Thursday, January 17, 2019

RC Wangabo azihamasishaTaasisi na wananchi kufika Msitu wa mbizi kuchuku...

Maafisa Kilimo na ugani watakiwa kuwafuata wakulima mashambani kutoa elimu ya viwavi jeshi vamizi.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza maafisa ugani wote wa mkoani humo kuhakikisha wanawafikia wakulima kwenye mashamba yao na kuwapa elimu ya kukabiliana na wadudu aina ya viwavijeshi vamizi ambao wanaonekana kuanza kuleta athari katika wilaya ya Nkasi.
Amesema kuwa wakulima wengi hawana elimu ya kukabiliana na wadudu hao hasa kujua aina ya dawa ya kutumia ili kuwaua na wasiendelee kuharibu mazao na kuongeza kuwa ni wakati wao sasa maafisa ugani kufanya kazi ya kuwasaidia wananchi kupata matokeo bora ya mavuno kwa kutoa elimu ya kukabiliana na wadudu waharibifu na magonjwa.
“Kitu cha kufanya ni maafisa ugani wote na maafisa kilimo wote washuke kwenda kwenye mashamba, wakague na kutoa ushauri wa moja kwa moja, dawa zipo zinapatikana wanaanzia dawa gani inayofuata ni ipi, ili tuweze kuwasaidia wakulima waweze kuokoa haya mahindi, DC hawa watu wasimamiwe washuke asibaki mtu kwenye ofisi zao,” Alisisitiza.
Ameyasema hayo baada ya kuona athari ya viwavi jeshi alipotembelea shamba la mkulima wa mahindi Alex Ndenge katika ziara yake ya kuangalia maendeleo ya kilimo kwa wakulima na changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo upatikanaji wa pembejeo pamoja na mashambulizi ya wadudu na magonjwa ya mazao Wilayani Nkasi.
Mkulima wa Zao la Mahindi, Namayere Wilayani Nkasi Alex Kwandenge (kulia) akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo (wa pili toka kulia) pamoja na timu ya ke ya wataalamu wa Mkoa na Wilaya juu ya athari ya viwavijeshi vamizi katika shamba lake.

Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Mkoa wa Rukwa Ocran Chengula alifafanua namna ya kupambana na wadudu hao na kutoa tahadhari kwa wakulima kuwa na tabia ya kupanda kwa kipindi kimoja na sio kupishana kwani hali hiyo hupelekea wadudu hao kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine ili kufuata mimea teke.

“Kuna sumu nyingine ukipiga inakuwa kwenye mmea, kwasababu huyu (mdudu) anatoa kinyesi kwahiyo ile sumu inaingia kwenye mmea kwahiyo anapokula anapata madhara anakufa, kwahiyo katika hatua za kwanza tunashauri (dawa aina ya) Duduba na hatua ya pili tunashauri dawa inaitwa “systemic” japo zina majina tofauti tofauti ni amjina ya kibiashara ila itumike hiyo baada ya kuona kwamba wameshaanza kutoa huu uchafu” Alieleza.
Kwa mujibu wa Afisa kilimo wa halmashauri ya wilaya ya Nkasi Emanuel Sekwao amesema kuwa viwavijeshi vamizi hao wameshaathiri kwa asilimia 2 mpaka 5 kutegemea eneo lakini bado haijafikia hatua ya wadudu hao kuharibu mimea kiasi cha kushindwa kuzaa.
Katika kipindi cha mwaka 2018/19 mkoa unalenga kulima jumla ya hekta 599,345.45 za mazao mbalimbali, kati ya hizo hekta 517,482.15 ni za mazao ya chakula na hekta 81,863.3 za mazao ya biashara.  Kutokana na eneo hilo mkoa unategemea kuzalisha jumla ya tani 1,817,171.84 za mazao ya chakula na biashara. Katika kiasi hicho tani 1,680,701.6 ni za mazao ya chakula na tani 136,470.25 ni za mazao ya biashara.

