Wednesday, October 11, 2017

RC Rukwa aitahadharisha TARURA kutorudia makosa ya Halmashauri.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameutahadharisha Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini kutorudia makosa yaliyokuwa yanafanywa na Halmashauri kabla ya wakala huo kuanzishwa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen (kushoto)  wakati akifungua kikao cha bodi ya barabara, 
(katikati) Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule pamoja na Katibu tawala wa Mkoa waRukwa Bernard Makali. 

Amesema kuwa matumizi mabaya ya fedha za barabara pamoja na barabara hizo kujengwa chini ya viwango na kuisababishia serikali hasara ya kufanya matengenezo ya mara kwa mara ni miongoni mwa changamoto ambazo serikali imeamua kuzitafutia ufumbuzi kwa kuanzisha Wakala huo.

“Ukiitwa Injinia na kazi yako iendane na cheo chako, sio unafanya kazi mpaka hata sisi ambao hatuna ujuzi huo tukiona tunasema hii ipo chini ya kiwango, na hapo mwanzo serikali ilikuwa inaelekeza pesa nyingi sana kwenye barabara lakini kiuhalisia barabara hazipo na muda mwingine mvua zinataka kuanza ndio utaona mkandarasi anaingia barabarani kwenda kutengeneza barabara,” Mh. Zelote alifafanua.

Ameyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha kwanza cha bodi ya barabara kwa mwaka wa fedha 2017/2018.

Amesisitiza kuwa kwa kuimarisha sekta ya barabara vijijini ndio miongoni mwa hatua za kuuendea uchumi wa Viwanda ambao ndio kipaumbele cha serikali ya wamu ya tano inayoongozwa na Mh. Dk. John Pombe Magufuli.


Hivyo ametoa wito kwa wakala huo kuhakikisha wanafanya kazi yao kwa uadilifu na kuhakikisha mabadiliko yanaonekana na kuwaasa kuacha kufanya kazi kwa mazoea na hatimae kurudisha nyuma azma ya serikali ya awamu ya tano. 

Rukwa wajipanga kuzalisha malighafi nyingi za viwanda kuvutia wawekezaji.

Katika kujiandaa na msimu wa kilimo Uongozi wa Mkoa wa Rukwa chini ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen wamezuru Taasisi ya Utafiti Kilimo (ARI) pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) nyanda za juu kusini - Uyole, Mkoani Mbeya.

Ziara hiyo iliyobeba Katibu Tawala wa Mkoa Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Rukwa na makatibu tawala wao walioambatana na wakulima, maafisa kilimo na mifugo wa wilaya pamoja na wenyeviti wa Halmashauri nne za Mkoa huo, na wataalamu wa kilimo na mifugo kutoka katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

Katika ziara hiyo mada mbalimbali zilitolewa kuhusu aina ya mazao yanayoweza kustawi katika Mkoa wa Rukwa, wadudu wanaoweza kushambulia mazao hayo na namna ya kuwadhibiti ili kuongeza uzalishaji, utafiti wa udongo pamoja na kilimo cha nyasi kwaajili ya mifugo na ufugaji wa kisasa.

Mh. Zelote alisema kuwa kwa miongo kadhaa Mkoa wa Rukwa umekuwa katika mikoa inayoongoza kwa kilimo lakini haikuwahi kuwa namba moja hivyo ziara hiyo ndio mwanzo wa kuiendea Rukwa mpya yenye kuzalisha mazao yenye kuleta tija kwa wakulima, mkoa na taifa kwa ujumla.

 “Lengo la kufunga safari kutoka Rukwa hadi hapa ni kwa lengo la kuleta mabadiliko ya Kilimo na mifugo, Rukwa kupitia kilimo ndio litakuwa ni chimbuko la viwanda, kama wataalamu walivyosema kuwa kilimo ndio chimbuko la viwanda,tunahitaji kuboresha kilimo katika Mkoa wa Rukwa ili tuwe na viwanda vya uhakika” Amesema.

