Friday, September 13, 2019

Mkurugenzi Manispaa ya Sumbawanga apita masokoni kuhamasisha vikundi kuomba mikopo.


Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga James Mtalitinya ameendelea kuwahamasisha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kuhakikisha wanajiunga katika vikundi ili kuweza kupata fursa ya kupewa mikopo ili kuweza kujiajiri hali itakayopelekea kupunga wimbi la wasio na ajira na hatimae kujiongezea kipato.

Amesema kuwa moja ya majukumu ya Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ni kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kuongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 halmashauri ilitoa shilingi milioni 253 na kusisitiza kuwa bado kuna milioni 32 zilizovuka mwaka ambapo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 halmashauri inatakiwa kutoa shilingi milioni 230.

“Kufikia Mwezi wa 10 tarehe 15 tunategemea kutoa kiasi cha shilingi milino 120 ikiwa ni makusanyo ya robo ya kwanza kwa maana ya Julai – Septemba, kwahiyo tunaomba wananchi wa bangwe pamoja na wananchi wa Sumbawanga wajiunge katika vikundi visivypongua watu watano mpaka kumi halafu waainishe shughuli wanayofanya na waje waombe mkopo wa kiasi chochote, tutawakagua na baada ya hapo tutawapatia mkopo,” alimalizia.

Mkurugenzi wa manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya

Ameyasema hayo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo walipokuwa wakitembelea masoko yaliyopo katika mji wa Sumbawanga ili kujionea hali halisi ya maendeleo ya biashara na kujua changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wananchi katika masoko hayo.


Rais Magufuli atekeleza 79% ya ahadi za barabara katika mji wa Namanyere Rukwa.


Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesifu juhudi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuhakikisha anatekeleza ahadi zake alizoahidi kipindi cha kampeni baada ya kutembelea barabara zinzoendelea kujengwa katika mji mdogo wa Namanyere, Wilayani Nkasi na kuona kasi ya ujenzi wa barabara hizo ikiendelea vizuri.

Amesema kuwa ahadi ya mheshimiwa rais ni kujenga barabara zenye jumla ya kilometa tano katika mji na mpaka kufikia mwezi Disemba mwaka 2019 zitakuwa zimefikia jumla ya kilometa 3.95 ambayo ni sawa na asilimia 79 ya utekelezaji wa ahadi zake na hivyo kumtaka mkandarasi nayeendelea na ujenzi wa barabara ya kilometa moja afanye haraka kumalizia ujenzi huo ili wananchi waweze kutumia barabara ambazo zimefungwa kwa muda wa mwaka ili kupisha ujenzi.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa tatu toka kushoto) akiwa na wataalamu mbalimbali wakati wa ukaguzi wa barabara zilizopo chini ya usimamizi wa Wakala wa barabara za Mjini na Vijijini Tanzania (TARURA) katika mji wa Namanyere katika Wilaya ya Nkasi.

“Huyu mkandarasi anayejenga kilometa moja kwa kiwango cha lami kazi yake inasuasua kwasababu mradi huu ulipaswa kukamilika mwezi wa sita mwaka huu na sasa ni mwezi wa tisa, kazi haijakamilika lakini pia kuna kero ambazo zipo ndani ya barabara hizi, kuna vivuko vimewekwa vya muda na kwengine hakuna, watu wanapata shida kuvuka mitaro kwenda kufanya biashara zao lakini pia kwenye matolea ya barabara kuna vifusi, hivyo nakupa siku 12 utoe vifusi na ujenge vivuko kwenye mitaro,” Alisisitiza.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara hizo ili kutimiza ahadi za Mheshimiwa Rais Mratibu wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijiji (TARURA) Mhandisi Boniface William alisema kuwa mbali na kujitahidi kuhakikisha barabara hizo zinajengwa kwa wakati lakini kumekuwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti pamoja na upatikanaji wa malighafi za ujenzi wa barabara hizo hasa kokoto.

“katika utekelezaji wa hii miradi kumekuwa na changamoto mbalimbali, changamoto mojawapo ni ufinyu wa bajeti, fedha tunayotengewa kulingana na hali halisi ya ‘site’ unakuta ile fedha ni kidogo kiasi kwamba kama ile barabara ya salala ilikuwa tutengeneze kilometa moja lakini kwa milioni 350 tulishindwa kutengeneza kilometa moja kwahiyo tukaweza kutengeneza mita 700 pekee, tatizo jingine ni malighafi kwa maana ya kuwa na chanzo kimoja cha kokoto katika mkoa, hii inachelewesha kazi,” Alisema.

Katika hatua nyingine, Mh. Wangabo wakati alipomaliza kutrembelea barabara zenye jumla ya kilometa moja katika manispaa ya Sumbawanga amewataka wakandarasi wazawa wanaopewa kazi za ujenzi na TARURA kuhakikisha wanaheshimu na kuzingatia masharti ya mikataba ili kufanya kazi kwa wakati na kuongeza kuwa ikiwa wakandarasi hao hawataonyesha uaminifu katika kazi hizo ndogo itakuwa vigumu kwao kupewa miradi mingine mikubwa.

Katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Nkasi wametengewa bajeti ya shilingi milioni 500 wakati TARURA upande wa Manispaa ya Sumbawanga wametengewa bajeti ya shilingi milioni 460 ili kuendelea kukamilisha ujenzi wa barabara katika kutimiza ahadi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli.


RC Wangabo ataka shida ya maji Namanyere ifanyiwe kazi kabla ya 2020


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameitaka Mamlaka ya Maji Safi Sumbawanga (SUWASA) kukaa na Wizara ya Maji kuona namna ya kuweza kumaliza shida ya maji katika mji mdogo wa Namanyere, Wilayani Nkasi ili wananchi waweze kuepukana na shida hiyo ya muda mrefu na hatimae kuwa na Imani na serikali juu ya utekelezaji wa ahadi zake kwa wananchi.

Amesema kuwa awali wananchi waliaminishwa kuwa baada ya upanuzi wa bwawa la mfili shida ya maji ingekuwa imekwisha, lakini matokeo yake baada ya upanuzi huo bado shida ya maji imeendelea kuwepo ambapo sasa kuna mradi wa ujenzi wa matenki mapya ambayo hayatakidhi mahitaji ya maji katika mji huo unaokuwa kwa kasi na hivyo kuwataka kujipanga kumaliza tatizo hilo.

“Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inasema huku kwenye miji mikuu ya wilaya inatakiwa kupata maji kwa asilimia 85, ninyi mtatoa asilimia 46, sasa SUWASA mkae na Wataalamu wa Wizara husika ya Maji muandae utaratibu ukae tayari tayari juu ya namna gani ya kuweza kukimbiza huu mradi, watu wamechoshwa na subiri subiri hata waswahili wanasema ngoja ngoja yaumiza matumbo,” Alisisitiza.

Ameyasema hayo alipotembelea mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji safi unaoendelea kujengwa katika mji mdogo wa Namanyere ili kujionea maendeleo ya mradi huo pamoja na kujua changamoto zinazoukabili na hatimae kuona namna ya kuupatia ufumbuzi huku akiwa ameambata na kamati ya ulinzi na Usalama ya mkoa pamoja na wataalamu wengine kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa.

Awali akisoma taarifa ya mradi huo meneja wa SUWASA Mhandisi Gibon Nzowa alisema kuwa shida inayosababisha mradi huo kutofikia asilimia 85 ya upatikanaji wa maji katika mji huo ni kutokana na kutokuwepo kwa mtandao wa kuyasambaza maji hayo kwa kilomita 15 lakini maji yalipo katika chanzo yanatosheleza kwa asilimia 85 endapo tatizo la mtandao litatuliwa na kisha kueleza shughuli za mradi huo.

“Kazi zinazotekelezwa ni ununuzi na ufungaji wa pampu mbili za kusukumia maji, ulazaji wa bomba kuu kutoka bwawa la mfili hadi kwenye tenki takriban kilomita 3.7, pia ujenzi wa tenki la lita 500,000 ambalo limeinuliwa kwa mita 12 ili kuwezesha maeneo mengi ya Namanyere kupata maji, ulazaji wa mtandao wa usambazaji maji kwa kilomita 6.5, vile vile katika mradi huu kutakuwa na dira za maji za kuunganishia wateja,” Alimalizia

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda wakati akielezea hatua walizochukua kupambana kumaliza tatizo hilo la upatikanaji wa maji katika mji wa Namanyere alisema kuwa kama wilaya walikaa na kuandika andiko na kuhitaji Shilingi Bilioni 2.5 na kuliwasilisha wizarani ambapo fedha hiyo ilipunguzwa hadi kufikia shilingi Bilioni 1.5 hali iliyopunguza asilimia ya upatikanaji wa maji katika mji huo.

“Tulitafuta wataalamu wakaandika huu mradi, wakaleta kwangu tukapitia tukaona ni mradi wa Shilingi bilioni 2.5 ambayo hiyo ingetuwezesha kusambaza maji maeneo yote yenye upungufu wa maji katika mji wetu, kwahiyo Waziri alipokuja tulimkabidhi akasema tuwape SUWASA nao baada ya kuipiti walipeleka wizarani ambapo wakapunguza kiwango cha fedha, huu mradi ulikuwa ni wa Bilioni 1.8 lakini Mheshimiwa waziri akasema ipungue hadi kufikia shilingi bilioni 1.5 lakini kama ingekuwa ule mradi wetu wa Shilingi bilioni 2.5 tungekuwa na mtandao wa kilomita 15 kuliko huu wa sasa wa kilomita 6,” alisema.

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.

Mradi huo wa uboreshaji wa huduma ya maji safi katika mji wa Namanyere unatarajiwa kumalizika mwezi Mei mwaka 2020 na kugharimu shilingi Bilioni 1.58 fedha zinazotolewa na serikali huku ukitarajiwa kuhifadhi maji kutoka lita 350,000 hadi lita 850,000 na kufikia asilimia 46 ya uaptikanaji wa maji katika mji huo.