Wanafunzi watoro na wazazi wao kusakwa na kukamatwa huku hostel ikibadilishwa matumizi.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza mkuu wa Wilaya ya Nkasi kuhakikisha anawatumia watendaji wa kata na vijiji pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kuhakikisha wanawasaka na kuwakamata wanafunzi watoro pamoja na wazazi waoili kuhakikisha wanafunzi wote wanafika shule.
Amesema kuwa kwa kufanya hivyo itakuwa fundisho kwa wazazi ambao kwa makusudi wanaacha watoto wao kutokwenda shule huku akipigia mfano faida ya elimu kwa kuwataja viongozi mbalimbali wa kiserikali akiwemo yeye mwenyewe pamoja na wataalamu waliozingatia elimu na matokeo yake wamefanikiwa kimaisha.
“Kuna wanafunzi 173 watoro, hawajafika shuleni, sasa Mkurugenzi fuatilia shule yako, mkuu wa wilaya tumia watendaji wa vijiji, wa kata, kamati yako ya ulinzi, sakeni wanafunzi wote kamateni wazazi wao mpaka walete watoto wao shule, hatubembelezani hapa,”Alibainisha.
Ameyasema hayo alipotembelea shule ya sekondari Korongwe Beach katika Kijiji cha korongwe, kata ya Korongwe Wilayani Nkasi ili kujionea mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza pamoja na ujenzi wa madarasa ambapo wanafunzi 50 wamepangiwa kuanza kidato cha kwanza huku 17 tu wakiwa wameripoti na shule ikiwa na jumla ya wanafunzi 383.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.

Awali akitoa taarifa ya shule hiyo Mwalimu Mkuu wa shule Nicomedi Ntepele amezitaja changamoto za shule hiyo ikiwemo utorowa rejareja na wa kudumu, ukosefu wa madarasa na nyumba za waalimu, ofisi za waalimu na maji.
“miongoni mwa changamoto tulizonazo hapa shule ni pamoja na utoro wa wanafunzi wa reja reja na wa kudumu, ukosefu wa madarasa, pia wazazi kutokuwa na uelewa kuwaleta Watoto wao kuishi hostel, uhaba wa maji eneo la shule, ofisi za walimu kutokamilika hivyo tunaomba changamoto hizi kufanyiwa kazi ili tufanye kazi kwa ufanisi,” Alimalizia.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Missana Kwangula aliamua kubadilia matumizi ya hosteli ya wanafunzi wa kike kutumiwa na wanafunzi wa kiume baada ya Mh. Wangabo kumtaka ajibu maombi ya mwanafunzi Ibrahimu Musa ambaye pia ni kaka mkuu wa shule hiyo juu ya kujengewa hosteli  baada ya Mkuu wa Mkoa kutoa nafasi kwa wanafunzi kuuliza maswali.
“Wanafunzi tunatembea umbali mrefu hasa Watoto wa jinsia ya kiume, sisi tulikuwa tunaomba ndugu Mkuu wa Mkoa uweze kutujengea sisi pia hosteli ili na sisi tuweze kukaa bweni nasi tuweze kufanya vizuri katika masomo yetu,”Alisema
Katika shule hiyo ya Korongwe Beach Sekondari kuna hosteli ya wanawake iliyojengwa kwa msaada wa watu wa Japan (JAICA) pamoja na serikali ya Tanzania, hosteli ambayo kwa mujibu wa taarifa ya mwalimu mkuu wa shule haijawahi kutumika tangu kumaliziwa kwake, ndipo Mkurugenzi aliposema.
“Hosteli ile ilipojengwa ilikuwa ni kwaajili ya kuawasaidia Watoto wa kike kwasababu ndio wanachangamoto zaidi, lakini kwasababu hosteli ile hawaingii walengwa ambao wako hapa, tuna uwezo tu wa kuibadilisha matumizi na uiandika hosteli ya wavulana kuliko kujenga hosteli nyingine, tutakapobadili matumizi ninyi Watoto wa kike msige kuidai tena wakati ipo sasa hamuingii,” Alimalizia.
Shule ya Sekondari Korongwe Beach ina wanafunzi 383 na kushika nafasi ya kwanza kiwilaya katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2018. Na wanafunzi 50 wamepangwa kuanza kidato cha kwanza huku 17 wakiwa wameripoti shuleni.

