Monday, July 31, 2017

RC Rukwa aagiza operesheni ya usafi wa vyoo wilaya nzima

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amemuagiza afisa afya wa wilaya ya Kalambo kuhakikisha anakagua usafi wa vyoo na maeneo yanayo zunguka nyumba kwa wilaya nzima ili kujiepusha na ugonjwa wa Kipindupindu katika Wilaya hiyo.

Ametoa agizo hilo katika mkutano na wananchi siku ya usafi wa mwisho wa mwezi maarufu kama “Magufuli Day” baada ya Mkuu huyo kukagua nyumba 12, maduka ya wafanyabiashara pamoja na soko katika makao makuu ya wilaya hiyo huku nia ikiwa ni kutaka kujua hali ilivyo wanakojisaidia, wanakohifadhi taka pamoja na hali ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo.

Katika ukaguzi huo amebaini kuwa wananchi wengi husafisha nje ya nyumba tu huku nyuma ya majumba yao hali ikiwa mbaya jambo ambalo hupelekea kuibuka kwa kipindupindu na kuisababishia serikali kuwa katika wakati mgumu kwa magonjwa ambayo yanaweza kuzuilika endapo usafi utazingatiwa.“Leo nilipenda nione usafi wa matai, nimeuona na nimetoa “marks” 60, Nimepita karibu maeneo mbali mbali, usafi mnaoufanya ni wakuficha uchadu kidogo, huku mbele kusafi lakini nyuma kuchafu sana, nawaomba hilo mlirekebishe” Alisema.

Pia aliishauri halmashauri hiyo ya kalambo kuweza kusimamia sharia za usafi zilizopo bila ya huruma ili kuleta mabadiliko na kuitaka halmashauri hiyo kutenga fedha za makusanyo ya ushuru ili kuweza kuboresha hali ya usafi katika mji huo.

Mwezi mmoja uliopita Wilaya hiyo ilikumbwa na ugonjwa wa kipindupindu na kuua mtu mmoja na kuwaacha wengine ishirini katika hali mbaya jambo ambalo serikali haitaki ijirudie.

“Juzi hapa kulitokea kipindupindu kule Kijiji cha Samazi, hapana hatutaki watu wafe kwa kipindupindu, sasa nimeona choo kinamwaga maji machafu kinyesi kinatoka nje bata wanapokea wanakula, hatupo salama,” Alimalizia.


Pamoja na hayo Mh. Zelote alisisita kuwa usafi ni wa kila siku si lazima kusubiri jumamosi ya mwisho wa mwezi na kueleza kuwa siku hiyo imewekwa maalum ili kuwakumbusha wananchi kuwa wanahitajika kufanya usafi maeneo wanayofanyia biashara pia na ku wa usafi ni muhimu. 

Naibu Waziri wa Elimu aagiza walemavu wajengewe vyoo vyao Kantalamba

Naibu Waziri wa Elimu Mhandisi Stella Manyanya amemuagiza msimamizi wa ukarabati wa shule ya Sekondari Kantalamba kuhakikisha kuwa walemavu wanajengewa vyoo vyao ndani ya mabweni wanamolalia nia ikiwa ni kujiepusha na kuwaamsha wenzao usiku pindi wanapotaka kwenda chooni.

Ametoa agizo hilo leo jumapili (30/7/2017) muda mfupi baada ya kufanya ukaguzi wa ukarabati wa shule hiyo iliyopo Wilayani Sumbawanga iliyopewa Shilingi Bilioni 1.1 ikiwa ni mpango wa serikali wa kuzirudishia hadhi shule kongwe nchini huku shule hiyo ikiwa ni ya tangu 1964.

Naibu Waziri wa Elimu Eng. Stella Manyanya akiongea na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kantalamba wilayani Sumbawanga 

“Lazima muhakikishe kwamba Mnakuwa na vyumba maalum kwaajili ya wanafunzi wenye ulemavu na kuwawekea miundombinu hasa kwa wale walemavu ambao mazingira yao ni magumu Zaidi, kwa mfano mwanafunzi ana ulemavu wa miguu na anatakiwa kwenda chooni hapaswi kutambaa kwenye mikojo ya wanafunzi wenziwe hii inawapelea wao kuwa katika mazingira hatarishi zaidi,” Alisema.

Mbali na agizo hilo pia Mhandisi Manyanya ametoa wiki tatu ukarabati wa shule hiyo kumalizika baaada ya muda waliopangiwa kumalizika huku kipaumebele kikiwa ni kuhakikisha wanafunzi wanaendelea na masomo yao katika hali ya utulivu.

“Sijaridhishwa na kasi ya ukarabati huu hivyo tumewaongezea wiki tatu mhakikishe mnamaliza ili wanafunzi waendelee na masomo maana yake kama mngekuwa hamwezi kumaliza kwa wakati kwanini msingesema mapema,” Alisisitiza.

Aidha alipokuwa anakagua bwalo la kulia wanafunzi aliagiza kutanuliwa kwa bwalo hilo baada ya kuona kuwa bwalo hilo ni dogo na wanafunzi ni wengi kiasi ambacho ingewabidi wanafunzi hao kula kwa zamu ili wote waweze kulitumia bwalo hilo na kuongeza kuwa ukarabati unaofanyika ni pamoja na utanuzi wa majengo kwani ukubwa wa jengo lililopo ni wa tangu 1964 na sasa ni 2017.