Amesema kuwa ili kuwakomboa wananchi wa hali ya chini ambalo ndio lengo la Rais Dk. John Pombe Magufuli Hakuna budi kuimarisha kilimo na hatimae kuinuka kutoka katika uchumi wa viwanda vidogo kwenda viwanda vya kati na kutoka katika uchumi mdogo kwenda uchumi wa kati.

Kwa upande wake mratibu wa ziara hiyo Benjamin Kiwozele alimshukuru Mh. Zelote kwa kuona umuhimu wa kuzitumia taasisi hizo kwa malengo yaliyowekwa na serikali.


Kabla ya Kumkaribisha Mh. Zelote, Mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa Kilimo Tulole Bucheyeki alisema kuwa wataendelea kutoa ushirikiano kwa uongozi wa Mkoa wa Rukwa kwa heshima kubwa walioionyesha kwa kufika kwenye Taasisi hiyo na kuweza kukutana na wataalamu wao kwa nia ya kuboresha uwekezaji na vipato vya wananchi.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kmaishna Mstaafu Zelote Stephen (aliyevaa miwani-kaundasuti) akiwa katika picha ya pamoja na watafiti mbalimbali katika Taaisi ya Utafiti wa Kilimo – uyole, Mbeya pamoja na baadhi ya wataalamu wa Kilimo na Mifugo kutoka Rukwa. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kmaishna Mstaafu Zelote Stephen (aliyevaa miwani-kaundasuti) akipewa maelezo ya kilimo cha maharage na mtafiti hifadhi ya mimea Reinfred Maganga (shati nyeupe) katika moja ya bustani ya mifano yaliyopo kwenye viwanja vya taasisi hiyo. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kmaishna Mstaafu Zelote Stephen (aliyevaa miwani-kaundasuti) pamoja na uongozi wa Mkoa wa Rukwa wakipewa maelezo ya kilimo cha maparachichi na mtafiti hifadhi ya mimea Reinfred Maganga (shati nyeupe- kushoto) katika moja ya vitalu vilivyopo kwenye viwanja vya taasisi hiyo. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kmaishna Mstaafu Zelote Stephen (wa tatu kutoka kulia) akisikiliza uwasilishaji kutoka kwa mtafiti rasilimali za mifugo Dk. Pius Mwambene (wa kwanza kulia) kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI)

Dk. Denis Mwakilembe (kulia) akielezea namna mabua ya zao la mahindi kuwa nia chakula bora cha mifugo mbele ya ujumbe mzima wa Mkoa wa Rukwa ulioongozwa na Mh. Zelote Stephen.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kmaishna Mstaafu Zelote Stephen akiangalia baadhi ya mifugo iliyopo katika viwanja vya Taasisi ya Utafiti wa mifugo (TALIRI)-Uyole. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kmaishna Mstaafu Zelote Stephen akiwa ameshika mbegu za nyasi wanazotakiwa kupatiwa ng’ombe zilizofanyiwa utafiti na TALIRI ili kuepukana na kuhama hama kwa wafugaji, Wa kwanza kushoto ni Kaimu mkurugenzi wa TALIRI Suleiman Nasibu Masola.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kmaishna Mstaafu Zelote Stephen akipewa maelezo ya namna maabara ya udongo inavyofanya kazi na mtafiti wa udongo Daudi Mujuni katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo-Uyole

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kmaishna Mstaafu Zelote Stephen (wa pili Kulia) akioneshwa madawa mbalimbali yanayotumika kuzuia uharibifu wa mazao shambani. 

Viongozi wa Mkoa wa Rukwa wakiendelea kupata somo kutoka kwa watafiti mbalimbali wa Kilimo katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nyanda za juu kusini -Uyole.
Baadhi ya Wataalamu na wakulima wakiendelea kusikiliza kwa makini mawasilisho ya tafiti mbali mbali za kilimo yaliyofanya na watafiti katika Taasisi ya Utafiti wa kilimo nyanda za juu kusini – uyole. 

(Kutoka kulia) Katibu tawala wa Mkoa wa Rukwa Benard Makali, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen. Tuesday, October 10, 2017

RC Rukwa aishauri benki ya NMB kufungua tawi bonde la ziwa Rukwa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameishauri benki ya NMB kufungua tawi katika bonde la Ziwa Rukwa ili kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi ambao shughuli zao kubwa za kiuchumi ni kilimo cha mahindi, mpunga pamoja na uvuvi.

