Wednesday, October 31, 2018

Milioni 151 zatumika kuongeza nguvu ya kupambana na Ukimwi Rukwa.


Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa kwa kushirikiana na mradi wa Military HIV Research Program (MHRP) umetumia Shilingi 151,109,042 kununua gari aina ya Land Cruiser Hardtop kwaajili ya shughuli zinazohusiana na mapambano dhidi ya Ukimwi.

Gari hiyo ambayo alikabidhiwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Bw.Msongela Palela na mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo imenunuliwa kutokana na fedha zilizovuka mwaka 2016/2017 ikiwa ni makubaliano baina ya katibu tawala na mradi juu ya fedha zilizovuka mwaka kupangiwa matumizi yanayolenga kuboresha huduma za Ukimwi.
Mwakilishi wa Mradi wa MHRP Bw. Riziki Kasimu (kulia) akimkabidhi funguo za gari litakalotumika kuongeza nguvu za mapambano dhidi ya maambukizi ya Ukimwi kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) mbele ya wadau dhidi ya maambuzi hayo. 


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo akiwasha gari lililokabidhiwa kupitia ushirikiano wa Ofisi yake na Mradi wa MHRP kwaajili ya mapambano dhidi ya maambukizi ya Ukimwi.

Wakati akikabidhi gari hiyo Mh. Wangabo alitahadharisha matumizi ya gari hiyo huku akipiga mfano wa gari ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) ya halmashauri ya Wilaya ya Kalmabo iliyokuwa na mazoea ya kwenda kwenye sehemu za starehe kuwa mshauri wa mradi huo tayari ameshachukuliwa hatua za kinidhamu.


“Tarehe 7 mwezi wa 10 gari hii tulilishika hapa Sumbawanga likiwa eneo la starehe na huyo mshauri wa mradi huo ndiye aliyekuwa anaendesha gari hilo, tulichukua hatua kali za kumuondoa na kumrudisha kwa mwajiri wake kwaajili ya hatua nyingine za kinidhamu, nitoe wito kwa madereva wa serikali kutumia magari kwa mambo yao binafsi, suala hili lisijitokeze, hatua kali zitachukuliwa,” alisisitiza.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi wa mradi huo Bw. Riziki Kasimu ameshukuru ushirikiano anaoupata kutoka katika halmashauri na serikali ya Mkoa ili kuhakikisha wanashusha na kutokomeza maambukizi ya Ukimwi na ameiomba serikali ya Mkoa wa Rukwa kutoa kipaumbele kwa kazi za Ukimwi katika matumizi ya gari.

“Pamoja na Kazi zote zilizopo Mkoani, tungependa kazi za mradi zipewe kipaumbele katika matumizi ya gari, ni kweli kwamba tuna kazi nyingi ama majukumu mengi ambayo hayo magari yangepaswa kufanya na sisi kama washirika kwenye maendeleo hatuwezi kusema gari hili litumike moja kwa moja kwa Ukimwi tu, lakini pale tunapokuwa na majukumu ya msingi ya Ukimwi tungependa msisitizo utolewe huko,”Alisema.

Mtadi huo tayari umeshatoa gari 7 katika Mkoa wa Rukwa, 4 katika Halmashauri zote za Mkoa na 3 katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa jambo lililosaidia kurahisisha shughuli za kupambana na maambukizi ya Ukimbwi na hatimae kushuka kutoka asilimia 6.2 mwaka 2015 hadi asilimia 4.4 mwaka 2018.

Jazia kupunguza uhaba wa Dawa Rukwa


Serikali kupitia ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeanzisha mfumo wa Jazia Prime vendor kwaajili ya kupata dawa na vifaa tiba pale vinapokosekana katika Bohari ya Dawa (MSD), mfumo ambao unakuwa na mzabuni mmoja atakayesambaza dawa na vifaa tiba ndani ya mkoa mzima.

Kupitia utaratibu huo Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa kupitia katibu tawala wa mkoa Bernard Makali wamewekeana saini na mzabuni ambaye ni kampuni ya Maranatha Pharmacy Ltd,  atakayesambaza dawa na vifaa tiba hivyo kuanzia katika ngazi ya zahanati katika halmashauri nne za mkoa, ili kuongeza upatikanaji wake.

Akifungua hafla hiyo fupi ya kuwekeana saini mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesema kuwa mfumo huo utawezesha na kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba muhimu pale ambapo vitakuwa havipatikani MSD.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Bw. Bernard makali (Kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Maranatha Pharmacy Ltd. Bw. Stephen Lengeni (kushoto) wakiweka saini katika mkataba wa kusambaza dawa na vifaa tiba kwa mkoa wa Rukwa. 

“Mfumo huu unaendeshwa kwa kumlipa mzabuni fedha mara tu baada ya vituo husika kuchukua dawa na vifaa tiba na si kwa mkopo. Maana yake vituo vya kutolea huduma za afya vinatakiwa kuhakikisha vina fedha kabla ya kupeleka mahitaji yao kwa mzabuni,” Alisema.