Kabla ya kumaliza ziara yake shuleni hapo aliwasisitizia wanafunzi kuwa nia ya Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha kuwa hakuna tofauti kati ya shule za serikali na shule binafsi kuanzia huduma za majengo, elimu na vifaa vya kusomea. 

Thursday, July 27, 2017

RC Rukwa ashirikisha wapinzani katika harambee ya ujenzi wa kituo cha afya

Katika kuendeleza dhana ya maendeleo hayana chama Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewashirikisha madiwani wa chama cha CHADEMA katika harambee ya ghafla iliyolenga kumalizia ujenzi wa jengo la huduma za afya ya uzazi na mtoto katika kituo cha afya Mazwi, Manispaa ya Sumbawanga.

Harambee hiyo ilifanyika muda mfupi kabla ya Mh. Zelote Kukabidhi jumla ya vitanda vya kujifungulia 16, vitanda vya wagonjwa 80, magodoro 80 pamoja na mashuka 200 kwa wakuu wa wilaya ikiwa ni sehemu ya mgawo wa vifaa hivyo uliofanyika nchi nzima kupitia juhudi za Rais Dk. John Pombe Magufuli katika kuimarisha huduma za uzazi nchini.
Kuanzia kushoto - Mh. Zelote Stephen Kushoto, Meya wa
Manispaa Mh. Justin Malisawa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Sumbawanga Kalolo Ntila, Diwani kata ya Majengo, Mh.Dickson Mwanandenje
(CHADEMA),Diwani kata ya Msua Mh. Vitalius Ulaya (CHADEMA), Diwani kata ya
Lwiche Mch.Gerson Lupinduko (CHADEMA),Diwani kata ya Mazwi Mh. Juma
Selemani (CCM) Mwenyekiti CCM Sumbawanga Mjini Mwikala

Akiongea mbele ya wananchi waliohudhuria katika tukio hilo Mh. Zelote alisema kuwa serikali ya awamu ya tano sio ya maongezi bali vitendo hivyo kuwataka waheshimiwa madiwani sita wakiwemo watatu wa CHADEMA wakiongozwa na Meya wa Manispaa ya Sumbawanga kuchangia ujenzi wa jengo hilo jipya ili kuboresha huduma kwa wananchi waliowachagua.

“Ili Manispaa iwe jiji tunahitaji huduma bora katika kituo hiki hivyo basi, Mimi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelote Stephen nachangia tani tano za “cement” ambayo ni mifuko 100,” alitangulia kusema.
Harambee hiyo ilikusanya ahadi ya vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 5.5 huku jengo hilo likiwa limegharimu Shilingi Milioni 16 hadi kusimama.

Awali akisomewa taarifa kabla ya kuzindua huduma ya kujifungua iliyoanza tarehe 1/7/2017 katika kituo hicho afisa muuguzi Mariam Kidya alieleza kuwa jengo lililopo la huduma ya afya ya uzazi na mtoto lina uwezo wa kuhudumia kina mama 2,327 lakini kwa mwaka 2016/2017 limeweza kuhudumia kina mama 31,257 jambo lililopelekea kuanzisha ujenzi wa jengo jipya ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa akina mama.
Maigizo yakiendelea mbele ya Mgeni Rasmi (hayupo pichani) katika kituo cha afya Mazwi, Muda mfupi kabla ya kukabidhi vifaa vya afya 


Aidha Mh. Zelote aliwasisitiza wananchi kuendelea kulipa kodi ili kuendelea kuboresha huduma na kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali nchini na kuonya kuwa wale watakaolipishwa ili kupata huduma ya afya ya uzazi na mtoto basi wafike ofisini kwake ili achukue hatua.

“Ndio maana Mheshimiwa Rais amesisitiza sana watu tulipe kodi wote ili kutatua kero mbalimbali za wananchi hususan watu wa hali ya chini.  Nataka nisisitize ulipaji wa kodi ili kazi kama hii na zingine zifanyike.

Kwa upande wake mganga mkuu wa mkoa Dk. Boniface kasululu alipokuwa akisoma taarifa ya huduma ya afya na uzazi ya mkoa, alisifu uamuzi wa Rais Dk. John Pombe Magufuli wa kununua vifaa hivyo kupitia bohari kuu ya dawa (MSD) kwani changamoto hizo zimekuwa zikiwasumbua kwa muda mrefu kuanzia ngazi ya mkoa hadi katika halmashauri.


“Sekta ya afya kukabiliwa na changamoto kadhaa kubwa ikiwa ni upungufu wa vifaa na vifaa tiba muhimu na ufinyu wa miundombinu ya kutolea huduma kwa maana ya majengo, hivyo tunapongeza juhudi za rais wetu mpendwa kutupatia vifaa hivi na tunaahidi kuvitunza ili viweze kuwasaidia kina mama wa mkoa wetu,” Alisema. 

