Monday, November 27, 2017

Wafanyabishara Soko la Soweto washtaki Manispaa kwa RC Wangabo

Wanachi wa Soko la Sabato wamlilia RC Wangabo

RC Wangabo asikiliza kilio cha wafanyabiashara Soko la Sabasaba

RC Wangabo alipotembelea Soko la matola, Manispaa ya Sumbawanga

RC Wangabo atembelea Soko la Bariadi Chanji, Sumbawanga

RC Wangabo ameitaka Manispaa ya Sumbawanga kuboresha masoko

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alipotembelea Soko la Soweto, kata ya Chanji Manispaa ya Sumbawanga katika ziara yake ya kutembelea masoko na kuongea na wafanyabiashara ili kujua changamoto zao.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akinunua bidhaa alipotembelea Soko la Soweto, kata ya Chanji Manispaa ya Sumbawanga katika ziara yake ya kutembelea masoko na kuongea na wafanyabiashara ili kujua changamoto zao

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Matola katika Manispaa ya Sumbawanga katika ziara yake ya kutembelea masoko na kuongea na wafanyabiashara ili kujua changamoto zao.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa tatu toka kushoto) akizungumza na wafanyabiashara wa samaki wa soko la Sabasaba katika Manispaa ya Sumbawanga katika ziara yake ya kutembelea masoko na kuongea na wafanyabiashara ili kujua changamoto zao

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akizungumza na wafanyabiashara wa soko la OTC Kizwite katika Manispaa ya Sumbawanga katika ziara yake ya kutembelea masoko na kuongea na wafanyabiashara ili kujua changamoto zao.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameitaka Manispaa ya Sumbawanga kuhakikisha wanaboresha mazingira ya masoko yaliyopo kwenye Manispaa hiyo ili wananchi waweze kupata huduma kwenye maeneo hayo bila ya kulazimika kufika katikati ya mji kupata huduma hiyo.

Amesema kuwa wakuu wa idara katika Manispaa hawanabudi kuhakikisha wanashuka kuwafuata wananchi na wafanyabiashara wa masoko hayo na kusikiliza kero zao na kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya masoko hayo ikiwemo majengo, usafi wa mazingira na vyoo.

“Nimeambiwa changamoto nyingi sana na wafanyabiashara wa soko la sabasaba na wamekuwa wakifanya biashara zao kwenye mazingira machafu hali ambayo haizoeleki na haifai kuendelea kuwepo, hivyo manispaa lazima iweke kambi kusikiliza kero zao na kuzitatua, kwani lipo kwenye uwezo wao,” Mh. Wangabo alisisitiza.

Aidha, ameitaka manispaa hiyo kuhakikisha usalama wa biashara za wafanyabiashara hao unaimarika ili kupunguza malalamiko yao na kuongeza kuwa atahakikisha malalamiko hayo yanafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.

Akielezea changamoto za soko la sabasaba, Mwenyekiti wa soko hilo Feston Mwilema amesema kuwa changamoto kubwa ya soko hilo ni usalama na kuwa hakuna kituo cha polisi na wala hawana mgambo wa kulinda soko hilo, na kuomba kusafisihiwa mazingira kutokana na uchache wa vi faa vya kuzolea uchafu unaozalishwa katika soko hilo.

“Tumelazimika kuchimba shimo la muda la kutupia uchafu unaozalishwa na wauza samaki kutoka na kutokuwepo kwa shimo la kisasa, na tuna kontena moja badala ya matatu ambalo huzidiwa na soko kukosa uzio ni jambo linalotoa mwanya kwa vibaka kuendelea na wizi,” Alisema Mwilema.


Mh. Wangabo alitembelea masoko nane yaliyopo kwenye manispaa ya Sumbawanga na kubaini kuwa masoko mengi hayatumiki kwa kukosa miundombinu bora na usimamizi na hatimae wananchi kuanzisha masoko yasiyorasmi na kuhatarisha usalama wa bidhaa zao na usalama wa vyakula kutokana na kuvidandaza chini na kuhatarisha usalama wa wanunuzi. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alipotembelea Soko la Soweto, kata ya Chanji Manispaa ya Sumbawanga katika ziara yake ya kutembelea masoko na kuongea na wafanyabiashara ili kujua changamoto zao.


Friday, November 17, 2017

RC Wangabo azihimiza Halmashauri kuongeza mashine za mapato kuongeza ukusanyaji

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amezihimiza Halmashauri zote Mkoani humo kuhakikisha zinaongeza idadi ya mashine za EFD ili kuongeza ukusanyaji wa mapato yao katika halmashauri.

Amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ilikisia kukusanya Shilingi bilioni 2.3 ambapo hadi sasa Wilaya imekusanya Shilingi bilioni 1.9 ikiwa ni ongezeko la asilimia 97 katika makusanyo ya ndani ya Halmashauri hiyo.

“Halmashauri Ziongeze hizo mashine, kama mnavyofahamu serikali hii inahimiza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kutumia mfumo wa Kielektroniki, wenyewe mmekuwa mashuhuda mmevuka kile kiwango mlichojiwekea na kupata ongezeko la asilimi 97 kama mlivyosoma kwenye taarifa yenu, mkiongeza mashine hizo zikafikia idadi inayotakiwa makusanyo ya ndani yatakuwa mengi zaidi,” Alieleza.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (juu ya meza) lipomkaribisha Kaimu Katibu tawala wa Mkoa Albinus Mgonya awatoe wasiwasi wananchi juu ya kuuza mazao yao nje ya nchi pamoja na suala la umemem vijijini, katika kata ya Mtowisa Wilayani Sumbawanga alipofanya mkutano wa hadhara kijitambulisha lakini pia aliwasihi wananchi hao kutunza vyanzo vya maji.  

