na serikali yao na kila ninapokwenda wananchi wanataka kusaidiwa katika kilimo na wataalamu tunao mpaka ngazi ya kata, na wanafahamu kinachostawi na kisichostawi, hivyo nataka waanchi wafaidike na wataalamu wa Halmashauri na wa ofisi ya Mkoa.”

Mkuu wa Mkoa alisisitiza uzalendo na umoja katika kuwawezesha wananchi tangu kuandaa mashamba, kuotesha, kukuza, kupalilia, pembejeo, kuvuna kuhifadhi, kuongeza thamani, kufanya biashara, na kutafuta masoko.


Pia mkuu wa Mkoa alisisitiza wataalamu wa kilimo kuwa na uhusiano wa karibu sana na watu wa hali ya hewa, na kufafanua kuwa mtaalamu pekee ndie anaeweza kutambua mbegu feki na kuweza kuwafahamisha wakulima. 

Mkuu wa Mkoa asikiliza vilio vya wafungwa kuondoa msongamano kwenye magereza.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kamishna Mstaafu Zelote Stephen ametembelea magereza mawili ya mkoa huo ili kusikiliza vilio vya wafungwa na kutafuta utaratibu wa kuweza kuwasaidia na kuondoa msongamano katika magereza hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen akielekezwa na maafisa wa magereza mifugo inayomilikiwa na jeshi hilo katika gereza la Mollo.
Mkuu wa Mkoa aliyeambatana na wawakilishi wawili wa Mahakama kuu pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kabla ya kuongea na wafungwa na mahabusu aliweza kuangalia miundo mbinu ya magereza hayo ikiwemo sehemu za kulalia, kupikia, vyoo wanavyotumiapamoja na huduma ya maji na umeme ili kujua ubora na uimara wa miundombinu hiyo.

Mkuu wa Mkoa ili kujiridhisha na huduma ya chakula katika gereza hilo aliomba bakuli la ugali pamoja na maharage na kuanza kula mbele ya wafungwa hao, jambo ambalo liliwashangaza wafungwa wengi na kushindwa kuamini kumuona Mkuu wa Mkoa ambaye ni mwakilishi wa Mh. Rais Magufuli katika Mkoa wa Rukwa akila chakula hicho.

Pamoja nae waliokula chakula hicho walikuwa ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Bw. Nixon Nzunda, Mtendaji mkuu wa watumishi wa mahakama Bw. Emanuela Munda pamoja na Katibu wa Mkuu wa Mkoa Frank Mateni.

Mkuu wa Mkoa aliridhishwa na Chakula hicho baada ya kuona maharage sit u yana chumvi na maji lakini pia yaliweza kuongezewa viungo na mafuta, jambo ambalo alishindwa kujizuia kuuliza kama chakula hicho kilikuwa imeandaliwa siku hiyo kwakuwa walijuwa kuwa mkuu wa mkoa huyo atafanya ziara.

“Chakula mbona kitamu sana, hiki kimeandaliwa hivi kwakuwa mna taarifa kwamba leo nafanya ziara katika magereza ama ndio kawaida ya kila siku?” Mkuu wa Mkoa aliuliza.
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen akielekezwa na maafisa wa magereza maeneo ya mashamba yanayomilikiwa na jeshi hilo katika gereza la Mollo.

Mmoja wa wafungwa Isaya Mwambe ambae yupo katika gereza hilo kwa muda wa miaka 16, alitoa ushuhuda kuwa chakula hicho ndicho wanachokula kila siku na kumtoa hofu mkuu wa mkoa juu ya ubora wa chakula hicho.

Katika kuliangalia suala la Afya Mkuu wa Mkoa alipeleleza utoaji wa huduma kwa wale wanaopatwa na magonjwa na kujibiwa kuwa mara kwa mara wafungwa pamoja na mahabusu hao hufanyiwa uchunguzi wa kiafya na zahanati ya magereza na hali ikiwa mbaya kwa mgonjwa basi hupelekwa hospitali ya Mkoa kwa uchunguzi Zaidi.
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen  kulia, katibu tawala. Nixon Nzunda kati kati na Emanuel Munda Mtendaji Mkuu wa watumishi wa mahakama wakila chakula kilichoandaliwa kwa wafungwa.
Kabla ya kutoa nafasi ya kusikiliza kilio cha mmoja mmoja Mkuu wa Mkoa alisomewa risala iliyobainisha malalmiko pamoja na changamoto wanazokumbana nazo katika kuruka viunzi ili kuweza kufikia haki zao.