Wednesday, July 26, 2017

Wanaosababisha hoja za ukaguzi wachukuliwe hatua - RC Rukwa

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameagiza kuchukuliwa hatua kwa wale wote watakaosababisha kuibuka kwa hoja za ukaguzi wa Hesabu za serikali katika Halmashauri zao.

aliyasema hayo alipohudhuria kwenye baraza maalum la madiwani la kujadili na kujibu hoja 147 za mkaguzi wa hesabu za serikali nchini kwa mwaka wa fedha 2015/2016 katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen akitoa nasaha katika baraza la madiwani la kujadili hoja za ukaguzi wa hesabu za serikali kwa mwaka 2015/2016. 
Akinukuu barua ya maagizo aliyoyatoa tarehe 4/5/2017 Mkuu wa Mkoa alisema kuwa kila mamlaka ya nidhamu ichukue hatua za kinidhanmu kwa mujibu wa sharia kwa watumishi ambao wamesababisha hoja za ukaguzi kwa uzembe au kwa kutotekeleza majukumu yao ipasavyo na taarifa juu ya hatua hizo apelekewe.

“Kwenye hoja zilizojibiwa ningependa sana hoja ziwe na data zinazoeleweka na za uhakika, na kuacha kitu kinachoitwa tunaendelea kuishughuilikia, iseme tumefikia wapi, sio tunaendelea, Hakuna kinachoendelea, lazima kupiga hatua kuondoka kwenye hoja hiyo, nimesikia kuwa kuna watu wamechukuliwa hatua lakini sijaziona,” Mh. Zelote alibainisha.

Aidha alibainisha kuwa wapo watu waliofanya madudu na wanapaswa kuchukuliwa hatua na kutowaachia kwani kufanya hivyo hakutasaidia kufutika kwa hoja na kusisitiza kuwa waliosababisha hoja watafutwe popote walipo ili warudi kujibu hoja walizoziibua.

Hata hivyo, Mh. Zelote ameusifu uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kwa kuweka misingi imara iliyowapelekea kupata hati safi kwa mwaka wa fedha 2015/2016 na kuwaasa kumtumia mkaguzi mkaazi wa mkoa pamoja na wakaguzi wa ndani kutoka ofisi yake ili kuzuia hoja zisitokee.

“Ni halmashauri pekee katika Mkoa huu ambayo imepata hati safi, kwa hilo niwapongeze sana, angalau mmenitoa kimasomaso, sijui ingekuwaje kama ingekuwa ni zote zimepata hati yenye mashaka,” Alisema.
Baadhi ya Waheshimiwa madiwani wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kmaishna Mstaafu Zelote Stephen
Na kuagiza kuwa hoja zote zilizo ndani ya uwezo wa mkoa zisijitokeze tena kwakuwa halmashauri zote zina mfumo unaojumuisha kanuni, sharia na taratibu lazima mambo hayo yasimamiwe kikamilifu.

Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Mh. Zeno Mwanakulya alisema kuwa lengo la halmashauri ni kuhakikisha kuwa hoja hizo zinafutika na hazijirudii.

“Lengo la Halmashauri ni kuhakikisha kwamba tunazifuta hoja zote, ndio lengo letu kubwa kwahiyo wakati tunachangia lazima tujiulize kwanini hoja hizi zimejitokeza, Je, zilikuwa na sababu ya kutokea, basi ni vizuri kama wawakilishi wa wananchi tuweke msisitizo hoja hizo zifutwe” Alisema.
Na pia aliahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa ili kuhakikisha kuwa Halmashauri hiyo inaendelea kupata hati safi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda alibainisha kuwa hoja zinasababishwa na uzembe wa watumishi katika kutekeleza majukumu yao na kukumbusha kuwa mwaka wa fedha 2014/2015 kulikuwa na hoja 80 ukilinganisha na mwaka wa fedha 2015/2016 wenye hoja 147.


“Kila mtu katika eneo lake akiwajibika hakutakuwa na hoja kwasababu Hakuna hoja isiyo na majibu, wakaguzi wanachotaka ni majibu, ukishawaridhisha kwa kuweka kumbukumbu zako vizuri, hoja haiwezi kujitokeza,” alimalizia. 

Monday, July 24, 2017

MKE WA WAZIRI MKUU AWASIHI WANAFUNZI KUTOKATISHA MASOMO

MKE wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa amewasihi wanafunzi wa kike nchini kujiepusha na vitendo vinavyoweza kusababisha kukatisha masomo yao.

Amesema ni vema wanafunzi hao wakatumia muda wao vizuri kwa kusoma kwa mfululizo kutoka kiwango kimoja cha taaluma kwenda kingine.

Mama Mary aliyasema hayo jana (Jumapili, Julai 23, 2017) alipozungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Vwawa wilayani Mbozi.

MKE wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa
Mke wa Waziri Mkuu ambaye ameambatana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika ziara ya mkoa Songwe, aliwaasa wanafunzi hao kutumia wakati huu kwa kusoma kwa bidii na kujiepusha na vitendo viovu.

“Nawasihi mtumie muda huu kusoma kwa bidii ili muweke msingi imara kwa ajili ya kujenga maisha yenu ya baadae. Msikatishe masomo yenu.”

