Thursday, March 29, 2018

RC Wangabo azigeukia NGOs na CSOs kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda kupambana na umasikini

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amezitaka asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali kuchukulia juhudi za uanziswaji wa viwanda nchini unaofanywa na serikali kama suala mtambuka na ukombozi kwa mwananchi katika kupambana vita dhidi ya Umasikini huku wakizingatia utunzaji wa mazingira na kushirikiana na SIDO.
Amesema kuwa takwimu zinaonesha kwamba takribani hekta 300,000 hadi 400,000 za misitu nchini huharibiwa kwa kuchoma Mkaa. Hivyo njia nyingine na muhimu kuokoa mazingira yetu ni kwa kuanzisha viwanda vya kutengeneza Mkaa kwa kutumia marando ya Mbao, Pumba za Mpunga, Mabua ya mahindi n.k. malighafi ambazo hupatikana kwa wingi Mkoani kwetu.
 “Kwa sababu hiyo ninapenda kutoa wito kwa NGOs na CSOs kushiriki kwenye kampeni hii ya uanzishwaji wa viwanda yenye kaulimbiu ya Mkoa wetu, Viwanda vyetu kwa kuanzisha viwanda. Viwanda tunavyovilenga ni vile vidogo vya thamani ya kuanzia milioni 2 hadi Milioni 10,” Alisisitiza.
Kwa upande wake Meneja wa SIDO Emanuel Magere amesema kuwa asasi pamoja na mashirika hayo yamekuwa yakitoa elimu mbalimbali kutegemea matatizo ama changamoto za wananchi lakini imefika wakati kutambua kuwa, wananchi hao wanahitaji pia elimu ya ujasiliamali ili kuanzisha viwanda, na kuziomba taasisi za fedha kuweza kutoa mikopo kwa wanaohitaji kuanzisha viwanda.
“Mwamko katika uazishwaji wa viwanda sio mkubwa sana, wengi wamekuwa wakijiwekeza kwenye sekta ya huduma mfano, mashule, migahawa, maduka na huduma mbalimbali ambayo “return” yake inakuwa ya haraka kuliko viwanda na pia changamoto ya masoko ya bidhaa za ndani ya mkoa kutoka kwa bidhaa za nje ya mkoa ama nje ya nchi imekuwa ni changamoto kwa mkoa,” Alimalizia.
Katika kuhimiza ushirikiano Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda amezitaka NGO na CSO hizo kuweza kufika kwenye ofisi za kiserikali ili kuweza kujitambulisha shughuli wanazofanya na kujitokeza kwenye songambele mbalimbali zinazofanywa na halmashauri katika ujenzi wa madarasa ya shule na vituo vya afya ili michango yao ijulikane na sio kusubiri kutafutwa na serikali.
Katika utekelezaji wa viwanda 100, ndani ya kipindi cha miezi minne kuanzia Disemba mwaka 2017 hadi 26, Machi, 2018 Mkoa wa Rukwa umezalisha viwanda vidogo 51 huku lengo la Mkoa ni kuwa na viwanda vingi zaidi ili kuchangia kwa kiasi kikubwa lengo la Kitaifa la kufikia nchi ya Uchumi wa Kati wa Viwanda ifikapo 2025.

Thursday, March 8, 2018

Wakurugenzi wasiotenga fedha za mikopo kwa wanawake kufikia June kutumbu...


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  Mh. Ummy Mwalimu ametoa miezi mitatu kwa
wakurugenzi wote nchini kuhakikisha wanatenga asilimia 4 za fedha za
halmashauri kwaajili ya kuwapa wanawake mikopo ili waweze kujikwamua kiuchumi
na kuunga mkono juhudi za serikali katika uchumi wa viwanda.

Amesema kuwa serikali haitasita kuwawajibisha wakurugenzi
watakaokiuka maelekezo ya serikali yanayolenga kutekeleza ahadi za Mheshimiwa
Rais kwa wananchi ili kuwawezesha wanawake wa mijini na vijijini kiuchumi na
hatimae kujiongezea kipato na kuwezesha uchumi wa viwanda.