Amesema kuwa kwa kufanya hivyo kutaepusha matukio ya uvamizi na mauaji yanayofanywa na baadhi ya watu wanaowavizia wakulima na wafanyabiashara wanaoweka fedha majumbani mara tu baada ya mauzo ya mazao yao.

“Mimi nashauri Benki ya NMB muwe na Tawi huku, si lazima kuwa na jengo, hata ile Mobile Banking ambayo mwananchi anaweza kupata huduma zote za kuweka na kutoa fedha katika gari hiyo, ili fedha zao hawa ziwe katika mikono salama,” Mh. Zelote Alisema.

Ametoa ushauri huo katika ufunguzi wa siku ya huduma kwa wateja iliyofanywa na benki ya NMB kanda ya nyanda za juu katika Kijiji cha Mfinga, kata ya Mfinga, Wilaya ya Sumbawanga, kabla ya kukabidhi vifaa vya shule pamoja na hospitali vyenye thamani ya Shilingi milioni 20.

Sambamba na hilo Mh.Zelote amewahamasisha wakulima pamoja na wafanyabiashara wa Kata ya Mfinga kufungua akaunti benki na pia kujiunga katika vikundi ili kuwa na urahisi wa kupata mikopo  na kuweza kuwainua kiuchumi.

“Mbali na kuhifadhi fedha pia benki inatoa mikopo kwaajili ya kujiendeleza na hatimae kuwainua wakulima waweze kuongeza thamani ya mazao yao na kupata soko pana hasa katika awamu hii inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli inayohamasisha uchumi wa viwanda kwa taifa,” Alisema.

Aidha aliwataka viongozi wa Kijiji na wanufaika wa vifaa hivyo kuvitumia vifaa hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa na ikiwemo kuwahudumia wananchi bila ya bugudha na kuonya kuwa wananchi wasiogope kuwashitaki watumishi wanaowahudumia kwa viburi.

Awali akisoma taarifa fupi ya Benki ya NMB Mkurugenzi wa Huduma kwa wateja makao makuu ya benki hiyo Richard Makungwa alisema kuwa Benki ya NMB hutenga asilimia moja ya mapato kwa mwaka ili kuirudishia jamii na kuweza kuisaidia katika mambo mbalimbali ikiwemo elimu na afya.

“Kwa kuunga mkono juhudi za Rais wetu tumeamua kama Benki kutoa kompyuta 7, vitanda 8 vya kulalia, vitanda 4 vya kujifungulia, magodoro 8 pamoja na mabati 204 vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 20 vilivyotolewa na benki hiyo kama marejesho ya faida kwa wateja watu,” Alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen (Kaunda Suti ya Ugoro) akikabidhi Kompyuta kwa Afisa Elimu Manispa ya Sumbawanga Silvestor Mwenekitete katika kuadhimisha siku ya huduma kwa wateja katika Kijiji cha Mfinga, Wilayani Sumbawanga. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen (Kaunda Suti ya Ugoro) akikabidhi Kompyuta kwa Afisa Elimu Manispa ya Sumbawanga Silvestor Mwenekitete katika kuadhimisha siku ya huduma kwa wateja katika Kijiji cha Mfinga, Wilayani Sumbawanga. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen (Kaunda Suti ya Ugoro) akikabidhi vitanda kwa mganga mfawidhi zahanati ya Mfinga Ephraim Matekele (shati ya draft) katika kuadhimisha siku ya huduma kwa wateja katika Kijiji cha Mfinga, Wilayani Sumbawanga. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen (Kaunda Suti ya Ugoro) akikabidhi vitanda kwa mganga mfawidhi zahanati ya Mfinga Ephraim Matekele (shati ya draft) katika kuadhimisha siku ya huduma kwa wateja katika Kijiji cha Mfinga, Wilayani Sumbawanga. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen (Kaunda Suti ya Ugoro) akiendeleza ujenzi kwa kuweka tofali katika jengo la shule ya msingi Mfinga waliopewa mabati 204 na Benki ya NMB.

