Thursday, January 25, 2018

“Bila ya Ushirikiano kati ya TBA na SUMA JKT ofisi ya DC Kalambo haitakwisha kwa wakati” RC Wangabo

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewasisitiza msimamizi mshauri wa ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kalambo ambao ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kushirikiana na Mkandarasi SUMA JKT kuhakikisha wanamaliza jengo hilo kwa wakati.

Amesema kuwa Ujenzi huo ulisimama zaidi ya miezi minne ambao ulitakiwa kumalizika mwezi wa 5 na kwa uchelewaji huo utasababisha kumalizika mwezi wa 10 jambo ambalo sio matarajio ya serikali ya awamu ya tano kufanya kazi kwa kusuasua.

“TBA wahakikishe wanashirikiana vizuri na SUMA JKT ili kumaliza ujenzi huu na ili hili jengo liende kwa kasi tunayoitaka kila mwezi tutakuwa tunapita kuangalia maendeleo ya ujenzi huo, sijaamini kwamba TBA wameshindwa kuwasimamia SUMA JKT ninachotaka makubaliano yote ya pande mbili yaheshimiwe ili kazi ziende kusiwe na mjuzi zaidi ya mwenziwe, mwelekezane” Mh. Wangabo alibainisha.

Hayo yamejitokeza baada ya Mh. Wangabo kutembelea ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kalambo na kuona kusuasua kwa ujenzi huo na kuamua kuitisha kikao ili kujua sababu za kujitokeza kwa hali hiyo ambayo sio makubaliano na hakuna taarifa za kuridhisha juu ya maendeleo ya ujenzi huo.

Awali akitoa taarifa ya kusuasua kwa ujenzi huo Meneja wa Wakala wa Majengo Mkoa wa Rukwa Arch Deocles Alphonce amesema kuwa ujenzi huo ulitakiwa kumalizika tarehe 16/5/2018 lakini kutokana na sababu za hali ya hewa na mabadiliko ya ramani kutokana na jiografia ya eneo ndio iliyopelekea kuchelewa kwa ujenzi huo kumalizika kwa wakati.

Nao Suma JKT wakimshukuru Mh. Wangabo kwa kuwakutanisha makundi matatu, wao kama Mkandarasi, Mteja ambae ni ofisi ya Katibu Tawala mkoa pamoja na Msimamizi Mshauri (TBA) kuelekezana palipokwenda tofauti na hatimae kufikia muafaka na kuendelea na ujenzi huo wenye thamani ya Shilingi Milioni 289.Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa maelekezo kwa SUMA JKT na TBA kushirikian ili kumaliza jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kalmabo (nyuma yao)

Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kalambo 19.1.2018

WanaRukwa Wahimizwa kulima Kahawa ili kuwa zao mbadala la biashara.

Wakulima wa mkoa wa Rukwa wamehimizwa kuona namna ya kujiwekeza katika kilimo cha kahawa ili kupata zao mbadala la biashara kuliko kubaki katika zao moja la mahindi ambalo mara nyingine huwa na shida ya kupanda na kushuka kwa bei kusikotabirika.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachima Wangabo alipotembelea kikundi cha watu 56 cha wakulima wa zao hilo katika Kijiji cha Katuka, Kata ya Msanzi, Wilayani Kalambo ikiwa ni miongoni mwa kuwatia moyo wakulima hao wachache ili wawe mfano kwa wakulima wengine na kuwasihi kuanzisha ushirika ili kuweza kupata soko.

Mh. Wangabo amesema kuwa kuwa kahawa huvunwa kila mwaka na kupandwa mara moja na kufanyiwa marekebisho madogo madogo pamoja na kuweza kuchanganya na baadhi ya mazao mengine ndani ya shamba moja tofauti na zao la mahindi ambalo hupandwa kila mwaka na kuongeza kuwa Serikali imejipanga kufufua zao la kahawa kwa nguvu zote.

“Changamoto ya soko serikali imeitafutia ufumbuzi, soko la kahawa litapitia kwenye Ushirika na linaenda kuuzwa kwa njia ya mnada kama inavyofanyika katika zao la korosho, kwa hali hiyo hakutakuwa na changamoto kubwa inayotarajiwa kwa zao hilo, kinachotakiwa ni kuimarisha ushirika wa kahawa” Alisema na kuongeza kuwa kama Mkoa utakuwa na Chama kikuu cha Ushirika cha kahawa.

Akisoma risala mbele ya Mh. Wangabo, Mkuu wa Idara ya kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Nicholas Mlango amesema kuwa halmashauri imeandaa kozi kwaajili ya wakulima wa kahawa na wataalamu kuendelea kuwaelimisha wakulima juu ya kujiunga na mfuko wa kahawa wataochangia ili kukuza mfuko huo.