“Linapokuja suala la kuwawezesha wanawake kiuchumi
hatutanii, chama cha mapinduzi tumepewa kura na wanawake wa Tanzania hasa
wanawake wa vijijini na tumewaahidi wanawake kwamba tutawapa mikopo yenye
masharti nafuu, kwahiyo pale ambapo mkurugenzi anashindwa kutenga fedha
kwaajili ya kuwapatia wanawake mikopo hatutaelewana, na tunasubiri mpaka tarehe
30 June 2018 wakurugenzi wote ambao hawajatenga fedha na kuzitoa kwaajili ya
wanawake  tutapeleka majina yao kwa Mh.
Rais Dk. John Pombe Magufuli,” Mh. Ummy alisisitiza.

Halikadhalika Mh. Ummy amepiga marufuku suala la kutoa fedha
ndogo kwa kikundi kikubwa cha kinamama huku akitolea mfano kikundi cha watu
sita kupewa 300,000 kuwa haitawasaidia kinamama hao katika juhudi za kujikwamua
kiuchumi na kuongeza kuwa ni heri fedha hizo zikabaki kwa mkurugenzi ili ifanye
shughuli nyingine lakini sio kuwakwamua kinamama.

Ameyasema hayo katika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Wanawake
Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kwa
kuanza na maandamano yaliyotokea ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa hadi katika
Uwanja wa mpira wa Nelson Mandela akiwa ni mgeni rasmi wa sherehe hizo.

Awali akisoma risala Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth
Binyura ameitaka serikali kuhakikisha wanafanya marekebisho ya sheria kinzani ili
kuendana na mabadiliko ya mfumo wa maisha kama vile sheria ya ndoa, mirathi,
maadili ya jamii na kiwango cha mchango wa mzazi katika malezi ya familia na
watoto huku akitaja mafanikio kadha ya kufikia idadi ya asilimia 50 kwa 50.

“Kuanzishwa kwa vikundi na kuunganishwa na taasisi za fedha kama
vile NMB, CRDB, Pride, SACCOS na SIDO kwaajili ya mikopo na vifaa kwaajili ya kufanyia
kazi, pia mkoa kwa kushirikiana na Halmashauri tumeweza kuwatambua wazee 48,732
wakiwemo wanawake na wanaume pia mkoa unaendelea kufuatilia masuala ya kijinsia
dhidi ya watoto, jumla ya watoto 1,307 walifanyiwa ukatili na mashauri yao yapo
polisi, dawati la jinsia na mahakamani,” Alisema.

Akichukua nafasi hiyo mbunge wa Sumbawanga Mjini Mh. Aesh
Hilally nae alimuomba Mh. Ummy kuona umuhimu wa kuongeza gari za wagonjwa nae
Mh. Ummy alikubali ombi hilo na kuahidi kutoa gari za wagonjwa mbili, moja
ikihudumia hospitali ya rufaa ya mkoa wa rukwa na nyingine katika kituo cha
afya kilichopo manispaa ya Sumbawanga. 


Monday, March 5, 2018

Uongozi wa Mkoa Rukwa wachangia Milioni 5.7 kumalizia Ujenzi wa Msikiti Sumbawanga.
Uongozi wa Waislamu Mkoani Rukwa umepokea kwa furaha mchango
wa Shilingi Milioni 5.7 uliotolewa na uongozi wa serikali ya Mkoa wa Rukwa
ukiongozwa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo katika kikao cha
maridhiano juu ya ujenzi wa msikiti uliosimama kwa muda.

Fedha hizo zilizochangwa zilijumuisha ahadi, fedha taslimu
pamoja na vifaa vya ujenzi vilivyotolewa kwa umoja wa viongozi wa serikali
kuonesha mshikamano uliopo kati ya serikali na wananchi bilaya kujali itikadi,
dini wala rangi huku Mh. Wangabo akichangia milioni 1.5

Kabla ya maridhiano hayo Mh. Wangabo alitoa salamu za rais
Dk. John Pombe Magufuli juu ya kuuendeleza msikiti huo na kunukuu kuwa Mheshimiwa
Rais ametoa kibali cha kuuendeleza msikiti hio na yupo tayari kuweka jiwe la
msingi ama kuuzindua msikiti huo.