Picha ya pamoja 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen (Kaunda Suti ya Ugoro) katika picha ya pamoja na viongozi wa NMB pamoja na Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mfinga, Wilayani Sumbawanga. 


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicho Godfrey Kalungwizi aliahidi kuvisimamia vifaa hivyo na kuendelea kuwahamasisha wananchi kuchangia katika shughuli za kimaendeleo. 

Uongozi wa Mkoa wa Rukwa waungana kuwafariji wafiwa ajali iliyoua 15 na kujeruhi 9

Uongozi wa Mkoa wa Rukwa chini ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kmaishna Mstaafu Zelote Stephen umeungana na ndugu wa majeruhi 9 na wafiwa wa vifo vya watu 15 vilivyotokea katika ajali ya lori aina ya fuso eneo la Ntembwa, Wilayani Nkasi.
Gari iliyopata ajali na kusababisha vifo vya watu 15 na kujeruhi 9
Gari iliyopata ajali na kusababisha vifo vya watu 15 na kujeruhi 9

Gari iliyopata ajali na kusababisha vifo vya watu 15 na kujeruhi 9

Gari iliyopata ajali na kusababisha vifo vya watu 15 na kujeruhi 9


Katika kuhakikihsa tukio hilo halijirudii Mh. Zelote amepiga marufuku ukiukwaji wa sheria ya kupandisha abiria katika magari ya mizigo na kuonya kuwa yeyote atajayefanya hivyo achukuliwe hatua haraka iwezekanavyo.

“Nimekataza binadamu kugeuzwa kuwa ni mifuko ya misumari, ni bora tubakie na wananchi wetu salama, watu wasipande kwenye malori, nimefikiria ni vyema tutumie zile chai maharage kuliko kupanda kwenye malori,” Alisisitiza.

Mh. Zelote alifika katika eneo la tukio mara tu baada ya kupokea habari hiyo ili kuweza kusaidia na kuhakikisha maiti na majeruhi hao wanapatiwa huduma stahiki na kufanikisha zoezi la uokoaji.

Ajali hiyo ilitokea baada ya lori aina ya fuso yenye namba za usajili T 425 BFF kuacha njia na kupinduka ilitokana na mwendo kasi wa dereva uliochangiwa na ugeni wa barabara hiyo.

Lori hiyo mali ya Bakari Ali Kessy iliyokuwa imetokea Kijiji cha Mvimwa kuelekea Kijiji cha Wampembe ilikuwa imepakiwa shehena ya viroba vya mahindi na watu iliacha njia, kupinduka na kusababisha vifo vya watu 15 kati yao wanawake 10 na wanaume 05.

Waliofariki katika ajali hiyo ni

1.   Domona Tenganamba, 41yrs, mfipa mkulima.
2.     Emmanuel Rashid 84yrs, mfipa mkulima, mkazi wa ntemba
3.     Restuta Sunga , 35yrs, mfipa mkazi wa ntemba
4.     Salula Revana 64yrs, mfipa mkazi wa mtapenda isale
5.     Ferisia Tenganamba , miaka 1 – 6/12
6.     Prisca Madeni, 45yrs, mfipa, mkulima, mkazi wa china
7.     Richard Chikwangara, 24yrs, mfipa, mwalimu mkazi wa kalambanzite
8.     Yusta Somambuto, 36yrs, mfipa, mkulima mkazi wa kizumbi
9.     Gilesi Ramadhan, 24yrs, mfipa, mkulima mkazi wa sumbawanga
10. Odetha Madirisha 46yrs, mfipa mkulima wa kizumbi
11. Megi Nalunguli, 52yrs, mfipa, mkulima mkazi wa wampembe
12. Abuu Amani @ mandevu, 37yrs, muha, biashara, mkazi wa liapinda
13. Nyandindi Batrahamu, 35yrs, mfipa, mkulima, mkazi wa sumbawanga
14. Magdalena Mbalamwezi, 50yrs, mfipa, mkulima mkazi wa ntuchi
15. Mtoto mchanga wa wiki mbili, mwanaume ambaye hajapewa jina
Majeruhi wa ajali hiyo ni:-
1.     Dismas Clement, 26yrs, mfipa, mkulima mkazi wa mwinza
2.     Sema Savery 25yrs, mfipa, mkulima mkazi wa wampembe
3.     Ally Haruna, 33yrs, mfipa, mkazi wa namanyere
4.     Yusta Mfundimwa, 50yrs, mkulima mkazi wa izinga
5.     Tenesfory Oscar, 36yrs, mfipa mkazi wa wampembe
6.     Amos Kitambale, 25yrs, mfipa, mkazi wa wampembe
7.     Neema Mwanandenje, 21yrs, mfipa, mkazi wa mlambo
8.     Joseph Sungula, 28yrs, mfipa, mkulima.
9.     Majeruhi mmoja mwanamke ambaye hajafahamika kwa jina yuko icu