RC Wangabo asisitiza ushirikiano baina ya watendaji wa ngazi zote kutatua changamoto za elimu.


Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Nkasi, kuhakikisha kila mtumishi kwa nafasi yake na majukumu yake anashirikishwa katika kutatua changamoto za wananchi ikiwemo elimu, afya, maji na kilimo pamojana kushirikiana na wananchi kutatua chnagmoto hizo.

Amesema kuwa ili kutatua hayo halmashauri inapaswa kuongeza vyanzo vya mapato ikiwemo kuzidisha malengo ya makusanyo kwa mwaka ili kuweza kukabiliana na changamoto anazokuwa anasomewa kila anapofanya ziara katika shule mbalimbali za halmashauri na kumuomba achangie kutatua changamoto zao.

“Mpige hesabu zote muwarudishie huko jamii ili jamii iguswe kwamba alaa! Kumbe kuna changamoto kubwa sana zisingoje sisi viongozi ambao pengine hatuna nafasi ya kuzunguka sekondari zote, lakini kama tutafanya hivi tutaondoa changamoto zote hizi na matatizo na haya yote mliyoyasema yako chini ya uwezo wenu, sio mambo ya mkuu wa mkoa haya, ni mambo ya Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Nkasi, kata na vijiji vyenu, kama ni “support” tunatoa ya kuhamasisha,naweza kusema nanunua bati mbili tatu, je, ninatatua matatizo yote hayo?”Alibainisha.

Ameongeza kuwa kazi ya shule ni kuandaa taarifa nzuri na kuikabidhi kwa watendaji wa halmashauri kuanzia Mtendaji wa kata na vijiji pamoja na viongozi wa kisiasa akiwemo diwani wa kata husika ili taarifa hizo ziwafikie wananchi watambue kupitia vikao vya kamati ya maendeleo ya kata ambao ni mfumo mzuri uliowekwa na serikali katika kutambua changamoto na kuzitatua.

Ameyasema hayo baada ya kupokea taarifa ya shule ya sekondari Chala, iliyopo kata ya Chala Wilayani Nkasi na mkuu wa shule hiyo Fatma Mchomvu aliyemuomba kufanya harambee ya haraka kutoka kwa msafara alioambatana naoi li kuweza kukarabati nyumba ya “Matron” ambapo hadi wanafikisha ombi hilo waalimu walikwishajichangisha shilingi 50,000/-.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akizungumza na wananfunzi wa Shule ya Sekondari Chala. 

“Walimu wamejitolea kuchangia 50,000/- kusaidia kukarabati nyumba moja ya mwalimu ya “matron” kwasababu kule wanafunzi wako peke yao hakuna ulinzi kwahiyo nao wakaomba kupitia msafara wako, na wewe ndio kiongozi wetu tupate harambee ya haraka ili angalau tuanze kufanya ukarabati wa jengo hilo ili angalau wanafunzi wawe salama kwasababu wanakaa mbali na hakuna mlezi wa kukaa nae kule,” Alifafanua.Nkasi waitikia wito wa serikali katika kukikuza kilimo cha kahawa Mkoani wa Rukwa.


Wakulima katika halmashauri ya wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa wameitikia wito wa kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza zao la kahawa mkoani Rukwa na kuhakikisha wanalima zao hilo kwa wingi ili kubadili kipato chao na hatimae kushawishi wawekezaji wa kuchakata zao hilo kuwekeza Mkoani humo ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Zao la kahawa ni miongozi mwa mazao matano ya kimkakati yanayohimizwa na serikali ya awamu ya tano katika kuinua kipato cha wananchi pamoja na pato la nchi kwa ujumla.

Wakulima hao wakiongozwa na mkulima mzoefu wa zao hilo Elias Mwazembe alisema kuwa zao la kahawa linastawi katika mkoa mzima wa Rukwa hivyo aliushukuru uongozi wa Wilaya pamoja na Mkoa kwa kuendelea kuwasaidia pale wanapokwama mbali na changamoto aliyoipata mara ya kwanza alipolima katika hifadhi yam situ wa mfili na kuondolewa na serikali.