Mama Mary aliongeza kwamba “utumieni muda huu vizuri ili msije mkaujutia baadae, kwani wakati ni mali ukipita umepita.”

Alisema ni vizuri wakasoma hadi chuo kikuu na kwamba wasikimbilie kufanya mambo yasiyowahusu kwa sasa kwani mshika mawili moja lazima limponyoke.

Mke wa Waziri Mkuu alisema wanafunzi hao wakisoma hadi elimu ya juu watakuwa na uwezo wa kutambua jambo lipi ni jema na lipi ni baya.

“Kilichonifurahisha zaidi ni kwa sababu mimi pia ni mwalimu kwa hiyo inavyoona wanafunzi wako vizuri kama hivi nafurahi sana, hivyo nawaomba msome kwa bidii.”

Serikali imetunga sheria kali dhidi ya watu wanaosababisha watoto wa kike kukatisha masomo yao kwa kuwapa mimba au kuwaoa.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, JULAI 24, 2017

Sunday, July 23, 2017

RC Rukwa asikitishwa na utendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna mstaafu Zelote Stephe amesikitishwa na kitendo cha halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa kuwa na hoja za kujibu zipatazo 60 ambazo zimesababisha halmashauri hiyo kupata hati ya mashaka wakati halmashauri hiyo imeajiri watumishi wenye uwezo wa kuepusha jambo hilo lisijitokeze.
Akizungumza katika kikao cha baraza la dharula la madiwani Jana Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa anasikitishwa sana na kitendo hicho kwani wataalamu hao wameajiriwa huku serikali ikiwa inamatumaini kuwa ni watu wenye uwezo sasa zinapotokea hoja hizo yeye binafsi zinamsikitisha sana.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen akitoa maelekezo kwa madiwani na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. 

Alisema kuwa halmashauri hiyo haipaswi kuwa na huruma na watu wote waliosababisha hoja hizo kwani wanaoumia ni wananchi kutokana na baadhi ya watendaji kusababisha hali hiyo ambayo inapelekea halmashauri kupata hati ya mashaka na hata chafu na yeye akiwa ni Mkuu wa mkoa hatakubaliana na hilo.
"Binafsi nachukizwa sana na hali hii, siipendi hata kidogo kwani inaumiza na kuonekana hatuna watendaji wenyeuwezo, abadani sitakubali hali hii katika mkoa wangu labda uwe mkoa mwingine," Alisema.
Aliongeza kuwa madiwani wanapaswa Kutambua kuwa wao ndio taa ya halmashauri, kwani wakilegalega na halmashauri ikiendelea kupata hati ya mashaka wajue watakwenda kujibu wenyewe kwa wananchi ambao wamewatuma kuwawakilisha ili kuleta maendeleo katika halmashauri. 
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mh.Kalolo Ntila alisema kuwa hoja hizo hazikutokana na baraza lililopo hivi sasa, na hata Mkurugenzi aliyopo hivi sasa na kuahidi kuwa wale wote waliosabaisha hoja hizo lazima watafutwe popote waliopo na kuchukuliwa hatua.
" hatutawaacha watu hawa bali tunazipitia hoja moja baada ya nyingine na kuzitolea majibu,lakini zile ambazo kitakuwa na matatizo ni lazima waliopo sababu sha wasakwe popote walipo na hatua dhidi yao zichukuliwe" alisema
Awali akizungumza katika baraza hilo la madiwani Mkaguzi mkazi na mdhibiti wa hesabu za serikali John Nalwambwa alisema kuwa ofisi yake ilibaini kuwepo kwa hoja 60 zenye utata ambapo hoja 25 kati ya hizo ndizo zilizopelekea kupata hati ya mashaka.
Alisema kuwa kuna fedha zaidi ya shilingi milioni 40 ambazo hazieleweki vizuri matumizi yake na baadhi ya vitabu vya makusavyo vikiwa vimepotea na hivyo nilazima ifahamike hatma ya suala hilo.
Alisema kuwa ofisi yake imefanya kazi kwa weledi mkubwa bila kuonea mtu na ndiyo imebaini hayo hivyo basi ni jukumu la halmashauri kuona ni jinsi gani itajibu hoja hizo ili zisijirudie tena.

"Wananchi tujitolee Damu" Dk. Kigwangala

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya Dk. Hamis Kigwangala amesikishwa na hali ya hospitali ya mkoa wa Rukwa kukosa damu ya kutosha kusaidia wagonjwa pindi dharura inapotokea.

Masikitiko hayo aliyatoa baada ya kufanya ukaguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa katika ziara yake ya siku moja ambapo alitembelea hospitali hiyo pamoja na vituo vya afya vitatu vya Laela Wilayani Sumbawanga, Wampembe na Nkomolo vya Wilaya ya Nkasi.
Dk. Hamis Kigwangala (kushoto) akiongea na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Mh. Julieth Binyura pamoja na watumishi wa Hospitali ya Mkoa wa Rukwa. 

