Thursday, August 29, 2019

RC Wangabo ataka ujenzi wa VETA Sumbawanga kuharakishwa ili kuanza kudahili wanafunzi.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemtaka mkandarasi wa Kampuni ya Tender International kuhakikisha anamaliza ujenzi wa Chuo cha Ufundi VETA kilichopo Kata ya Sumbawanga Wenyeji Wilayani Sumbawanga ndani ya mwaka huu ili kufikia mwezi Januari mwaka 2020 kianze kudahili wanafunzi katika fani mbalimbali za ufundi.

Chuo hicho ambacho ujenzi wake ulitakiwa kumalizika Septemba 21, 2019 bado haujakamilika kutokana na Mkandarasi huyo kutegemea fedha za ujenzi kutoka serikalini na hivyo kuomba kuongezewa muda wa miezi minne ili aweze kumalizia ambapo hadi sasa ameshalipwa shilingi bilioni 2.6 kwaajili ya ujenzi wa majengo 22 ikiwemo karakana mbalimbali za mafunzo, mabweni, madarasa na nyumba za watumishi.

Mbali na changamoto hiyo Mh. Wangabo pia amepongeza kiwango cha ubora wa majengo hayo ambayo kwasasa yapo katika hatua ya kupauliwa na kuongeza kuwa kama kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa imeridhishwa na kiwango cha majengo ya chuo hicho hadi hapo kilipofikia.

“VETA hii ilianza kujengwa mwaka jana mwezi wa tisa na ilitegemewa iwe imemalizika mwaka huu, kipindi cha mwaka mmoja. Lakini kumekuwa na changamoto za hapa na pale upande wa mkandarasi n ahata upande wa wizara inayohusika, basi hizi changamoto zimefikia kwenye hatua ambayo sasa tunaweza kwenda vizuri, Mkandarasi ameomba kuongezewa miezi minne na hii mimi nitaifuatilia, kuhakikisha kwamba hii ‘extention’ inakwenda haraka ili ikamilike ili ianze kuchukua wananfunzi Januari 2020,” Alisema.

Ameyasema hayo leo tarehe 29.8.2019 alipotembelea katika eneo la Ujenzi wa Chuo hicho kinachotarajiwa kudahili wanafunzi 600 wa masomo ya muda mrefu na wanafunzi 2000 wa masomo ya muda mfupi katika fani za umeme wa majumbani, umeme wa magari, ushonaji, mapishi, ufundi wa kompyuta, ufundi wa magari, useremala, na usindikaji wa chakula.

Awali akizungumza wakati wa kutoa taarifa ya ujenzi wa Chuo hicho karani wa Mradi Mhandisi Jeremiah Longido alisema kuwa endapo serikali italipa fedha za ujenzi kwa wakati wana uhakika kwamba majengo hayo yatakamilika katika kipindi hicho cha miezi minne waliyoiomba na hatimae kufikia mwezi January, 2020 kuanza kudahili wanafunzi.

“Kama ‘Cash flow’ itakwenda vizuri, hii miezi minne kama kazi itafanyika kwa nguvu tunaweza kumaliza kazi, kwasababi amelipwa ‘certificate’ namba nne ambayo ni kama milioni 130 lakini kuna ‘certificate’ namba tano kama milioni 640 amabyo ipo tayari ambapo mda wowote anaweza kulipwa kwahiyo kama hiyo atapokea inamaanisha tutakuwa vizuri,” Alisema.

Katika Hatua nyingine, Mh. Wangabo amesikitishwa na kasi ya konokono katika ujenzi wa hospitali za Wilaya ambazo kwa mujinbu wa tarehe za Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, hospitali hizo ziliongezewa muda wa kuisha kwake na zilitakiwa kumalizika na kukabidhiwa tarehe 31.8.2019 kwaajili ya kuanza kutumika.