Aidha alitoa wito kwa wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanasimamia vyema mapato na matumizi ya fedha kutoka katika vyanzo mbalimbali kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kuhakikisha fedha zilizotengwa kwaajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba zinatumika kwa mujibu wa miongozo iliyopo.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Maranatha Pharmacy Ltd alisema kuwa anaishukuru serikali kwa kuiamini kampuni yake ambayo hadi sasa imeingia mikataba na mikoa ya Iringa, Ruvuma, Mbeya pamoja na Rukwa ambapo mara ya mwisho kufanya kazi na serikali ilikuwa mwaka 2006 wakati ambao mifumo ilikuwa haiku sawa.

Mbali na kutoa huduma kwa wananchi wa mkoa mfumo huu unatarajiwa kuboresha huduma kwa wazee, ambapo mkoa una jumla ya wazee 14,832 waliopatiwa vitambulisho vya kupatiwa matibabu bure.


Monday, October 29, 2018

Rukwa wajipanga kutumia Mkaa mbadala kuokoa mazingira.


Mkoa wa Rukwa umejipanga kupambana na uharibifu wa mazingira kwa kuhakikisha wanatumia rasilimali za makaa ya mawe yanayopatikana katika kijiji cha Nkomolo tu, Wilayani Nkasi kuwa mkaa mbadala na kuanza kutumika majumbani.

Mkaa wa Mawe unavyowaka katika jiko la kawaida. Mkakati huo ulioanza kwa mafunzo ya siku mbili yaliyoendeshwa na mtaalamu wa makaa hayo kutoka katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe bi. Halima Mpita ukiwakutanisha makatibu tawala wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, madiwani, wataalamu wa mazingira kutoka katika halmashauri, mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoshughulikia mazingira pamoja na wazee maarufu.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya nishati mbadala inayotokana na makaa ya mawe mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachima Wangabo amesema kuwa tunafanya kila liwekanalo kuokoa kile kilichopo na kuhakikisha kwamba mazingira hayaendelei kuharibiwa kwa namna yoyote hasa masuala ya kukata miti kwaajili ya kuni na mkaa.

“Makaa ya mawe yapo kilomita 45 toka hapa tulipo (sumbawanga mjini), yale makaa yam awe tunaweza kuyatumia kama mkaa mbadala kwa matumizi ya majumbani, na hili ndio lengo la mafunzo ya leo, mtaalamu wetu atatueleza kule Songwe wanafanyaje, kile wanachofanya kule watatumegea hapa uzoefu wao, na sisi tutaona na kujipanga tufanye nini na haya makaa yam awe tuliyonayo,” Alisema.

Ameongeza kuwa endapo mafanikio yatapatikana na kuanza kutumia makaa ya mawe majumbani, kiwango kikubwa cha uvunaji wa miti kitaokolewa na kutahadharisha kuwa mpango huo ukifanikiwa gharama za kununua bidhaa hiyo isiwakatishe tamaa wanunuzi ili wasirudi tena kukata miti na hatimae kutofikia lengo.

Kwa upande wake Bi. Mpita alisifu muitikio wa wadau wa mazingira wa mkoa wa Rukwa na kusema kuwa endapo nguvu hiyo itafikisha elimu kwa wananchi basi mkoa wa Rukwa utakuwa wa kuigwa na kuongeza kuwa atashirikiana bega kwa bega ili kuhakikisha mafanikio yanapatikana kwa faida ya kizazi hiki na kijacho.

Akieleza faida za mkaa unaozalishwa na makaa yam awe alisema, “Haya makaa ni suluhisho la kudumu juu ya matumizi mbadala la mkaa wa miti kwa kuwa miamba ya makaa ya mawe ni ya asili na inaweza kuvunwa zaidi ya miaka 500. Pia unaweza kuwaka kwa saa 3 hadi 4  mfululizo na hautoboi wala kuchafua sufuria, ni mkombozi wa ajira maana uanzishaji wa kiwanda chake ni rahisi na majivu yake hustawisha mimea,” Alisisitiza.

Ili kuuwasha Mkaa wa makaa ya mawe unahitaji jiko la mkaa lililotengenezwa kwa udongo, utawasha vijiti viwili maalum vya kuwashia moto utaweka vipande 4 hadi 5 acha viwake pamoja kwa dakika 3, ongeza mkaa na uache uko kwa dakia 15 hadi makaa ubadilike na kuwa rangi nyekundu kuanzia chini. Vipande 34 vya mkaa vinatosha kumaliza mapishi ambapo mkaa huo huwaka kwa masaa 3 hadi 4.


Wednesday, October 24, 2018

Barabara za ULGSP zapendezesha mji wa Sumbawanga

RC Wangabo aagiza kushughulikia udumavu kuongeza ufaulu.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza wakurugenzi kushirikiana na madiwani kuhakikisha suala la kupunguza udumavu katika mkoa wa Rukwa linakuwa ni ajenda ya kudumu katika vikao vya mabaraza ya madiwani pamoja na mikutano ya hadhara katika kuwaeleimisha wananchi juu ya athari ya udumavu.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo

Amesema kuwa suala la udumavu lisisahaulike pindi tunapoangalia ufaulu wa watoto wetu mashuleni, na kuwa mstari wa mbele kutoa ahadi za kuhakikisha watoto wanaongeza ufaulu huku udumavu ukiwa bado haujashughulikiwa.