Baada ya kusababisha ajali hiyo dereva alitoroka lakini juduhudi za kumtafuta mtuhumiwa zinaendelea kufanyika.

Saturday, September 30, 2017

RC Rukwa awatahadharisha wananchi kujiandaa na msimu wa mvua

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewatahadharisha wananchi wa Mkoa huo kujihadhari na mvua  zilizoanza na upepo ulioezua baadhi ya paa za nyumba na vituo vya kutolea huduma katika baadhi ya maeneo ya mkoa.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen aliposhiriki kwenye usafi wa mwisho wa mwezi 30.9.2017

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen aliposhiriki kwenye usafi wa mwisho wa mwezi 30.9.2017

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen aliposhiriki kwenye usafi wa mwisho wa mwezi 30.9.2017

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen aliposhiriki kwenye usafi wa mwisho wa mwezi 30.9.2017

Amesema kuwa sasa ni wakati wa wazazi kuwachunga watoto katika msimu huu wa mvua na kuongeza kuwa wenye nyumba hawanabudi kuimarisha majengo yao mapema ili kuepukana na hasara ambayo wangeweza kuipata baada ya madhara kutokea.

“Ni wakati muafaka hivi sasa kila mtu kuchukua tahadhari kuangalia watoto, kukagua majengo yetu kuona kuwa yapo imara na pale ambapo ninatokea basi wajue sehemu salama ya kukimbilia ili kuokoa Maisha,”alifafanua

Ameyasema hayo aliposhiriki kufanya usafi nyumbani kwake eneo la Mkoani, mjini Sumbawanga. Ambapo alisema kuwa suala la usafi linaanzia nyumbani kwa mtu na kuwa wananchi wafanye usafi kwa faida yao wenyewe na kuendelea kuwasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuendelea kusimamia usafi kuanzia ngazi ya Kijiji au mtaa ili kutekeleza agizo lake la kufanya usafi kuanzia katika ngazi hizo.

“Nimewaagiza wakurugenzi na wataalamu wake wakague usafi kwasababu suala la usafi ni faida kwa kila mtu, siyo faida ya rais wa la mkuu wa mkoa pekee, kwasababu tukiingiliwa na magonjwa halitakuwa la rais peke yake,” Alisema

Pamoja na hayo Mh. Zelote aliwaonya wenye tabia ya kuchoma misitu hasa katika kipindi hiki cha kukaribia msimu wa kilimo, hivyo amewasisitiza viongozi kuanzia ngazi ya Kijiji kushirikiana kuhakikisha kuwa jambo hilo halijitokezi.


“Katika kipindi hiki uchomaji hovyo wa mioto unaonekana kushika kasi, ni juu ya serikali ya Kijiji ama kata kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba mioto haiwashwi ovyo ovyo na atakayefanya hivyo achukuliwe hatua za kisheriakwani mambo haya huaribu mazingira na pia usipodhibitiwa hule madhara,” Alisisitiza. 

Rc Rukwa apongeza juhudi za wanafunzi wa Mlimani kufanya utafiti wa uhun...