“Kasi yenu ni ndogo, kasi ya konokono, vifaa havipo hata ujenzi katika jengo hili la utawala hakuna, hali kwakweli ni hovyo na si nzuri ni mbaya muda umekwishaisha, kwahiyo nashindwa hata kuwaambia kuna siku za nyongeza kwasababu kuna ‘deadline’ ya TAMISEMI. Sasa fanyeni juu chini kwa siku zilizobakia mmalize hapa sasa sijui mtaweka hema ama mtafanyaje lakini fanyeni juu chini hii kazi iishe,” Alisisitiza

Ameyasema hayo baada ya kukagua ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga akiwa na kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, viongozi na wataalamu wa wilaya ya Sumbawanga ambapo kabla ya kufika hapo pia alitembelea hospitali ya Wilaya ya Nkasi na hospitali ya Wilaya ya Kalambo.


Wanaoharibu Miundombinu ya Daraja la Shilingi biloni 17.7 Kukamatwa


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameliagiza jeshi la polisi mkoa wa Rukwa kuhakikisha wanafanya msako kwa wale wote waliohusika kuharibu na kung’oa ‘reflectors’ zilizowekwa kwenye vyuma vya kingo za barabara katika darala la Momba lililopo mpakani mwa Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Songwe katika Bonde la Ziwa Rukwa, Wilaya ya Sumbawanga.

Amesema kuwa ung’oaji huo wa ‘reflectors’ hizo unaweza kusababisha ajali itakayopelekea kupoteza maisha ya watu nyakati za usiku na kupoteza malengo ya ujenzi wa daraja hilo na kuonya kutoendelea kwa uharibifu huo wenye lengo la kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi, mkoa na nchi kwa ujumla.

“Jeshi la Polisi mzisake bodaboda zote ambazo zikikutwa zina ‘reflector’ hizi, kwasababu zinafahamika kama hamjui, iwe kwenye bodaboda, iwe kwenye baiskeli, kamata na fikisha mahakamani, hatuwezi kufumbia macho uharibifu huu, utakuja kesho utakuwa wameng’oa kila kitu wataharibu. Kumbukeni kwamba bilioni 17.7 zimelala hapa, na manufaa yote mmeyasikia na ninyi mnajua zaidi, sasa mnataka kuturudisha wapi, hatutakubali uharibifu wa aina yoyote ile,” Alisisitiza.

Mh. Wangabo aliyasema hayo tarehe 28.8.2019 alipotembelea daraja la Mto Momba kuona maendeleo ya daraja hilo lililojengwa na mkandarasi Jianxi Geo – Engineering (Group) Corporation kutoka China na kusimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia kitengo chake cha ushauri wa miradi TANROADS Engineering Consulting Unit (TECU) ambapo hadi sasa daraja hilo limeshakamilika kwa asilimia 100.

Wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa Daraja hilo Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Rukwa Mhandisi Jetrovas August alisema kuwa kazi ya nyongeza ambayo ilikuwa nje ya mkataba ni kuweka taa katika barabara ya km 1.125 ambayo ni kiunganisho cha mikoa ya Songwe na Rukwa na kuongeza kuwamiongoni mwa changamoto ni un’goaji wa ‘reflector’ katika barabara hiyo.
 
“Pamoja na Mkandarasi kumaliza na kukabidhi mradi kwa serikali kumeanza kujitokeza uharibifu wa baadhi ya miundombinu ya barabara, moja ya uharibifu ambao tayari umeanza kujitokeza ni ung’oaji wa ‘reflector’ zilizowekwa kwenye vyuma (guardrail) vya kingo la tuta la barabara kwaajili ya kuongozea magari na vyombo vingine vya usafiri wakati wa usiku,” Alisema.

Katika Hatua nyingine, Mh. Wangabo amewapongeza wakandarasi pamoja na Mhandisi Mshauri wa  ya ujenzi wa barabara ya kutoka Sumbawanga – Matai – Kasanga yenye urefu wa Km 107 ambayo imefikia asilimia 91 ya ujenzina kubainisha kuwa barabara hiyo imetimiza miaka tisa tangua kuanza kwa ujenzi wake lakini pamoja na mambo mengine yaliyosababisha hayo ni maelewano mabovu yaliyokuwepo baina ya Mkandarasi na Mshauri jambo ambalo hivi sasa limemalizika na kazi inakwenda vizuri.