“Tuone kwamba kama huna hali mbaya ya matokeo ya kielimu yanachangiwa pia na udumavu kwasababu udumavu umekuwa wa muda mrefu na kama tunaukubali upo, sasa kwanini usikubaliane pia na matokeo yanayotokea, tuweke jitihada kubwa sana kuondoa udumavu ili watoto wetu waongeze ufaulu,” Alisisitiza.

Ameongeza kuwa kama si hivyo basi itabidi takwimu udumavu ziangaliwe upya, ama kama kwenye elimu kuna kupasi sana basi kuna wizi wa mitihani ama kuna wageni wengi sana wanaotoka nje kuja kusoma Kwetu.

Mwanzoni mwa mweze wa nane Mh. Wangabo aliingia mkataba wa utendaji kazi na kusimamia shughuli za lishe baina ya Ofisi yake pamoja na wakuu wa wilaya ambapo ni utekelezaji wa maagizo ya Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mikoa juu ya kupunguza utapiamlo ambao kitaifa ni asilimia 34.

Kwa upande wake mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu alisema kuwa utapiamlo unasababisha udumavu wa akili na mwili na ubongo wa mtoto unaendelea kukua tangu ujauzito mpaka anapofikisha miaka mitano.

“Wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha juu ya masuala ya lishe bora na athari za utapiamlo.  Pamoja na kuwa Mkoa unazalisha vyakula vya aina mbalimbali tena kwa wingi, lakini wananchi wengi bado wanatumia aina moja au aina za vyakula vilivyozoeleka kwa muda mrefu bila kuchanganya na aina nyingine za vyakula ili kufikia mahitaji halisi ya virutubishi.” Alisema.

Mkoa wa Rukwa una kiwango cha utapiamlo cha asilimia 56.3 wakati kitaifa ni asilimia nne, na kitaifa mkoa wa rukwa umeshika nafasi ya 19 mwak huu tofauti na mwaka jana ulikuwa wa 15 kitaifa katika matokeo ya darasa la saba.
Tuesday, October 23, 2018

DC Sumbawanga aeleza mikakati ya kukitangaza Chuo cha VETA


Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule ameeleza mikakati yake ya kufanya ziara wilaya nzima yenye kata 48 kwa lengo la kukitangaza Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kinacheondelea kujengwa katika Manispaa ya Sumbawanga kwa lengo la kuwaweka tayari wazazi na wanafunzi watakaokuwa na sifa ya kujiunga na chuo hicho.

Amesema kuwa anataka chuo hicho kiwafaidishe wazawa wa Mkoa wa Rukwa kwasabau chuo hicho kitatumiwa na vijana kutoka katika mikoa mbalimbali hivyo ni vyema vijana wazawa wakapata elimu na kuweza kuusaidia Mkoa kufikia lengo la Tanzania ya viwanda hadi ifikapo mwaka 2025.

Pia katika kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa Dkt. Haule amekubaliana na Mstahiki Meya pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kuwa ajenda ya Chuo cha VETA iwe ni ya kudumu kwenye vikao vyao vya madiwani.

 “Hatutaki tena watu wabebe mageti kutoka Ilemba wayalete hapa mjini, watengenezee kule kule na pia fursa za viwanda kwa mafundi wa mashine za kukobolea mpunga wapate amfunzo hapa na kuweza kutumia ujuzi kule vijijini,” Alisema.

Ameyasema hayo wakati wa ziara ya kujua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho akiwa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo pamoja na wataalamu wengine kutoka katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga wakiongozwa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo pamoja na Mstahiki Meya.

Kwa upande wake Mh. Wangabo alitoa msisitizo kwa wanafunzi juu ya kuzingatia masomo ya sayansi ambayo ndio kipaumbele cha elimu nyingi za ufundi zitakazoanzishwa katika Chuo hicho cha VETA.

“Nitoe rai pia kwa upande wa wanafunzi wenyewe, ili uje kusoma kwenye chuo hiki, fursa ipo kwa wale wanafunzi wa masomo ya sayansi, kwasababu ufundi unaendana na masomo ya sayansi na hisabati, basi wanafunzi watilie umuhimu sana masomo ya sayansi, kwasababu haya ndio yanayotupeleka katika uchumi wa kati wa viwanda,” Alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule (katikati) akizungumza na wananchi (hawapo pichani) katika moja ya mikutano ya hadhara ya kukitangaza chuo cha Ufundi Stadi (VETA). Wa Kwanza kuanzia kushoto ni Mstahiki Meya wa manispaa ya Sumbawanga mh. Justin Malisawa, akifuatiwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo. baada ya Mkuu wa Wilaya anafuata Mkurugenzi wa Halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya na Katibu tawala wa Wilaya ya Sumbawanga Christina Mzena. 

Ujenzi ukikamilika chuo kitaweza kuchukua wanafunzi 900 wa kozi ndefu na 600 wa kozi fupi hivyo, kitakuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 1,500.