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa maagizo ya kuongezwa kwa mashine za EFD katika halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ili iweze kuongeza mapato mara baada ya kusomewa taarifa ya halmashauri hiyo kabla ya kuanza ziara yake ya siku mbili kwenye halmashauri hiyo. 

Ameongeza kuwa makusanyo ya ndani yakiwa mengi zaidi itasababisha shughuli za kimaendeleo kufanyika kwa wingi zaidi, ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, huku upungufu wa vyumba hivyo ukiwa ni 1399.

Ameyasema hayo baada ya kusomewa taarifa ya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga katika Ziara yake ya siku mbili yenye lengo la kutembelea miradi mbalimbali, kujitambulisha kwa watumishi pamoja na kuongea na makundi mbalimbali ya wananchi katika halmashauri hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa H/W ya Sumbawanga John Msemakweli amesema kuwa hadi sasa Halmashauri ina mashine za Kielektroniki 64 na uhitaji ni mashine 114 na kusababisha upungufu wa mashine 50 huku akiahidi kuzikamilisha ili kuweza kuongeza mapato ya Halmashauri hiyo.

“Tuna upungufu wa vyumba vya madarasa 1399 na hadi sasa kwa mpango wa kujenga vyumba vitatu kwa kila shule tuna vyumba 98 ambavyo vipo usawa wa linta na kwengine tunaendelea kuwahamasisha wananchi kuweza kuchangia katika ujenzi,” Alisema.

Nae Mh. Wangabo aliwaagiuza kuangalia upya mpango wao wa ujenzi wa madarasa hayo kwani itawachukua muda mrefu ikiwa watajenga madarasa 98 kwa mwaka. 

“Asiyetaka kupunguza mifugo yake ahame, hatutaki kupoteza Ziwa Rukwa,” RC Wangabo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameiagiza kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga kuhakikisha wanashirikiana na Halmashauri kupunguza idadi ya mifugo iliyopo kwenye halmashauri hiyo ili kudhibiti utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na hifadhi za misitu na kuliokoa ziwa Rukwa.

Amesema kuwa shughuli hizo za ufugaji karibu na vyanzo vya maji ndizo zinazopelekea kujaa kwa tope katika ziwa Rukwa, ziwa linaloasisi jina la Mkoa huo na kuongeza kuwa serikali haipo tayari kuona ziwa hilo likipotea na kusisitiza kuhifadhiwa kwa namna yoyote ile ikiwemo kupiga marufuku kufanbya shughuli za ufugaji kwenye vyanzo vya maji.

“Nashkuru kwamba zoezi la kupiga chapa linaendelea ila baada ya kumaliza zoezi hilo muanze kwenda boma kwa boma muhakikishe kwamba animal Unit “idadi ya mfugo kwa eneo” inazingatiwa, mtu ashauriwe kupunguza mifugo yake au ahame akatafute mahali pengine, kwasababu hatuwezi kujaza mifugo kwenye bonde la ziwa Rukwa halafu ziwa likafutika, serikali haitakubali.” Alibainisha.

Ameyasema hayo baada ya kusomewa taarifa ya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga katika Ziara yake ya siku mbili yenye lengo la kutembelea miradi mbalimbali, kujitambulisha kwa watumishi pamoja na kuongea na makundi mbalimbali ya wananchi katika halmashauri hiyo.

Katika taarifa hiyo ilionesha kuwa idadi ya wanyama iliyopo katika bonde hilo ni 143,346 huku idadi inayotakiwa ni 36,666 huku ikionesha kuongezeka mara tatu zaidi ya mahitaji ya uwepo wa Wanyama hao katika bonde hilo.

Katika kulisisitiza hilo Mh. Wangabo amewatahadharisha wananchi kufuga kisasa kwa kuwa na mifugo michache yenye kuleta tija huku ikizingati uhitaji wa ardhi kwaajili ya kilimo na shughuli nyingine za kibinaadamu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa skimu ya umwagiliaji Kijiji cha Ng’ongo, kata ya Mtowisa Wilayani Sumbawanga, Justin Amon amesema kuwa wafugaji wamekuwa wengi katika bonde hilo hasa katika skimu yao hiyo na kuwasababishia hasara pale wanapopeleka mifugo yao kwaajili ya malisho.


“Kama taarifa ilivyosomwa wafugaji wapo wengi ambao wamegeuza eneo hili kuwa sehemu ya machungio, tunapojaribu kuwafuatilia wanatushishia na mawe, fimbo, sime na mapanga na wapo tayari kupambana kwa lolote litakalotokea, na kesi zipo mahakamani lakini  tunaambiwa hatujakamilisha vigezo, hivyo tunashindwa na kushindwa kujua kwamba tunasaidiwaje na serikali yetu, wafugaji wanatunyanyasa sana,” Alisema. 
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (juu ya meza) lipomkaribisha Kaimu Katibu tawala wa Mkoa Albinus Mgonya awatoe wasiwasi wananchi juu ya kuuza mazao yao nje ya nchi pamoja na suala la umemem vijijini, katika kata ya Mtowisa Wilayani Sumbawanga alipofanya mkutano wa hadhara kijitambulisha lakini pia aliwasihi wananchi hao kutunza vyanzo vya maji.  

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule akitoa maelezo ya Kumtambulisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo kwa wananchi wa kijiji cha kizumbi kata ya Laela, Wilayani Sumbawanga.

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiwatahadharisha wananchi wa kikijiji cha Kizumba Wilayani Sumbawanga kuhusu kuweka mpango wa chakula mashuleni  pamoja kutunza vyanzo vya maji.  

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiwatahadharisha wananchi wa kikijiji cha Zimbam, Bonde la Mtowisa Wilayani Sumbawanga kuhusu kutunza vyanzo vya maji katika Ziwa Rukwa. 