“Nimesikitishwa na changamoto ya upatikanaji wa damu, kwanza mna units chache mlipaswa kuwa na units karibu 120 ili kuendana na idadi ya watu milioni 1.2 wa mkoa mzima, lakini kwa bahati mbaya hamna hata damu moja ambayo imekuwa “screened” na tayari kwa matumizi, hii inasikitisha sana lakini kwa ujumla maabara iliyopo ni nzuri sana, kuna mapungufu machache sana kwenye “theatre” na pia nimefurahishwa na “labour ward” iko vizuri sana.

Dk. Kigwangala alibainisha kuwa changamoto ya upatikanaji wa damu ipo katika kanda ya nyanda za juu kusini na kuahidi kulishughulikia jambo hilo huku akiwaasa wananchi kuweza kujitokeza kwa wingi kuchangia damu na si kukaa vipembeni na kulalamika pindi wanapokosa damu hospitali wakati wanashindwa kujitolea damu.

“Mimi binafsi najitolea damu mara tatu kwa mwaka, wananchi tunatakiwa kujitolea damu ili kuweza kuwasaidia wale wanaohitaji, huwezi jua inaweza kumsaidia ndugu, jirani ama rafiki, hivyo tuwe na moyo wa kujitolea.” Alisema.

Katika ziara yake hiyo mambo aliyoyapa kipaumbele ni kuangalia huduma za maabara, vyumba vya upasuaji, vyumba vya kuzalia pamoja na akiba ya damu salama, ambapo vituo hivyo vilionekana kufanya vizuri katika maeneo hayo.

Huduma ya maji katika vituo hivyo ilioneka kuwa ni kikwazo katika upatikanaji wa huduma bora hivyo Dk. Kigwangala aliwaagiza wakurugenzi wa Sumbwanga Vijijini pamoja na Halmashauri ya Nkasi kuhakikisha jambo hilo linatafutiwa ufumbuzi wa haraka kwa kutambua umuhimu wa maji na ubora wa huduma za afya.

Dk. Kigwangala hakutaka ziara hiyo iwe ya kiutendaji pekee hivyo alikutana na wananchi wa maeneo ya Laela pamoja naWampembe na kuwapa nafasi ya kueleza vikwazo wanavyokutana navyo katika kupata huduma bora ya afya.

Ndipo alipojitokeza ndugu Nassoro Ibrahim na kutaka kufahamu nafasi ya walemavu katika kupata huduma bure kama ilivyo katika makundi ya wazee, watoto na wajawazito, “Naomba Serikali ituangalie na sisi walemavu tunnapata shida sana maana wenzetu wazee, watoto na kinamama wanasaidiwa,”Alisema.


Katika kujibu swali hilo Dk. Kigwangala alimtaka mlemavu huyo kuonana na uongozi ili aweze kufuata taratibu za kuweza kutibiwa bure lakini alimuahidi kuwa serikali ipo katika mkakati kuona namna ambayo wanaweza kuwasaidia walemavu katika kupata huduma bure.

Wednesday, July 19, 2017

Shule siyo “Clinic” wala siyo “Maternity” – RC Rukwa

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameonya vikali wale wanaoendeleza gumzo la kuwatetea wanafunzi wanaopata mimba wakitaka warudishwe shule huku watoto wao wakiwa wanawalinda na kuhakikisha wanafanikiwa katika maisha.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen akiongea na wanafunzi wa shule ya Sekondari Milundikwa juu ya kuachana na mapenzi shuleni na kuweka mbele masomo tu. 

Ameyasema hayo alipofanya ziara kujionea maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha tano katika shule mbili za Wilaya ya Nkasi kwa muhula wa mwaka 2017/2018, ambapo kwa Mkoa wa Rukwa wanafunzi 1,155 wamepangiwa kujiunga na shule 13 zinazochukua wanafunzi wa kidato cha Tano.

Mkuu wa Mkoa alisema kuwa kwa Mkoa wa Rukwa pekee kuna kesi 165 za wanafunzi kupata mimba tangu Januari hadi Juni mwaka huu na kesi zao zinaendelea kushughulikiwa ili kuwapata watuhumiwa na kuwachukulia hatua.

“Katika Mkoa wangu huu adui yangu namba moja ni yule ambae anampa mtoto wa kike mimba na yeyote anayetetea masuala yanayozunguka mimba, tusije tukaruhusu watu ambao wameshafanikiwa na watoto wao kielimu halafu wanakuwa kwenye majukwaa ya kuwaharibia watoto wa wazazi wengine, shule siyo Clinic wala siyo Maternity, wanafunzi hawaji shuleni kuapata mimba ni kusoma tu,” Mh. Zelote alisisitiza.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen akikagua baadhi ya viti vya wanafunzi wa shule ya Sekondari Milundikwa akiwa pamoja naMkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda (wa tatu toka kulia)

Sambamba na hilo aliwataka wazazi wote kukemea vitendo hivi vinavyolenga kukatisha ndoto za wanafunzi hawa ambao wanaandaliwa kuijenga Tanzania ya viwanda, na kuongeza kuwa watoto ni wa watanzania si lazima awe wa kumzaa hivyo inampasa kila mzazi kuwa na uchungu pale anapoona mtoto wa mwenziwe amekatishwa ndoto zake kwa kupata mimba.
“Kwa wazazi na watu wazima hili lazima tulisimamie wote, mzazi, mtu mzima akimwona mtoto anafanya kitu kibaya achukue hatua, akemee na sio kupiga makofi na kutetea,” Alisema.