Monday, October 22, 2018

Mkurugenzi aondoa sintofahamu kuhusu Sumbawanga mpya


Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya ameondoa sintofahamu iliyokuwa imesambaa juu ya maagizo na maelekezo mablimbali aliyoyatoa katika kuboresha huduma kwa kukusanya mapato na kumsaidia mwananchi mmoja mmoja kujiboreshea maisha katika manispaa hiyo.

Mtalitinya alisema kuwa sula la vibali vya ujenzi na leseni za makazi imetafsirika tofauti lakini azma ni kuipima Manispaa kwa asilimia 100 na kuwa huo ni mwendo wa kufanya upimaji.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya. 


Tangu kuwasili kwa Mkurugenzi huyo mapema mwezi wa nane mwaka huu wananchi wengi wamekuwa wakipotosha maelekezo anayoyatoa na matokeo yake kueleweka vibaya kwa wananchi wengi wa Manispaa ya Sumbawanga.


 “Unapotaka kujenga jengo lako, unashauriwa kuepuka usumbufu, upate kibali kutoka ofis ya Mkurugenzi na utaratibu wa jengo utakaolifanya, tumeweka nguvu sana kwenye kata za mjini lakini haimaanishi hata kata hizi za pembezoni hazitakiwi kutii sheria hiyo. Leseni ya makazi tunakusudia kuipima Manispaa yetu kwa asilimia 100,” Alibainisha.

Pia alizitaja faida za leseni ya makazi ikiwa ni pamoja na kuwa mmiliki halali wa eneo, kurasimisha makazi ili kupata huduma za msingi kama vituo vya afya, barabara na maeneo ya wazi pamojanna kupata hatimiliki itakayodumu kuanzia mika 33 hadi 99.

Ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika soko la Kaswepepe, kata ya Sumbawanga Asilia, Wilayani Sumbawanga jambo ambalo lilipendezwa na wananchi waliohudhuria katika mkutano huo na hatimae kuelewa lengo la Mkurugenzi.

Mmoja wa wananchi waliohudhuria Ditmali Mwageni alisema kuwa walishangazwa na kitendo cha mkurugenzi huyo kuwaamuru watu kupaka rangi mabati kulingana na maagizo ya kila kata kuwa na rangi yake, lakini kwa ufafanuzi alioutoa nadhani ameeleweka vyema na wananchi waliohudhuria.

“Kusema kwake kuwa agizo hilo linawahusu wale tu ambao wanaanza kujenga sasa, hapo tumeelewa kuliko tulivyokuwa tunasikia kwamba watu wote wapake rangi za mabati kulingana na rangi ya kila kata, kwakuwa tu ni agizo la mkurugenzi, hiyo haikuwa sawa, nyumba zenyewe za zamani, mabati yamechoka, utekelezaji wake ungekuwa mgumu, lakini kama katoa miaka mitano Kwetu basi sawa,” Alisema.

Miongoni mwa masuala yaliyozua mzozo ni agizo la kila kata kuwa na rangi yake ya bati, kupata kibali cha ujenzi kabla ya kuanza ujenzi, kuwa na leseni ya makazi pamoja na mazoezi mbali mbali ya upimaji yanayoendelea katika manispaa hiyo.


RC Wangabo achangia mifuko 10 ya Saruji ujenzi wa Choo Kaswepepe.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amechangia mifuko 10 ya saruji kwaajili ya ujenzi wa choo kilichopo katika soko la mtaa wa Kaswepepe, kata ya Sumbawanga asilia, Mjini Sumbawanga ili wafanyabiashara wasipate shida ya huduma hiyo.

Mh. Wangabo amesema kuwa ameamua kuwekeza kwa wananchi na kuweza kumfuatilia Mkurugenzi ili kuona kama anatoa huduma stahiki kwa wananchi.

Ametoa ahadi hiyo baada ya kusimamisha msafara uliokuwa ukipita katika mtaa huo na kuona soko likiwa limeanzishwa kwenye barabara na kutaka kujua changamoto wanazokutana nazo katika shughuli zao za kila siku, ndipo mmoja wa wananchi hao alipotaja changamoto ya choo.

“Kama alivyosema Mkurugenzi, najua manispaa imeshajiandaa, na mimi nitatoa mifuko 10 ya “Cement” kuwaunga mkono na ninatoa hiyo mifuko 10 ili huyu mkurugenzi asinichenge kwasababu na mimi ni mdau nimekwisha wekeza hapo kwenye soko ili hawa kinamama wapate amahali pazuri pa kufanya biashara zao kwenye kivuli, wasinyanyaswe kwasababu wako kwenye maeneo kama haya,” Alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya alikiri kuwa uongozi wa soko hilo ulifika ofisini kwake ili kutatuliwa shida hiyo ya choo na kuelekeza kuwa ipo kwenye mpango wa kuboresha masoko katika kata 19 za Manispaa ya Sumbawanga.