“Mshirikiane na SIDO kuwa na Viwanda 25 kwa kila Halmashauri hadi Disemba 2018,” RC Wangabo

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameziagiza halmashauri nne za mkoa huo kushirikiana na Shirika la viwanda vidogo nchini SIDO kuhakikisha wanakuwa na viwanda vipya 25 hadi kufikia Disemba mwaka 2018 ili kutimiza agizo la serikali la kuwa na viwanda 100 vipya kwa kila Mkoa.

Amesema kuwa SIDO ndio msaada mkubwa wa kuhakikisha kuwa ndoto hii inatimia kwani shirikia hilo limejaa wataalamu lakini pia hutoa mafunzo ya viwanda vidogo na vya kati kwa wajasiliamali hivyo hawana budi kuwa nao karibu.

“Serikali imekwishaagiza tuwe na viwanda 100 hadi kufikia Disemba mwaka 2018 na kwa mahisabu ya haraka mkoa una Halmashauri nne, 100 ukigawa kwa nne ni 25, kwahiyo hadi kufikia Disemba 2018 kila Halmashauri iwe na viwanda hivyo vipya, na msaada upo kuna SIDO hapo ambao wataalamu wamejaa na wanatoa mafunzo kila siku ya viwanda vidogo na vya kati watawasadidia na mimi nitalisismamia,” Alisema

Ameyasema hayo baada ya kupokea malalamiko ya diwani wa kata ya Mtowisa Mh. Edgar Malini. alipomkabidhi Mh. Wangabo Skafu iliyotengenezwa na kilichokuwa kiwanda cha nguo katika kata hiyo ambacho kilifungwa miaka zaidi ya 30 na kubaki majengo.

Mh. Edgar Malini alisema kuwa kiwanda hicho kilifunguliwa na Aliyekuwa Waziri Mkuu Mh. Rashid mfaume Kawawa lakini kwa sasa uzalishaji wake umekwama kwani pamba haipatikani kwenye maeneo yao na hivyo kuwa na mazingira magumu ya uzalishaji wa nguo katika kiwanda hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule akitoa maelezo ya Kumtambulisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo kwa wananchi wa kijiji cha Zimba kata ya Mtowisa, Wilayani Sumbawanga. wakati walipofika kwenye kijiji hicho kuona kiwanda cha kukamulia alizeti. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akisalimiana na Mzee Gabriel Joseph wakati wa kujitambulisha kwa wananchi wa kijiji cha Zimba Wilayani Sumbawanga.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa tatu kutoka kulia) akiuliza swali kwa mhandisi wa maji wa Wilaya Patrick Ndimbo (wa kwanza kushoto) wakati walipotembelea mradi wa maji wa kutumia umeme wa jua mji mdogo Laela Wilayani Sumbawanga wenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.8. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akivishwa Skafu na Diwani wa Kata ya Mtowisa Mh. Edgar Malini, Skafu hiyo ni mabaki ya miongoni mwa skafu zilizokuwa zikitengenezwa na kiwanda cha nguo kilichokuwepo katika kata hiyo na hivi sasa kimebaki majengo tu.


Kwa sasa Mkoa wa Rukwa una jumla ya viwanda 950 huku kukiwa na kiwanda kikubwa kimoja, viwanda vya kati 2 na viwanda vidogo 947. 

RC Wangabo amezitaka kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kukamata wazazi wa wanafunzi watoro.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amezitaka kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya kwa kushirikiana na watendaji wa kata na vijiji kuwakamata wazazi wa wanafunzi watoro ili kukomesha utoro mashuleni nahatimae kuongeza kasi ya ufaulu katika Mkoa.

Amesema kuwa haiwezekani wanafunzi wawe watoro na wazazi wapo hawafanyi lolote ili kuhakikisha watoto wao wanapata elimu stahiki kwaajili ya maendeleo yao, kuongeza ufaulu katika mkoa na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

“Nimesikitika kwamba matokeo ya shule yenu sio mazuri hayaridhishi, kuna utoro wa reja reja na utoro wa kudumu, nimeshaagiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya watoro lakini kamati ya ulinzi na usalama muendele mbali zaidi watoro wote wakamatwe hata wazazi pia wakamatwe, isiwe mtoto tu aliyetoroka, si ana wazazi wake, kamata mzazi mtoto peleka polisi wakajieleze vizuri,” Alisisitiza.

Ameyasema hayo alipotembelea Shule ya Sekondari ya Vuma iliyopo kata ya Mtowisa, Bonde la Ziwa Rukwa, Wilayani Sumbawanga kwa lengo la kujionea maendeleo ya wanafunzi hao katika ufaulu na changamoto zilizopo kwenye shule hiyo.

Aidha Mh. Wangabo amewasisitiza wanafunzi hao kuwa na maadili na nidhamu wawapo shuleni kwani kufanya hivyo kutawaongezea ufaulu na mafanikio katika maisha yao na kuongeza kuwa wanafunzi watukutu siku zote hawafanikiwi katika maisha yao na matokeo yake huishia mitaani.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akisalimia waalimu na wanafunzi wa Shule ya msingi Mtindilo, Kata ya Laela Wilayani Sumbawanga, (kushoto kwake) Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule.

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) akiongea na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Vuma iliyopo kata ya Mtowisa Wilayani Sumbawanga, akiwatahadharisha na utoro na suala la mimba mashuleni wakati alipokwenda kuangalia maendeleo ya shule hiyo yenye kidato cha tano na sita kwa bonde zima la ziwa Rukwa. 

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) akiongea na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Vuma iliyopo kata ya Mtowisa Wilayani Sumbawanga, akiwatahadharisha na utoro na suala la mimba mashuleni wakati alipokwenda kuangalia maendeleo ya shule hiyo yenye kidato cha tano na sita kwa bonde zima la ziwa Rukwa. 

