Wednesday, February 28, 2018

RC Wangabo asisitiza usafi katika mahindi kujikinga na Kansa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wakulima
wote mkoani Rukwa kuhakikisha wanayasafisha mahindi yao kabla ya kuyauza ili
kupata soko la uhakika na pia kujiepusha na magonjwa mbalimbali ikiwemo kansa
endapo mahindi hayo yatauzwa yakiwa na mchanganyiko wa mahindi yaliyooza na
takataka.

Amesema kuwa mahindi yaliyooza yana sumu Kuvu ambayo
hutengenezwa yakiwa na upepo na unyevu, sumu ambayo huleta kansa kwenye miili
ya binadamu endapo mahindi hayo yatasagwa na athari hiyo haitakuwa kwa
watanzania peke yao bali hata walaji waliopo nje ya nchi.

“Muhakikishe kwamba mahindi yale mnayoyachambua hambakishi
mahindi yaliyooza na matakataka yale mahindi yaliyooza ni sumu ile inaitwa sumu
kuvu inakuja kutengenezwa baadae kukiwa na upepo na unyevu na kusababisha
kansa, lakini pia mawe yakiingia kwenye mfumo wa kusaga unga, chakula kikiwa na
mawe kitasababisha kidole tumbo, ambapo hadi ufanyiwe upasuaji ndipo upone,”
Alisema

Na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia kutangaza
bidhaa nzuri zitakazo Mkoa wa Rukwa katika mikoa mbalimbali nchini lakini pia
kama usafi huo utazingatiwa utaleta sura nzuri katika soko la kimataifa na
hatimae kuitangaza nchi kwa bidhaa zake bora.

Ameyasema hayo alipotembelea kiwanda cha kuzalisha unga cha
Mbasira Food Industries kilichopo kata ya Malangali, Wilaya ya Sumbawanga
kujionea maendeleo ya kiwanda hicho chenye uwezo wa kuzalisha tani 36,000 za
unga kwa mwaka na kuongea na vibarua wa kiwanda hicho waliokuwa wakitenga
mahindi mazima na mabovu kwaajili ya uzalishaji.

Nae Mkurugenzi wa Mbasira food Industries Ltd Mikidadi
Kassanda amesema kuwa changamoto kubwa wanayopambana nayo katika kununua
mahindi kutoka kwa wakulima ni kupata machanganyiko wa mahindi mabovu na
kusababisha kupoteza kilo nne za mahindi mabovu katika kila kilo 100 za mahindi
wanayouziwa na wakulima.

“Moja ya changamoto tunazokumbana nazo ni ukosefu wa mafunzo
bora kwa wakulima juu ya uzalishaji bora wa mahindi na hatimae kupata mahindi
yasiyo na viwango,” Alisema.

“Hatutaki kusikia Zero Kantalamba Sekondari” RC Wangabo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameitahadharisha
bodi ya shule ya Sekondari Kantalamba kuhakikisha wanaweka mikakati ya kuondoa
daraja la sifuri katika shule hiyo kongwe nchini iliyoanzishwa mwaka 1964 na
Kanisa Katoliki na hatimae kukabidhiwa rasmi serikali mwaka 1968.

Amesema kuwa shule hiyo haina hadhi ya kuwa na daraja la
sifuri kutokana na kutoa viongozi mbalimbali walioiongoza nchi hii na kuwa
serikali kwa makusudi imetoa shilingi Bilioni 1.1 ili kuboresha miundombinu ya
shule hiyo hivyo haipendezi kusikika ikiendelea kutoa daraja la sifuri kuanzia
kidato cha pili hadi cha sita.

“Mjumbe wa bodi ziondoeni hizi sifuri zitoke kabisa, na hata
four taratibu zitoeni, yaani hapa pana hadhi ya Division one nyingi, two
zinafuata na three mwisho hiyo ndio hadhi ya Kantalamba sekondari na ukongwe
wake, na sasa tunatumia mabilioni kuboresha miundombinu halafu bado sifuri,
sifuri katika mazingira haya, na anakaa bweni miaka minne sifuri?” Alisema.