“Mh. Rais ameniagiza niseme yafuatayo kuwa ametoa kibali cha
kuendelea kujenga msikiti huu ahdi umalizike, ameyafikiria mambo mengi sana mpaka
kuja kufikia maamuzi haya, ili yalete muskabali wa maridhiano, ilete amani,
ilete utulivu, mshikamano, maoelewano na umoja ili Rukwa yetu iweze kusonga
mbele kama kitu kimoja., la pili alisema kuwa yupo tayari kuweka jiwe la msingi
ama la kuzindua msikiti huu,”

Kwa kuongezea hilo Mh. Wangabo aliuomba uongozi wa uislamu
mkoa kuendelea kushirikiana na kudumiasha amani na kuhakikisha wanajenga Rukwa
moja isiyoyumbishwa na tofauti yoyote kwani ushirikiano huo umekuwa wa muda
mrefu hovyo asingependa pawepo na tofauti.

Pia alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga
kuhakikisha vikwazo vyote vianondolewa na kumtaka kamishna wa ardhi nyanda za
juu kusini kufanya haraka kupitisha kibali ili msikiti huo upatiwe hati.
Kwa upande wake Shekhe Mkuu wa mkoa wa Rukwa Rashid
Akilimali amesifu maamuzi ya Rais Dk. John Pombe Magufuli na kukubali ombi lake
la kutaka kuja kuweka jiwe la msingi ama kuuzindua msikiti huo na kuwa waislamu
wataendelea kuungana nae na kumuombea amalize vipindi vyake salama.
“Mh. Mkuu wa Mkoa kwa niaba ya waislamu wa mkoa wa Rukwa kwanza
tunatoa shukrani za dhati kwa Mh.Rais wa nchi Mh. Dk. John Magufuli, nimeamini
kama alivyosema kuwa yeye ni msikivu na yeye anatuomba kila siku tumuombee dua na
sisi mwisho wa khotuba yetu kila ijumaa tunadua huwa tunaiomba, Eee Mola wetu
linda amani ya nchi yetu na uwalinde viongozi wetu,” Shekh Akilimali
alimalizia.
Uongozi wa mkoa wa Rukwa uliowajumuisha kamati ya ulinzi na
usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa halmashauri, Mbunge wa jimbo la
Sumbawanga mjini, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sumbawanga pamoja na kaimu
Kamishna wa Ardhi nyanda za juu kusini.

Thursday, March 1, 2018

Nyumba 20 NHC Rukwa kuendelezwa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amekataa maombi ya
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kufanya ukandarasi wa majengo mbalimbali ya
serikali mkoani Rukwa kutokana na kusimama kwa mradi wanaousimamia kutokamilika
kwa muda wa miaka minne.

Maombi hayo yaliwasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa na meneja wa Mkoa
wa shirika hilo Mhandisi Musa Kamendu baada ya Mh. Wangabo kutembelea mradi wa
nyumba 20 za NHC zilizopo sumbawanga mjini ili kujionea maendeleo ya ujenzi wa
nyumba hizo ambazo umefikia asilimia 60.

Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 ambao
ulianza mwezi juni 2014 na kusimama kutokana na shirika kukosa fedha za
kuendeleza na kutarajiwa kuendelea ifikapo mwezi machi mwaka huu amabpo hadi
kufikia hapo shilingi 867,990,367 zimeshatumika kati ya 1,532,473,872.

“Tunaona wakati mwwingine serikali inatoa kazi kwa SUMA JKT
na kukarabati shule kama Kantalamba Sekondari, sisi kama mkandarasi daraja la
kwanza, Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine tunawaalika na tunawaomba mtupe hizo
kazi, tutazifanya vizuri sana na kwa ufanisi mkubwa, tumesikia kuna miradi
mingi, sisi kama wakandarasi tunaomba mtupe hizo kazi,” Mhandisi Kamendu
alimalizia.

Katika kujibu maombi hayo Mh. Wangabo alitoa angalizo kuwa
endapo mradi wa shirika umeshindikana kumalizika kwa wakati hali hiyo itakuwaje
kama wakipewa mradi na taasisi nyingine ya serikali na kuwataka kwanza kumaliza
mradi wao ili wawe na ushahidi wa kuonekana katika Mkoa wa Rukwa na sio kuishia
kutoa mifano kwa miradi iliyofanyika katika mikoa mingine.

Thamani ya nyumba moja ni shilingi 139,680,000 na ikiwa
haikumalizwa gharama yake ni shilingi 118,080,000 bila ya VAT.