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akimkabidhi mti 
(haupo pichani) mwanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Vuma Kenani James muda mfupi baada ya kuupanda ili autunze hadi atakapomaliza kidato cha nnena kumsihi afanye vizuri kwqenye masomo yake

 Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Basilo Matondwa amesema kuwa wanafunzi wa eneo hilo huwa na utoro zaidi katika kipindi cha msimu wa kilimo na kusema kuwa chaguo la kwanza la wanafunzi hao ni kujipatia fedha halafu shule hufuata.


“Wanafunzi watatu watoro zadi ya siku 90 wamefukuzwa shule mwezi wa nane na bodi ya shule na wanafunzi 22 watoro wa leja leja majina yao yamepelekwa kwa mtendaji wa kata kuwashughulikia ili warejee tena darasani,” Alisema.

Thursday, November 16, 2017

RC Wangabo aendelea kusisitiza mshikamano kuchangia maendeleo kwa vyama vyote.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewasifu wananchi wa kata ya Mtowisa, Tarafa ya Mtowisa, Wilayani Sumbawanga kwa kuonyesha mshikamano katika ujenzi wa shule ya Sekondari Vuma pamoja na ujenzi unaonendelea wa kituo cha polisi kitakachohudumia tarafa ya mtowisa.

Tarafa hiyo yenye kata 4 ina shule moja ya kidato cha tano na sita jambo alilosifu Mh. Wangabo kuwa imetimiza ilani cha Chama Tawala kwa kuwa na Shule moja ya aina hiyo kwa kila tarafa.
Amesema kuwa ataendelea kusisitiza kauli ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa maendeleo hayana vyama, hivyo alisisitiza wananchi hao kutobaguana kwa itikadi zao bali wahimizane katika kutatua changamoto na kuleta maendeleo katika tarafa yao.

“Mmenivuti mliponieleza kwamba mnashirikiana katika nyanja mbalimbali, kuna majengo yale ya shule mnashirikiana na jengo hili la polisi mnashirikiana ili kuhakikisha kwamba changamoto mbalimbali zilizopo ndani yenu mnazitatua, hili limenifurahisha na ningependa muendelee nalo, na umeoja na mshikamano uliopo muudumishe bila ya kujali vyama vyenu.” Alisifu.

Ameyasema hayo katika Mkutano wa hadhara katika Kijiji cha mtowisa, kata ya mtowisa Wilayani Sumbawanga katika ziara yake ya siku mbili katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga yenye lengo la kutembelea miradi mbalimbali na kujitambulisha kwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (juu ya meza) akihutubia katika kata ya Mtowisa kwenye mkutano wa hadhara alioufanya kwa nia ya kujitambulisha kwa wananchi. pembeni yake ni Kaimu Katibu tawala wa mkoa Albinus Mgonya. 

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo Akiongea na wananchi wa Kijiji cha kizumbi, Wilayani Sumbawanga 

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akipokea Zawadi kutoka kwa Wanakijiji wa kijiji cha Kizumbi Wilayani Sumbawanga, kwa lengo la Kumkaribisha baada ya kutembelewa na Kiongozi huyo. Mara ya mwisho kutembelewa na Mkuu wa Mkoa ilikuwa mwaka 1974

Kwa upande wake diwani wa Kata ya mtowisa Mh. Edgar Malini alisema kuwa wananchi wa mtowisa hawana tabu wa kutoa ushirikiano ili kujiletea maendeleo wenyewe isipokuwa wamekuwa na kilio cha muda mrefu kuhusu umeme na maji.


Sunday, November 12, 2017

Chuo cha VETA kuanza Januari 2018 - Rukwa

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Julius Kiondo ameahidi kuanza kwa chuo cha ufundi VETA katika Kijiji cha Paramawe Wilayani Nkasi mwezi januari mwaka 2018 baada ya kumaliza vipimo na kupata hati ya majengo hatu itakayomalizwa Desemba mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo Akisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa Mkurugenzo mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi juu ya uanzishwaji wa chuo cha ufundi VETA katika kijiji cha Paramawe Wilayani humo wakati alipotembelea majengo ya chuo hicho ambayo hapo kabla yalikuwa kambi ya kampuni ya ujenzi wa barabara kutoka China. 

Majengo yatakayotumika kwaajili ya chuo hicho yalikuwa kambi ya kampuni ya ujenzi wa barabara China Hunan iliyojenga barabara ya Kanazi - Kizi wilayani Nkasi, yenye urefu wa Kilometa 84, majengo ambayo yamejengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 50 na kupitishwa na baraza la madiwani la Halmashauri hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewasisitiza walinzi kuhakikisha wanayalinda majengo hayo ili yasifanyiwe hujuma na kumuagiza mkurugenzi huyo kuhakikisha Kijiji hicho kinakuwa na Zahanati na huduma muhimu za kijamii ili wanafunzi wataoanza kusoma hapo wasipate tabu.


Kijiji hicho ambacho ndio makao makuu ya kata ya paramawe hadi sasa kina jengo la zahanati ambalo linahitaji shilingi milioni 10 kuweza kumaliziwa hivyo mkurugenzi mtendaji ameahidi kuwa karibu na ujenzi huo ili ukamilike kwa wakati maana kwa sasa ili mwananchi apate huduma ya afya ni lazima kusafiri kwa umbali wa kilomita 9 hadi 12. 

RC Wangabo asifu kikundi cha kinamama kinachojishughulisha na ujenzi

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesifu kikundi cha kinamama wanaojishughulisha na kazi za ujenzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi alipotemnbelea maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya Nkomolo wilayani humo.