“Mkandarasi pamoja na ‘Consultant’ hay ani matokeo ya kuelewana, ‘Consultant’ na Mkandarasi wameelewana na wanafanya kazi usiku na mchana na matokeo yake mnayaona kazi imefanyika vizuri sana mimi nawapa pongezi sana, kwahiyo mimi nategemea kama mlivyoniambi kwenye taarifa yenu kwamba kufikia tarehe 30 mwezi Septemba barabara hii itakuwa imekwishafika bandarini kasanga na tutakuwa tumemaliza mchezo lambda marekebisho ya hapa na pale,” Alieleza.
Mradi huo wa barabara ya Sumbawanga – Matai – Kasanga unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania na kugharimu Shilingi Bilioni 133.2 ambapo ujenzi wake unategemewa kumalizika mwezi Septemba mwaka 2019 chini ya Mkandarasi Joint Venture of China Railway 15G/New Century Company Ltd.

Stendi ya Mabasi Sumbawanga Kuwa ya Mfano Mikoa ya Nyanda za juu kusini


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo amewataka wananchi wa Mji wa Sumbawanga pamoja na wakandarasi wa ujenzi wa stendi ya mabasi katika mji wa Sumbawanga kutohujumu miundombinu ya eneo hilo na badala yake wasaidie kuimarisha ulinzi na wakandarasi kujenga kwa uzalendo ili kituo hicho kiweze kuwa nembo ya mkoa wa Rukwa.
Mhandisi wa Manispaa Suleiman Mziray (T-shirt ya Zambarau) akitoa maelezo ya uzio unaozunguka stendi ya Mabasi Sumbawanga Kwa Mkuu wa Mkoa na Kamati ya ulinzi na Usalama pamoja na viongozi na wataalamu wengine waliofika kukagua ujenzi wa stendi hiyo. 

Amesema kuwa hajawahi kuona ndani ya jengo lastendi kukiwa na vyumba vya kulala wageni, migahawa,  mabanda ya mamalishe, sehemu ya kuegeshea bodaboda na bajaji pamojana mabasi  na kufananisha eneo hilo na kiwanda kwakutarajiwa kuzalisha ajira kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa.

“Stendi hii katika Manispaa ya Sumbwanga itakuwani nembo ya Mkoa wa Rukwa, Sisi Wana Rukwa tutajivunia sana hii stendi , stendi ambayo sijaona popote ambapo kuna vyumba vya kulala ndani ya stendi, iko hapa, kuna ‘restaurant’ kuna mabanda ya mama lishe kuna sehemu ya bodaboda, bajaji, kuna mabasi, kuna kila aina ya mambo inajitosheleza, hiki kitakuwa nikama kiwanda kidogo maana kitaajiri watu wengi sana hapa, wale wanaojenga hapa wasihujumu miundombinu hii,” Alisema.

Ameyasema hayo leo tarehe 28.8.2019 alipotembelea stendi hiyo ya mabasi yam ji wa Sumbawanga iliyoanza kujengwa mwanzoni mwa mwezi wa tano mwaka 2019 na kutarajiwa kumalizika mwezi Disemba mwaka huu akiwa ameambatana na Kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga pamoja na Wataaalamu wengine kutoka Ofisi ya mkuu wa Mkoa na Manispaa ya Sumbawanga.

Akitoa taarifa ya ujenzi huo Mhandisi wa Manispaa ya Sumbawanga Suleimani Mziray alisema kuwa kutokana na ufinyu wa fedha stendi hiyo itajengwa kwa awamu mbili na mpaka sasa ujenzi huo umefikia asilimia 40 na bado mkandarasi anaendelea na ujenzi na kuongeza kuwa katika jengo hilo kutakuwa na eneo la kuwahifadhi abiria zaidi ya 400 watakaokuwa wakisubiri safari zao za nje na ndani ya mkoa.

