Thursday, December 19, 2019

Hospitali za Wilaya 67 zafanyiwa tathmini juu ya maenedeleo ya ujenzi wake.


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamuhanga amesema kuwa  Ofisi ya Rais inaendelea kufanya tathmini kwa hospitali zote 67 kuhakikisha kwamba shilingi bilioni 100.5 ambazo zilitolewa kwa ujenzi wa hospitali hizo kuwa zimetumika vizuri.

Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano imejenga hospitali 67 nchini na mkoa wa Rukwa umejengewa hospitali tatu za wilaya ambapo Mhandisi Nyamuhanga aliweza kutembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kalamnbo, katika mji mdogo wa Matai iliyopokea shilingi Bilioni 1.5 lakini hakuridhishwa na ujenzi wa hospitali hiyo.

 “Kwa halmashauri ambazo fedha hizi zitakuwa hazijatumika vizuri kwakweli tutachukua hatua na katibu tawala wa mkoa kama nilivyoagiza jana, najua kuna vifaa ambavyo tayari vimeshanunuliwa pale ambavyo bado havijawekwa, havijajengwa kwa mfano maru maru na vifaa vingine uhakikishe kwamba kazi hiyo inaendelea ili vifaa hivyo vikishawekwa tuvitathmini sasa kiwango cha ukamilishaji wa hospitali ile ya halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kabla hatujafikiria kutoa fedha nyingine za kukamilisha,” Alisema.

Ameongeza kuwa halmashauri hiyo ya Kalambo imetaja mahitaji ya shilingi milioni 700 ili kuweza kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo jambo ambalo Mhandisi Nyamuhanga hakukubaliana nalo kutokana na tathmini iliyofanywa ya mahitaji ya fedha walizotoa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hizo kuwa yangebaki mambo machache ambayo yasingeweza kuzidi shilingi milioni 300 na kuongeza kuwa anahitaji maelezo ya ziada kutoka katika halmashauri hiyo ambayo hospitali yake imefikia ukamilifu wa asilimia 76 ambacho ni kiwango cha chini cha ukamilishaji.

Katika hatua nyingine amesema kuwa mwezi Aprili mwaka 2019 Ofisi ya Rais TAMISEMI ilitoa shilingi milioni 400 kwaajili ya upanuzi wa Zahanati ya Kijiji cha Samazi katika halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ambapo zahanati hiyo inapandishwa hadhi na kuwa kituo cha Afya lakini amesikitishwa na malumbano yanayoendelea katika kijiji hicho juu ya eneo la ujenzi wa kituo hicho jambo lililopelekea kushindwa kuanza kwa ujenzi huo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamuhanga 

“Ofisi ya Rais TAMISEMI imetoa maelekezo kwamba upanuzi ufanyike katika eneo la zahanati iliyopo iongezewe majengo ili kiwe kituo cha afya cha Samazi kiweze kukamilika ili kiweze kufanya kazi, tusiendelee na malumbano tena tumeshatoa maamuzi kwamba upanuzi ufanyike pale kwenye zahanati ili tukipandishe hadhi ikiwe kituo cha afya, tunategemea kazi hiyo ianze mara moja na ikamilike ndani ya miezi mitatu,” Alisisitiza.