Amesema kuwa serikali itaendelea kutoa ajira kwa vikundi mbalimnbali kwa makundi yote ya wananwake na vijana wanaojishughulisha na ujenzi kutokana na kuwa na miradi mingi inayohitaji ujuzi wao na kuwaasa wanawake na vijana waige mfano huo ili waweze kujiwezesha kuliko kukaa vijiweni na kuendelea kuilaumu serikali.
Wakinamama wakijishughulisha na ujenzi wa kituo cha afya Nkomolo Wilayani Nkasi

“Nimependezwa na ujasiri wa hawa kina mama amabo sikutegemea kuwaona hapa, kwa namna wanavyofanya kazi nimefarijika sana, itabidi na wanawake wengine wanaokaa majumbani waige mfano wao kuliko kukaa tu na kusubiri kuletewa,” Alibainisha.

Ujenzi huo unaofanywa kwa mradi wa kuboresha vituo vya afya 172 nchini kwa fedha zilizotolewa na Wizara ya OR – TAMISEMI zilizochangwa na wadau wa maendeleo duniani wakiwemo benki ya dunia na wengineo.


Kwa upande wake mmoja wa wanawake hao Salome Sululu amethibitisha kuwa wamekuwa wakifaidika kwa kibarua hicho walichokipata na fedha wanazopatiwa kuwa zinawasaidia kujikimu katika familia na kuwawezesha kupata mitaji ya kujiendeleza kwenye kilimo na kusifu utaratibu wa serikali wa kuajiri vibarua wa maeneo husika bila ubaguzi. 

RC Wangabo atatua changamoto za mradi wa bwawa la Mfili - Nkasi

RC Wangabo atoa wito kwa wafanyabiashara nchini kununua mahindi Rukwa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa wito kwa wafanyabiashara wote nchini ambao wanahitaji mahindi kufika haraka katika mkoa wa Rukwa kununua zao hilo kwani kumekuwa na ziada ambayo wananchi wanahitaji kuuza lakini soko hakuna.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo

Amesema kuwa katika wilaya ya Nkasi pekee kuna zaidi ya tani 23,000 za chakula ambacho ni ziada ya wilaya na imekosa wanunuzi na kumuagiza katibu tawala wa Mkoa kuhakikisha anafanya mawasiliano na mikoa mingine ambayo ina upungufu wa chakula ili kuja kununua ziada hiyo ambayo wananchi wamekuwa wakilalamika kukosa soko.

Pia, amemuagiza katibu tawala wa Mkoa kuhakikisha kuwa kunakuwa na mratibu wa mahindi katika kila wilaya ili kuwasaidia wafanyabiashara wa mahindi kutoka nje ya mkoa kupata urahisi wa kununua mahindi na kuwaepusha na utapeli.

 “Tani zaidi ya 23,000 ipo kwenye wilaya moja tu, hii ni fursa kwa wafanyabiashara waliopo kwenye mikoa ambayo ina upungufu wa chakula kuja kununua mahindi na kuyapeleka huko wankoyahitaji, hivyo nakuagiza katibu tawala kuhakikisha kuwa unafanya mawasiliano na mikoa na ambayo ina upungufu pamoja na wafanyabishara wenye kuhitaji ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu lakini kuwe na mratibu wa kuweza kusimamia hili ili wafanyabiashara hao wasipate tabu,”

Ameyasema hayo baada ya kusomewa taarifa ya wilaya ya Nkasi iliyobainisha uwepo wa ziada ya tani 23,000 za mahindi kwaajili ya kuuza ambapo wakulima wa wilaya hiyo na kwengineko Mkoani humo wamekuwa wakilalamikia soko la zao hilo.


Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa wilaya ya Nkasi Mwanaisha Luhaga alipokuwa akisoma taarifa hiyo alisema kuwa changamoto kubwa inayowakabili hivi sasa ni upatikanaji wa mbolea kwa wananchi ambapo mpaka sasa wilaya imepokea tani 20 tu kati ya 850. 

RC Wangabo awashauri wakulima kuanzisha mpango wa chakula mashuleni.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wakulima kushirikiana na uongozi wa shule za msingi na sekondari Mkoani Rukwa kuanzisha utaratibu wa kuwalisha wananfunzi wanapokuwa mashuleni.

Amesema kuwa anafahamu kwamba Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa mikoa sita inayotegemewa kwa uzalishaji wa chakula nchini lakini haina utaratibu wa kuwalisha wananfunzi wanapokuwa mashuleni jambo linaloshusha ufaulu kwa wananfunzi hao.

“Tangu nimefika katika Mkoa huu wazee wananiambia hapa Rukwa kuna chakula cha kutosha, utakula kuanzia asubuhi hadi kesho yake asubuhi, namna chakula kilivyokuwa kingi lakini Je, humo mashuleni mwetu wanafunzi wanapewa chakula?” Aliuliza.

Ameyasema hayo alipokuwa akiongea na wazazi, walimu na wanafunzi katika shule ya Msingi kipili kata ya kipili, Wilayani Nkasi katika ziara yake ya kwanza tangu kuteuliwa na rais Dk. John Pombe Magufuli kuwa Mkuu wa Mkoa huo na lengo ikiwa ni kutembelea na kukagua miradi mabalimbali ya wilaya hiyo pamoja na kujitambulisha kwa wananchi. 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akizungumza na wananchi wa kijiji cha Paramawe, Wilayani Nkasi katika ziara yake ya kutembelea majengo kwaajili ya chuo cha ufundi VETA katika Wilaya hiyo.

Ameongeza kuwa wanafunzi wamekuwa wakitembea umbali mrefu kwenda shule huku matumbo yakiwa matupu na hatimae wanashindwa kuelewa wanachofundishwa darasani kwa kusikilizia njaa.


“Kuwa na chakula kingi haitakuwa na maana kama watoto wetu wanashinda njaa mashuleni.”