“Kutokana na Ufinyu wa fedha ujenzi wa kituo cha mabasi eneo la katumba Azimio utafanyika kwa awamu mbili ambapo mpaka sasa kazi zimekwishafanyika kwa asilimia 40 na bado inaendelea kwenye maeno tofauti kulinngana na Mkataba, jengo Kubwa litakuwa nae neo kwaajili ya kusubiria abiria ambalo litakuwa na uwezo wa kubeba abiria 400,” Alisema

Aidha Msimamizi wa ujenzi huo kwa upande wa Mkandarasi Said Rajabu Mbelwa ameongeza kuwa ili kufika kwenye ghorofa ya kwanza ya jengo hilo kutakuwa na Lifti ili kuwasaidia walemavu na wale ambao afya zao haziruhusu kutumia ngazi

“Hapa kuna Lifti ambayo itatumika kwaajili ya Walemavu n ahata ukiwa mgonjwa kwasababu itakuwa siyo rahisi kupita kwenye ngazi ya kupanda kwa mguu kama una matatizo ya afya, kwahiyo imewekwa kwaajili ya walemavu na watu amba afya zao si nzuri sana,” Aliongezea.

Hadi kufikia hatua hiyo mkandarasi SUMRY ENTERPRISES LTD tayari ameshalipwa Shilingi Bilioni 1.72 ambayo ni sawa na asilimia 28.89 ya Shilingi bilioni 5.95 ambayo ni gaharama ya ujenzi wa stendi hiyo, ambayo inategemewa kuwa na vyumba vya kulala waheni, vymba maalumu vya kufanyia mazoezi(Gym), kituo cha polisi, sehemu ya migahawa mikubwa na mama lishe na sehemu za kuegeshea Baiskeli, Bodaboda, Bajaji, Teksi na mabasi yanayosafirisha abiria ndani ya Mkoa na nje ya Mkoa.


Saturday, August 17, 2019

Wananchi Rukwa waendelea kujitolea damu kwaajili ya majeruhi ajali ya Morogoro


Timu ya Afya ya mkoa wa Rukwa inayojishughulisha na ukusanyaji wa damu kutekeleza maelekezo ya mkuu wa mkoa huo Mh. Joachim Wangabo ijumaa hii iliweka makazi yake nje ya Ofisi ya mkuu wa mkoa ili kukusanya damu kutoka kwa watumishi wa ofisi hiyo pamoja na wananchi mbalimbali wanaofika hapo kupata huduma mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule akiwa amelala katika kitanda maalum kwaajili ya kujitolea damu kusaidia ili kuunga mkono juhudi za mkoa wa Rukwa kusaidia majeruhi wa ajali ya Morogoro iliyoua zaidi ya watu 90

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule (kushoto) akiendelea kuwahamasisha watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa kujitolea damu ili kuunga mkono juhudi za mkoa pamoja na kufuata maelekezo ya mkuu wa mkoa huo katika kuwasaidia majeruhi waliungua kutokana na kulipukwa kwa lori katika eneo la msamvu mkoani Morogoro na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 90. 

Mmoja wa Watumishi wa Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa Joyce Mwanandenje akiendelea kujitolea damu kuunga mkono juhudi za mkoa kusaidia majeruhi waliopata ajali Mkoani Morgoro kutokana na kulipuka kwa lori la mafuta wiki moja iliyopita. 

Timu hiyo inayoongozwa na mganga mkuu wa mkoa ilianza kutekeleza maelekezo hayo tangu tarehe 14.8.2019 kwa kupita katika maeneo mbalimbali ya mji wa Sumbawanga kukusanya damu hiyo kwa kushirikiana na timu nyingine za Afya katika ngazi ya halmashauri ambazo nazo zinaendelea na zoezi hilo katika halmashauri nne za mkoa huo.

Taarifa hiyo imethibitishwa na mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu wakati alipokuwa akiongea na vyombo vya habari huku akiendelea kuwahamasisha watumishi wa serikali, waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini, viongozi wa kisiasa pamoja na wananchi wenye mapenzi mema kujitolea kutoa damu ili kuweza kuwasaidia majeruhi walioungua kutokana na kulipuka kwa lori la Mafuta katika eneo la Msamvu mkoani Morogoro Wiki moja iliyopita.

“Sisi kama wataalamu tumejipanga baada ya mheshimiwa mkuu wa mkoa kutoa haya maelekezo, kazi hii inafanyika katika halmashauri zote nne za mkoa wa Rukwa na katika halmashauri zetu kuna timu maalum ya ukusanyaji wa damu, kwahiyo toka agizo limetolewa timu zetu katika halmashauri zinaendelea na hiyo kazi,” Alisema.