Nae mmoja wa wakulima waliotembelewa shamba lake alisema kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni kutokuwa na vifaa  na elimu ya kutosha kuweza kutunza mashamba hayo ya kahawa japo wana nia ya kuendeleza kilimo hicho jambo lililopelekea Mkurugenzi wa halmashauri hiyo James Ngagani kuahidi kuwapeleka wakulima 20 wa zao hilo katika mafunzo Wilayani Mbozi na kutoa miche 30,000 bure kwa wananchi wanaohitaji kulima zao hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiukagua mmea wa kahawa alipotembelea shamba la mmoja wa wakulima wachache wanaolima zao hilo katika kijiji cha Katuka, Kata ya Msanzi Wilayani kalambo. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo  akipata maelezo kutoka kwa Mkulima John Kapapalata aliyelima eka moja ya kahawa katika shamba lake ili kuona faida ya zao hilo huku akiendelea kulima mahindi. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo James Ngagani (wa kwanza kulia) juu ya kuwapatia mafunzo wakulima hao wa kahawa

Kahawa

“Halmashauri isiyopanda Miti Milioni 1.5 mwaka huu itatozwa faini,” RC Wangabo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameziagiza Halmashauri nne za Mkoa wa Rukwa kuhakikisha zinafikia lengo la kupanda miti milioni 1.5 kila moja hadi kufikia mwisho wa mwaka wa 2017/2018 ili kufikia lengo la Mkoa la kupanda miti milioni 6 katika kutekeleza sera ya kupanda miti kitaifa.

Amesema kuwa Halmashauri itakayoshindwa kufikia lengo itatakiwa kulipa faini ya shilingi Milioni 1 kuilipa Halmashauri itakayofika lengo ambapo Halmashauri Mshindi inategemewa kupata shilingi Milioni 3 na fedha hizo itapewa taasisi itakayopanda miti mingi kuliko taasisi nyingine ya serikali ndani ya Halmashauri iliyoshinda hasa mashule ili kuwafundisha wanafunzi umuhimu wa kupanda miti.

“Halmashauri ambayo haikufikia lengo imuume kutoa shilingi Milioni 1 kumlipa mwenzake, katika hizo Halmashauri 4, kwa maana mshindi atapata shilingi Milioni 3, lakini endapo Halmashauri zote zitafikia malengo nitazipa Halmashauri Shilingi Milioni 1, na hiyo fedha itakwenda kwenye taasisi iliyopanda miti mingi kuliko taasisi nyingine hasa mashule,” Mh. Wangabo alibainisha.

Ameongeza kuwa mwaka ujao wa 2018/2019 halmashauri itakayoshindwa kufikia lengo la kupanda miti Milioni 1.5 italipa faini ya shilingi Milioni 5 ili kila halmashauri iweze kufikia lengo na kutimiza maelekezo ya serikali na kuwaonya wote wenye tabia ya kuchoma misitu jambo linalokwamisha jitihada za kutunza mazingira.

Ameyasema hayo alipokuwa akizindua wiki ya kupanda miti  Kimkoa iliyofanyika katika katika Shule ya Sekondari Matai, Wilaya ya kalambo ambapo miti 100 ilipandwa katika uwanja uliopewa jina la Msitu wa Wangabo kama kuunga mkono juhudi za Mh. Joachim Wangabo katika kuhakikisha kuwa Mkoa wa Rukwa haubaki kuwa jangwa hasa kwa kilimo kinachotegemea mvua.

Nae akisoma risala Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura kabla ya kumkaribisha Mh. Wangabo alisema kuwa miongoni mwa mikakakti iliyowekwa na Wilaya hiyo ni kuhakikisha kila Kaya inapanda miti mitano na kuhakikisha kila shule inatenga eneo la kupanda miti ya matunda na mbao.
Pia alitumia nafasi hiyo kutoa takwimu za miti iliyopandwa na Wilaya hiyo, “kwa mwaka 2016/2017 miti 497,896 ilipandwa na kwa mwaka 2017/2018 mategemeo ya Wilaya ni kupanda miti Milioni 1.5 pamoja na changamoto za mifugo pamoja na wananchi kukosa hamasa ya kupanda miti tutahakikisha tunatoa elimu na kutenga bajeti kwaajili ya shughuli hiyo,” Alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule amesema kuwa mkakati wa Wilaya ni kuhakikisha kila mwanafunzi kwa shule za msingi na sekondari anapatiwa mti na uongozi wa shule autunze na ukivunwa asilimia 40 atapewa mwanafunzi na asilimia 60 itabaki shuleni.

Nazo taasisi mbalimbali za utunzaji wa mazingira wameahidi kushirikiana na Halmashauri katika kutoa elimu na kuwa na vijiji vya mfano ambavyo wanakijiji wanaweza kutoa ushuhuda juu ya elimu ya mti waliyoipata na faida mabazo zimepatikana kutokana na wingi wa miti watakayokuwa nayo katika vijiji.


 Kwa mwaka 2016/2017 Mkoa wa Rukwa ulipanda miti 2,489,296 ambayo ni sawa na asilimia 41.5 ya lengo na mwaka 2017/2018 hadi sasa Mkoa umepanda miti 2,173,649 ambayo ni sawa na asilimia 36.22. 

Mwenyekiti wa Tasisi ya REYO Abdallah Rubega (Flana Nyeupe) akitoa maelezo juu ya aina ya miti itakayopandwa katika msitu wa Wangabo kwa heshima ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa mazingira huku ameshikilia bango la kuhamasisha wananchi kuacha kuchoma moto misitu na kuendelea kutunza vyanzo vya maji. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akipanda mti ishara ya kufungua upandaji miti Mkoani Rukwa iuli kufikia lengo la mkoa la kupanda miti milioni 6, Maadhimisho yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Matai, Wilayani kalambo. 

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule (kulia) akisaidiana na baadhi ya wananfunzi wa Shule ya Sekondari Matai kupanda miti ikiwa ni juhudi za kuwaelimisha wananfunzi umuhimu wa kupanda miti. 

Mmoja wa Wananfunzi wa Shule ya Sekondari Matai, Joseph Katepa akiwa amepumua baada ya kupanda miti kadhaa katika eneo lililoandaliwa maalum kwa kupanda miti katika shule hiyo.