Mingoni mwa changamoto walizoziwasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa kupitia risala hiyo iliyosomwa na Oswald Usambo, wafungwa hao walilalamikia mahakama kuweka masharti magumu kwaajili ya kupatiwa dhamana, kucheleweshwa kupelekwa mahakamani pamoja na kuchelwa kwa upelelezi.

Lakini wafungwa hao hawakusita kumshukuru na kumpongeza Mkuu wa Mkoa kwa Kutenga muda wake na kuweza kufika katika magereza hayo ili kuweza kusikiliza vilio vyao. “Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tunatoa shukrani zetu za dhati kabisa kwa kuweza kufika kwetu na kusikiliza kilio chetu, ni Imani yetu kuwa ujio wako ni kama Musa kwa wana wa Izraeli na kutokana na historia yako tunaamini utatusaidia.”

Baada ya kusikiliza risala hiyo Mkuu wa Mkoa alitoa nafasi kwa Wafungwa 10 ili kuelezea kero na manung’uniko yao ambayo risala hiyo haikuyagusia, nafasi ambazo wafungwa hao walizitumia vilivyo a kuweza kutoa machozi yao.

Mongoni mwa Wafungwa waliopata bahati hiyo ni Edes Kamanda ambae alifurahia ujio wa Mkuu wa Mkoa katika gereza na alielezea ujio huo ni alama ya kutatuliwa matatizo yao, lakini kilio chake kilikuwa ni kuachiwa na kukamatwa tena hapohapo mahakamani na wenzie wanane jambo ambalo hawakulielewa mpaka anapata nafasi ya kuongea na Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen akielekezwa na maafisa wa magereza maeneo ya mashamba yanayomilikiwa na jeshi hilo katika gereza la Mollo.
Mfungwa Mwingine aliyekaa katika gereza hilo kwa miaka sita Adam Abdallah alitoa ushauri kwa serikali ili kuweza kuondoa msongamano hawana budi kutoa adhabu ambazo zitamalizikia vituoni kama vil kwa walevi kuchapwa bakora na kuhoji kuwa kwa wale wanaume waliowatelekeza wake zao, kuwepo kwenye mahabusu hakusaidii bali warudishwe kwa wake zao.

Katika kuhakikisha kila sauti ya Mfungwa inasikika Mkuu wa Mkoa alimuamuru kamanda wa gereza hilo awape karatasi kila mfungwa ili aweze kuandika yale aliyoyaona hakufanyiwa haki katika kesi zao zinazoendelea.

“Nataka kuwahakikishia kwamba hayo mliyoyaelezea kwenye risala, na wale waliopata nafasi ya kujieleza, na yale ambayo hatujayasikia, yote tunayafahamu, tumekuja kuwasikiliza shida na kila mtu aeleze kero yake, Lakini mueleze ukweli, uwongo hautamfikisha mtu popote.” Mkuu wa Mkoa alifafanua.
Pia Mkuu wa Mkoa aliendeleza kuwakumbusha kuwa Tanzania ni nchi nchi inayoendeshwa kwa misingi ya sheria na haitakiwi suala hili liwekwe mchagoni, na hapendi kuona mrundikano katika magereza hayo.

“Hamkuniita, nimeamua kuja mwenyewe kwakuwa natambua wajibu wangu na pia nafuata maagizo ya Mh. Rais John Pombe Magufuli, na Nimekuja na timu yangu ambayo sina wasiwasi nayo, hivyo kuweni watulivu na wavumilivu” Mkuu wa Mkoa alisisitiza.