Ameyasema hayo alipotembelea shule hiyo ili kujionea marekebisho
ya ujenzi wa majengo kadhaa yaliyofanywa ili kuboresha mazingira ya shule
kwaajili ya wanafunzi.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule Hiyo Martin Kasensa amesema
kuwa ufaulu wa wanafunzi umekuwa ukipanda mwaka hadi mwaka.

RC Wangabo asifu bidhaa zinazotengenezwa na Energy Sembe pamoja na Dew Drop
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka
watanzania kutumia unga wa Energy Sembe pamoja na maji ya Dew Drop
yanayozalishwa Mkoani Rukwa na kusambazwa zaidi ya Miko saba nchini ili kuona
ubora wa bidhaa zinazotengenezwa katika Mkoa wa Rukwa.

Ameyasema hayo alipotembelea kiwanda cha Unga cha Energy
Sembe pamoja na Kiwanda cha Maji ya Dew Drop vyote vinamilikiwa na mwekezaji
mzawa wa Mkoa wa Rukwa Aziz Sudi katika ziara ya siku moja aliyoifanya katika
Manispaa ya Sumbawanga ili kujionea maendeleo ya Viwanfda mablimbali pamoja na
miradi ya maendeleo inyaotekelezwa na manispaa.

“Nitoe rai kwa wananchi wote Tanzania watumie Energy Sembe
kutoka Rukwa ni bora yenye viwangona kingine ni hiki kiwanda cha Dew Drop
ambacho kinatengeneza maji yenye kiwango cha juu sana na yanasambazwa zaidi ya
mikoa saba nchini, tutumie maji haya, tujivunie viwanda vyetu vya hapa hasa
hivi ambavyo vinazalishwa na wazawa wenyewe,” Alisema.

Kwa upande wake Mwekezaji huyo Aziz Sudi amesema kuwa maji
ya Dew Drop ni maji yasiyotumia kemikali ya aina yoyote na kuwa ni maji halisi
na kuongeza kuwa ni tofauti na maji mengine yanayowekwa kitu kinachofanana na
“water guard” jambo linalobadilisha ladha ya maji.

Wednesday, February 21, 2018

“Kamwe Sitauingilia mhimili wa mahakama” RC Wangabo.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewatahadharisha wananchi juu ya kuingilia Mhimili wa mahakama baada ya kupokea malalamiko ya wakulima 112 waliouza tani 622 za mahindi kwa chama cha ushirika cha mazao MUZIA AMCOS bila ya kulipwa fedha zao kwa msimu wa 2016/2017 ambapo kesi hiyo ipo mahakamani na kutegemewa kusikilizwa tarehe 27/2/2018.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akipokea muhtasari wa malalamiko ya wakulima wa Tarafa ya Mwimbi kutoka kwa Katibu wa  wakulima kata ya Mambwekenya Geofrey Siyame muda mfupi baada ya kusoma malalamiko hayo. 

Mrajis wa Vyama vya ushirika Mkoa wa Rukwa Wallace Kiama akitoa somo kwa wakulima juu ya taratibu za kisheria zinafuatwa na vyama vya ushirikia nchini.

Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo akitoa ufafanuzi kwa wakulima wa zao la mahindi juu ya mipaka iliyopo kati ya mihimili mitatu inayoendesha nchi.

Wananachi hao wanaokidai chama hicho Shilingi Milioni 315 wameiomba serikali kuchukua mzigo huo wa deni baada ya chama hicho kutoa ahadi kadhaa za malipo tangu tarehe 10/10/2017 na kushindwa kulipa na kupelekea wananchi hao kushindwa kujiendeleza kiuchumi.

Amesema kuwa haingilii mahakama pale anaposikiliza kero za wananchi isipokuwa kesi ikiwa mahakamani hana mamlaka ya kumlazimisha Jaji cha kufanya kwani mahakama zinataratibu zao za kuendesha kesi na kuwasihi wakulima kusubiri hukumu ya kesi hiyo ndipo aweze kushughulikia na kuwahakikisha kupata haki yao pindi hukumu itakapotoka.

“Tumeambiwa hapa kuwa hilo suala ltasikilizwa tarehe 27/2/2018, sasa hebu tusubili tuone ile hukumu itatoka na itakuwa ya namna gani kwahiyo siwezi kuisemea, nikiisemea inamaana nitakuwa naingilia uhuru wa mahakama, tusubiri tusikie hukumu itasemaje juu ya kuipata hiyo fedha milioni 315, wakulima watapataje na mhukumiwa atapewa adhabu gani, ikishatoka ndipo serikali tutajua tufanye kitu gani,” Alisisitiza.

Awali akisoma risala fupi kwa niaba ya mrajisi wa vyama vya ushirikia Mkoa wa Rukwa Nicolas Mrango alisema kuwa baada ya kubaini kasoro kadhaa katika chama hicho waliitisha kikao cha bodi na wajumbe wa bodi hiyo walielekeza lawama kwa Mwenyekiti na katibu wa chama hicho na kupelekea viongozi hao kufikishwa polisi na hatiame kesi kufikishwa mahakamani.

“Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuwasimamisha uongozi viongozi waliotuhumiwa kuhusika na upotevu wa mahindi ya wakulima ili kupisha vyombo vya uchunguzi kutekeleza majukumu yake pasipo kuingiliwa,” Alisema.

Nae katibu wa wakulima kata ya Mambwekenya Geofrey Siyame aliitaka serikali kuchukua mzigo wa deni kwakuwa serikali ndio iliyotoa uwakala wa kununua mahindi ya wakulima kwa chama hicho na kueleza kuwa hadi sasa wameshindwa kununua pembejeo ili kuendelea na shughuli za kilimo na kuwa hawana Imani na mahakama.

“Tumepata taarifa kwamba serikali imepeleka madai mahakamani, mahakama imekuwa ikirusha tarehe kile kesi inapotanjwa kwa madai upelelezi unaendelea, kwanininuchunguzi unachukua muda mrefu, wakulima mpaka sasa hawana Imani na mahakama baada ya kutishiwa na mdaiwa kuwa anadili na mahakama,” Alisema.

RC Wangabo atoa mwezi mmoja kukamilika kwa kituo cha afya Mwimbi


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya kalambo kuhakikisha wanamaliza ujenzi wa kituo cha afya cha mwimbi, kituo kilichoanza kujengwa tarehe 1/8/2017 na kufikia hatua ya kupauliwa.

Mkandarasi wa ujenzi huo mwakilishi wa SUMA JKT amesema kuwa kinachokwamisha kuendelea kwa ujenzi huo ni fedha ambapo wameomba kuidhinishiwa shilingi milioni 120 ili kuendelea na hadi Mkuu wa Mkoa anawasili kukagua maendeleo ya ujenzi huo fedha hizo hazijafika huku siku 14 zikiwa zimekatika bila ya mafanikio.

“Baada ya mwezi mmoja nitakuja hapa mnikabidhi wenye jengo likiwa limekamilika, hakuna sababu ya kuchelewesha kama fedha ipo, mkandarasi yupo, kwanini ujenzi umekwama, Mkurugenzi ndani ya siku mbili fedha hiyo iwe imetoka ili washambulie hili jengo liweze kuisha, vitu vichache sana vimebaki hapa” Alisema.

Na kuongeza kuwa uzembe huo ndio unaosababisha usumbufu wa huduma za afya kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo hasa kina mama na watoto chini ya miaka mitano jambo linalorudisha nyuma juhudi za serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais mpendwa Dk. John Pombe Magufuli. 

Awali akitoa maelezo ya maendeleo ya ujenzi huo Mwakilishi wa SUMA JKT amesema kuwa tangu kuanza kwa ujenzi huo wametumia shilingi milioni 50 kati ya shilingi milioni 355 ambazo zinatakiwa kutumia hadi kumaliza mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 400.


Add caption

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo(wa kwanza kushoto)  akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya  Kalambo Mh. Julieth Binyura (mbele wa kwanza kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya kalambo ( Hayupo pichani) baada ya kufika kwenye kituo cha Afya mwimbi na kukuta jengo hilo bado halijamalizika baada ya miezi sita wakati ilitakiwa kumalizika ndani ya miezi mitatu. (katikati) Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dk.Boniface Kasululu

Jengo la kituo cha Afya Mwimbi, Wilayani kalambo kinachotakiwa kumalizwa ndani ya mwezi mmoja. 

RC Wangabo aridhishwa na ujenzi wa kituo cha afya cha Nkomolo.

Mmoja wa mafundi wa mtaani akiendelea na ujenzi wa moja ya jengo jipya la kituo cha Afya Nkomolo - Wilayani nkasi

Moja ya jengo jipya la wodi za kinamama katika kituo cha afya Nkomolo - Wilayani Nkasi

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo(mwenye gunboot za kijani)  akikagua moja ya majengo mapya ya kituo cha afya cha Nkomolo - Wilayani Nkasi.

Jengo la Wodi ya kinamama na Upasuaji Kituo cha Afya Nkomolo - Wilayani nkasi

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesifu maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya cha Nkomolo, kilichopo Namanyere Wilayani Nkasi pamoja na changamoto kadhaa zilizokuwa zikikabili maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.

Ametoa kauli hiyo alipofanya ziara katika kituo hicho ili kujionea maendeleo ya upanuzi wa majengo matano katika kituo hicho ikiwa ni miongoni mwa fedha za serikali zilizotolewa ili kuimarisha vituo vya afya nchini.

“Ujenzi huu ulianza mwezi Oktoba, 2017 na kutakiwa kuisha baada ya miezi mitatu lakini sasa ni mwezi wa nne lakini hiyo ni kutokana na changamoto ya ukubwa wa majengo haya ambayo yamesababisha kuchelewa kwa ujenzi huu, lakini mpaka sasa tumeridhika ujenzi unaenda vizuri, sasa rai yangu ni kwamba ujenzi huu ukamilike mwisho wa mwezi huu,” Alisema.

Mh. Wangabo alitumia nafasi hiyo kupongeza ujenzi huo kwa kuwashirikisha kina mama tangu mwanzo wa uchimbaji wa msingi hadi kumalizika kwa ujenzi huo na kuongeza kuwa ubora wa majengo huo unashinda ule unaojengwa na makandarasi ambao hutumia fehda nyingi kwa ubora usio wa uhakika.

Nae mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda alimuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa ujenzi huo utaisha kwa wakati aliotoa maelekezo na kwamba hadi kufikia tarehe 2/3/2018 ujenzi huo pamoja na usafi wa mazingira utakuwa umekamilika.

Tuesday, February 13, 2018

Maadhimisho siku ya sheria Rukwa Feb 2018


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesema maboresho ya TEHAMA yanayofanywa na mhimili wa mahakama nchini utasaidia kupunguza foleni za wananchi wanaofika ofisi za Wakuu wa Wilaya na kwa Mkuu wa Mkoa kutafuta haki zao.
Amesema kuwa kitendo cha mwaanchi kuweza kujua mwenendo wa kesi bila ya kufika mahakamani ni maendeleo makubwa yanayofikiwa na mhimili huo na kuwaasa kuanza kufanya kazi baada ya kuwa likizo ya mwisho wa mwaka.
Ameyasema hayo kwenye maadhimisho ya wiki ya sheria ambayo hufanyika tarehe 1, Februari ya kila mwaka katika Viwanja wa mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga inayojumuisha mikoa ya Rukwa na Katavi.
“Mwaka 2018 na jitihada zilizofanyika na mahakama umekuwa mwanzo mzuri, wananchi watajitokeza kutafuta elimu hii ya sheria na wanapoipata itatupunguzia msongamano kwenye ofisi zetu za Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa ili tufanye kazi za maendeleo sio kusuluhisha migogo ya ndoa, mirathi na ardhi ambayo yote imekaa katika misingi ya kisheria,” Alieleza.
Na kuongeza kuwa elimu hii ya sheria iendelee kutolewa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakati huku wakizingatia kaulimbiu ya maadhimisho hayo inayosema “Matumizi ya TEHAMA kwa kutoa haki kwa wakati na kwa kuzingatia maadili.”
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga John Mgeta ametahadahrisha matumizi mabaya ya Teknolojia katika kuvunja maadili na misingi ya mahakama na utu kwani watu hutumia teknolojia hiyo kuendeleza rushwa kupitia namba za simu za mahakama.
“Mtumishi wa mahakama anaweza kutumia simu kuwasiliana na mtu akimuomba rushwa au kufanya miamala ya pesa, vyombo vya habari na wananchi ambao wanakiuka maadili kwa kutumia simu na TEHAMA, sisi tunasisitiza matumizi haya yazingatie maadili,” Alibainisha.
Awali akitoa taarifa ya chama cha wanasheria Tanzania Wakili Baltazar Chambi amesema kuwa mahakama ya Tanzania kwa kutumia TEHAMA itafikia suluhu mojawapo ya uhakika wa utoaji wa haki kwa wakati kwa kulitambua hilo wadau wa haki ni vyema wakajua matumizi ya TEHAMA ili kuleta ufanisi katika kazi zao.

Sunday, February 4, 2018

RC Rukwa aagiza kusitishwa ujenzi wa kiwanda

Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo ameagiza kusitishwa ujenzi wa kiwanda cha unga katika eneo la jirani na zahanati ya Kilimahewa kata ya Malangali wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa maelekezo ya kusimamishwa kwa ujenzi wa kiwanda katika kata ya Malangali, Manipaa ya Sumbwanga kwa kukiuka taratibu za ujenzi na kujenga karibu na Zahanati.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Hamid Njovu(Kushoto) ya kusimamishwa kwa ujenzi wa kiwanda katika kata ya Malangali, Manipaa ya Sumbwanga kwa kukiuka taratibu za ujenzi na kujenga karibu na Zahanati. (katikati) Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Mh. Julieth Binyura.


Timu iliyokwenda kuona ujenzi wa kiwanda cha London Agro Factory kinachojengwa karibu na zahanati ikiongozwa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.
Mh. Wangabo ametoa agizo hilo baada ya kupokea kero za wananchi aliporuhusu maswali katika Mkutano uliofanyika Malangali sokoni, baada ya mkazi wa eneo hilo Raymond Mwanazyumi kuhoji sababu za kiwanda hicho kendelea kujengwa karibu na zahanati wakati waliugomea ujenzi huo.
“Uwekezaji na hospitali amabyo itakuwa inahusu kelele vitaoana kweli, watu watashindwa kulala na hao wagonjwa si wataugua mara mbili, hoja ya msingi kuna eneo limetengwa la uwekezaji hajaanza kujenga hajapewa kibali cha kuendeleza ujenzi kwahiyo asiendeleze hapo mahali,” Alisisitiza.
Kufuatia malalamiko hayo Mh. Wangabo alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga, Hamid Njovu kutoa majibu ya madai hayo. Nae alisema kuwa mwekezaji huyo wa Kampuni ya London Agro Factor inayomilikiwa na Asayile Masaku alizuiwa  kuendelea na ujenzi huo kwa kuwa eneo hilo si rafiki kwa ujenzi wa viwanda.
Amesema taarifa alizonazo ni kwamba mwekezaji huyo yupo katika mchakato wa kutaka kubadili matumizi ya eneo hilo kutoka kuwa la viwanda hadi kuwa la makazi.

"Tunahitaji wawekezaji na tumetenga maeneo ya viwanda. Hili eneo ambalo Masaku anataka kujenga kiwanda cha unga analimiliki kihalali lakini lipo kwa ajili ya makazi ya watu, tulimwambia tupo tayari kumpa kiwanja eneo maalum la uwekezaji Kanondo” amesema.

“Wote waliolima na kuchoma mkaa msitu wa malangali wakamatwe maramoja” RC Wangabo.

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameagiza kuwasaka na kuwakamata wananchi wote waliokiuka amri ya mahakama ya kutoutumia msitu wa hifadhi yaMalangali kwaajili ya matumizi ya kibinadamu.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo 


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa agizo la kukamatwa kwa waliokiuka amri ya mahakama na kufanya shughuli za kibinadamu kwenye msitu wa Malangali Mjini Sumbawanga katika Mkutano wa hadhara. Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa agizo la kukamatwa kwa waliokiuka amri ya mahakama na kufanya shughuli za kibinadamu kwenye msitu wa Malangali Mjini Sumbawanga katika Mkutano wa hadhara. 

Amesema kuwa pamoja na kukamtwa, wananchi hao wasimamiwe kuhakikisha kuwa wanapanda miti maeneo ambayo wameyaharibu na kusisitiza kusakwa kwa wale wote waaofanya shughuli za kibinadamu kando ya vyanzo vya maji huku akitaja bonde la mto lwiche.

“Mpite shamba kwa shamba, kamateni watu wote ambao wamevamia kule, ule msitu uache kama ulivyo, vyanzo vyetu vya maji vitakauka, Mkurugenzi fanya msako wa bonde lote hilo kwa wale wote ambao wameanza kufyeka na kulima, kamata. DC simamia hili, tunataka kukomesha uharibifu wa mazingira wa aina yoyote ile,” Alisisitiza.

Ametoa agizo hilo katika mkutano wa hadhara alioufanya baada ya kutembelea msitu huo wa malangali uliopo kata ya Malangali, Wlayani Sumbawanga na kujione namna wananchi hao walivyoharibu msitu huo uliojaa miti ya miombo ambayo inakatwa na kugeuzwa mkaa.
Msitu huo wa Malangali ulianzishwa rasmi mwaka 1986 na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa huo Mh. Tumainieli Kihwelu wenye eneo la ekari 278 kwa lengo la kupunguza mmomonyoko na vimbunga.

Wakati akisoma taarifa ya Msitu huo Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbwanga Hamid Njovu amesema kuwa baada ya miaka 29 wananchi waliwasilisha malalamiko ya kupokonywa ardhi na kufanywa msitu shauri lililofikishwa mahakamani na kuamuliwa wananchi hao kulipwa fidia huku hukumu ya kesi hiyo ikisitisha shughuli zote za kibinadamu kutofanyika katika msitu huo.

“Tarehe 28/4/2016 hukumu ilitolea na kuamuliwa Manispaa ya Sumbawanga kulipa fidia huku Hukumu hiyo ikisitisha shughuli zote za kibinadamu ndani ya msitu lakini bado wananchi hao walirudi kufyeka miti na kulima na tarehe 13/11/2017 Manispaa ilitoa maelekezo kwa wananchi kutoutumia msitu kwa shughuli za kibinadamu,”Alimalizia.


Mmoja wa wadau wa Mazingira Mzee Zeno Nkoswe amesema kuwa usalama wa mji wa Malangali unatokana na msitu huo na kwamba endapo utaendelea kuharibiwa mji huo utafunikwa na mmomonyoko wa udongo.