Maswali na majibu kwa RC Wangabo Kijiji cha Paramawe, Wilayani nkasi

Maendeleo yanaletwa kwa mshikamano wa Madiwani, DC na Halmashauri

RC Wangabo asisitiza Unyenyekevu, Uadilifu na Uwajibikaji kwa watumishi.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesisitiza Uwajibikaji, na kujituma kwa watumishi wote wa serikali mkoani humo ili kuweza kupeleka mbele gurudumu la maendeleo na kuwatumikia wananchi ambao wapo ili waweze kuhudumiwa na watumishi.

Amesema kuwa bila ya uadilifu katika matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinazotolewa na serikali katika halmashauri hakutakuwa na maendeleo lengwa jambo litakaoiingizia serikali hasara na kurudi nyuma kimaendeleo.

Ameyasisitiza hayo alipokutana na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi katika ziara yake ya siku mbili iliyolenga kutembelea miradi mbalimbali ya halmashauri pamoja na kujitambulisha kwa watumishi na makundi mbalimbali ya wananchi katika wilaya.

“Jambo ninalosisitiza la kwanza ni uwajibikaji, kila mtumishi wa serikali anatakiwa kuwajibika kufanya kazi kwa bidii na kujituma, kwani serikali hutoa pesa nyingi za miradi ya maendeleo hivyo tusipokuwa waadilifu na kufanya kazi kwa bidi rasilimali zetu tutazipoteza, tunataka thamani ya fedha ionekane huko kwenye utekelezaji wa miradi hiyo,” Alisisitiza.

Pamoja na hayo RC Wangabo amewataka watumishi hao kuwa wanyeyekevu wanapokuwa wanawahudumia wananchi na kutotumia vyeo vyao kuwanyanyasa wananchi hao kwani kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakiogopa kuingia kwenye ofisi za kiserikali ili kutatuliwa changamoto na matatizo yanayowakumba kutoka katika maeneo yao.


Amesema kwa kufanya hivyo kutaipa sifa serikali na pia kujiwekea akiba ya uaminifu kwa wananchi wanaopewa huduma hiyo. 

Saturday, November 11, 2017

RC Wangabo awasihi wazee kutokaa kimya pindi wanapoona wataalamu wanakwe...


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewasihi wazee wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kutokaa kimya pindi wanapoona wataalamu wa halmashauri hiyo wanakwenda tofauti na uhalisia wa mambo katika kutekeleza miradi mbalimbali ya halmashauri hiyo.

Amesema kuwa kumekuwa na miradi mingi inayokwama kwasababu ya wataalamu hao kushindwa kujua historia za sehemu husika na matokeo yake serikali inapoteza pesa nyingi kufanya marekebisho ya miradi hiyo pale panapotokea hitilafu inayogharimu halmashauri na maisha ya wananchi wanaotegemea ukamilifu wa miradi hiyo.

Ametoa kauli hiyo alipofanya kikao na umoja wa wazee wa halmashauri ya Nkasi katika ziara yake ya siku mbili kwenye halmashauri hiyo yenye lengo la kutembelea miradi na kujitambulisha kwa makundi mbalimbali ya wananchi.

“Mkiona mambo yanakwenda sivyo kwenye mradi mnajikusanya, Mwenyekiti na Katibu hapa mnakwenda kumuona mkurugenzi na kumshauri, hayo ndio maendeleo shirikishi na maendeleo shirikishi hayawabagui wazee, wazee nao wana neon lao katika maendeleo.” Alisisitiza.


Aidha aliwasisita kuendelea kudumisha maadili katika jamii ili kupunguza mimba kwa wananfunzi wa Wilaya ya Nkasi ambazo zinazoendelea kuzorotesha maendeleo ya wanafunzi wa kike na kuwaomba watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola pale inapotokea jambo hilo. Na kubainisha kuwa katika kipindi cha miezi 6 tangu kuanza kwa mwaka huu mimba 46 zimebainika.

“Marufuku kuuza mbolea tofauti na bei elekezi,” – RC Wangabo


1.       Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameagiza kukamatwa kwa wafanyabiashara wote wanaouza wanaouza pembejeo kwa zaidi ya bei elekezi iliyotolewa rasmi na serikali kwani kufanya hivyo ni kukiuka utaratibu uliowekwa na serikali kwaajili ya kuwanufaisha wakulima.

Amesema kuwa kumekuwa na baadhi ya maduka katika Manispaa ya Sumbawanga wanauza mbolea kwa bei isiyo halali na hivyo tayari ameshaagiza vyombo vya dola viwashughulikie watu hao haraka iwezekanavyo.

“Ni marufuku kwa wauzaji wa pembejeo kuuza mbolea kwa bei ambayo ni nje ya bei elekezi, msako mkali utafanyika kwa halmashauri zote kuhakikisha kuwa bei elekezi ndio inayotumika na kuwabaini wale wote wanaouza kinyume na bei hii elekezi,” Alisisitiza.

Ameongeza kuwa bei hizo zinatofautiana kati ya Halmashauri na Halmashauri na kwa Manispaa ya Sumbawanga bei elekezi kwa mbolea ya kupandia (DAP) ni shilingi 55,427 na ya kukuzia (Urea) ni 42,848. Halmashauri ya Nkasi mbolea ya kupandia (DAP) ni shilingi 55,961 na ya kukuzia (Urea) ni 43382. Halmashauri ya Kalambo mbolea ya kupandia (DAP) ni shilingi 57,022 na ya kukuzia (Urea) ni 44,443 na Sumbawanga Vijijini mbolea ya kupandia (DAP) ni shilingi 56,808 na ya kukuzia (Urea) ni 44229.

Mwanafunzi mwenye mimba, wazazi wote jela hadi muhusika ajulikane - RC W...