Akimuwakilisha Mkuu wa mkoa wa Rukwa katika zoezi hilo la kuwahamasisha watumishi wa serikali kujitolea damu, mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule ameendelea pia kuwahamasisha wananchi kuanzia ngazi za mitaa na vijiji waendelee kujitolea damu kupitia timu hiyo ya mkoa pamoja na timu za halmashauri zilizoteuliwa maalum kwaajili ya zoezi hilo lakini pia kufika katika hospitali ya mkoa kushiriki kujitolea damu.

“Damu inahitajika tunawaomba wananchi waendelee kujitolea kama ambavyo ratiba ilivyotangazwa, hii timu itakuwa inapita kwenye mitaa yetu kwenye kata zetu lakini pia kwa wale ambao watakuwa wamekosa hiyo nafasi, bado hospitali yetu ya mkoa itaweza kuwapokea waweze kuchangia damu kwaajili ya kuwanuru wenzetu ambao wamepata ajali kule Morogoro,” Alieleza.

Aidha, mmoja wa watumishi waliojitolea kuchangia damu Elvira Malema alieleza kuwa mahitaji ya damu ni makubwa na kujitolea damu hiyo huenda kukaokoa majeruhi wengine waliobakia na kudhani kuwa kama damu ingelikuwa ya kutosha huenda vifo hivyo visingevuka idadi iliyopo na hivyo kuwaomba wananchi  ambao hawajafanya maamuzi ya kujitolea damu washiriki kufanya hivyo.
“Zoezi hili sikwamba linachukua muda mwingi, ni dakika tu unatolewa damu kama una uzito unaostahili, una damu ya kutosha, nawahamasisha watu wajitokeze kuchangia kwasababu leo unaweza ukaona ni kitu kinachotokea kwa mtu mwingine kwasababu hakijakufika kwenye familia yako ukadharau, kwahiyo nawahamasisha watu wajitokeze kuchangia,” Alisema.

Kwa upande wake mmoja wa madereva wa boda boda aliyefika katika ofisi hiyo kupata huduma Ayoub Wangoma ameishukuru serikali kwa kuwahamasisha madereva wa bodaboda kuchangia damu kwa kutanabahisha kuwa madereva hao wanahitaji damu kutokana na shughuli zao zinazowaweka barabarani kila kukicha na hivyo kuguswa na kampeni hiyo na hatimae kuamua kuunga mkono juhudi za mkoa kwa kujitolea damu.

“Sisi ka vijana tunaojishughulisha na bodaboda imetugusa sana na kujitoa kwa moyo kwasababu jambo kama lile waliopoteza maisha pale kuna ndugu zetu kuna wazazi wetu, kwahiyo tunapojitolea damu leo kwao kesho kwetu, inawezekana jambo kama lile tunaliongelea kwa udogo lakini mbeleni huko linaweza kutokea likatuhusu sisi wenyewe bodaboda kulingana na shughuli tunazofanya,” Alisema.

Zoezi la uchangiaji wa damu kwaajili ya kusaidia majeruhi wa ajali ya Morogoro inatarajiwa kuamalizika tarehe 18.8.2019 na taarifa ya jumla ya zoezi hilo kutolewa tarehe 19.8.2019 na hatimae damu hiyo kusafirishwa kwenda sehemu husika kulingaana na malekezo ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.  

Thursday, August 15, 2019

RC Wangabo apania kufufua kasi ya vyama vya ushirika kuimarisha uchumi wa wananchi Rukwa


Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amevitaka vyama vya ushirika katika Mkoa wa Rukwa kujiunga na chama kikuu cha Ushirika cha Mkoa ili kuwa na umoja na nguvu katika kutafuta masoko ya mazao yao, kuachana na walanguzi, kulima kwa tija na kuzalisha mazao bora kwa kupata pembejeo kwa wakati na hatimae kufanya kazi kwa karibu na wataalamu wa kilimo waliomo ndani ya mkoa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo. 
Amesema kuwa chama kikuu cha Ushirika cha Mkoa Ufipa Cooperative Union Ltd (UCU) ni chama kipya na kinahitahi nguvu ya vyama vya ushirika vya mkoa mzima ili kiwe na uongozi uliokamilika, kiweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuweza kumnyanyua mkulima wa mkoa wa Rukwa kutoka alipo sasa na kuwa wakulima wa hadhi ya kimataifa.