“Nilipoona kwenye Mkoa inakubali na kwenye wilaya ikabidi nije huku (Kijiji cha) Kalundi nikaanzisha kulima mwezi wa tatu nikaona ile kahawa inastawi vizuri kwahiyo nikaona hapa sio pa kuachilia niendelee na zao la kilimo lakini sikutulia niliendeleza hamasa kwa watu wengine kuwaambia kuwa zao la kahawa mkoani Kwetu linakubali ingawa changamoto ikawa mtu alikuwa anahitaji avune kwa mwaka huo huo nikasema mbegu iliyopo ni miaka miwili unaweza kuvuna kahawa na kwa umri nilionao nitavuna mpaka vitukuu,” alisema.

Nae Afisa kilimo wa Kijiji cha Kalundi Jiasi Muyunga alikiri kuwa kitendo cha mkulima huyo Elias Mwazembe kufika katika Kijiji hicho kumepelekea wakulima wengi kutaka kujihusisha na kilimo hicho cha kahawa baada ya kuona kuwa kinastawi vizuri katika Kijiji hicho na hivyo kutoka wito kwa maafisa ugani wenzie juu ya kuwasaidia wakulima na kuwakikishia kuwa zao hilo ndilo litakalokuwa mkombozi.

Kwa upande wake Afisa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi alisema kuwa baada ya kubaini kwamba kata 18 zilizopo ufipa ya juu zenye eneo la hekta 48,000 kuwa zinafaa kulima zao hilo hal,mashauri ilianisha maeneo ya kuanza nayo huku wakishirikiana na kituo cha utafiti cha Tacri kilichopo Mbimba Wilaya ya Mbozi, ili kujua mbegu inayofaa katika maeneo hayo na hatimae kuwapeleka wataalamu na wakulima kwenda kujifunza.

“Mkulima ambaye tumemtembelea leo ndugu Mwazembe ni mmoja wa wakulima hao ambao nae alikwenda kujifunza Mbimba na baada ya kutoka huko aliendeleza juhudi za kufanya kilimo hiki cha kahawa na tunae mkulima mwingine yupo Kijiji cha Kakoma kata ya Namanyere nae pia mepanda kahawa karibu miche 500 na kitaluni ana miche karibu 12,000 na kuna taasisi zaidi ya sita ambazo tumepa miche iliyotokana na kilo 100 za mbegu ambapo kila kilo moja inatoa miche 4000, hivyo tunaamini baada ya miaka mitatu halmashauri itaanza kuona faida yake,” Alisisitiza.

Aidha Afisa kilimo wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ocran Chengula aliwashauri wakulima wote wanaotarajia kuanza kilimo hicho cha kahawa kuhakikisha kuwa wanaandaa mashimo mapema na kuweka mbolea ili iweze kuchangayikana na udongo.

“Tunatakiwa kuandaa mashimo mapema, kama unategemea kupanda mwaka huu maana yake unaze kuandaa mashimo mwezi wa nane ama wa tisa kwa kuchimba mashimo na kuweka mbolea ili mbolea iweze kuchanganyikana na udongo ikishaanza mvua mwezi wa kumi na moja ile miche inatakiwa ihamishwe kwenye mashamba ili mvua itakavyonyesha iweze kushika na kuwa na nguvu zaidi ya kuweza kukua,” Alifafanua.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiwa amesimama katikati ya kitalu cha miche ya mikahawa katika shamba la mkulima Elias Mwazembe wa kijiji cha Kalundi, kata ya Myula, Wilayani Nkasi. 

Mkoa wa Rukwa unategemea kuwa na miche 1,040,000 ifikapo mwakani inayotokana na kilo 260 za mbegu za kahawa inayopandwa kwenye vitalu mwaka huu ili kuweza kuisambaza kwa wakulima na taasisi mbalimbali ikiwa ni kuhamasisha kilimo cha zao hilo pamoja na kuinua kipato cha wananchi, mkoa na taifa kwa ujumla.