Lakini katika kuhakikisha mazingira yanatunzwa Mkuu wa Mkoa alishauri gereza hilo kutafuta nishati mbadala kwaajili ya kupikia kama vile kinyesi cha ng’ombe kuliko kutumia kuni ambazo zinapatikana kwa kukata miti.

Baada ya kuona tofauti ya umri katika gereza hilo, Mkuu wa Mkoa aliamua kuwainua vijana 21 wa chini ya umri wa miaka 18 ili kujua makosa yao na kuweza kuanza kuyafuatilia.

Katika safari yake hiyo ya gereza la Mahabusu la Sumbawanga Mkuu wa Mkoa hakuwasahau wanawake waliokuwa wamefungwa katika gereza hilo, ambapo aliweza kupata nafasi ya kuona sehemu wanazolala na miundo mbinu mingine na hatimae kutumia muda wa dakika 55 kusikiliza kero na changamoto za wafungwa hao.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen akielekezwa na maafisa wa magereza mifugo inayomilikiwa na jeshi hilo katika gereza la Mollo.
Pia Mkuu wa Mkoa alitoa nafasi 14 kwa wafungwa hao ambapo mmoja wa wafungwa hao Magreth Musa aliishauri serikali kuweza kuwapa vifungo vya nje wale wenye vifungo vya chini ya miezi sita ili kuepusha msongamano katika gereza hilo.

Mkuu wa Mkoa aliwatoa wasiwasi na kuwasihi kuwa wasione kuwa wametengwa isipokuwa serikali yao inawakumbuka na kuyashughulikia matatizo yao.

“Msijione kuwa sio watanzania, kumbukeni kuwa tunawajali na kero zenu tutazifuatilia.” Mkuu wa Mkoa alimalizia.

Gereza La Kilimo la Mollo

Mkuu wa Mkoa aliweza kufika katika gereza la kilimo la Mollo na kuweza kuangalia miundombinu kama sehemu za kulalia na jiko la kupikia lakini pia aliangalia vyanzo vya maji.

Kabla ya kuweza kutoa nafasi kwa wafungwa kueleza kero zao, Mkuu wa mkoa aliweza kusomewa risala iliyotawaliwa na kukwama wa rufaa pamoja, kuosekana kwa umeme na  kutumia umeme wa jua na kushindwa kuelewa utendaji kazi wa bodi ya “parole”.

Baada ya risala msomaji Datus Uleti aliweza kumshukuru mkuu wa mkoa kwa ziara yake na kumuomba iwe ni kawaida yake kufanya hivyo, lakini pia hakusita kumuombea mkuu wa Mkoa afya njema.

“Tunashuru kwa ujio wako, hatuna cha kukulipa ila tunakuombea afya njema katika utendaji wako wa azi” Msomaji risala alimaliza.

Mkuu wa Mkoa alitoa nafasi tano kwa wafungwa hao ambapo miongoni mwa waliotoa kilio ni Michael Mika aliyemuomba Mkuu wa Mkoa kuwasaidia kupata madawa kwaaijili ya wagonjwa mbalimbali.

Mkuu wa Mkoa pia alitoa nafasi kwa wafungwa hawa kupewa karatasi na kila mmoja kuweza kuandika kero yake na kuwasisitiza kuwa yote watakayoandika yawe ya kweli na kuwa uwongo hauna faida kwa yeyote.

“Msifikie kuwa tunafurahia mkijaa, tunapenda magereza yawe matupu lakini haiepukiki maana kuna wale wa sikio la kufa halisikii dawa lakini pia hatupendi kuona mpo kizani, mpo hapa ili kuona mwanga na sio kuongezewa kiza.”

Mkuu wa Mkoa katika kuyaweka mambo sawa alitoa nafasi kwa timu aliyoongozana nayo kuweza kuzungumza yale yenye majibu ya hapo hapo, ambapo Mkuu wa gereza Jairo Mwamgunda alisema kuwa wengi wa wafungwa hao hawafikii vigezo vya kupewa parole n ahata wale wenye sifa, ndugu wa wafungwa hao hawako tayari kuwapokea ndugu zao napia wale waliofanyiwa makosa hawataki kutoa msamaha.