Katika kulisisitiza hilo Mh. Zelote aligawa nakala ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 2 ya mwaka 2016 ambayo katika kifungu 60A (1 – 4) imebainisha adhabu kwa watu wanaowapa mimba au kuoa ama kuolewa na mwanafunzi, kwa kifungo cha miaka 30 jela.

Awali akisoma taarifa fupi ya hali ya mimba katika Shule zilizopo Wilaya ya Nkasi Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nkasi Abel Adam Ntupwa alisema kuwa wananchi na wazazi wengi hawaifahamu sharia ya elimu inayotaka mwanafunzi akipata mimba taarifa na vielelezo vinapelekwa kwa afisa mtendaji kata au Kijiji na kesi kupelekwa polisi kisha mahakamani.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen akiongea na mkandarasi wa Nyasa Drilling anayechimba kisima kwaajili ya Shule ya Sekondari Milundikwa, Wilayani Nkasi. “Baadhi ya wazazi na watendaji wanakula njama ya kutaka kumaliza kesi kienyeji kwa wazazi wa pande mbili kupatana, hivyo uongozi wa wilaya utatoa elimu pana juu ya haki ya msichana kusoma mpaka kumaliza na kuwachukulia hatua wale wanaosaidia kuficha wahalifu wa mimba,” Alisema.


Katika kuonesha umakini wa kulifuatilia suala hilo Afisa Elimu wa Mkoa wa Rukwa Robert Nestory alisisitiza kuwa upimwaji mimba kwa wanafunzi ufanywe mara kwa mara isiwe tu wakati shule zinapofunguliwa.

“Huu utaratibu wa kuwapima wanafunzi wakati shule zinapofunguliwa tuuache, upimwaji huu uwe ni wa mara kwa mara, na maafisa elimu wanapokwenda kutembelea shule mbali mmbali basi ni jukumu lao kuonana na wazazi ili wawape elimu ya sharia hii na sio tu kumuachia Mkuu wa Wilaya kazi hiyo,” Aliongeza.

Wakati akimkaribisha Mkuu wa Mkoa nae Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda alibainisha mpango wa kuwatangaza kwenye redio watuhumiwa wote ili jamii isikie na kuondoa dhana ya kuwaficha katika maeneo yao wanayoishi.

“Orodha yao watuhumiwa wote tunayo na redio tunayo, Nkasi FM, tutawangaza kwa majina ili wafamu kwamba wanatafutwa ili kuwatia hofu hasa maeneo ya huku vijijini,” Mh. Mtanda alimalizia.

Tuesday, July 11, 2017

RC Rukwa awatoa wasiwasi wakulima kuhusu suala la barabara vijijini.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstafu Zelote Stephen Zelote amewatoa wasiwasi wakulima wanaolalamikia ubovu wa barabara vijijini kwa kusisitiza mpango wa serikali kuanzisha wakala wa barabara mijini na vijijini ili kuondoa kero hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Lt. Mstaafu Chiku Galawa (katikati), akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen(kushoto) pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Gen. Mstaafu Rafael Muhuga (kulia) pamoja na wadau wa usindikaji wa mafuta ya alizeti wa mikoa hiyo.

Ameyasema hayo wakati alipokuwa akijibu hoja ya mmoja wa wakulima Frank Enock aliyeilalamikia serikali kushindwa kuboresha miundombinu vijijini ili kupata urahisi wa kusafirisha mazao kwa kipindi chote cha mwaka.

Hoja hiyo iliibuka wakati wa majadiliano katika mkutano wa uzinduzi wa mradi wa Taasisi ya Kuendeleza Mifumo ya Kimasoko katika Kilimo AMDT uliofanyika Mkoani Songwe na kuhudhuriwa na wakuu wa mikoa mitatu ya Songwe, Rukwa na Katavi ambapo mgeni rasmi wa uzinduzi huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Chiku Galawa. 

Mbali na wakuu wa Mikoa mkutano huo pia ulijumuisha wakurugenzi wa Halmashauri, mafisa kilimo wa mikoa na halmashauri, wakulima, pamoja na wasindikaji wa mafuta ya alizeti huku lengo kuu likiwa ni kuboresha zao la kilimo cha alizeti ili kumkomboa mkulima mdogo.

“Kuhusu suala la miundiombinu serikali imeliona hilo tatizo na ndio maana kimeanzishwa kitu kinaitwa TARURA wakala wa barabara mijini na vijijini kwaajili ya kuboresha barabara kuona kuwa zinatengenezwa na zinapitika, kwahiyo msiwe na wasiwasi, barabara hizo zimelenga kuwainua wakulima kwa kuwawezesha kusafirisha mazao yao kwa urahisi na hatimae bei za mazao kupungua kutokana na kurahisishwa kwa njia za kusafirishia,” Mh. Zelote alisisitiza.