Ujumbe wa “Niache Nisome” kutawala katika “T-shirt” za wananfunzi Rukwa.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza Wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wananfunzi wa shule zote za serikali katika halmashauri za mkoa huo zinaandikwa ujumbe wa “Niache Nisome” kwa herufi kubwa mbele ya flana zao za shule ili kuufikisha ujumbe huo kwa wale wote wenye nia na dhamira ya kukwamisha masomo ya wanafunzi hao kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha sita.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili toka kushoto nyuma) katika picha ya pamoja na viongozi wa kiserikali na wawakilishi wa wananchi pamoja na baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Kate waliovalia flana zilizoandikwa "Niache Nisome"

Amesema kuwa kwa kufanya hivyo kutapunguza idadi ya wanafunzi wa kike kupata mimba pamoja na kumaliza utoro kwani ujumbe huo utawalenga wazazi pamoja na vijana wenye tabia ya kuwanyemelea wanafunzi wa kike na kuwalaghai kwa kuwanunulia chipsi pamoja na kuwapakiza bure katika usafiri wa pikipiki maarufu kama Bodaboda ili waweze kuwapa mimba na hatimae kukatisha masomo yao.


“shule zote ziandikwe maneno “niache Nisome” Mkurugenzi kama kuna “T-shirt” imeandikwa maneno mengine zifutwe, ziandikwe “Niache Nisome” tena ziwe na herufi kubwa nzuri, ujumbe huu ufike mbali, ujumbe kwa watanzania, ujumbe wa watu wote wa mkoa wa Rukwa “Niacheni Nisome” Msitusumbue, vichipsi chipsi vile hakuna kwa Watoto wa kike, sijui bodaboda, utoro utoro, “Niacheni Nisome””, Alisema.

Aliyasema hayo alipotembelea katika shule ya sekondari Kate, iliyopo Kata ya Kate, Wilayani Nkasi na kupokea taarifa ya shule hiyo iliyoonyesha ufaulu mzuri kwa wananfunzi wa kidato cha sita na ufaulu mbovu kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne jambo lililopelekea Mkuu wa Mkoa kushtushwa na hali hiyo ya wanafunzi kuwa katika shule moja na kuwa na ufaulu tofauti.

Halikadhalika alielezea kuwa kitendo cha wanafunzi wa kidato cha kwanza kushindwa kufika shuleni kwa wakati na kuwa watoro ni sababu mojawapo ya kupelekea kushindwa mitihani ya kidato cha pili kutokana na kuwakuta wanafunzi wenzao wakiwa wamekwishapiga hatua katika masomo na ukizingatia kuwa lugha ya kufundishia ni ya kigeni hivyo hupelekea mwanafunzi huyo kushindwa kuwa sawa na wanafunzi wenziwe na hatimae kukata tamaa, hali inayopelekea kushindwa kidato cha nne.

Kwa upande wake makamu mkuu wa shule ya sekondari Kate alisema kuwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2019 katika shule hiyo, wa kiume ni 144 na wa kike ni 155 na kufanya jumla yao kuwa 299 huku walioripoti wa kiume wakiwa 27 na wa kike 19 na kufanya jumla yao kuwa 46 na hivyo wanafunzi 253 bado kuripoti shuleni hapo tangu shule kufunguliwa tarehe 7.1.2019.

Wiki ya Kwanza ya Ufunguzi wa Shule za Sekondari na mahudhurio ya Kidato cha Kwanza katika Shule za Sekondari alizozitembelea Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.

Shule
Waliopangiwa
Walioripoti
1.
Shule ya Sekondari Kate
299
46
2.
Shule ya Sekondari Chala
100
37
3.
Shule ya Sekondari Korongwe beach
50
17
4.
Shule ya Sekondari Kala
153
38

Wananchi kata ya Kala wamlilia RC baada ya kukosa mawasiliano ya simu na radio.


Wananchi wa kata ya Kala yenye vijiji vitano iliyopo katika wilaya ya Nkasi wamefikisha kilio chao cha kukosa mawasiliano ya simu kwa mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ili aweze kuwasaidia kutatua kero hiyo ambayo inakwamisha maendeleo ya kata.