Wahasibu waaswa kufanya kazi kwa uadilifu

Katibu tawala msaidizi serikali za mitaaa wa Mkoa wa Rukwa Albinus Mgonya amewaasa watumishi wapya wa kada wa uhasibu katika Halmashauri za Mkoa wa Rukwa kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia sheria, taratibu na miongozo inayotolewa ili kuwaepusha kufanya kazi kwa mazoea.
Katibu tawala msaidizi serikali za mitaaa wa Mkoa wa Rukwa Albinus Mgonya 

Ameyasisitiza hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya uhasibu katika ngazi ya vituo vya kutolea huduma (FFARS) akimuwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa yaliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
baadhi ya washiriki wa mafunzo

baadhi ya washiriki wa mafunzo

baadhi ya washiriki wa mafunzo

“Ni matumaini yangu kuwa baada ya mafunzo haya mtakuwa mmejenga uelewa wa kutekeleza majukumu yenu kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali inayotolewa na mamlaka mbalimbali,” Alisema.

Aidha mafunzo hayo yamelenga kuwaboreshea ujuzi na stadi za kazi ikiwemo dhana ya kwenda na mahitaji ya wakati kutokana na mabadiliko ya Sayansi na Technolojia.

Mafunzo hayo ambayo yaliwashirikisha waajiriwa wapya wahasibu wasaidizi katika halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Sumbawanga vijijini, Nkasi na Kalambo, walioambatana na maafisa utumishi pamoja na maafisa takwimu wa Halmashauri hizo.


Pamoja na mafunzo hayo watumishi hao wapya walipata fursa ya kueleimishwa kuhusu mifuko mbalimbali ya jamii ikiwemo, PSPF, LAPF, NSSF, na mfuko wa bima ya afya wa Taifa (NHIF) ili kuwapa nafasi watumishi hao wapya kuamua kwa hiari bila ya kulazimishwa mfuko ambao watapenda kujiunga. 

"Kupima maleria ni bure, TB Bure" Mh. Ummy Mwalimu akiwa Kirando

Tuesday, September 19, 2017

RC Rukwa atoa siku 7 kupatiwa orodha ya boti na mitumbwi mwambao wa ziwa Tanganyika.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kamishna Mstaafu Zelote Stephen ametoa siku saba kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Kalambo pamoja na Mamlaka ya usimamizi wa usafiri wa nchi kavu na majini (SUMATRA) kumpatia orodha kamili ya vyombo vyote vya majini vinavyofanya shughuli zake katika mwambao wa ziwa Tanganyika katika Wilaya za Nkasi na Kalmbo za Mkoa wa Rukwa.
Miongoni mwa mitumbwi iliyokuwa imezagaa katika mwambao wa ziwa Tanganhyika Kijiji cha Wampembe ambayo mingi haikuwa na usajili na kuipotezea serikali mapato katika sekta ya uvuvi.

Ametoa agizo hilo alipotembelea mwambao wa Ziwa Tanganyika katika Kijiji cha Wampembe, Kata ya Wampembe Wilaya ya Nkasi na kubaini mitumbwi kadhaa iliyokuwa ikizagaa kwenye mwambao huo ikiwa haijafanyiwa usajili na kusababisha upotevu wa mapato ya serikali kupitia sekta hiyo ya uvuvi.

“Halmashauri zimekuwa zikilalamika hazina mapato ya kutosha wakati naona pesa zikielea tu hapa na Hakuna chochote kinachoendelea, sasa natoa siku saba kwa Halmashauri na SUMATRA nipate orodha kamili ya vyombo vyote vya usafiri wa majini, usajili wao na leseni zao zinazowaruhusu kufanya shughuli za uvuvi katika mwambao huo.” Amesema.
Mmoja wa maafisa wa Sumatra (mwenye overoli la bluu) akitoa ufafanuzi mbele ya Mh. Zelote (mwenye kaunda suti0 pamoja na maafisa mbalimbali walioambatana katika ziara hiyo kwenye kijiji cha Wampembe, Wilayani Nkasi.

Mkuu wa mkoa wa Rukwa kamishna Mstaafu zelote Stephen (kushoto) akimuonesha Afisa Uvuvi wa Kata Godfrey kashengebi (kulia) nyavu zilizobainika kutokidhi vipimo vilivyokubalika na serikali katika shughuli za uvuvi na kuagiza kukamatwa kwa kokoro hizo zilizokuwa zikiendela kutumiaka bila ya kukaguliwa na afisa huyo.

vijana wakiwa wamebeba kokoro zilizoagizwa kukamatwa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa na kufikishwa ofisi ya kata. 