Na kuongeza kuwa uanzishwaji wa wakala huo utaondoa ubabaishaji uliokuwa katika halmashauri ambazo hudanganya katika utekelezaji wao wa kujenga barabara za uhakika na ama kuzichelewesha.
Katika kukazia suala la maendeleo na nia ya serikali ya awamu ya tano katika kumkomboa mwananchi, Mh. Zelote alisisitiza msimamo wa Rais Dk. John Pombe Magufuli wa kuhakikisha wananchi wa kipato cha chini ndio wanaoangaliwa kwa jicho la pekee ili anyanyuke, Mh. Zelote alisema,

“Tukitaka kuendelea katika taifa hili tufate yale rais wetu anayosema kila siku kwamba tusihangaike na mtu ambaye ameshasonga mbele, tuhangaike na mtu ambaye anataka kusonga mbele, mwananchi wa kawaida”

Pamoja na hayo Mh. Zelote aliahidi kuwa balozi mzuri katika kuwafikishia ujumbe wananchi juu ya umuhimu wa zao la alizeti katika kujikomboa katika umasikini.

“Tukirudi katika mikoa yetu tutakwenda kuhangaika na yule mwananchi ambae anataka kujikomboa ili tumkomboe na mkombozi mmoja wapo ni alizeti kwani hatujajitosheleza kwenye suala la mafuta lakini tunaweza kujitosheleza kwasababu tuna kila kitu kwenye jambo hili, watu wapo, nguvu ipo, ardhi ipo, wataalamu wapo na mahitaji yapo”.

Kwa upande wake mgeni rasmi wa mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Songwe Lt. Mstaafu Chiku Galawa amewasisitiza watumishi kufanya kazi kwa umoja kuanzia kwa maafisa ugani hadi kwa wakuu wa idara na kusisitiza kuwa Hakuna anayemiliki miradi na kuwa miradi yote ni ya serikali.

“Utamkuta afisa ugani anasema mradi huo haunihusu unasimamiwa na Fulani, tukimkuta kama huyo tutamshughulikia na wakulima wanakijiji wote mkikutana na afisa ambaye hatoi ushirikiano kwenye miradi ya serikali badi nyie tupigieni simu ili tumshughulikie, haiwezekani alipwe mshahara halafu asifanye kazi, wakati wote anavizia posho tu,” Mh. Galawa alisema

Monday, July 10, 2017

MZEE WA MIAKA 67 AUAWA HUKO LAELA.


Mzee mwenye umri wa 67, Mfipa, Mkulima wa Lyapona, aitwaye VICTORY LANDANI KALUNGUZWI, Aliuawa kwa kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia fimbo na watu watatu waliotambuliwa kwa majina.

Chanzo cha kufanya mauaji hayo ni wizi wa mahindi ambapo marehemu alishukiwa kuwa ni mwizi wa katika shamba la MICHAEL MKOMBOZI.

MAuaji hayo yalitokea baada ya  watu hao kumvizia marehemu akiwa shambani na kuanza kumshambulia kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia fimbo na kumsababishia kifo.
  
Watuhumiwa walitoroka mara baada ya kutenda kosa hilo na juhudi za  Jeshi la Polisi  za kuwatafuta zinaendelea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa Kamishna Msaidizi wa Polisi GEORGE SIMBA KYANDO   anatoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani ni kosa la jinai.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa Kamishna Msaidizi wa Polisi GEORGE SIMBA KYANDO

Aidha anatoa ushauri kwa wananchi kujijengea tabia ya kutoa taarifa katika vituo vya Polisi pale wanapomuhisi mtu kuwa kafanya uhalifu na sio kujichukulia maamuzi kama walivyofanya.

Pia anatoa angalizo kwa wale wote walioshiriki kufanya mauaji hayo ni vyema wakajisalimisha wenyewe mapema iwezekanavyo pia anaomba ushirikiano kwa wananchi kuwa endapo watawaona watu ambao siyo wenyewe katika maeneo yao watoe taarifa harakasana ili washukiwa waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua zaidi.


SERIKALI YAPUNGUZA TOZO YA ARDHI KWA ASILIMIA 5

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuanzia mwaka huu wa fedha, Serikali imepunguza gharama za malipo ya awali ya thamani ya ardhi iliyopimwa kutoka asilimia 7.5 hadi asilimia 2.5.

“Serikali inaendelea kupunguza gharama za umilikaji wa ardhi nchini na katika mwaka wa fedha 2017/2018, imepunguza tozo ya awali ya ardhi iliyopimwa (premium) kutoka asilimia 7.5 ya thamani ya ardhi hadi asilimia 2.5 tu. Natoa wito kwa wananchi kuchangamkia punguzo hili na kujitokeza kupimiwa na kumilikishwa ardhi,” amesisitiza.
 
Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Mh. Dk. John Pombe Magufuli akisalimia na Waziri Mkuu wa Tanzania Mh. Kasim Majaliwa, Mbele ya Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Julai 5, 2017), bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa saba wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Septemba 5, mwaka huu.

Amesema Serikali itahakikisha kuwa kila kipande cha ardhi ya Tanzania kinapimwa ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015. “Serikali imeweka mkakati na mpango kazi wa kuwezesha kufikia lengo la kupanga matumizi bora ya ardhi katika vijiji 1,500 na wilaya tano kila mwaka.