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza wakuu wa wilaya na wakuu wa shule Mkoani humo kumkamata na kuwaweka ndani wazazi na mwanafunzi yeyote wa kike atakayebainika kuwa na mimba hadi hapo watakapomtaja aliyesababisha mimba hiyo.

Amesema kuwa kumekuwa na tabia ya kumalizana kienyeji huko majumbani na matokea yake watuhumiwa hawafikishwi sehemu husika ili waweze uwajibishwa na hatimae kupunguza kasi hiyo ya mimba kwa wananfunzi.

“Mwalimu Mkuu unapogundua tu kwamba mwananfunzi ana mimba mweke pembeni ita wazazi wake, washirikishe polisi wawachukue wawekwe ndani kwa muda wa masaa 48, hadi hapo watakapomtaja muhusika wa mimba hiyo, ukifanya hivyo mara kadhaa mabadiliko yatatokea,” Amesisitiza

Ametoa agizo hilo baada ya kusomewa taarifa ya shule ya sekondari Kirando, Wilayani Nkasi wakati alipotembelea kukagua ujenzi wa maabara wa shule hiyo pamoja na na kuongea na wanafunzi, taarifa iliyobainisha kupatikana kwa mimba saba kwa kipindi cha Januari hadi oktoba mwaka huu na kesi zote zipo polisi.

Halikadhalika alitahadharisha kuwa shule yeyote atakayoitembelea katika ziara yake hiyo ya kujitambulisha katika Halmashauri nne za mkoa huo, ihakikishe inabainisha hatua zilizochukuliwa kwa watuhumiwa na zilipofikia na si kueleza tu idadi ya kesi na kuwepo kwa kesi hizo polisi.

 Kwa upande wake mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kirando Erneo Mgina amesema kuwa kati ya wanafunzi saba waliopata ujauzito wanafunzi watatu ni wa “A – Level” na wanne ni wa “O – Level” na kueleza kuwa wengi wao hupata mimba wakati wa likizo na huwabaini pale tu wanaporudi shule na kuwapima.


Wednesday, November 8, 2017

MAWAZIRI MSITOE MATAMKO YASIYOTEKELEZEKA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Mawaziri na Naibu Mawaziri wajiepushe na utoaji wa matamko yasiyotekelezeka ili kuepuka mikanganyiko Serikali.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Novemba 7, 2017) wakati akifungua Kikao Kazi cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina Mjini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema ni vema  viongozi hao kabla ya kutoa matamko wakajiridhisha iwapo jambo hilo halitaleta athari za kibajeti na kisera na kama lipo katika bajeti za wizara zao.

Pia amewataka viongozi hao wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya uongozi ili kuithibitishia jamii kuwa Rais Dkt. John Magufuli aliwateua kutokana na uadilifu na uwezo wao kiutendaji.

“Tunao wajibu mkubwa kuhakikisha kwamba kila mmoja wetu anafanya kazi kwa nguvu na bidii ili kutimiza matarajio ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli na wananchi wote kwa ujumla.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao wajiwekee utaratibu wa kusikiliza hoja na shida za Wabunge na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni.

Pia amewataka wafanye ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo inayohusu sekta zao kwa kuwa wao ni wasimamizi wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

Waziri Mkuu amesema Mawaziri na Naibu Mawaziri wanatakiwa wasimamie utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021. 

Pia wasimamie utekelezaji wa ahadi zote zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 pamoja na ahadi alizozitoa Rais Dkt. Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi.


 (mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATANO, NOVEMBA 08, 2017.

RC Wangabo amuagiza RPC awapumzishe DTO na Msaidizi wa RTO kupisha uchunguzi

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa George Kyando kuwaweka pembeni Mkuu wa Usalama barabarani wa Wilaya Inspector Suleiman Africanus pamoja na Msaidizi wa Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa Inspector Michael Mwakasungula ili kupisha uchunguzi kufuatia tuhuma kadhaa zilizoelekezwa dhidi yao.
Agizo hilo amelitoa wakati akijibu kero za madereva wa bajaji na bodaboda wapatao 4352 kwa mkoa mzima waliowakilishwa na wenzao wa mjini Sumbawanga baada ya kukutana nao na kusikiliza vilio vyao katika Mkutano uliofanyika katika Viwanja vya Nelson Mandela mjini Sumbawanga.
Madereva 13 walipata nafasi ya kumuelezea Mh. Wangabo kero wanazopata wakiwa barabarani huku miongoni mwa kero hizo ambazo ni pamoja na kupokea rushwa, uonevu usio wa lazima barabarani na kuwaweka mahabusu kwa visingizio mbalimbali zilielekezwa kwa maafisa hao wa usalama barabarani.

“Hawa wawili hawa na tuhuma mlizozitoa huenda zina ukweli, RPC nakuagiza nenda kazichunguze hizi tuhuma zote zilizotolewa hapa kwa kina na nyinyi muwe mashahidi kwenda polisi kutoa shuhuda zenu, halafu uchukue hatua stahiki, lakini wakati huo huo unapozichunguza hizi tuhuma wao uwaweke pembeni, uwape kazi nyingine,”

Amesema kuwa hakuna mtendaji wa serikali ambaye amepangiwa sehemu akae milele na milele na kuwa mtumishi asijidanyanye kwamba bila ya yeye kazi za serikali haziwezi kwenda huku akijitolea mfano kuwa yeye ni Mkuu wa Mkoa wa 15 tangu kuanzishwa kwa Mkoa huu mwaka 1974, wote walionitangulia wamepiga kazi wameondoka nae ataondoka.

Aidha, Mh. Wangabo amewasisitiza madereva hao kusomea sheria za barabarani na kupata leseni ilikupunguza ajali za barabarani katika Mkoa wa Rukwa huku akiwapongeza kwa takwimu zinzoonyesha kupungua kwa ajali hizi ukilinganisha na mwaka 2016.