“Kwasababu wao tayari wana eneo, tulisema suala la choo tutalishughulikia, tufanye ukamilishaji wa hicho choo, ili wananchi sasa kwa hiyari yao bila ya kuwalazimisha wala kuleta vurugu, tuwaombe waende eneo ambalo ni la soko kwaajili ya kupunguza hatari inayoweza kujitokeza,” Alibainisha.
Baadhi ya kinamama wakiendelea na biashara zao huku Wakimsikiliza mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (hayupo pichani) katika soko la Kawepepe, Sumbawanga mjini. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili kutoka kushoto) akiongea na wananchi wa soko la kaswepepe, Kata ya Sumbawanga Asilia, Mjini Sumbawanga. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule (waliosimama) wakiulizana juu ya vitu vya kununua katika Soko la Kaswepep. 

Suala hilo la choo liliibuliwa na mmoja wa wananchi wa mtaa huo Ditmali Mwageni ambae alimueleza Mkuu wa Mkoa juu ya sababu ya wao kufanya kazi pembeni ya barabara hadi kukutwa na msafara wake ni kutokuwa na choo katika eneo la soko jambo ambalo tayari wameshalifika katika Ofisi ya mkurugenzi wa Manispaa.

Friday, October 19, 2018

RC Wangabo amtaka DED Kuhamishia ofisi zake karibu na wananchi.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemtaka Mkurugenzi wa Halmauri ya Wilaya ya Sumbawanga kuhakikisha anahamishia ofisi zake karibu na wananchi ambao wanishi katika mipaka ya halmashauri yake na sio kubaki mjini.

Amesema kuwa kwa kufanya hivyo mji utatanuka na maendeleo yatapatikana na pia kupunguza gharama za kuwahudumia wananchi pindi majanga yanapotokea kwani kuwa nao karibu kutasababisha kutotumia pesa nyingi kuwafuata na wao kupata urahisi wa kufika katika ofisi hizo.

“Rai yangu mkurugenzi mtafute mahala kwingine kwa kujenga ofisi za halmashauri ya wilaya, mahala pengine ambapo ni ndani ya halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga na sio ndani ya manispaa, ofisi hii inapaswa iwe nje ya eneo la manispaa, faida yake ni kupanua huduma kuliko kila kitu kufikiria manispaa,” Alisema

Ameyasema hayo alipokwenda kukagua jengo jipya la halmashauri hiyo ambalo lilianza kujengwa mwaka 2012 na kutegemewa kumalizika mwaka 2013 japokuwa bado kukamilika ambapo serikali ilitenga shilingi bilioni 2.3 lakini hadi kufikia katika hatua ya sasa, tayari shilingi bilioni 1.6 zimeshatumika kupitia fedha za Ruzuku ya Miradi ya Maendeleo (CDG) ambapo kwa sasa imefutwa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (mbele) akikongoza ukaguzi wa jengo lililojengwa kwa madhumuni ya kuhamia ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. 


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (mbele kulia) pamojana na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule wakikagua jengo lililojengwa kwa madhumuni ya kuhamia ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. Jengo lililojengwa kwa madhumuni ya kuhamia ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. 


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo  (katikati) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga (kulia) na Mstahiki Meya Manispaa ya Sumbawanga Mh. Justin Malisawa (Kushoto)


Awali akitoa taarifa ya jengo hilo Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga John Msemakweli amesema kuwa halmashauri tayari imekwisha tuma andiko maalum na kupeleka wizara ya fedha na OR – TAMISEMI ili kuwezeshwa kumalizia jengo hilo litakalokuwa na ofisi 76 na kumbi 2.


“Hadi sasa tumeandika andiko maalum la jumla ya shilingi 716,933,989 ili kukamilisha mradi huu, tunategemea jengo hili likikamilika litakuwa na ofisi 76 na kumbi 2 ambazo zitakuwa zinatosheleza mahitaji ya ofisi za watumishi wote walio katika makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya,” Alibainisha.

Jengo hilo ambalo lipo karibu na jengo la Manispaa ya Sumbawanga halijatengewa fedha za kuliendeleza tangu mwaka wa fedha 2015/2016 hadi sasa.

Katika hatua nyingine, Mh. Wangabo alimuagiza Mkurugenzi huyo kuunda timu ya kuhakikisha wanapambana na mifugo inayoharibu barabara kwani serikali inatumia mabilioni kuzitengeneza na kuzikarabati na hivyo si vyema uharibifu huo ukaendelea.Thursday, October 18, 2018

RC Wangabo ataka “work plan” ujenzi wa VETA wenye thamani ya Bil.10.7


Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametaka kupewa mpango kazi wa ujenzi unaoendelea wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) cha Mkoa, kinachojengwa katika mtaa wa Kaswepepe, kata ya Sumbawanga asilia, Wilayani Sumbawanga ili kufuatilia kwa ukaribu na kuweza kukosoa pale mkandarasi atakapokwenda kinyume na alichokiandaa.

Amesema kuwa kwa kufanya hivyo, itasaidia kukosoa maendeleo ya ujenzi mapema kabla mambo hayajaharibika na si kulalamika baada ya kukamilika kwa ujenzi na kulaumu ubadhirifu uliojitokeza wakati fursa ya kufuatilia ilikuwepo.