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha Ofisi za Ardhi za Kanda kwa kupeleka wataalam wa kada mbalimbali na kuwawezesha kwa kuwapatia vitendea kazi stahiki. “Kazi ya upimaji wa ardhi haiwezi kufanikiwa bila ya rasilmali watu. Lengo letu ni kuwawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za ardhi katika kanda badala ya kufuata huduma hizo makao makuu ya wizara,” amesema.

Amewasihi watumishi watakaohamishiwa katika ofisi za kanda pamoja na wale waliopo katika Halmashauri, wafanye kazi kwa ushirikiano na watekeleze majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia sekta ya ardhi na kutoa huduma kwa wananchi bila ubaguzi wa aina yoyote.

 (mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA.
JUMATANO, JULAI 5, 2017.

WATUHUMIWA 4,809 WA DAWA ZA KULEVYA WAKAMATWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika kipindi cha miezi minne, Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imewakamata watuhumiwa 4,809 na kufungua majalada ya kesi 3,222.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Julai 5, 2017), bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa saba wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Septemba 5, mwaka huu.

“Katika kipindi kifupi tangu Februari, 2017 Mamlaka hii ilipozinduliwa, imefanikiwa kukamata watuhumiwa 4,809 wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroine (gramu 327.173); cocaine (kilo 26.977); bangi (kilo 18,334.83); mirungi (kilo 11,306.67) na lita 6,338 za kemikali bashirifu zilikamatwa bandarini,” amesema.


Amesema mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi za Mikoa imefanya operesheni za kuteketeza ekari 569.25 za mashamba ya bangi na ekari 64.5 za mashamba ya mirungi na kazi hiyo inaendelea. Kutokana na hatua hizo, jumla ya majalada ya kesi 3,222 yamefunguliwa.

“Dawa za kulevya zina athari kubwa kwa ustawi wa familia zetu na Taifa kwa ujumla. Hivyo, napenda kurejea wito wangu kwa Watanzania wote kuunga mkono jitihada za Serikali katika mapambano haya kwa kuendelea kutoa taarifa kuhusu watu wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Amesema azma ya Serikali ya awamu ya tano ni kutokomeza kabisa mtandao wa dawa za kulevya nchini kwa kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanakuwa endelevu, yanafanyika kisayansi na yanaleta mafanikio. “Tuungeni mkono kwenye mapambano haya, ili tutokomeze kabisa mtandao huo,” amesisitiza.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA.
JUMATANO, JULAI 5, 2017.

WAZIRI MKUU AMUAGIZA MWAKYEMBE AICHUNGUZE BMT

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe alifanyie mapitio Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na iwapo hatoridhika na utendaji wake alivunje.


“Ninamuagiza Waziri mwenye dhamana kufanya mapitio na kutathmnini upya utendaji kazi wa Baraza la Michezo Tanzania juu ya usimamizi wake wa  michezo nchini na kama hataridhika, anayo mamlaka ya kulivunja Baraza hilo.”  

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Julai 5, 2017) katika hotuba yake ya kuahirisha Mkutano wa Saba wa Bunge mjini Dodoma.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano haitafumbia macho usimamizi mbovu na utawala wa michezo usiojali maslahi ya Taifa. Serikali imeazimia kuimarisha utendaji kwa vyombo vya michezo nchini ili kila mwenye dhamana awajibike ipasavyo.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameipongeza timu ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys iliyoshiriki na kutoa upinzani mkubwa kwenye mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika.

Amesema licha ya timu hiyo kumaliza ikiwa na jumla ya pointi 4 sawa na timu iliyoshika nafasi ya pili, ila Vijana hao wameonesha vipaji na uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yao.

Msisitizo wangu kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni kuendelea kuwatunza vijana hao, na kusimamiavilabu vya michezo nchini kuwekeza kwenye soka la vijana ili tujenge timu imara kwa miaka michache ijayo.”

Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua umuhimu wa michezo kwa afya, umoja wa kitaifa na kama fursa ya ajira kwa vijana nchini.

“Wiki iliyopita, mkoani Mwanza yamehitimishwa mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA. Wananchi wa Mwanza na Watanzania kwa ujumla wamejionea uwezo wa kimichezo, vipaji na hamasa kubwa iliyopo miongoni mwa vijana wetu kutumia vipaji vyao. “
Amesema Serikali itaendelea kuratibu michezo shuleni, ikiwa ni pamoja na kusimamia  ufundishaji wa michezo kama somo.  “Maelekezo yetu ni kwamba kila Mkoa uwe na shule angalau mbili zenye mchepuo wa michezo na walimu wenye sifa stahiki za kufundisha michezo.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini, wahakikishe kwamba kila shule inakuwa na viwanja vya michezo mbalimbali ili kuwapa fursa wanafunzi kushiriki michezo ili kupandisha na kuinua vipaji vyao.

Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli kwa kuunga mkono jitihada za michezo nchini kwa dhamira yake ya kujenga uwanja mkubwa wa michezo mjini Dodoma kwa kushawishi mataifa rafiki kama vile Morocco ambao wanajenga uwanja huo.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA.        
JUMATANO, JULAI 05, 2017