“Mkulima ana mahangaiko makubwa sana, sasa huu ushirika ni chombo cha kumkomboa mkulima, ni chombo cha kunyanyua uchumi wa mkulima, ni chombo cha kuikomboa Rukwa, ni chombo cha kuikomboa nchi yetu ya Tanzania, nchi ambayo sasa inaelekea kwenye uchumi wa kati wa viwanda, sasa ushirika ni kitovu cha uzalishaji n ani kitovu cha viwanda, sasa kila tunachokifanya tuchote kwenye ngazi ya mkulima, lazima tujue namba moja kwenye viwanda ni uzalishaji na malighafi za kilimo zinatokana na wakulima, ni lazima azalishe na akizalisha zaidi tutakuwa na viwanda endelevu kutokana na uzalishaji mwingi” Alisisitiza

Ameongeza kuwa hali ya hewa ya mkoa wa Rukwa ni sawa na hali ya hewa za mikoa yote ya nyanda za juu kusini ambayo mikoa hiyo inaongoza kwa kulima matunda na mbogamboga na hivyo kuwa na mazao mengi mbadala kuliko kutegemea mahindi ambapo soko linaposhuka na wananchi wanakosa pa kukimbilia na hivyo kuwataka wajitafakari kutoka katika kilimo cha kutegemea mahindi na hatimae kuanza kulima mbogamboga na matunda ya kutosha kwaajili ya matumizi ya wana-Rukwa ili kupunguza udumavu pamoja na kuuza nje ya mikoa na hatimae nje ya nchi.

Mh. Wangabo ameyasema hayo katika Mkutano wa Vyama vya ushirika Mkoani humo aliouitisha ili kuwatafutia wanachama wapya chama kikuu cha Ushirika cha Mkoa pamoja na kusikia mipango yao waliyojiwekea kuanzia wa mawaka mmoja hadi miaka kumi katika kuelekea Tanzania ya uchumi wa kati chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Akitoa taarifa fupi ya hali ya vyama vya ushirika Kaimu Mrajisi vyama vya Ushirika wa mkoa wa mkoa wa Rukwa Anosisye Mbetwa amesema kuwa miongoni mwa mafanikio ya mkoa ni kuanzisha chama cha kikuu cha ushirika (UCU) ambacho kimesajiliwa tarehe 9.1.2019 kikiwa na wanachama 58 na kwa ujumla hadi kufikia tarhe 31.6.2019 mkoa umeweza kutoa mikopo yenye thamani ya Shilingi 17,781,678,000/=.

“Vyama vya Ushirika 81 vimeweza kukaguliwa na shirika la Ukaguzi la vyama vya Ushirika nchini (COASCO) na kuhusu masoko kwa mwaka 2018/2019 soko la Serikali kwa maana ya NFRA liliwezesha upatikanaji wa shilingi 3,010,467,520/= kwaajili ya ununuzi wa mazao ya wakulima kupitia vyama vya Ushirika vya msingi,” Alisema.

Akielezea mpango wa Miaka 10 ya Chama kikuu cha Ushirika Mkoani Rukwa Makamu Mwenyekiti wa UCU Gaspar Chipeta amesema kuwa lengo kuu la chama hicho ni kuwaleta pamoja wakulima wa mkoa wa huo, kuwa na sauti moja, kutambua mahitaji ya pembejeo kwa kila mkulima kupitia vyama vya msingi pamoja na kutafuta soko lenye bei nzuri ili kuweza kuinua uchumi wa wakulima.

“Mkakati mwingi ni kuhakikisha ndani ya hii miaka kumi kuna matokeo ya uboreshwaji wa miundombinu inayotumika katika kilimo, asilimia kubwa ya wakulima katika mkoa wa Rukwa hawatumii miundombinu ya kisasa, kama ulivyosema awali kwamab lazima twende kwenye kilimo cha kisasa, sisi kama chama kikuu tunataka walau kila chama cha ushirika cha msingi, Kila AMCOS iweze kumiliki walau Trekta ambalo litaweza kuwasaidia wakulima wa vyama hivyo,” Alisema.