“Ningependa nipatiwe “Work plan” mpango kazi ambao mnao, hatua kwa hatua ili na mimi nikikaa kule najua mwezi lazima mko hatua Fulani, nikiona inafaa ntakuja kukagua, mwenyekiti wa ulinzi na usalama Wilaya nae apewe mpango kazi, Mstahiki Meya nae apewe ili tufuatilie kwa pamoja ili kama kuna mapungufu tuambiane mapema, tusingoje kuviziana kwamba hili limeharibika,” Alisisitiza.


Ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Mkoa wa Rukwa. Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (mbele kulia) akitoa akitaka ufafanuzi juu ya uwakilishi wa  majengo kwa mashimo yaliyochimbwa. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) akitaka ufafanuzi juu ya uwakilishi wa majengo kwa mashimo yaliyochimbwa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiangalia ubora wa matofali yatakayotumika katika ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) ambapo Mkandarasi alisemakuwa anatumia mfuko mmoja wa saruji kutoa matofali 20. 

Ameongeza kuwa kwenda vibaya kwa mambo na kufika mwisho itashindikana kurudisha nyuma na matokeo yake ni kumfunga mhusika aliyesababisha uharibifu wakati fedha za serikali zimekwishapotea na huku wananchi bado wanahitaji maendeleo. Ameyasema hayo alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa chuo hicho.


Kwa upande wake akisoma taarifa ya ujenzi Mkadiriaji majengo wa ujenzi huo Faraji Selemani alisema kuwa ujenzi huo utagharimu shilingi bilioni 10.7 hadi kukamilika kwake ambapo kutakuwa na majengo tisa yatakayohusisha fani mbalimbali pamoja na jengo la utawala.

“mradi utakuwa na majengo yafuatayo, majengo ya utawala, madarasa pamoja na maktaba, “workshops” mbali mbali 9, mabweni ya wanafunzi wa kike na wakiume, vyumba vya waalimu na makazi yao na sehemu ya kufanyia mazoezi kwa vitendo,” Alimalizia.

Ujenzi huo ambao umeanza mapema mwezi wa tisa mwaka huu baada ya makabidhiano baina ya VETA makao makuu Dar es Salaam, VETA kanda ya nyanda za juu kusini Mbeya pamoja na Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa kumkabidhi mkandarasi TENDER Intarnational kwaajili ya ujenzi wa chuo hicho huku mshauri elekezi akiwa Sky Architect Consultancy Ltd.

Ujenzi ukikamilika chuo kitaweza kuchukua wanafunzi 900 wa kozi ndefu na 600 wa kozi fupi hivyo, kitakuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 1,500.


Wednesday, October 17, 2018

Wanafunzi 1,500 kupata nafasi ya kusoma VETA Sumbawanga.


Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewahakikishia wanafunzi wanaokisubiri kwa hamu chuo cha ufundi stadi (VETA) cha Mkoa kuwa kinatarajiwa kukamilika mwezi wa nane mwaka 2019 na kitakuwa na uwezo wa kusomesha wanafunzi 1,500 kwa wakati mmoja.
 
Eneo la Ekari 95 linalojengwa Chuo cha Ufundi Stadi eneo la Kashai, Manispaa ya Sumbawanga. 

Katibu tawala Msaidizi Seksheni ya Serikali za mitaa Albinus Mgonya akipewa ufafanuzi wa ujenzi unaoendelea na Mkandarasi wa ujenzi wa chuo hicho cha VETA wakati alipokwenda kutembela kuona maendeleo ya ujenzi wa Chuo hicho. 

Ujenzi huo ambao umeanza mapema mwezi wa tisa mwaka huu baada ya makabidhiano baina ya VETA makao makuu Dar es Salaam, VETA kanda ya nyanda za juu kusini Mbeya pamoja na Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa kumkabidhi mkandarasi TENDER Intarnational kwaajili ya ujenzi wa chuo hicho huku mshauri elekezi akiwa Sky Architect Consultancy Ltd.

Chuo hicho kinachotarajiwa kujengwa katika manispaa ya Sumbawanga eneo la Kashai (MUVA) lina ukubwa wa Ekari 95, kiwanja ambacho tayari kina hati iliyotolewa mapema mwezi wa tatu mwaka huu kwa umiliki halali wa VETA.

“Gharama za ujenzi za mradi huu ni Tsh. 10,700,488,940.05. Ujenzi ukikamilika chuo kitaweza kuchukua wanafunzi 900 wa kozi ndefu na 600 wa kozi fupi hivyo, kitakuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 1,500.” Alisema.

Mbali na chuo hicho cha VETA cha Sumbawanga, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi pia tayari imekabidhiwa majengo ya aliyekuwa mshauri elekezi wa mradi wa mradi wa barabara ya Sumbawanga – Kibaoni yaliyopo katika kijiji cha Paramawe kwaajili ya kuanzisha chuo cha VETA na hivyo kufanya Mkoa kuwa na vyuo viwili vya VETA.

Daraja la Bil. 17.7 linalounganisha Rukwa na Songwe kukamilika Februari 2019.


Katika kuhakikisha kuwa mawasiliano ya wananchi wa mikoa miwili katika sekta ya uchumi na uzalishaji yanakuwa serikali ya awamu ya tano imeendelea kuboresha hayo kwa kujenga daraja kubwa lenye urefu wa mita 84 linalounganisha Mkoa wa Rukwa na Songwe kupitia kijiji cha Kilyamatundu, bonde la ziwa rukwa katika mto Momba.