Kilio hicho kimetolewa wakati wa kusoma risala ya maendeleo ya kata na msoma risala Felix Kapoze alipokuwa akielezea changamoto mbalimbali zinazoikabili kata hiyo kwa muda mrefu jambo linalokwamisha utendaji kazi pamoja na kufanya mawasiliano kuwa magumu.

“Changamoto nyingine kubwa ilipo hapa Kijijini kutokuwapo kwa mtandao wa simu, hii inapelekeana kukwama kwa taarifa nyingi hasa katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo hivyo tunaiomba ofisi ya Mkuu wa Mkoa itusaidie kupatikana kwa mtandao wa simu ili kurahisisha mawasiliano,” Alifafanua.

Halikadhalika jambo hilo liliungwa mkono na mbunge wa jimbo la Nkasi Kusini Mh. Desderius Mipata wakati akielezea changamoto hiyo na hatua alizochukua kuhakikisha kuwa mawasiliano hayo yanapatinaka na hatimae kurahisisha utendaji kazi wa shughuli za maendeleo katika kata hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akipokea risala ya Kata ya Kala, muda mfupi baada ya kusomewa risala hiyo na msomaji Felix Kapoze (kushoto)

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akizungumza na wananchi wa kata ya kala wilayani Nkasi.

“Hawa wananchi ni pekee ambao hawazungumzi na wenzao katika taifa na katika jimbo, juhudi nilizozifanya kama kiongozi wa jimbo ni kuitaka wizara ihakikishe kwamba tunapata mtandao, tunashukuru mungu wametusikiliza na sasa wanajenga minara miwili katika Kijiji cha kilambo cha mkolechi na Kijiji cha Kala, wanasema Kala itazungumza wantuambia katika kipindi kisichozidi miezi miwili,” Alibainisha.

Nae Mh. Wangabo aliwahakikishia wananchi wa kata hiyo kuwa mawasiliano yataimarishwa “Tutaimarisha hayo mawasiliano na juzi nilikuwa naongea na waziri wa ujenzi alikuja pale ofisini na tuliongea swala hili la minara ya mawasiliano, uzuri wameshaanza kufanyia kazi, kwahiyo tutaongeza nguvu kule ili mitandao ya mawasiliano ifanye kazi n ahata radio nkasi iweze kuwafikia huku,” Alisema.

Shule ya Sekondari kala yatekeleza agizo la RC Rukwa.


Katika kuhakikisha wananfunzi wa shule ya sekondari Kala iliyopo kata ya Kala, Wilayani Nkasi wanapata uelewa wa kutosha na kuweza kuwashawishi wazazi wao kuanza kulima zao la alizeti shule hiyo imeanza kulima zao hilo ili kuona faida watakayoipata na hatimae kuwashawishi wananchi wanaozunguka shule hiyo kulima zao hilo.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Kala Albert Mlonge pia alimuomba mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo kuweza kusaidia kuendelea kuwashawishi wananchi wa eneo hilo kuweza kulima zao hilo ambalo katika ekari moja ya shule iliyolimwa zao hilo inaonekana kufanya vizuri.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa katika kuitikia agizo lako uliowaita wadau na kuwashawishi kuhusu mazao ya biashara, sisi kama washawishi na watoa elimu tumeitikia kwa asilimia kubwa kwa kilimo cha Alizeti, tumejaribu kuanza ekari moja ya alizeti na linaenda vizuri, katika jitihafda hizi katika Kijiji cha King’ombe kata ya Kala ni sehemu ambayo alizeti inakuwa vizuri n ahata bila ya mbolea, tunakuomba uendelee kuwashawishi wananchi walime zao hili,” Alisema.