Kwa upande wake Meneja wa kanda ya Sumbawanga Wakala wa Taifa wa Hiafadhi ya Chakula (NFRA) Abdillah Nyangasa ametahadharisha wakulima wengi wamekuwa wakilima eneo kubwa lakini mazao yanayopelekwa sokoni hayafanani na viwango na hivyo kuwataka kuzingatia ubora wa mazao katika hatua ya mwisho ambayo inapelekwa kwa mlaji, hali ambayo ipo katika mazao mengi yanayolimwa katika Mkoa.

“ Eneo la Ubora baada ya mavuno ni la msingi mno katika kupata soko zuri, wakati mwingine unaweza kuwa umevuna vizuri lakini unaleta mahindi yako sokoni utaambiwa pepeta, utaambiwa pembua mahindi yaliyooza, ondoa punji zilizoharibika na wadudu, ile ni hatua ya ziada mabayo uneifanya mwenyewe kwenye ngazi ya kaya na kwenye hatua ya chama cha msingi, tukazane kuhakikisha mazao yetu tunayaandaa vizuri kwaajili ya soko ili kupunguza gharama zisizo za lazima,” Alifafanua.


Mkoa wa Rukwa una jumla ya vyama vya Ushirika 172, kati ya hivyo 87 ni vyama vya ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS), 74 ni vyama vya Mazao na Masoko (AMCOS), 4 vyama vya Uvuvi, 3 vyama vya Wafugaji, 1 chama cha Wafuga Nyuki, 3 vyama vya wauza Bidhaa/huduma na Chama Kikuu cha Ushirika kimoja vyenye jumla ya wanachama 19,321.

Tuesday, August 13, 2019

Wananchi Rukwa kushiriki kuchangia Damu kusaidia Majeruhi ajali ya Morogoro

Wananchi Rukwa kushiriki kuchangia Damu kusaidia Majeruhi ajali ya Morogoro


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wananchi wa mkoa huo kushiriki katika zoezi la kuchangia damu litakalofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 14 hadi 18.8.2019 katika halmashauri nne za mkoa, ili kusaidia majeruhi walioungua na moto uliosababishwa na kulipuka kwa lori la Mafuta katika ajali iliyotokea eneo la Msavu mkoani Morogoro, na kusababisha vifo vya watu 76 na majeruhi 54.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo

Mh. Wangabo amesema kuwa zoezi hilo litawajumuisha Waendesha Bodaboda na Bajaji, Madereva wa Magari, Vijana, Watumishi wa Serikali, Wanafunzi, Vyama za Siasa, Madhehebu ya Dini, Viongozi mbalimbali na wale wote wenye mapenzi mema na moyo wa kujitolea kwaajili ya majeruhi hao.

“Nafahamu kuwa mtu yeyote aliyeungua sehemu yoyote ya mwili, miongoni mwa madhara makubwa anayoyapata ni pamoja na kupoteza kiasi kikubwa cha maji mwilini (Dehydration) na kupungukiwa damu mwilini (Anaemia).  Kwa hiyo natoa wito na kuwaomba Wananchi wa Mkoa wa Rukwa kuchangia Damu kwa ajili ya wenzetu majeruhi wanaoendelea na matibabu.  Damu hiyo pamoja na salamu zetu za pole tutaiwasilisha kwa Dkt. Kebwe Steven Kebwe, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,” Alisema.

Aidha Mh. Wangabo kwa niaba ya Wananchi wa Mkoa wa Rukwa anaungana na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro pamoja na Viongozi wa Mkoa huo, Familia za Marehemu, Ndugu, Jamaa na Marafiki kwa kuondokewa na Wapendwa wao.  Na kumuomba Mwenyezi Mungu awape Moyo wa Subira na Uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

“Mungu awape pumziko la milele waliopoteza uhai na awaponye Majeruhi wote wanaoendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pamoja na hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro.  ‘Bwana Alitoa na Bwana Alitwaa Jina lake lihimidiwe’.” Alimalizia.