Wanafunzi mbalimbali wakiendelea kupanda miti  katika eneo lililoandaliwa maalum kwa kupanda miti katika shule hiyo. 

RC Wangabo atoa miezi mitatu kwa wavuvi kuhama kambi kuepuka kipindupindu.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa miezi mitatu kwa wananchi wanaoishi katika kambi ya uvuvi ya Nankanga iliyopo kando ya ziwa Rukwa kuhama kwa hiyari baada ya kambi hiyo kuwa katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kipindupindu kwa kutokuwa na vyoo.

Mh. Wangabo amesema kuwa kuondoka huko kwa hiari kuwepo ndani ya mwezi huu wa kwanza hadi wa nne baada ya kuona wingi wa wananchi wanaoishi katika kambi hiyo pamoja na kutokuwepo kwa kipindupindu kwa wakati huu ila zoezi hilo ni la tahadhari ili kujikinga na ugonjwa huo.

“Hatuwezi kuendelea kuishi mahali hapa ambapo vyoo vyenyewe vinaingiliana na maji ya kunywa, na ili kisije hapa kipindupindu ni lazima watu wasifanye shughuli kwenye ziwa ili kuwe salama, lakini mkiruhusu kipindupindu kuingia hapa tutawafurusha, tena tutawasimamia kweli kweli, tutawapiga quarantine (kuwaweka kwenye kizuizi) mkipona tutawaswaga,” Amesisitiza

Ameyasema hayo alipofanya ziara kwenye kambi ya Nankanga iliyopo katika Kijiji cha Solola Wilayani Sumbawanga ili kujionea hali halisi ya maisha ya wavuvi katika kambi zisizo rasmi na namna ya kuweka mpango salama wa kuweza kuwaepusha na ugonjwa wa kipindupindu ulioenea katika makambi hayo yanayozunguka ziwa Rukwa. 

Nae Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule alitoa hadi tarehe 1/5/2018 wananchi hao wawe wameyahama makazi hayo na kujisogeza kwenye vitongoji vya jirani huku akiwasihi viongozi wa vijiji na vitongoji hivyo kushirikiana kuhakikisha wanatoa maeneo kwaajili ya wananchi hao kuhamia.

“Kuanzia tarehe 1 mwezi wa 5 hapa hatutaki kumuona mtu, kama una kibanda chako ama bati lako anza sasa hivi kwa kushirikiana na mwenyekiti wa Kijiji na Mtendaji wa Kata mtafute nafasi katika kitongoji cha Isanga kila mtu ajenge nyumba,” Alisisitiza.


Hatua hiyo imekuja baada ya ugonjwa wa kipindupindu kusambaa kwenye kambi kadhaa za wavuvi pembezoni mwa ziwa rukwa na kusababisha watu 210 kuumwa ugonjwa huo na watu nane kupoteza maisha, ambapo hadi sasa kambi zisizo rasmi zaidi ya tisa zimefungwa huku zoezi hilo likitegemewa kuendelea hadi hapo Mwezi wa tano. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa kwanza mbele kulia) akiwa ameambatana na mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule walipotembelea kambi ya mererani waliyohamishwa wavuvi kwa nguvu ili kuepuka kipindupindu na kulinda mazingira ya ziwa hilo. 

Moja ya kibanda cha kilichokuwa katika kambi ya Wavuvi ya Mererani kikiwaka moto ikiwa ni juhudi za kuwaondoa wavuvi waliopo ndani ya Ziwa Rukwa kuwaepusha na kipindupindu na kulinda ziwa lisipotee. 


Miongoni mwa wananchi waliokuwa wakiishi katika makambi ya wavuvi yalipo ndani ya Ziwa Rukwa yaliyoathiriwa na kipindupindu wakisimamiwa kuhama kambi hiyo ili kujiepusha na kipindupindu na kuliza Ziwa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa tahadhari kwa Wavuvi waliohamishwa kwenye makambi (hawapo pichani) kutorudi katika makambi hayo kwa usalama wa afya zao na kuendelea kulitunza ziwa Rukwa. 


Miongoni mwa Vyoo vinavyotumiwa na Wavuvi wa kambi ya Nankanga waliopewa miezi mitatu kuihama kambi hiyo kabla ya kipindupindu kuwamaliza. 

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alipoongozana na kamati ya ulinzi na Usalama kuangalia moja ya choo kinachotumiwa na wavuvi wa kambi ya Nankanga, choo ambacho si salama kwa matumizi ya binadamu. 

Wavuvi waaswa kulima pindi Ziwa Rukwa linapofungwa Januari hadi April Kila Mwaka.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaasa wavuvi wanaozunguka ziwa Rukwa kuhakikisha wanatafuta ardhi kwaajili ya kilimo, biashara pamoja na ufugaji katika kipindi cha kunzia mwezi wa kwanza hadi wanne kila mwaka ili kuwaacha samaki wa ziwa hilo kuzaliana.