Ujenzi wa daraja hilo ulianza mwanzoni mwa mwezi wa nane mwaka 2017 ambapo ulipaswa kukamilika baada ya miezi 13 yaani mwezi wa nane mwaka huu. Aidha kutokana na changamoto za mafuriko ya mto huo wakati wa mvua za masika, kazi za ujenzi ziliahirishwa na kutegemewa kukamilika mwezi wa pili mwaka 2019.
Ujenzi unaendelea wa daraja la mto Momba katika kijiji cha kilyamatundu.

Katibu Tawala msaidizi Secsheni ya Serikali za Mitaa Albinus Mgonya (Kulia)  akiagana na mkandarasi wa ujenzi wa daraja hilo. baada ya kutembelea ili kuona maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo.  

Katibu Tawala msaidizi Secsheni ya Serikali za Mitaa Albinus Mgonya (shati la kitenge kushoto)  akitaka maelezo kutoka kwa mshauri elekezi wa ujenzi wa daraja hilo baada ya kulitembelea kujua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo.


Ameyasema hayo katibu tawala msaidizi seksheni ya serikali za mitaa Albinus Mgonya wakati wa kuwasilisha taarifa mbalimbali kwa mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ambapo amesema gharama ya ujenzi wa daraja hilo Shilingi Bilioni 17.7.

Hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 65 ambapo tayari mkandarasi amekwishajenga nguzo (pivers) mbili na kingo (abutments) mbili za upande wa Kilyamatundu na Kamsamba pia ujenzi wa beams na sakafu (deck slab) umekamilika,” Alisema.

Kukamilika kwa Daraja hili kutaongeza fursa za kiuchumi katika eneo la Bonde la Ziwa Rukwa hivyo kuendelea kuifungua Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla.

Hatimae Rukwa wapata hatima ya soko la mahindi.

Kutokana na zao la mahindi kuwa ni zao la chakula na biashara katika mkoa wa Rukwa, kuyumba kwa soko hilo kwa mwaka 2017/2018 kumewafanya wananchi waliowengi kukosa kipato cha uhakika ambacho kingewasaidia kukidhi mahitaji yao mbalimbali.
Mahindi

Ili kuhakikisha kuwa wakulima wanaondokana na kadhia hiyo na hatimae kupata soko la uhakika serikali ya mkoa wa Rukwa imeandaa mikakati mbalimbali kukabiliana na kusuasua huko kwa soko la mahindi.

Akizungumza mbele ya mkuu wa mkoa wa Rukwa, Kaimu Mkuu wa Seksheni ya Uchumi na Uzalishaji Ocran Chengula amesema kuwa serikali ya mkoa umefanya jitihada kadhaa ili kuhakikisha mwananchi wa Rukwa anaondokana na kadhia hiyo ya soko la mahindi na hatimae kupata suluhisho la kuuza mazao yake kwa bei nzuri.
“Tumedhamiria kuwaunganisha wakulima na masoko ya mahindi kama WFP (Worl Food Programme) kupitia  taasisi ya BRITEN (Building Rural Income Trough Enterprise) ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wafanyabiashara na wajasiriamali kwa kuwaelekeza taratibu za kufuata ili kukidhi vigezo vya kuuza mazao nje ya nchi.” Alisema
Aidha, Aliongeza kuwa kuviunganisha vikundi vya wakulima (SACCOS na AMCOS) ili kuuza mahindi kwa Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Sumbawanga. Ambapo ununuzi wa Mahindi meupe utaanza kupitia vikundi hivyo jambo litakalosaidia kuongeza wigo wa soko la Mahindi.
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Sumbawanga katika msimu huu wa 2018/2019 wamepanga kununua kiasi cha tani 5,500 tu za mahindi meupe katika Mkoa wa Rukwa, kiasi ambacho ni kidogo kulinganisha na ziada ya tani 453,049.2 zilizozalishwa kwa msimu wa 2017/2018.

Monday, October 15, 2018

Wasanii Rukwa Waomba Uwekezaji kwenye Utayarishaji wa “Audio” na “Video”

Wasanii wa fani mbalimbali mjini Sumbawanga, Mkoani Rukwa wameeleza kilio chao juu ya utayarishaji mbovu wa sauti za muziki na picha za video unaofanywa na watayarishaji waliopo ndani ya mkoa na kuwaomba wadau wa sanaa kutoka katika mikoa iliyoendelea katika fani hiyo kuja kuwekeza ili waweze kuleta ushindani katika sanaa.

Msanii Martin Gongwe akiimba wakati wa mashindano ya Super Nyota yaliyofanyika mjini Sumbawanga na kuendeshwa na Clouds Media Group. 


Kilio hicho kimetolewa baada ya Afisa utamaduni wa Manispaa ya Sumbawanga, Charles Kiheka, kuwaita wasanii hao wa fani mbalimbali ili kujua changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo pamoja kuwaelimisha miongozo na taratibu mbalimbali zinazotakiwa kufuatwa ili kutokiuka taratibu za kiserikali katika kufanya shughuli zao za sanaa.