Tuesday, September 10, 2019

RC Wangabo avitaka vyama vya Ushirika kujiepusha na madeni


Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amevitaka vyama vya msingi vya ushirika mkoani Rukwa kuhakikisha wanalipa madeni wanayodaiwa na wadau wa kilimo ikiwemo mabenki pamoja na wauzaji mbalimbali wa pembejeo ili wadau hao waweze kuendeleza uaminifu na hatimae kuwa na mahusiano mazuri yatakayoleta maendeleo ya wananchi katika mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo 

Amesema kuwa kutolipa madeni chama kinajiweka katika mazingira ya kutokopesheka na wadau kukosa uaminifu hata kwa vyama vingine na kunasababisha wadau hao kushindwa kufikisha huduma kwa wakulima na hatimae kilimo kukosa tija, vyama vya ushirika kuyumba  na kuongeza kuwa dawa pekee ya kukopa ni kulipa.

“ Vyama vya Msingi vina madeni tena madeni makubwa, kwa mfanokuna kile chama cha Katazi AMCOS pamoja na Rukwa Farmers vyote vipo kule Wilaya ya Kalambo vinadaiwa shilingi milioni 395, vyama viwili sijajua kwengine lakini pale Mpui wanadaiwa Shilingi Milioni 485 au 490, lakini wao wamejipanga nilikuta mzigo mkubwa sana wa mahindi, tani zaidi ya 600, na waliniambia deni wanamaliza, lakini vile vyama viwili hata mahindi yaliyoko kwenye maghala yalikuwa hayazidi magunia 250 sasa watalipaje deni, ukiuliza wanasema kwamba hawakupata mavuno ya kutosha, lakini nje ya hapo wanauza” Alieleza.

Hivyo alitoa rai kwa vyama vya ushirika kuliangalia jambo hilo kwa karibu kwa kuchambua vyama vyote vinavyodaiwa, wadau wanaowadai, siku waliyokopa na siku wanayotakiwa kurudisha mikopo, aina ya mikopo,  walichorejesha tangu kukopa ili kuwa na orodha kamili na kuwafuatilia katika urejeshaji wa mikopo hiyo kwani kwa kufanya hivyo watajenga Imani kwa wanaowakopesha na hatimae kukopesha zaidi.

Mh. Wangabo aliyasema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Ufipa Cooperative Union Ltd (UCU) katika mkutano uliowajumuisha wadau wa kilimo katika mkoa ili kuona namna ya kuinua kilimo chenye tija pamoja na kuhuisha ushirika ndani ya mkoa.

Aidha, Wakati akiwasilisha mada yake kwa wakulima Meneja wa Benki ya Manedeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Kanda ya Nyanda za juu Kusini Dickson Pangamawe alisema kuwa viongozi wa shirika ndio nguzo ya wanaushirika, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha kuwa wanachama wanafaidika na ushirika huo na kuhakikisha kuwa mikopo wanayoipata inawafikia wakulima wao.

“ Nyinyi ndio mtakaotujengea uamini kule kwa wakulima, sisi kama benki ya kilimo tuna fursa ya mikopo ya aina zote, kama wakulima wapo ‘serious’ na uongozi wao utasimama imara, tutawakopesha wataweza kufanya shughuli zao za kilimo bila ya shida yoyote, kwahiyo nitoe rai kwa viongozi wa ushirika, mara nyingi kumekuwa na shida na wakulima wanashindwa kuwa waaminifu kwasababu wanashindwa kusimamiana vyema katika vyama vyao, kwahiyo nyie muwe imara ili kuturuhusu sisi tuweze kuwawezesha,” Alisisitiza.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Sumbawanga Abdillahi Nyangasa alishauri kuwa ili wakulima waweze kujikomboa alitaja mambo matatu makubwa ikiwemo Fedha, Masoko na Mkulima mwenyewe na kuongeza kuwa wao kama NFRA wanasimama katika kumhakikishia mkulima masoko na hivyo wakulima wanahitaji fedha za mikopo kutoka katika mabenki na wao kuwa tayari kutumia fedha hizo kwaajili ya manufaa ya kilimo chao.

“Mtazamo wa NFRA ni kuwafanya Wana Rukwa na Watanzania wengine tubadilike tuwe na uwezo wa kuuza bidhaa zetu za mazao ndani na nje ya nchi, bahati nzuri mkoa umeshaweza kulichukua hili na kulifanyia mkakati kwa maana ya ndugu zetu maafisa ugani, kazi ianzie shambani, tuna kiwango kikubwa sana tunachokipoteza cha mahindi tunayolima kwa hatua ya mwisho ya ubora, asilimia 30 mpaka 40 wakati mwingine mazao yanaharibika kwasababu ya kutozingatia kilimo chenye tija,” Alisitiza.  

Mkoa wa Rukwa una matrekta 124 yanayomilikiwa na wakulima binafsi hali iliyopelekea Mh. Wangabo kuvitaka vyama vya ushirika kusimamia kauli mbiu yao ya “ Ushirika, Pamoja tujenge uchumi” kwa kuanza na kumiliki matrekta ili kuwawezesha wanachama wao waweze kulima kwa tija na kuongeza mazao na sio kutegemea kilimo cha majembe au kutumia wanyama.