Nae, Mh. Wangabo aliipongeza shule hiyo kwa kuitikia wito wake na kuwa mfano bora kwa wananchi wa Kijiji cha King’ombe na hatimae kuweza kuwafundisha wananfunzi juu ya mtazamo wa zao hilo la kibiashara.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili Kulia) akitambulishwa kwa waalimu wa shule ya sekondari Kala na mkuu wa Shule hiyo Albert Mlonge (wa Kwanza Kulia) muda mfupi baada ya kuwasili katika shule hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kala 

RC Wangabo ashtushwa baada ya kuona vijiji vitatu vinachangia shule ya msingi moja.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wananchi wa Kata ya Paramawe yenye vijiji vitatu vya Lyazumbi, Paramawe ‘A’ na ‘B’ kuchangia shule moja ya msingi huku shule hiyo ikiwa na upungufu wa madarasa ya kuwahifadhi wananfunzi 1400 wa shule hiyo iliyopo wilayani Nkasi.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo akiingia kati ya moja ya madarasa ya Shule shikizi ya kijiji cha Lyazumbi.

Viongozi mbalimbali na wataalamu wa ngazi ya Mkoa na Wilaya ya Nkasi pamoja na serikali ya Kijiji cha Lyazumbi wakiangalia moja ya madarasa ya shule shikizi ya kijiji cha Lyazumbi (wa pili toka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo)

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiangalia moja ya madarasa ya shule shikizi ya kijiji cha Lyazumbi, Wilayani Nkasi. 

Amesema kuwa umefika wakati wa kila Kijiji katika kata hiyo kuhakikisha wanaanza ujenzi wa shule shikizi ili kuweza kuisaidia mzigo wa wananfunzi uliopo katika shule hiyo mama iliyopo katika Kijiji cha Paramawe ‘A’ na hatimae shule hizo shikizi zitakazoanzishwa katika vijiji hivyo ziendelezwe na kusajiliwa na kuwa shule kamili.

Ameyasema hayo wakati alipoitembelea kata hiyo ili kujionea maendeleo ya elimu ya shule ya msingi ambapo Kijiji cha Lyazumbi tayari kimeshajenga madara matatu yaliyokamilika pamoja na vyoo na ofisi ya walimu huku Kijiji cha paramawe ‘B’ kikikosa shule hiyo shikizi na hatimae kuwapeleka Watoto wa katika shule ya msingi Paramawe ‘A’.

“Muanze kujipanga sasa hivi, Mkurugenzi tuma watu waje wakae huku waone namna gani ya kuwasaidia hivi vijiji vitatu namna gani ya kuondokana na changamoto hii ya msongamano ya Watoto kwa kuhakikisha kwamba kila Kijiji kinakuwa na shule yake ya msingi na kwa kuanzia wawe na shule shikizi, weka mkazo mkubwa kumaliza ile shule ya msingi Lyazumbi na isajiliwe na hawa paramawe ‘B’ watafute eneo la kujengea shule hiyo,” Alisema

Aidha, katika kubainisha vigezo vya shule ya msingi kukamilika na kuweza kusajiliwa, kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Missana Kwangula alivitaja vigezo vinne vinavyopelekea shule ya msingi kusajiliwa na kufafanua kuwa vigezo hivyo vimewekwa baada ya Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kubaini kuwa shule nyingi zikianzishwa kama shikizi na kusajiliwa huwa haziendelezwi na wananchi na hivyo kuupa mzigo serikali.

“Sasa hivi ili shule ya msingi isajiliwe lazima iwe na vitu vya msingi vinne, cha kwanza vyumba visipungue saba kwa maana ya darasa la kwanza mpaka la saba na cha pili kuwe na walau nyumba moja ya mwalimu kwasababu mwalimu mkuu lazima akae shuleni, lakini cha tatu lazima kuwe na vyoo vya makundi matatu vyoo vya wanafunzi wavulana na wasichana na vyoo vya walimu na cha mwisho ni viwanja vya michezo na hasa mpira wa miguu na “netball””, Alisema.

Shule Shikizi ya Kijiji cha Lyazumbi ina wanafunzi 375 wa darasa la kwanza hadi la tatu hali iliyomelekea Mtendaji wa Kijiji hicho Elizabeth Alex kuomba msaada wa nguvu za wananchi, serikali pamoja na wadau wa elimu nchini kusaidia ujenzi wa kumalizia shule hiyo.

Wednesday, January 16, 2019

“Asiyetaka kuchukua kitambulisho cha ujasiliamali asubiri kubughudhiwa” RC Wangabo.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo amewataka wajasiliamali wote mkoani humo kujitokeza kupatiwa vitambulisho vya ijasiliamali vilivyotolewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa mikoa na wilaya zote nchini ili kuwaepusha wajasiliamali hao na bughudha wanazozipata katika kuendesha biashara zao za kila siku.

Amesema kuwa kila halmashauri kati ya halmashauri nne za mkoa wa Rukwa ilipatiwa vitambulisho 6,250 katikati ya mwezi Disemba mwaka 2018 lakini hadi kufikia leo katikati ya mwezi wa kwanza vitambulisho vilivyogawiwa havizidi 150 kwa mkoa mzima hali iliyopelekea Mh. Wangabo kuahirisha ziara ya siku nne aliyopanga kuifanya katika halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ili kujionea miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo 

“Nawataka waende katika halmashauri zote haraka iwezekanavyo vinginevyo watakosa hii nafasi ya kuapata vitambulisho na kitakachofuata kinaweza kisiwe kizuri kwa wajasiliamali, kwasababu hiki ni kitambulisho ndicho kinachomfanya mjasiliamali huyu mdogo atambulike na asibughudhiwe kama mheshimiwa rais alivyosema, sasa usipopata kitambulisho maana yake ni kinyume chake ndicho kitakachokuja, unapata kitambulisho ili usibughudhiwe, lakini wewe hujapata kitambulisho inamaana utabughudhiwa, mimi nisingependa wajasiliamali wapate bughudha,” Alibainisha.

Ameyasema hayo baada ya kupata taarifa ya Wilaya ya Kalambo juu ya miradi mbalimbali ya kimaendeleo, mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza, ukusanyaji wa mapato na matumizi ya halmashauri, ugawaji wa vitambulisho hivyo pamoja na hali ya kilimo ya Wilaya kabla ya kutaka kuanza ziara yake katika wilaya hiyo.

Aidha amesisitiza kuwa tathmini ya ugawaji wa vitambulisho hivyo itafanyika baada ya siku kumi tangu leo tarehe 15.1.2019 hadi tarehe 25.1.2019 ili kuona muitikio wa wajasiliamali hao kwa halmashauri zote na kuwaagiza wakurugenzi wa halmashauri hizo kuhakikisha wanaongeza kasi ya kuwasajili na kuwakabidhi wajasiliamali hao vitambulisho vyao bila ya bughudha yoyote.

Wakati akiwasilisha taarifa ya wilaya, katibu tawala wa wilaya ya Kalambo Frank Sichalwe alisema kuwa tangu kufanyika kwa uzinduzi wa ugawaji wa vitambulisho hivyo mwanzoni mwa mwaka huu ni wajasiliamali kumi tu ndio waliopatiwa vitambulisho hivyo pamoja na kuendelea na hamasa ya kuwatambua wajasiliamali wengine.

“Zoezi la hamasa na ugawaji wa vitambulisho linaendelea ili vitambulisho vingi zaidi viweze kutolewa na kuwanufaisha wajasiliamali katika sekta isiyorasmi kama mheshimiwa Rais alivyokusudia, mpaka sasa Ulumi tumepata wajasiliamali 80, Mwimbi 30, Kasanga 30, Mwazye 20 na Matai wamejitokeza wajasiliamali zaidi ya 100 mpaka sasa,” Alisema.

Vitambulisho vya ujasiliamali viligagiwa kwa wakuu wote wa mikoa 26 mwanzoni mwa mwezi Disema mwaka 2018 na kila mkoa kupata vitambulisho 25,000 ili kuweza kuvigawa kwa wakuu wa wilaya na hatimae kufika mikononi mwa wakurugenzi ili kuwapatia wahusika wa vitambulisho hivyo kwa lengo la kupunguza bughudha kwa wajasiliamali wataopata vitambulisho hivyo vyenye gharama ya shilingi 20,000 kwa kila kitambulisho.