Mhandisi Nyamuhanga apongeza kituo cha afya Mazwi Sumbawanga.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamuhanga amepongeza juhudi zinazofanywa na watumishi kituo cha afya cha Mazwi, Manispaa ya Sumbawanga baada ya kuona namna wanavyokabiliana na ongezeko la wateja wanaohitaji huduma za afya katika kituo hicho ambacho huzalisha wajawazito wapatao 373 kwa mwezi.
Amesema kuwa kabla ya hapo kituo hicho kilikuwa kidogo sana na kushindwa hata kutoa huduma za upasuaji jambo ambalo lilipelekea hospitali ya rufaa ya mkoa kuzidiwa na wagonjwa lakini hali hiyo kwa sasa ni tofauti baada ya upanuzi wa kituo hicho ambacho kutokana na huduma zake wateja wengi huvutiwa kufika na kupata huduma.
Amesema kuwa serikali inatoa fedha nyingi kupata dawa pamoja na vifaa tiba hivyo kinachotegemewa katika kituo hicho ni huduma bora ya afya na kuongeza kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli imejenga vituo vya afya zaidi ya 352 ambapo mojawapo ya vituo hivyo ni kituo cha afya cha Mazwi katika Makispaa ya Sumbawanga ambapo walipatiwa shilingi milioni 500 na sasa kituo hicho kimekamilika na kuanza kutoa huduma.
“Nimefurahishwa kwa upanuzi ambao umefanyika katika kituo hiki cha Mazwi, kilikuwa kituo kidogo tu nakumbuka siku za nyuma lakini kimekarabatiwa kimekuwa kituo kizuri na kinapendeza lakini kitu cha kufurahisha ni kwamba kinahudumia wateja wengi lakini na huduma inayotolewa hapa nimetoka kukagua katika maeneo mbalimbali katika wodi kwakweli nimeridhika na huduma ambazo zinatolewa, changamoto ni kwamba wameongezeka wateja baada ya ukarabati kufanyika, tunashukuru wataalamu wetu wanajitahidi kuwahudumia,” Alisema.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamuhanga

Wakati akitoa taarifa ya kituo cha Afya cha Mazwi Mganga Mkuu wa halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga Dkt. Archie Hellar alisema kuwa kuanzia mwezi Januari hadi Novemba kituo hicho cha afya kimezalisha wajawazito 4,103 na kati ya hao waliofanyiwa upasuaji ni wajawazito 426 na kupatikana vifo viwili kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo katika harakati za kuwafanyia wajawazito hao upasuaji..
“Kwajhiyo changamoto tunazozipata ni kwamba wateja ni wengi zaidi wanaichukulia hospitali hii ni kama ya mkoa na wengine wanatoka nje ya manispaa n ahata nje ya Wilaya nyingine kuja kujifungua hapa, sasa ukilinganisha watumishi pamoja na rasilimali fedha unakuta kituo kinaelemewa, lakini hata hivyo tunajitahidi kwa kushirikiana na Mkurugenzi wetu wa manispaa Jacob Mtalitinya kwakweli anatiupa nguvu na kutusaidia sana kufanikisha kutoa huduma,” Alisema.
Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ilipata shilingi milioni 500 za kupanua ujenzi wa kituo cha Afya cha Mazwi pamoja na kupewa shilingi milioni 400 kwaajili ya ujenzi wa kituo cha Afya kipya kilichopo katika kata ya Katumba azimio ikiwa ni kilometa 12 kutoka katika kituo cha afya cha Mazwi.

Friday, December 6, 2019

Utoro, Uvivu na kutoshirikisha wazazi kwatajwa kuwa kikwazo cha ufaulu Rukwa.

Pamoja na ufaulu wa matokeo ya darasa la saba kupanda kwa asilimia 8.01 kwa mwaka 2019 katika mkoa wa Rukwa na kupelekea kushika nafasi ya 13 kitaifa baada ya kufanyika mtihani wa darasa la saba mwezi septemba mwaka huu viongozi wa ngazi mbalimbali katika mkoa wameendelea kutaja utoro na uvivu wa waalimu kuwa ni kikwazo katika kuinua ufaulu katika Mkoa wa Rukwa.
Hayo yalianza kusemwa na Afisa Elimu Mkoa wa Rukwa Nestory Mloka baada ya kutoa taarifa ya matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019 pamoja na taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2020 katika Mkoa huo.
“ Mwalimu kutokuwepo shuleni, kutokuja kabisa shuleni, watoro wapo, pwngine hawaripotiwi ipasavyo katika vyombo vya maamuzi vyenye kutoa maamuzi kwa wakurugenzi hawajui na yawezekana hata maafisa elimu hawajui, wapo waalimu anatoroka yupo Mbeya anafanya mambo yake, lakini mwalimu Mkuu hasemi. Sasa hili ni tatizo,” Alisema
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Kalolo Ntila alisema kuwa waaalimu wengi wamekuwa wakifika shuleni na kufanya kazi ya ‘kuchati’ na sumu zao mpaka muda wa kazi unakwisha na kwenda nyumbani na hivyo kuutaka uongozi wa mkoa kutafuta mwarobaini wa tabia hizo za waalimu.
“Bado naendelea kujitafakari hivi hao waalimu wamesomea mbinguni, hao wanaofundisha shule za binafsi, nidhamu na uwajibikaji ni kubwa sana katika hizi shule binafsi, waalimu hawa watuambie ni mambo gani yanayowapelekea kutowajibika ili tuelewe,” Alisema.
Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Apolinary Macheta alisema kuwa shule ambazo waalimu hawana mahusiano na wazazi kitaaluma, shule hizo daima huwa chini sana kitaaluma na kuongeza kuwa waaalimu wanahitajika kufanya vikao na wazazi ili kutambua changamoto mbalimbali za shule na kuweza kushirikiana kuzitatua.
Ambapo katika kuunga mkono jambo hilo mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga John Msemakweli amezitupia lawama bodi za shule kushindwa kutatua matatizo ya utoro wa wanafunzi, waalimu pamoja na kuona namna ya wanafunzi hao kupata chakula mashuleni ili kuweza kuongeza ufaulu kwakuwa wanafunzi hao hushinda njaa jambo linalowafanya kushindwa kuwa makini na masomo.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa
Katika kulitafutia mwarobaini suala hilo la chakula masuleni mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Mazwi Godson Mwaibingila ameuomba uongozi wa mkoa kutoa maelekezo kwa halmashauri ili suala hilo la chakula liwekwe katika sheria ndogo za halmashauri na kuweza kuwalazimisha wazazi kuchangia chakula katika shule za msingi na sekondari ndani ya mkoa.
Aidha, Diwani wa Kata ya Chala, Wilayani Nkasi Michael Mwanalinze alisema kuwa sera ya elimu bure itolewe kwa upana wake ili kuhakikisha wazazi wanaielewa, tofauti na hali ilivyosasa kuwa wazazi hawachangii chochote wakisema kuwa elimu ni bure na kuonya kuwa endapo hali hiyo itaendelea basi ufaulu utaendelea kushuka.
Kwa upande wake kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Winnie Kijazi aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanashughulikia matatizo hayo kwani yapo chini ya mamlaka yao kama halmashauri pamoja na mabaraza yao na kuongeza kuwa mkoa umekuwa ukitoa ushirikiano katika kuhakikisha wanafunzi wanaodhulumu haki za kusoma za wanafunzi wanafikishwa katika vyombo husika kwa taratibu za kisheria.
Jumla ya Watahiniwa 16,069 sawa na asilimia 81.01 wakiwemo wavulana 7,953 na wasichana 8,116 wamefaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019. Huku ufaulu huo ukipanda kwa asilimia 8.01 ukilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2018 uliokuwa asilimia 73.00 na kupelekea kushika nafasi ya 13 kitaifa kati ya mikoa 26.

Mawakala wa Mbolea watolewa wasiwasi huku wakulima wakikataa rangi ya mbolea

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewatoa hofu mawakala wa mbolea mkoani Rukwa kutokana na kupata changamoto ya kulipishwa kibali cha kuingiza malori katika mji w Sumbawanga huku akiwaelewesha wakulima wa mkoa huo kuwa rangi ya mbolea isiwarudishe nyuma wao kutumia mbolea bali waangalie kilichomo ndani ya mbolea hiyo.
Amesema kuwa wananchi wasiangalie rangi kwakuwa awali walizoe mbolea ya kupandia aina ya DAP ikiwa na rangi nyeusi na sasa inaletwa ya rangi nyeupe na hivyo kuwafanya wakulima hao kukosa imani na rangi hiyo na hivyo kushindwa kuitumia hali itakayopelekea kushindwa kufikia lengo la kilimo chenye tija ndani ya Mkoa.
“Kiutaalamu ile rangi siyo hoja, hoja ni kemikali ambazo zipo kwenye ile mbolea yenyewe, mbolea ambayo tunayo kwa mwaka huu ni nyeupe na wakulima wetu walizoea kuiona ikiwa katika rangi nyeusi kwahiyo wanakuwa wanasita, nitoe wito kwamba wasisite kuwa kinachojalisha ni kemikali, kemikali zipo sahihi isipokuwa rangi ambayo haina uhusiano na kemikali,” Alisisitiza
Aidha, amewaondoa hofu mawakala wa mbolea katika Mkoa wa Rukwa kwa kuwahakikishia kupewa vibali maalum na Manispaa ya Sumbawanga kwaajili ya kuingiza malori ya mbolea katika maghala yao ambayo yapo katikati ya mji wa Sumbawanga.
“Kwa vile ni hitaji kubwa la mbolea sasa hivi Wasitozwe “fee” yoyote wanapokuwa wanakwenda kupakua hii mbolea, kwasababu ukiweka vipingamizi zaidi, matokeo yake mbolea itapanda bei, ikipanda bei itamuathiri sana mkulima lakini pia na walaji, kwahiyo kwa hawa ambao yanakwenda kwenye magodown ambayo yanafahamika na yatahakikiwa yatapewa vibali vya kushusha mbolea kule kwenye magodown,” Alisema.
Mh. Wangabo ameyasema hayo baada ya kufanya ziara katika maghala 7 yanayomilikiwa na mawakala hao yaliyopo katika mkoa na kupokea malalamiko juu ya ushuru wanaotozwa shilingi 50,000/= na Manispaa ya Sumbawanga ili kuweza kupitisha malori yao katikati ya mji.
Wakati Mawakala wao wakiwasilisha changamoto na malalamiko yao mmoja wa mawakala hao Mkurugenzi wa Ikuwo General Enterprises Sadrick Malila alisema kuwa wananchi wengi wamekuwa wakidanganywa na wafanyabiashara wa mbolea ambao hununua mbolea ya kupandia DAP nyeupe na kuimwagia Kaboni na kuwa nyeusi na kuwauzia wakulima.
“Wanachokifanya wanachukua hii wanamwaga wanapuliza kaboni inakuwa nyeusi halafu wanawapiga wakulima sasa hii ni hatari sana, nimewaeleza mara nyingi kwamba tangazeni kwenye redio maana ile hata kuuza wanauza kwa kificho, kwasababu watu wanaakili ya kuwa DAP nyeusi ndio inayofanya kazi lakini sio kweli hiyo ndio chnagamoto kubwa tuliyonayo,”Alisema.
Nae Meneja wa kampuni ya ETG Hassan Habibu alisema kuwa changamoto kubwa waliyonayo ni kutozwa shilingi 50,000/= na Manispaa ya Sumbawanga hali inayorudisha nyuma nguvu za mawakala wa mbolea kuingiza mbolea kwa wingi katika mkoa wa Rukwa.
“Kumekuwa na changamoto iitwayo “off loading and loading fee” ambapo gari la uzito wa zaidi ya tani saba wanatakiwa kulipa shilingi 50.000/= hii nadhani nimeona kwenye mkoa huu, wakati wa kushusha hapa na ili iingie mjini lazima ilipe shilingi 50,000/=, kwahiyo imetuletea changamoto kubwa sana wasafirishaji kugoma kuja,” Alilalamika.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili toka kushoto) Afisa kilimo wa Mkoa Ocran Chengula (kushoto) pamoja maafisa wengine walipotembelea moja ya maduka ya pembejeo na mawakala wa mbolea mjini Sumbawanga ili kujua hali ya upatikanaji wa mbolea katika Mkoa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) pamoja na Mkuu waWilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule (kulia) walipotembelea moja ya maghala ya mbolea mjini Sumbawanga ili kujua hali ya upatikanaji wa mbolea katika Mkoa.
Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Mkoa wa Rukwa Ocran Chengula alisema kuwa Mkoa umejipanga vizuri katika kuhakikisha unazalisha mazao mbalimbali zaidi ya milioni 1.7 ambapo kati ya hizo mahindi ni zaidi ya tani 700,500 na kuwa Mkoa umejipanga kuona malengo hayo yanafikiwa katika uzalisha na kuwatoa hofu wakulima juu ya upatikanaji wa pembejeo.

Wanarukwa wahamasishwa kulima kwa tija ili kujiongezea kipato

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wakulima wa Mkoa huo kuhakikisha wanafuata maelekezo ya maafisa kilimo waliopo kwenye ngazi za vijiji na kata ili kuweza kulima kwa tija na hatimae kuongeza upatikanaji wa chakula katika mkoa na pia kujiongezea kipato.
Amesema kuwa ni dhamira ya mkoa kuhamasisha kilimo kinachoongeza uzalishaji kwa ekari moja, hivyo ni lazima wakulima wapande kwa kutumia utaalamu huku wakizingatia ubora wa mbegu ambazo zimehakikiwa na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu nchini (TOSC) pamoja na kutumia mbolea zinazostahili kwa ekari kama ambavyo wataalamu wanashauri
“Sio mtu anachukua mfuko mmoja wa mbolea halafu anakwenda kuuweka katika ekari mbili matokeo yake uzalishaji  unakuwa ni mdogo, lakini pia baada ya mahindi kuwa yameota na kuwekewa mbolea ni lazima pia kuangalia upande wa visumbufu, wadudu wale waharibifu wa mazao, lazima tuweke dawa mapema tutumie viuatilifu ambavyo vinashauriwa na wataalamu wa kilimo, baada ya hpo tuangalie mashamba yetu kwa kupalilia kwa kufanya hivi tunaweza kuzidfi hata gunia 20 kwa ekari,” Alisema.
Ameyasema hayo alipokuwa katika ziara yake maalum ya kuhamasisha kilimo chenye tija katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Mkoani humo akiwa pamoja na wataalamu wa kilimo wa mkoa na halmashauri pamoja na mkuu wa Wilaya hiyo.
Kwa upande wao mmoja wa wamiliki wa shamba lililotembelewa na Mkuu wa Mkoa Bwana Rojas Lukas amesema kuwa changamoto ubwa inayowakuta wakulima na kushindwa kuendelea kulima kilimo chenye tija ni mitaji pamoja na mdudu mharibifu aina ya kiwavi jeshi.
“Kuna mdudu Fulani anaitwa Kiwavi jeshi Yule anatusumbua sananingeomba serikali ijaribu kututafutia dawa ambayo inaweza ikamuua Yule mdudu, kingine tunaomba serikali itusaidie kama inawezekana watukopeshe ili tukuze kilimo chetu kiende mbele,” Alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili toka kulia) akiwa pamoja na wakulima katika kijiji cha Kalalasi kata ya Mkali wilayani Kalambo akiwa pamoja na wakulima wa kijiji hicho wakisaidiana kusukuma plau ikiwa moja ya njia ya kuhamasisha kilimo katika maeneo ya vijijini.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akielekeza namna ya kupanda mahindi kwa kufuta vipimo vinavyoelekezwa na wataalamu wa kilimo na hatumae kufanya kilimo cha Tija.
Akimkaribisha Mkuu wa mkoa katika shamba la mmoja wa wakulima hao mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Juliet Binyura alisema kuwa watalaamu wameendelea kutoa ushauri kwa wananchi mbalimbali na hivyo kuwaomba kuendelea kufanya hivyo ili kuwasaidia wakulima kuweza kufikia kilimo chenye tija.
“Tumekuja kuangalia utaalamu aliopewa kwa wataalamu ambao ni maafisa ugani katika kata yake na wanapanda kwa kutumia kamba na wanapima vipimo vinavyokubalika naamini ya kwamba mazao atavuna vizuri,” Alisema.

TARURA watakiwa kushughulikia maeneo korofi msimu wa mvua

Wakala wa Barabara za mijini na Vijijini (TARURA) wametakiwa kuhakikisha Barabara zote za Vijijini zinapitika mwaka Mzima kwa kufanyiwa matengenezo na endapo itashindikana basi ni muhimu kuyapa kipaumbelea maeneo korofi, hasa katika kipindi hiki cha Mvua jambo ambalo litawasaidia wananchi kuendelea na shughuli zao za Kiuchumi bila vikwazo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo katika kikao cha Bodi ya barabara baada ya wabunge wa mkoa huo pamoja na wenyeviti wa halmashauri kuilalamikia TARURA juu ya utendaji wake wa kazi pamoja na mipangilio yao ya bajeti katika kutekeleza majukumu yao.
“Wakala wa Barabara za Vijijini (TARURA) kuhakiki Barabara zote za vijijini katika Halmashauri zote za Mkoa wa Rukwa ili kwanza wawe na orodha kamili ya Barabara za Vijijini na  zipo kwenye hali gani,Baada ya kuhakiki wawe na orodha ya Barabara zilizoingizwa kwenye Mtandao wa  Barabara za TARURA na Barabara zipi hazipo kwenye mtandao wa Barabara za TARURA na kwanini?,” Alihoji
Aidha alisema kuwa kwa kufanya hivyo itawasaidia TARURA kuwa na picha ya Barabara zote za Mkoa wakati wa upangaji wa Bajeti ya mwaka 2020/2021 ili waweze  kuziweka kwenye Bajeti Barabara ambazo zinahitaji Matengenezo.
Wakati wakiwasilisha malalamiko hayo miongoni mwa wabunge hao walisema kuwa hawaridhishwi na bajeti inayotengwa na TARURA na hata hiyo inayotengwa haifikishwi kwa wakati hali ambayo inasababisha hata hicho kidogo kilichotengwa kushindwa kufanya kazi iliyokusudiwa.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini Mh. Ali Kessy alisema, “Tumepanga bajeti milioni 400 wazilete zote milioni 400, hauwezi kupanga bajeti milioni 400 unaleta milioni 20, nimemuuliza mratibu wa (TARURA) Mkoa, mmeleta shilingi ngapi anasema tumeleta milioni 20 kwenye bajeti ya serikali ya milioni 400, walitenga kabia daraja la Kavunje, wakadarasai wamekwama daraja haliendelei na mvua ndio hiyo kama unavyoona.”
Naye Mbunge wa Nkasi Kusini Mh. Desderius Mipata alisema kuwa wananchi wa kata ya Ninde watatengwa kutokana na TARURA kushindwa kutenga bajeti kwaajili ya ukarabati wa barabara inayowaunganisha wananchi wa kata hiyo na kata za jirani.
“Kwahiyo naomba mtafute njia yoyote ya dharura ya kuwezesha eneo hilo lipitike hakuna namna nyingine ya kufanya, nikiwa bungeni daraja la kwenda ninde lilikuwa limevunjika, nikapiga kelele bahati nzuri walikuja wakatengeneza kwa pesa kidogo lakini barabara yake haipitiki,” Alimalizia.
Wakati akitoa malalamiko yake kwa niaba ya wakandarasi wenzie Bwana Anyosisye Kiluswa amesema kuwa wakandarasi bado wanazidai halmashauri fedha za matengenezo ya barabara kadhaa kabla ya barabara hizo hazijahamishiwa kwa TARURA na kuongeza kuwa halmashauri hizo zilishapewa fedha na serikali lakini matokeo yake wametumia kwa matumizi mengine.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa mbele) akitoka kuangalia daraja la mto Kanteza linalowaunganisha wananchi na kituo cha afya cha Laela, Wilayani Sumbawanga, daraja ambalo limetengewa shilingi milioni 163.2 katika mwaka wa fedha 2019/2020 huku kazi zikiwa zinaendelea.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) akizungumza na baadhi ya wananchi wa mji mdogo wa Laela juu ya adha wanayoipata kabla ya dalaja la mto Kanteza kuanza kutengenezwa na kutaka kujua maoni yao juu ya ujenzi huo muda mfupi baada ya kukagua daraja hilo.

“Sasa kwa sasa hivi wakandarasi tunashindwa kutekeleza wajibu wa kufanya kazi kwasababu pesa zetu wenyewe ni za kuunga unga, ukifanya kazi umelipwa halafu pesa hiyo hiyo unaichukua unakwenda kufanya kazi sehemu nyingine, sasa unapokuwa unafanya kazi bila ya kulipwa na nyingine ambazo zipo wanazitumia kwenye maeneo mengine matokeo yake wakandarasi wa mkoa wa Rukwa tunaonekana hatufanyi kazi vizuri,” Alisisitiza.
Kwa upande wake Kaimu mratibu wa TARURA Mkoa wa Rukwa alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2019/2020 jumla ya fedha shilingi bilioni 4.133 kwaajili ya matengenezo ya barabara km 346.63 na vivuko 48 huku kutoka mfuko wa barabara zikitengwa shilingi bilioni 1.763 kwaajili ya miradi ya maendeleo ambapo daraja la mto Kavunja likitengewa shilingi milioni 400 na daraja la mto Kanteza lilopo Laela likitengewa shilingi milioni 163.2.

Viongozi wapya wa serikali za mitaa wafundwa baada ya kuapishwa

Viongozi wapya 2,766 wa vijiji na vitongoji walioshinda katika uchaguzi wa serikali za  mitaa uliofanyika tarehe 24.11.2019 katika wilaya ya Kalambo wametakiwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanatatua kero na malalamiko ya wananchi wanaowahudumia katika vijiji na vitongoji ili kupunguza msongamano wa wananchi wanaohitaji kutatuliwa kero zao katika ngazi ya wilaya na mkoa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo muda mfupi baada ya viongozi hao kula kiapo mbele yake na mbele hakimu wa mahakama ya Wilaya ya Kalambo ambapo wenyeviti wa vijiji na vitongoji kutoka katika kata 10 za tarafa ya Matai wilayani humo walishiriki katika kiapo hicho.
“Katika ngazi hiyo ya vijiji, vitongoji na mitaa, wenyeviti wa maeneo hayo mimi nikipata mtu anatoka kwenye vijiji vyenu analalamika kwa jambo ambalo ni dogo sana, nitakuita. Utapata usumbufu wa kuja Sumbawanga, uhisabu kuwa utatumia gharama zako kuja na kurudi kutoka kule kweny kijiji chako. Nitakusumbua kwasababu wewe hutaki kusumbuka nikilipata tu nitakusumbua, kwahiyo nendeni mkatatue kero za wananchi katika ngazi zenu, yako mambo mengi mtusaidie sio kila kitu mkuu wa mkoa, kila kitu mkuu wa Wilaya na wengine wanakwenda wanaandika mpaka kwa Rais,”Alisisitiza.
Aidha amewataka viongozi hao kuwaumikia wananchi wote bila ya kujali vyama vyao vya kisiasa, dini wala kabila na kuwataka katika utekelezaji huo kuwa shirikishi kwani wasipofanya hivyo wananchi watashindwa kushiriki katika shughuli za kimaendeleo jambo litakalorudisha nyuma juhudi za mkoa kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma stahiki na kwa wakati.
“Mambo ambayo mnapaswa kwenda kuyasimamia katika maeneo yenu kuwashirikisha wananchi katika kupanga maendeleo, sio unakurupuka tu unasema mimi nataka hiki kifanyike bila ya kuwashirikisha wananchi , lazima wapange waamue wao wenyewe na wakishaamua wao wenyewe watashiriki katika kutekeleza lakini pia watasimamia kulinda yale maamuzi yao na hiyo ndio demokrasia na hili ndilo mkalifanye kule, viongozi wengine wakishachaguliwa kama hivi wanakuwa miungu watu, hatupendi kuona miungu watu kwenye vijiji vitongoji na mitaa,” Alisema.
Na katika kuhakikisha viongozi hao wanatekeleza majukumu yao bila ya visingizio amewaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri nne za mkoa huo kuwapatia mafunzo viongozi hao wapya pamoja na wale ambao ni muhula wao wa pili au zaidi jambao litakalotawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa Mujibu wa Sera za Kisekta, Mikakati ya Kisekta, Sheria, Kanuni, Miongozo na Taratibu zinazosimamia Sekta husika.

Wakati akitoa muhtasari wa taarifa ya uchaguzi wa serikali za mitaa mratibu wa uchaguzi mkoa Albinus Mgonya alisema kuwa mitaa 165 iliyopo katika Manispaa ya Sumbawanga imechukuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo ni sawa na asilimia 100 wakati katika ngazi ya vijiji CCM imechukua vijiji 336 huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikichukua vijiji 2 kati ya vijiji 339 vya mkoa wa Rukwa.

“Vitongoji vilivyoshiriki katika uchaguzi ni 1,816 na kwa nafasi ya vitongoji Chama cha Mapinduzi kimepata nafasi 1,807 sawa na asilimia 99.4 Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimepata nafasi za wenyeviti wa vitongoji 8 sawa na asilimia 0.6. kwa faida ya wadau waliopo hapa nafasi hizi 8 mgawanyo wake ni kama ifuatavyo, Sumbawanga Manispaa nafasi 1, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga nafasi 1 na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi nafasi 6,” Alimalizia. 
Baadhi ya Wenyeviji wa vijiji, vitongoji, viti maalu na wajumbe mchanganyiko wakila kiapo wakati wa hafla fupi ya uapisho wa viongozi hao iliyohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (hayupo Pichani) tarehe 29.11.2019.

Baadhi ya Wenyeviji wa vijiji, vitongoji, viti maalu na wajumbe mchanganyiko wakila kiapo wakati wa hafla fupi ya uapisho wa viongozi hao iliyohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (hayupo Pichani) tarehe 29.11.2019.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiongea na viongozi wapya wa vijiji na vitongoji muda mfupi baada ya viongozi hao kula kiapo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akimsalimia baadhi ya wenyeviti wa kijiji muda mfupi kabla ya kuondoka eneo hilo baada ya viongozi hao kula kiapo tayari kwa kuwatumikia wananchi katika maeneo yao.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akimkabidhi zawadi mtoto wa mmoja wa wenyeviti wa vitongoji muda mfupi kabla ya kuondoka eneo hilo baada ya viongozi hao kula kiapo tayari kwa kuwatumikia wananchi katika maeneo yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Mh. Daudi Sichone wakati akitoa neon la shukurani aliwataka viongozi hao wapya kuhakikisha wanawapatia elimu ya kutosha wananchi wanaowaongoza juu ya kutatua kero na malalamiko katika ngazi hizo zao na sio kumshawishi mwananchi afike ngazi mkoa.
“Hawa viongozi wetu wanantumia mkoa na taifa, hebu ifike mahali tutoe elimu kwa wananchi wetu, kabla hajafika huko angalau akifika kule ionekane sisi sote tunasapoti kwamba kwa tatizo lako hili ni vyema ukafika kwa mkuu wa mkoa lakini sio tu unaamka tu na masimu yako unamyuhangaisha mzee wa watu anashindwa kufanya kazi za watu,”Alisema.
Maeneo yaliyofanya uchaguzi katika mkoa wa Rukwa ni vijiji 67, vitongoji 348, mitaa 9 na wananchi walioshiriki kupiga kura ni 118,887 huku zoezi hilo la uchaguzi likiwa limefanyika katika hali ya amani na utulivu.