Amewaasa kutotegemea shughuli moja tu kwaajili ya kuwaingizia kipato, “Wavuvi msitegemee kuvua tu, jishughulisheni na kazi nyingine za kuwaingizia kipato kama vile kilimo, biashara pamoja na ufugaji, hatufungi kambi hizi kwaajili ya kipindupindu tu lakini pia ili kuweza kuwaacha samaki wazaliane katika kipindi cha kuanzia mwezi wa kwanza hadi wanne,”

Ameyasema hayo alipofanya ziara kwenye kambi ya Nankanga iliyopo katika Kijiji cha Solola Wilayani Sumbawanga ili kujionea hali halisi ya maisha ya wavuvi katika kambi zisizo rasmi na namna ya kuweka mpango salama wa kuweza kuwaepusha na ugonjwa wa kipindupindu ulioenea katika makambi hayo yanayozunguka ziwa Rukwa. 

Tangu ugonjwa huo uingie Mkoani Rukwa tarehe 15/11/2017 tayari watu 210 wanaugua ugonjwa huo na watu nane wamepoteza maisha wote wakiwa wanatokea katika makambi hayo yasiyo rasmi ambapo hadi sasa kambi zisizo rasmi zaidi ya tisa zimefungwa huku zoezi hilo likitegemewa kuendelea hadi hapo Mwezi wa tano.


Nae Diwani wa kata ya Nankanga kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule amesema kuwa katika kambi hiyo kuna watoto 270 walio na umri chini ya miaka 7 ambao wamekosa kwenda shule na hivyo wananchi kujenga madarasa mawili ya shule shikizi katika kitongoji kilichopo Km 9 kutoka kwenye kambi hiyo yaliyofikia usawa wa linta na kumuomba Mkuu wa Mkoa kuwaunga Mkono jambo lililompelekea Mh. Wangabo kutoa bati 50 na kuitaka Halmashauri kuongezea bati 50 ili kukamilisha ujenzi huo. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo

RC Wangabo aitaka idara ya Kilimo kujipanga kitakwimu baada ya upungufu wa mbolea kushtusha.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza Katibu tawala wa Mkoa Bernard Makali kuitisha kikao maalum cha wataalamu wa kilimo kutoka katika Halmashauri zote Mkoani humo ili kubaini mahitaji sahihi ya mbolea kwa manufaa ya sasa nay a baadaye.

Amesema kuwa wataalamu wanaelewa kiasi cha mbolea inayohitajika kulingana na hekta za zilizopo katika Mkoa kwa kukokotoa hesabu na kupata jibu sahihi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo ili takwimu hizo zifanane.

“Katibu Tawala itisha kikao cha wataalamu wote wa kilimo kutoka katika Halmashauri zote, mkae mtafakari na kuja na takwimu sahihi, takwimu zikitupotosha tunapotea wote hata serikali inapotea kwasababu tunaweza kuagiza kiasi kikubwa mno na kupoteza pesa nyingi kumbe mahitaji ni kidogo, na ndio maana kunakuwa na sense hata za watu ili watu wapange mambo yao vizuri, kwenye Kilimo kuna lega leg asana,” Ameeleza.

Amesema kuwa walio wengi wanafanya kazi kwa ubabaishaji ambao unaonekana kwenye takwimu ambapo hapo awali ilionekana kuwepo na uhitaji wa tani 97,000 tofauti na takwimu zilizopo sasa zinaonyesha kuwepo kwa uhitaji wa tani 27,000 ambapo kati ya hizo tani 11,000 tayari zimepatikana ikiwa tani 5,000 za UREA na tani 6,000 za DAP jambo mabalo haliendani na uhalisia maana uhitaji wa mbolea kwa sasa sio mkubwa baada ya tani hizo kufika kulinganisha na tani tunazozisubiri.

Katika kuhakikisha idara hiyo inafanya kazi yake kwa ufanisi Mh. Wangabo amesema kuwa aliyekuwa akikaimu ukuu wa Idara hiyo katika ofisi yake amewekwa pembeni na kumpisha kaimu mwingine kwa malengo ya kuiboresha idara hiyo.

Amesema kuwa ikiwa ni miongoni mwa Mkoa unaotegemewa kwa uzalishaji wa chakula nchini haipendezi kwa idara hiyo kutokuwa na mpango sahihi wa maandalizi ya kilimo tangu kumalizika kwa msimu wa kilimo wa 2016/2017 hadi kuingia msimu wa kilimo wa 2017/2018 na kuiagiza idara hiyo kuwa karibu na waagizaji wakubwa wa mbolea kila ukikaribia msimu wa matayarisho ya mashamba kwa wakulima ili kujua kiasi cha mbolea kinachohitajika.

Ameyasema hayo katika kikao cha majumuisho ya ziara yake fupi ya kutembelea maghala ya wafanyabiashara wakubwa wa mbolea ya mjini sumbawanga ili kujionea changamoto na mafanikio yaliyofikiwa baada ya juhudi za serikali kuhakikisha kuwa Mkoa wa Rukwa unapata mbolea ya kutosha ili wakulima waweze kufikisha lengo la uzalishaji wa chakula katika Mkoa.

Kwa msimu wa 2016/2017 Mkoa wa Rukwa ulilima Hekta zipatazo 556,975.9 na kuvuna tani 1,109,055.6 za mazao ya chakula kati ya hizo mahindi yalikuwa tani 710,602. Kwa msimu huu wa Kilimo wa 2017/18 Mkoa umelenga kulima jumla ya eneo la Hekta 554,310.6 na kuvuna tani 1,669,746.2 za mazao ya chakula.
Wednesday, January 24, 2018

Wakulima na Wasambazaji mbolea Rukwa Waridhishwa na upatikanaji wa mbolea hadi vijijini.

Wafanyabiashara wakubwa wa mbolea Mkoani Rukwa pamoja na wakulima wameridhishwa na upatikanaji wa mbolea na kusifu juhudi za serikali baada ya kupaza sauti zao na kusikika na Rais Dk. John Pombe Magufuli na jambo hilo kufanyiwa kazi ndani ya muda mfupi.

Wafanyabiashara hao wamesema kuwa wakulima hivi sasa hawapangi tena foleni kusubiri mbolea iliyokuwa ikipatikana kwa taabu na kwa kunyang’anyiana na kuwa foleni hizo zimekwisha na wakulima hawana haja ya kutoka Kijiji kuja mjini kufuata mbolea kwani mbolea hizo zinawafuata huko waliko hasa baada ya marekebisho ya bei elekezi iliyotolewa na Uongozi wa mkoa wa Rukwa chini ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.

Mmoja wa Wafanyabiashara hao wakubwa Mohamed Rashid Mdangwa wa Kampuni ya ETG amesema “Sasa wakulima wameanza kupata mbolea kwa wingi, mwanzo walikuwa wanapanga foleni hapa lakini kuanzia ile Jumatatu agizo la Rais kuwa mbolea iende Mkoa wa Rukwa, sasa hivi population (wingi) ya watu imepungua sana,  sasa hivi mahitaji ya mbolea sio makubwa sana kama miezi miwili iliyopita,na mbolea ipo nyingi njiani inakuja, na bei elekezi aliyoitoa Mkuu wa Mkoa imesaidia mbolea kufika vijijini kupitia wakala wadogo wa mbolea.”

Yamewsemwa hayo baada ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kupitia maghala makubwa ya mbolea yaliyopo Sumbawanga Mjini pamoja na baadhi ya wasambazaji wadogo ili kujionea upatikanaji wa mbolea hizo tangu kutolewa kwa agizo la Rais Dk. John Pombe Magufuli la kusambaza mbolea hizo katika Mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini tarehe 8.1.2018.

Mh. Wangabo aliwasihi wasambazaji wadogo wa mbolea kuendelea kujitokeza na kununua mbolea hiyo ambayo bei iliyopo sasa imezingatia maoni yao na haiumizi, hivyo kufanya hima kuhakikisha kuwa mkulima hakosi mbolea ili kuweza kubaki katika lengo la kuzalisha chakula kwa wingi na kuleta ushindani na mikoa mingine inayozalisha chakula.

“Mimi nitoe wito tu kwa wale Agrodealers (wasambazaji wadogo wa mbolea) wafike kuendelea kununua mbolea, hata bei tumekwishazifikiria tena upya, kila Halmashauri katika Wilaya wamekwisha kaa na kutoa mapendekezo yao halisi ya kiusafirishaji, kwahiyo wafike wanunue mbolea na kutakuwa na faida, bei imezingatia hadi miundombinu iliyoharibika hakutakuwa na usumbufu,” Mh. Wangabo alifafanua.

Mh. Wangabo alitembelea maghala matatu ya wafanyabiashara wakubwa waliopo mjini sumbawanga, TFC pamoja na maduka ya wasambazaji wadogo matatu na kuongea na baadhi ya wakulima ili kujithibitishia upatikanaji wa mbolea hiyo kwa maeneo ya mjini na inayopelekwa vijijini.


Kwa msimu wa 2016/2017 Mkoa wa Rukwa ulilima Hekta zipatazo 556,975.9 na kuvuna tani 1,109,055.6 za mazao ya chakula kati ya hizo mahindi yalikuwa tani 710,602. Kwa msimu huu wa Kilimo wa 2017/18 Mkoa umelenga kulima jumla ya eneo la Hekta 554,310.6 na kuvuna tani 1,669,746.2 za mazao ya chakula.

Mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa, Kamanda wa Zimamoto Mkoani Rukwa akikagua mbolea katika ghala la Kampuni ya Mbolea ya Taifa (TFC) lililopo Sumbawanga Mjini.

 Mmoja wa Wasambazaji wakubwa wa mbolea Mkoa wa Rukwa Mohamed Mdanga (Kulia) akitoa maelezo ya upatikanaji wa mbolea Mkoani humo mbele ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo(kushoto) alipokwenda kumtembelea kwenye ghala lake na kukuta mbolea zai ya tani 300.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa mbele wa kwanza kushoto)alipokuwa akipita mtaa kwa mtaa katika mji wa Sumbawanga kujionea biashara ya mbolea inavyokwenda katika maduka ya mbolea (hayapo pichani) huku akiwa ameambatana na Meya wa manispaa ya Sumbawanga Mh. Justin Malisawa (koti la Draft).

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili kutoka kulia) akiwa amesimama mbele ya duka la mbolea kuulizia upatikanaji wa bidhaa hiyo katikati ya mji wa sumbawanga, Mkoani Rukwa.

Timu ya wataalamu wa Kilimo, Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na Viongozi wa Manispaa ya Sumbawanga,  wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kupita duka hadi duka kujionea upatikanaji wa mbolea katika mkoa wa Rukwa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akivuka daraja baada ya kutoka kutembelea ghala la mbolea (nyuma rangi ya kijani) na kujiridhisha juu ya upatikanaji wa mbolea katika mkoa wa Rukwa, Wilaya zake na Vijiji kwa Ujumla.

Thursday, January 11, 2018

RC Wangabo atoa mwezi mmoja kuwa na mkakati wa kuzuia uvuvi haramu kuokoa viwanda vya samaki mwambao wa Ziwa Tanganyika

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kalambo pamoja na kamati yake ya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kukaa pamoja na kuandaa mkakati wa kuzui uvuvi haramu unaoendelea katika mwambao wa ziwa Tanganyika ili kuokoa viwanda vilivyopo katika mwambao huo.

Amesema kuwa uvuvi haramu unaoendelea katika mwambao huo unahatarisha maendeleo ya viwanda vya samaki vilivyopo na hatimae kudhoofisha ajira za wananchi waliopo karibu na viwanda hivyo na hatimae kurudisha nyuma juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kuibua na kuimarisha viwanda vilivyopo.

“Mwisho wa mwezi huu nataka taarifa ya namna mlivyojipanga kupiga marufuku uvuvi haramu ikiwa ni pamoja na kutoa elimu na kuwakamata wale wanaokaidi na kuendesha uvuvi haramu, uvuvi haramu ukiendelea hiki kiwanda hakitakuwepo, kwasababu ya kuua samaki na watoto wake, achene uvuvi haramu, mnamaliza samaki katika ziwaletu hili,” RC Wangabo Alisisitiza

Ameongeza kuwa samaki ndio rasilimali pekee inayowaajiri pamoja na kuendesha kiwanda na kuwataka wananchi kuungana pamoja kuhakikisha wanatunza rasilimali hiyo, na kupiga marufuku aina zote za uvuvi haramu na kuonya kutosikia kiwanda kimefungwa kutokana na kukosa samaki amabao wamekwisha kwasababu ya uvuvi haramu.

Ameyasema hayo alipotembelea viwanda viwili vya samaki vya Mikebuka Fisheris Tanzania Limited pamoja na Akwa Fisheries Tanzania Limited vilivyopo katika kata ya Kasanga ambapo kiwanda pekee kinachojikongoja ni Mikebuka fisheries huku AkwaFisheries kikiwa kimesimamisha uzalishaji.

Awali alipokuwa akisoma taarifa ya Kiwanda cha Mikebuka Fisheries Tanzania Limited Mtendaji wa Kijiji cha Muzi Gasper Kateka amesema kuwa mbali na ukosefu wa samaki ametaja kuwa changamoto nyingine ni Umeme na barabara jambo linalowafanya kutumia gharama kubwa kendesha kiwanda hicho kwa majenereta na kupakia samaki kwenye boti hadi bandari ya kasanga ili kuweza kuwasafirisha kwenda Sumbawanga kukwepa kipande cha barabara cha Km 1.2 kilichojaa mawe.

“Mikebuka Fisheries in maeneo mawili ya kuchakata samaki ikiwa Sumbawanga yenye uwezo wa kilo 8000 kwa siku na kasanga yenye uwezo wa kilo 15000 kwa siku lakini kutokana na uhaba wa samaki uwezo umeshuka na kuchakata kilo 3000 hadi 4000 kwa siku na kuajiri watu 30 na vibarua 55,” Kateka alieleza.

Kwa upande wake Afisa uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Godfrey Makoki alitoa ufafanuzi wa makubaliano ya matumizi ya ziwa Tanganyika yaliyofanya na nchi nne (Zambia, Burundi, Tanzania na DR Congo) katika kikao kilichofanyika 18/10/2012 Mjini Bujumbura katika kanuni ya nne ya makubaliano hayo imekataza uvuvi wa dagaa mchana katika ziwa Tanganyika.

“jambo linalotupa shida ni uvuvi wa kuvua dagaa mchana, kitaalamu dagaa huwa wanakuja kutaga mchana hivyo wanakuwa wakubwa kwasababu wana mayai na usiku huwaoni, sasa huwa tunawaambia kuwa huo ni uvuvi haramu hapo inakuwa ni tatizo,” Makoki Alibainisha.

Katika Kutatua tatizo la Umeme na Barabara Mh. Wangabo amemuagiza Meneja wa Tanesco Mkoa wa Rukwa kuhakikisha umeme wa REA awamu ya tatu unawafika haraka katika Kijiji hicho kwani kipo kwenye mkakati na kuwaagiza TARURA na TANROAD kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha ndani ya miezi mitatu wanairekebisha barabara ya Km 1.2 ili iweze kupitika.

Mwambao wa Ziwa Tanganyika kwa Mkoa wa Rukwa una Viwanda Vinne vya Samaki, Viwili vipo Kata ya Kipili, Wilaya ya Nkasi na Viwili vipo Kata ya Kasanga, Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi wa Mikebuka Fisheries Tanzania Ltd Azim Premji muda mfupi baada ya kuwasili katika kiwanda hicho.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa tatu kutoka kulia) akipewa maelezo na Mkurugenzi wa Mikebuka Fisheries Tanzania Ltd Azim Premji (wa pili kutoka kulia) katika kiwanda cha Mikebuka Fesheries Tanzania Ltd.

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akipiga marufuku uvuvi haramu katika ziwa Tanganyika ili kuokoa viwanda vilivyopo katika mwambao wa Ziwa hilo, (kushoto aliyekaa) Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura. 

Kiwanda cha Akwa Fisheries Tanzania Ltd. kilichosimamisha uzalishaji.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (Katikati) akitoa maelekezo kwa Meneja wa Tanesco Mkoa wa Rukwa Mhandisi Herini Mhina (Kulia) na (Kushoto) Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Juleth Binyura.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa tatu kushoto) akipokea maelezo kutoka kwa Mhandisi Mshauri Martin Hossey (wa pili kushoto) kuotoka Kampuni ya Nicholas O'Dwyer inayosimamia ujenzi wa Barabara ya Sumbawanga - Matai - Kasanga yenye urefu wa Km 112 ya thamani ya Bilioni 133 iliyomalizika kwa kiwango cha Km 71.5. 
Monday, January 8, 2018

RC Wangabo apiga marufuku mwalo wa Kirando kutumika kama bandari

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amepiga marufuku mwalo wa mwambao wa Kijiji cha Kirando kutumika kama bandari baada ya kufika katika mwalo huo na kukuta lori likiwa linapakua mizigo kwa lengo la kusafisirisha mizigo kwenda kwenye visiwa vya ziwa Tanganyika.

Amesema kuwa wananchi wasipotoshe malengo ya mwalo huo ambayo ni kwaajili ya kuuza na kununua samaki wavuliwao kwenye ziwa Tanganyika, “Lengo la Mwalo huu ni kuuzia samaki na dagaa lakini naona mizigo hii, imegeuzwa kuwa bandari, narudia aliyoyasema Mh. Mbunge (Ali Kessy) irudishwe kwenye hali yake ile ile,” Alisisitiza

Mh. Wangabo aliongeza kuwa kama sehemu iliyokuwa ikitumika kama bandari hapako vizuri basi waone namna ya kupaboresha ili sehemu hiyo ilirudi kama ilivyokuwa na sio kuikimbia na kuiacha kama ilivyo na kusisitiza kuwa kukimbia tatizo sio suluhisho bali kupambana na changamoto zilizopo.

Awali kabla ya Kukaribishwa Mkuu wa Mkoa, Mbunge wa Nkasi Kaskazini Mh. Ali Kessy alikemea kitendo cha wananchi hao wa Kirando kutumia mwalo huo kama bandari jambo ambalo ni kinyume na sheria na kuwasisitiza kuacha tabia hiyo mara moja.

“Nawaomba ndugu zangu kuanzia sasa hii sehemu isitumike kama bandari, hii sio bandari na haipo chini ya TPA, bandari ni ile ya zamani na iendelee kutumika ile ile na hapa tuwaachie wavuvi,” Mh. Kessy alimalizia.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda aliwasisitiza wanaotumia vyombo vya ziwani kwa usafiri kuzingatia kuvaa maboya na kuonya kutozidisha mizigo na kuwa na abiria wengi kueleza kuwa watumiaji wa vyombo hivyo ndio wawe wa kwanza kutoa taarifa endapo wataona taratibu hizo zinakiukwa kwakuwa wasafirishaji hao huangalia faida kuliko usalama wa maisha ya abiria. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa mbele) alipotembelea mwalo wa mwambao wa ziwa Tanganyika katika Kijiji cha Kirando.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiongea na baadhi ya watumiaji wa vyombo vya maji katika mwalo wa Kijiji cha Kirando


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa kwanza kushoto) akizungumza na baadhi ya abiria wa kisiwa cha Mvuna wanaosubiri usafiri wa boti kurudi makwao wakati alipotembelea kuona maendeleo ya mwalo huo unaotumika kama bandari katika kijiji cha Kirando Wilayani Nkasi, akiwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mh. Said Mtanda (aliyevaa bluu)

Baadhi ya mizigo iliyoteremshwa kutoka kwenye lori tayari kwaajili ya kusafirishwa kupelekwa kwenye visiwa vya ziwa Tanganyika kwa kutumia mwalo wa Kirando. 


Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda akitoa maelekezo kwa watumiaji wa Mwalo wa Kijiji cha Kirando kilichopo mwambao wa Ziwa tanganyika juu ya kuzingatia sheria za matumizi ya mwalo huo.


 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiwaasa watumiaji wa mwalo wa Kirando kuacha kuutumia mwalo huo kama bandari na badala yake waiboreshe bandari iliyopo ambayo inatambulika na Mamlaka ya Bandari Tanzania.

Wingi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kupelekea kuanzishwa kwa shule m...


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameishauri
Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kuona namna ya kuanzisha shule mpya ili kuleta
uwiano wa waalimu katika shule hizo unaoendana na idadi ya wanafunzi ambao wanatarajiwa
kuongezeka kila mwaka mpya wa masomo.

Ameyasema hayo aliposhiriki kwenye songambele ya ujenzi wa madarasa
nane ya Shule ya Sekondari Kirando yanayotarajiwa kutumiwa na wanafunzi 422
waliofaulu kuingia kidato cha kwanza kwa mwaka 2018 katika shule hiyo inayobeba
wanafunzi kutoka katika kata mbili zilizopo wilayani Nkasi.

“tunapoangalia kutatua changamoto ya shule hii ya Kirando
Sekondari tuangalie ufumbuzi wa kudumu zaidi, muangalie uwezekano wa kujenga
shule nyingine, huo ndio utakuwa ufumbuzi, shule hii ina O – level na A –
level, sasa kama kutakuwa na shule nyingine ya O – level peke yake na hii mkaipunguzia
mzigo wa kuchukua wanafunzi wengi na walimu wengi katika shule moja”

Ametoa rai kuwa kwa eneo la ekari 60 linalomilikiwa na shule
hiyo ya Sekondari Kirando inawezekana kugawa walau ekari 20 kwa shule hiyo mpya
jambo litakalowapelekea kupewa waalimu wapya kwa shule mpya na kuleta uwiano wa
waalimu kuliko hali ilivyo sasa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda aliyapokea
maagizo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi kuanzia ngazi ya Kijiji hadi ngazi ya
halmashauri ya Wilaya na kuongeza kuwa suala hilo litawekwa katika bajeti ya
mwaka 2018/2019 na kuongeza kuwa wananfunzi wote waliofaulu kuingia kidato cha
kwanza watasioma.

“wanafunzi waliofaulu kuingia kidato cha kwanza katika shule
hii ya Kirando ni 422 na tumekubaliana kuwa hadi kufungua shule wananfunzi wote
hao wanatakiwa wawe madarasani, lakini tumekubaliana na wazazi kuwa kama
serikali tutanunua meza zote 422, lakini tumewahamasisha kuchangia walau
mchango wa kiti ili mwanafunzi anapokuja akute meza na kiti ili tulimalize
jambo hilo,”
Awali Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari kirando Erneo Mgina
akitoa taarifa fupi ya shule hiyo alisema kuwa shule ina wanafunzi 677 na
kutaraji kupokea wanafunzi 422 na upungufu wa madara nane ambayo matatu tayari
na mengine yapo katika hatua ya msingi na kutaraji kurekebisha vyumba vitatu
vya maabara ili kuwahifadhi wanafunzi kwa muda hadi madarasa yatakapokamilika.Hili limekuja ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Nchi
OR – TAMISEMI kuitaka mikoa iliyokuwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliochaguliwa
kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2018 ukiwemo mkoa wa Rukwa kuhakikisha
kuwa wanafunzi wote wanapata madarasa ya kusomea, madawati na vyoo pale shule
zitakapofunguliwa tarehe 8/1/2018.

Friday, January 5, 2018

RC Wangabo aziagiza kamati za ulinzi na Usalama kusimamia usambazaji wa pembejeo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amezitaka kamati za ulinzi na usalama ngazi ya Mkoa kushirikiana na za Wilaya kusimamia usambazaji wa mbolea ili kufikia malengo ya kuzalisha chakula kwa wingi katika mkoa baada ya kutokea upungufu wa mbolea za kupandia (DAP) na za kukuzia (UREA) katika Mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo

Ameagiza hayo katika kikao cha kutafuta suluhisho la upatikanaji wa mbolea Mkoani Rukwa baada ya taarifa za upatikanaji wa mbolea hizo kutoridhisha hasa katika kipindi hiki cha msimu wa kilimo ambapo asilimia 80 ya wananchi wa Mkoa wa Rukwa wanategemea kilimo kujipatia kipato cha kujiendesha Kimaisha.
Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya kilimo ilichukua hatua za makusudi kubadili mfumo wa ruzuku uliokuwa ukiwafaidisha wakulima wachache kupitia vocha za pembejeo na hatimae kupitia mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) iliweka mfumo wa uuzaji na usambazaji wa mbolea kwa uagizaji wa pamoja na kutoa bei elekezi kwa kila Halmashauri.
Ameongeza kuwa hali ya upatikanaji wa mbolea Mkoani Rukwa si ya kurudhisha na kubainisha kuwa hadi kufikia tarehe 3/1/2018 Mkoa umepokea mbolea ya kupandia (DAP) tani 3,746.6 kati ya tani 47,869 upungufu ni tani 44,122.9 na mbolea ya kukuzia (UREA) tani 2,599.6 kati ya mahitaji ya tani 49,669 na kuwa na upungufu wa tani 47,069.4.
“Ndugu zangu hivi sasa tuko vitani, na adui yetu ni upatikanaji wa pembejeo, kwahiyo hapa Mkoa mzima tuungane tuwe kitu kimoja, tulidhibiti hili jambo, haya ni maagizo mbolea yoyote inayokuja hapa katika ngazi ya Mkoa, kamati ya ulinzi na usalama lazima isimamie, sio suala la Sekretariet hya Mkoa peke yake, lazima tujue kama mbolea hiyo imefika ama la,” RC Wangabo alisisitiza.
Aidha amewataka mawakala wa mbolea Mkoani humo kuhakikisha wanaagiza mbolea ya kutosha kutoka nje ya mkoa ili wasambazaji wadogowadogo waweze kuisambaza mbolea hiyo katika vijiji vya halmashauri zote nne za Mkoa wa Rukwa.
Akiwawakilisha mawakala wa usambazaji wa mbolea mkoani humo Mmiliki wa Kampuni ya usambazaji Ikuwo General Enterprises Sadrick Malila amesema kuwa upungufu mkubwa uliopo ni upatikanaji wa mbolea ya kukuzia (UREA) na sio mbolea ya kupandia (DAP) ambayo mpaka sasa ana tani 200 katika ghala lake peke yake, na kuiomba serikali kuongeza shilingi 1000 katika bei elekezi ili kufidia usafirishaji wa mbolea hizo.
Mmoja wa Wakulima waliohudhuria katika kikao hicho Godfrey John ameiomba serikali kwa kushirikiana na mawakala hao kuongeza kasi ya upatikanaji wa mbolea hiyo ili kunusuru maisha ya wanarukwa wanaotegemea kilimo kujikimu kimaisha.
Kwa msimu wa 2016/2017 Mkoa wa Rukwa ulilima Hekta zipatazo 556,975.9 na kuvuna tani 1,109,055.6 za mazao ya chakula kati ya hizo mahindi yalikuwa tani 710,602. Kwa msimu huu wa Kilimo wa 2017/18 Mkoa  umelenga kulima jumla ya eneo la Hekta 554,310.6 na kuvuna tani 1,669,746.2 za mazao ya chakula.