Katika kulisisitiza hilo Mh. Wangabo alimualika mwalimu wa mafunzo ya usalama barabarani ili kutoa mafunzo hayo ya siku 3 bure kwa madereva hao kwa lengo la kutokuwa na ajali katika Mkoa wa Rukwa.huku akimpa miezi 7 kamanda wa polisi mkoa kuhakikisha bodaboda wote 4352 wanakuwa na leseni na vitambulisho.

Kwa upande wake kamanda wa polisi Mkoa ACP George Kyando ameeleza kuwa kwa ajali za bajaji na bodaboda mwaka 2016 kulikuwa na ajali 18 huku 11 zikisababisha vifo vya watu 20 wakati mwaka 2017 kuemtokea ajali 9 huku 5 zikisababisha vifo vya watu 7.
 Baadhi ya Bajaji zikiwa zimepaki katika uwanja ulipofanyikia Mkutano wa madereva wa Bajaji na Bodaboda na Mkuu wa Mkoa. 


Kamanda wa polisi Mkoa wa Rukwa ACP George Kyando akitoa elimu ya usalama barabarani na kujibu baadhi ya kero zilizotolewa na madereva wa Bodaboda na bajaji wa Manispaa ya Sumbawanga. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akizungumza na madereva wa Bodaboda na Bajaji wa Manispaa ya Sumbawanga katika uwanja wa Nelson Mandela.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akizungumza na madereva wa Bodaboda na Bajaji wa Manispaa ya Sumbawanga katika uwanja wa Nelson Mandela.


baadhi ya bodaboda zikiwa zimepaki uwanja wa Nelson Mandela Mjini Sumbawanga.


Yona Mwangoka ni mmoja wa madereva wa bodaboda aliyedai kuwa na ushahidi wa video unaoonyesha ukusanyaji wa shilingi 40,000 kuwapa polisi ili kuachiwa kwa makosa mbalimbali huku risiti zao zikionesha shilingi 30,000, fedha ambazo zilikusanywa na kiongozi wa boda boda baada ya boda boda hao kukamatwa kwa kosa la kumpiga askari wa usalama barabarani tukio lililotokea siku mbili kabla ya Mkutano huo. 

Sunday, November 5, 2017

“Malezi bora ndio chanzo cha Amani na utulivu katika jamii” – RC Wangabo


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameusisitiza umoja wa wazee mkoani Rukwa kuendelea kuhimiza malezi bora katika jamii ili kujiepusha na uvunjifu wa amani unaofanywa na vijana hao pindi wasiposimamiwa vizuri katika makuzi yao.

Amesema kuwa uhalifu mwingi unaoendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi hufanywa na kundi la vijana ambao wamekosa usimamizi bora wa malezi ya jamii katika makuzi yao na hatimae hujihusisha na matukio yanayopelekea kuitikisa amani ya mji ama mkoa.

“Uhalifu mwingi nchini hufanywa na kundi la vijana sijawahi kusikia uhalifu umefanywa na kundi la wazee hata siku moja na yote hayo ni kukosa malezi bora kutoka kwenu wazee, kama wazee mlilelewa vizuri kwanini na hawa watoto, au mmewashindwa?” Aliuliza.

RC Wangabo ameyasema hayo alipofanya kikao na umoja wa wazee wa mkoa wa Rukwa pamoja na viongozi wa dini kilichofanyika katika ikulu ndogo Mkoani humo na kuwaeleza mikakati aliyonayo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha amani na utulivu unaendelea kudumishwa katika mkoa.

Aidha, RC Wangabo amesisitiza kuwa vijana wamekuwa wakijifunza mambo mengi machafu kupitia simu za “smartphone” ikiwemo namna ya kufanya uhalifu na mambo yanayokwenda kinyume na maadili ya mtanzania.

Ameonya kuwa baadhi ya wazazi hutetea uovu wa watoto wao jambo linalowakatisha tamaa waalimu katika kujenga maadili ya wananfunzi ili kutengeneza viongozi bora katika jamii na kuongeza kuwa watoto wasio na maadili hushusha kasi ya ufaulu mashuleni.

RC Wangabo hakuacha kuwashauri wazee hao kuacha kujishughulisha na siasa za maandamano na badala yake wawe washauri wa vijana wanaotaka kuharibu amani ya nchi kupitia siasa


“Sidhani kama itakuwa ni heshima mzee umeshikwa ‘Tanganyika jeki’ na mtoto mdogo, huko ni kudhalilishwa, wazee mnatakiwa kuwa washauri wa hawa vijana wanaotumia siasa vibaya na matokeo yake kuharibu amani ya nchi,”

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa nasaha kwa wazee wa Mkoa wa Rukwa (hawapo pichani) wakati alipofanya nao kikao katika ikulu ndogo Mkoani humo na kuwaeleza mikakati aliyonayo katika kuhakikisha Mkoa unasonga mbele katika sekta zote za maendeleo.

Mzee Joseph Sangu akitoa neon la ukaribisho kwa niaba ya wazee wa Mkoa wa Rukwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (hayupo Pichani) katika kikao kilichofanyika Ikulu ndogo Mkoani Rukwa. 

Baadhi ya Viongozi wa Dini waliohudhuria kwenye kikao hicho kilichowahusisha wazee wa Mkoa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akisalimiana na Mzee Zeno Nkoswe mara baada ya kikao chake na wazee wa Mkoa wa Rukwa kilichofanyika katika Ikulu ndogo Mkoani humo. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akisalimiana na Kaimu mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Hamidu Masare muda mfupi baada ya kumaliza kiako na wazee wa Mkoa wa Rukwa.