Pamoja na hayo agizo hilo pia limekuja baada ya wiki moja iliyopita boti ambayo mmiliki wake hakujulikani kuzama ziwa Tanganyika ikitokea katika Kijiji cha Kalila, Kata ya kabwe, tarafa ya Kirando, Wilayani Nkasi  kuelekea Kijiji cha Kyala Mkoani Kigoma na kupelekea kifo cha mtoto mmoja na watoto wengine wawili kuhofiwa kufa maji huku watu 11 wakiokolewa. Na wafanyakazi wawili wa boti hiyo kukimbia.

Katika kuhakikisha usalama wa Kijiji cha Wampembe unaimarika Mh. Zelote aliagiza kuhamishwa kwa watumishi wawili, Afisa Mtendaji wa kata ya Wampembe Faustine Wakulichamba pamoja na Afisa uvuvi wa Kata Godfrey Kashengebi kwa makosa mbalimbali moja ikiwa kutosimamia makusanyo ya mapato ya uvuvi jambo lililopelekea kudorora kwa makusanyo ya mapato  pamoja na kuwepo kwenye kata hiyo kwa miaka zaidi ya sita jambo ambalo linapunguza ufanisi wao wa kazi.

Katika doria hiyo Mh. Zelote pia alikamata kokoro na nyavu kadhaa zilizokuwa hazikukidhi vipimo vya serikali katika matumizi yake jambo ambalo maafisa hao walifumbia macho na kuisababishia serikali upotevu wa mapato.


Kwa mujibu wa sheria za halmashauri mtumbwi wenye urefu wa mita 4 hulipiwa dola 4 kwa mwaka kama ada ya usajili. 

RC Rukwa atoa Siku tatu kuhakikisha huduma ya upasuaji inapatikana Wampembe

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameipa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi siku tatu kuhakikisha kuwa wanafanya marekebisho ya mfumo wa maji unaohudumia kituo cha afya cha Wampembe jambo ambalo linakwamisha huduma ya maji katika kituo hicho.

Ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya ghafla katika kituo hicho ili kuona utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa tangu kuanza kwa mwaka huu, ziara hiyo ya siku tatu ililenga kuangalia utekelezaji katika sekta ya elimu, afya, maji, na uwekezaji wa viwanda.

Katika kuhakikisha jambo hilo linakamilika aliagiza mhandisi wa maji wa Halmashauri hiyo Eric Namakonde ambaye aliambatana na msafara huo kubaki siku hizo na kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika na kupatiwa ripoti.
Mkuu wa Mkoa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen (aliyevaa kaunda suti) akitoa maelekezo juu ya urekebishaji wa mfumo wa maji kutoka ziwa tanganyika kwenda katika kituo cha afya Wampembe. 

“Nimekuja mwezi wa tano na kuagiza hili jambo likamilike mpaka sasa sioni kinachoendelea, huwa sipendi kurudia maagizo sasa mhandisi wa maji ubaki hapa hadi marekebisho yakamilike na taarifa inifikie mezani ndani ya siku tatu,” Amesema

Kijiji cha Wampembe kipo mwambao wa Ziwa Tanganyika, Wilaya ya Nkasi na kutoka makao makuu ya wilaya hadi katika Kijijini hapo ni kilomita 117 umbali ambao unasababisha hali mbaya kwa wananchi ambao wanataka kufanyiwa upasuaji katika kituo hicho ambacho kina maabara iliyokamilika ila inakosa huduma ya maji tu, na gharama ya marekebisho ya uharibifu Shilingi 800,000/=.

Mabomba (yaliyolala) yaliyofanyiwa uharibifu na kusababisha kushindikana kupandisha maji kutoka ziwa Tanganyika kuelekea katika kituo cha Afya Wampembe kilichopo kwenye mwambao wa Ziwa hilo


Mhandisi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Shabani Daudi (mwenye sati jekundu) akitoa ushauri juu ya kuimarisha mfumo wa maji utakaosadidia upatikanaji wa maji katika kituo cha afya Wampembe. 