Mh. Wangabo ametoa maelekezo hayo kabla ya kuanza kwa kikao cha baraza la madiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kilichohusu utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali nchini.

Thursday, August 1, 2019

DC Mtanda awatahadharisha kinababa wenye tabia ya kunyonya maziwa ya mama


Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda amewatahadharisha kinababa wenye tabia ya kunyonya maziwa ya kinamama wanaonyonyesha kwani hicho ni chakula maalum kwaajili ya mtoto aliyezaliwa na yeyote anayefanya hivyo anadhulumu haki ya mtoto ambaye hutegemea maziwa ya mama kwa muda wa miezi sita bila ya kula chakula cha aina yoyote.  

Amesema kuwa kazi kubwa ya kinababa ni kuwawezesha kinamama kupata lishe bora ili wawe na afya thabiti kutoa maziwa ya kutosha na kuweza kuwanyonyesha watoto wao na kuongeza kuwa katika mkoa wa Rukwa asilimia 81 ya watoto wenye umri chini ya miezi sita wanalishwa vyakula vingine vya ziada, jambo ambalo halikubaliki kwa maendeleo ya mtoto.

Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda

“Ujumbe wa Leo ni kwamba watoto wadogo chini ya Miezi Sita ndio wanaotakiwa kunyonyeshwa, kwahiyo kinababa na wao wenye kupenda maziwa ya baba waache kwasababu hicho sio chakula chao ni lishe kwa watoto wachanga, tusidhulumu haki za watoto za unyonyeshaji, tuache tabia ya kunyonya maziwa ya mama kwa wasiohusika,” Alisisitiza.
Baadhi ya kinamama wanaonyonyesha wakipita kwa maandamano maalum mbele ya mgeni rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya Unyonyeshaji iliyofanyika katika kijiji cha Kisumba Wilayani Kalambo.

Aidha alisema kuwa tafiti zinaonesha kuwa asilimia 17 ya watoto wenye umri chini ya miezi 6 wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kupewa kinywaji au chakula kingine kama inavyoshauriwa na Shirika la Afya Duniani. Hii ina maana kuwa asilimia 83 ya watoto wenye umri huo hawanyonyeshwi ipasavyo.

Mh. Mtanda aliyasema hayo katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji kimkoa katika Kijiji cha Kisumba, kilichopo Wilaya ya Kalambo akimwakilisha aliyetakiwa kuwa mgeni rasmi wa uzinduzi huo Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Albinus Mgonya aliisifu timu ya afya ya Mkoa kwa kuwezesha kufanyika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji katika Kijiji cha kisumba kutokana na Kijiji hicho kuwa na kinamama wengi wanaonyonyesha.

“Katika Kijiji hiki Mheshimiwa mgeni rasmi kuna Kaya 1300, na kwa takwimu ambazo tunazo kupitia idara yetu ya afya kinamama wanaonyonyesha watoto katika Kijiji hiki cha Kisumba ni 234, hivyo utaona kwamba tumekuja kuhakikisha kuwa ujumbe huu unafika kwa wadau kwa njia muafaka,” Alieleza.

Halikadhalika alisema kuwa maadhimisho hayo yankwenda sambamba na utekelezaji wa mradi wa Lishe Endelevu unaolenga kuongeza idadi ya watoto wenye umri kati ya miezi 6 – 23 kuhakikisha kwamba wanapata vyakula vyenye mchanganyiko sahihi na kusisitiza kuwa ni muhimu kinababa kushiriki katika maadhimisho hayo ili wawe msaada mkubwa kwa kinamama.

Wakati akitoa neno la Shukrani Meneja wa Mradi wa Lishe Endelevu Ali Omar alishukuru ushirikiano anaoupata kutoka serikalini na kuwasisitiza kinamama kuwa unyonyeshaji wa maziwa ya mama huchangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha afya, kulinda uhai na maisha ya mtoto.

Asilimia 67 ya watoto wa umri kuanzia miezi 6 – 23 wanapewa vyakula ambavyo havina mchanganyiko wa kutosha, yaani mlo usiokamilika, hali inayodhihirisha kuwa, taratibu duni za ulishaji watoto ni mojawapo ya sababu za utapiamlo katika Mkoa wa Rukwa.