Mmoja wa wasanii wa Hip-hop, Martin Gondwe amesema kuwa ‘studio’ zilizopo zimekosa vifaa vizuri vitakavyomwezesha msanii aliyerekodi nyimbo yake mjini Sumbawanga kuweza kuleta ushindani katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
“Vile vile tukizungumzia upande wa “video”, wasanii wanakuwa wanafanya nyimbo inakuwa na “quality” (ubora) ndogo, “Audio” inakuwa ya kawaida, pamoja na “video” pia inakuwa ya kawaida yaani kila kitu kibovu, huwezi kuifikisha hiyo nyimbo yako sehemu yoyote,” Alisisitiza.

Nae Steven Stanley, msanii wa Hip-hop aliongeza kuwa kutokana na ubovu wa kazi zinazofanywa na watayarishaji wa muziki katika upande wa sauti na picha inapelekea wasanii wengi kushindwa kuwashawishi wadau wa sanaa na hatimae kukosa kusaidiwa ili kuweza kusonga mbele zaidi.
“”Video” zinakuwa ziko “local” kiasi kwamba huwezi ukamshawishi mtu anunue, kwasababu kila mtu anapenda kitu kizuri, kwahiyo mtu akiona “video” nzuri anasema hii nimeipenda na akiona kitu kibaya anasema piga chini, ila ukosefu wa “production” ndio “una-cost” kabisa, kwasababu siwezi nikarekodi nyimbo hapa ambayo “production” ipo “local” halafu nikatuma Dar,” Alibainisha.
Kwa upande wake Charles Kiheka alileza kuwa wasanii hawatakiwi kusubiri sherehe za kiserikali pekee kama fursa ya kujitangaza bali ni jukumu la msanii kuwa mbunifu katika kuandaa matamasha hayo na hatimae kuonana nae ili kuona namna ya kumsaidia katika kukamilisha mipango ya msanii aliyonayo ili kujiongezea kipato kwa kumpa vibali vyote stahiki pamoja na ushauri wa mikataba mbalimbali anayotaka kuingia na wadau wa burudani.
Afisa utamaduni wa Manispaa ya Sumbawanga akitoa elimu kwa wasanii wa Sumbawanga (hawapo pichani) juu ya namna ya kutafuta fursa za kujipatia kipato kwa kuanzisha matamasha mbalimbali.
“Leo hii msanii anakwambia serikali iandae “event” aje “kuperform” wasanii wapo wangapi na matukio ya serikali sio ya kila siku, wewe kama mdau wa sanaa, kama msanii ni jukumu lako kuandaa matukio mbalimbali, unakuja na mipango yako ofisini tunaelekezana namna ya kufanya na kuzitafutia ufumbuzi changamoto unazoweza kukabiliana nazo,”Alisema Kiheka.
Katika juhudi za kuhakikisha wasanii hao wanajifunza namna ya kuandaa matamasha, Kiheka anatarajia kuzindua tamasha la “Amka Kijana, Onesha Kipaji Chako” litakalojumuisha mashindano ya sanaa za fani mbalimbali, kuanzia kuimba, kuigiza, ngoma za asili, pamoja na kucheza nyimbo za kisasa (ku-dance) kabla ya kuisha mwaka 2018.

Manispaa ya Sumbawanga yaibuka mshindi wa kitaifa mbio za mwenge wa uhuru

Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa imeibuka mshindi wa kitaifa wa mbio za za Mwenge wa Uhuru uliowashwa mwezi April katika viwanja vya magogo Mkoani Geita na na kuzimwa mwezi oktoba siku ya kumbukumbu ya kifo cha Mwl. Julius Nyerere katika Kiwanja Mkwakwani Mkoani Tanga na kukimbizwa katika Halmashauri 195 nchini.
Mkimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa Charles Kabeho ( Kushoto) akimnong'oneza na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo wakati wakisubiri mwenge ukitokea Mkoa wa Katavi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Walemavu Jenista Mhagama amesema kwamba halmashauri hiyo itapewa zawadi ya kikombe na shilingi milioni tano.

“Mheshimiwa Rais wa Zanzibar naomba sasa nimtaje mshindi wa kitaifa ambae ni Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kutoka mkoa wa Rukwa, mshindi huyu watapewa zawadi ya kikombe cheti na fedha taslimu shilingi milioni tano,” Mhagama alisema.
Manispaa ya Sumbawanga ilitumia zaidi ya Shilingi Bilioni 11.2 katika miradi 10 ikiwemo, ujenzi wa kituo cha afya Mazwi, ujenzi wa Zahanati katumba azimio, miradi minne ya maji, ujenzi wa shule mpya, ujenzi wa barabara zaidi ya Km 5.
Wengine ambao wamechukua ushindi na kupewa kikombe na cheti ni Mkoa wa Geita kwa Kuwasha mwenge huo, Mkoa wa Tanga kwa kuuzima mwenge huo, na washindi wengine wa kanda tano ambao watapewa cheti, kikombe na fedha taslim shilingi milioni moja ni Halmashauri ya Jiji la Arusha, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze na Wilaya ya kusini.