“Msafara huu ambao nimekuja nao, si ushafikia hiyo gharama tayari, sasa mnataka tuwe tunakuja huku kila siku kwaajili ya jambo hili tu, sasa sitaki kurudi huku kwa jambo hili tena,” Amesema.


kwa muda wa miaka miwili wananchi wamekuwa wakilazimika kuchota maji katika visima vilivyopo Kijiji hapo na kufikisha kituoni hapo pindi ndugu yao anapotaka kufanyiwa upasuaji jambo ambalo Mh. Zelote hakukubaliana nalo. 

Kikongwe kupatiwa kiwanja karibu na Ikulu ndogo halmashauri ya Nkasi.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kumtafutia kiwanja cha nyumba Bibi Georgina Kapilima ili waweze kujenga nyumba na kuishi bila ya bughudha.
Ushauri huo umetolewa baada ya bibi huyo kumuomba Mkuu wa Mkoa katika siku maalum ambayo Mkuu wa Mkoa aliiweka maalum kwaajili ya kusikiliza kero na maombi mbalimbali ya wananchi ambao walijitokeza kuzungumza moja kwa moja na Mkuu huyo.

Bibi huyo ambaye alianza kwa kuilaumu Halmashauri hiyo baada ya kufika katika ofisi hizo mara kadhaa akidai kutafutiwa kiwanja cha kununua baada ya kuona majumba yakiendelea kujengwa katika mji huo unaoendelea nae akiumia kwa kulipa kodi ya shilingi 45,000 kwa miezi mitatu, jambo ambalo linamuweka katika wakati mgumu kutafuta pesa ya kodi hiyo.

“Ombi la huyu bibi ni la msingi sana, maana kila kukicha anaona nyumba zinamea tu lakini yeye akihitaji kiwanja anaambiwa hakuna jambo ambalo halimuingii akilini, kwahiyo Mkurugenzi, na Katibu tawala fanyeni utaratibu huyu bibi apatiwe kiwanja aweze kujenga nyumba,” Mh. Zelote alieleza.
Bibi Georgina Kapilima akisikiliza maamuzi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa (hayupo pichani) mara baada ya kutoa malalamiko yake juu ya kukosa kiwanja cha kununua ili ajenge nyumba.

Awali alipokaribishwa kueleza shida yake mbele ya Mkuu wa MKoa Bibi Kapilima mwenye miaka 60 alisema kuwa kila akifika ofisi za halmashauri kuomba kiwanja anaambiwa hakuna huku akiona watumishi wa halmashauri hiyo wakiendelea kujenga majumba na kuongeza kuwa hataki kiwanja hicho bure na kuwa yupo tayari kukilipia ili nae awe na kwake. 
  
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen (katikati kwenye meza kuu) akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi na Katibu tawala wa Wilaya juu ya kushughulikia tatizo la Bibi Georgina Kapilima.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen (katikati) akitoa ufafanuzi wakati alipokuwa akisikiliza kero na maombi mbalimbali ya wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, kuliani kwake ni Katibu tawala wa Wilaya ya Nkasi Festo Chonya na Kushotoni kwake ni Kaimu Mkurugenzi wa H/W ya Nkasi Abel Mtupwa.

Kwa kulipatia ufumbuzi jambo hilo katibu tawala wa Wilaya ya Nkasi Festo Chonya alitoa ahadi ya kumpatia kikongwe huyo moja ya viwanja 35 vilivyopo karibu na ikulu ndogo ya Wilaya ya Nkasi, Mjini Namanyere.

Mbali na kikongwe huyo Mh. Zelote alisikiliza kero za wananchi 14 kwa siku hiyo na kuweza kuzipatia ufumbuzi na wananchi hao kuondoka wakiwa wameridhika na maamuzi ya Mkuu wa Mkoa katika kutatua kero zao hizo.


Katika kusikiliza kero hizo Mkuu wa mkoa alikuwa na wakuu wa Idara za halmashauri hiyo, wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa Wilay pamoja na baadhi wa wakuu wa idara kutoka katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa.